Jinsi vita vya Iran vinavyoathiri mahujaji wanaokwenda Umrah

Chanzo cha picha, Getty Images
Waumini wa dini ya kiislamu haswa kutoka bara Afrika waliopo Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya Umrah katika mwezi wa Ramadhan, wamejipata katika njia panda, kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, yaliyosababisha kukatizwa kwa usafiri.
Vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeathiri usafiri wa ndege, na kuathiri oparesheni za mawakala wa usafiri wanaowapeleka watu kufanya Umrah.
Mamilioni ya waumini wa kiislamu hushiriki Umrah nchini Saudi Arabia katika mwezi wa Ramadhan.
Watu millioni 122 walishiriki Umrah mwaka wa 2025.
Ila vita vinavyoendelea kwa sasa Mashariki ya Kati, imesabibisha viwanja vya ndege kufungwa na kuwaacha waliokwenda huko kushiriki Umrah haswa raia wa Nigeria kushangaa iwapo wataweza kufanikisha malengo yao.
Iran, Iraq, Israel, Syria, Kuwait, Qatar, na Falme za kiarabu zimefunga viwanja vyao vya ndege, baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kulemaza usafiri wa anga.
Kufikia sasa mamlaka za Saudi, hazijatangaza kufunga uwanja wao wa ndege, ila kuna hofu kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yakiendelea, huenda usafiri wa kuenda eneo hilo ukaathirika.
Alhaji Zaharaddeen Abubakar,mmoja wa mahujaji wanaotarajia kushiriki Umrah Saudi Arabia, aliiambia BBC kuwa anahofia kuwa walikuwa wamejiandaa kusafairi hadi kulipia hoteli, na kukata tiketi ya ndege na huenda wasiweze kusafiri.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Wale walioko huko Saudi Arabia pia wanafaa kurudi baada ya kukamilisha ibada yao. Ikiwa safari za ndege za kurudi hazitakuwepo, unaona, hilo pia ni jambo la kutia wasiwasi," alisema Alhaji Zaharaddeen.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba kwa kuwa ni shughuli ya kidini, haitakuwa ya kuchosha mradi tu kuna fursa ya kusafiri.
Alhaji Zaharaddeen Abubakar pia aliomba mamlaka za Saudi kuchukua hatua kuhakikisha kwamba Waislamu kutoka kote duniani wanapata fursa ya kufanya Umrah bila changamoto yoyote.
Aliongezea kuwa "katika Hajj iliyopita, kulikuwa na vita kati ya Iran na Israel, na waumini wa Iran waliathirika, ila Saudi Arabia iliwapa makazi na kuwasaidia wasikumbane na changamoto yoyote hadi vita hivyo vilipokwisha." Na anatumai Saudi Arabia itafanya hivyo tena mwaka huu.
Alhaji Musa Rabi'u Muhammed ni mkurugenzi mtendaji wa Murna Travel Agency, kampuni ya usafiri iliyoko Kano,nchini Nigeria, aliiambia BBC kwamba "kuna watu waliopanda ndege na walikuwa karibu kuondoka, lakini walilazimika kukatiza safari zao, na sasa wako nyumbani."
Aliongeza kwamba katika ufahamu wake, kwa sasa hakuna hofu kubwa, lakini kila anapokuwa akizungumza na watu walioko mjini Jeddah wanasema bado kuna hofu.
Marekani na Israel zinaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Iran.















