Je, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran linaweza kutangazwa kuwa magaidi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza na EU hivi karibuni huenda zikatangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa shirika la kigaidi.
IRGC ni jeshi la serikali, jeshi la kisiasa na kiuchumi ambalo linapambana na vitisho kwa utawala wa Kiislamu wa Iran nyumbani, na kusisitiza nguvu zake nje ya nchi.
Kwa nini IRGC inaweza kuitwa shirika la kigaidi?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly anasema anazingatia hatua hiyo baada ya kunyongwa kwa Alireza Akbari, waziri wa zamani wa serikali ya Iran ambaye alihamia Uingereza na kuwa raia wa Uingereza.
Bw Cleverly alisema "alishawishiwa" kurudi Iran, ambako "alikuwa chini ya mchakato wa kisheria unaojulikana na wa kiholela wa utawala".
Bw Akbari alikutwa na hatia ya kufanya ujasusi nchini Uingereza. Alikanusha shtaka hilo na kusema maafisa wa ujasusi wa Iran walimtesa ili aweze kukiri.
Idara za kijasusi za Uingereza pia zilisema kuwa wenzao wa Iran wamelenga watu wengine 10 nchini Uingereza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wakiwemo waandishi wa habari wa Iran.

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock na rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wote wameutaka Umoja wa Ulaya kuiweka IRGC kwenye orodha yake ya magaidi pia.
Wanataja jukumu la IRGC katika kukandamiza maandamano ya hivi karibuni yaliyozuka nchini Iran baada ya kifo cha mwanamke wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22, Mahsa Amini.
Alikuwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili ya nchi alipofariki.
Bunge la Ulaya limepitisha azimio la kuunga mkono kuorodheshwa kwa IRGC kama kundi la kigaidi, lakini nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitahitaji kuidhinisha hatua hiyo.
Marekani iliiweka IRGC kwenye orodha yake ya magaidi mwaka 2019 kwa sababu ya uungaji mkono wake wa muda mrefu kwa makundi yenye silaha kama vile Hezbollah.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni nini?
IRGC ilianzishwa mwaka 1979, baada ya mapinduzi ya Iran, ili kutetea mfumo mpya wa Kiislamu.
Hapo awali ilifanya kazi kama jeshi mbadala la jeshi la kawaida la Iran. "Ilikuwa ni kikosi kimoja cha wanamgambo, lakini sasa kimekua na kuwa shirika kubwa," anasema Dk Sanam Vikal kutoka taasisi ya kimataifa ya masuala ya Chatham House huko London.

Chanzo cha picha, AFP
IRGC ina vikosi vyake vya ardhini, majini na anga, ambavyo kwa pamoja vinakadiriwa kuwa na wafanyakazi 190,000. Inaendesha programu za Iran za makombora ya balistiki na nyuklia.
IRGC pia imejenga himaya kubwa ya biashara, inayomiliki makampuni katika sekta kama vile ulinzi, uhandisi na ujenzi, na inadhaniwa kudhibiti theluthi moja ya uchumi wa Iran.
Je, IRGC imekuwa ikifanya nini nchini Iran?
IRGC inaweka usalama wa ndani nchini Iran kupitia mrengo wake wa kijeshi, Basij Resistance Force.
Imekuwa mstari wa mbele katika kuzima maandamano dhidi ya serikali katika kipindi cha miezi minne iliyopita.
Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Kibinadamu lenye makao yake nchini Marekani linasema takriban watu 522 wameuawa. "Basij imefanya vitendo vingi vya unyanyasaji usiodhibitiwa, na kupigwa hadi kufa," anasema Prof Maryam Alemzadeh kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.
"Haisaidii serikali, kwa sababu ghasia zimechochea maandamano zaidi."

Chanzo cha picha, Reuters
Je, IRGC inafanya nini nje ya nchi?
Tawi la kigeni linalojulikana sana la IRGC ni Kikosi cha Quds (Jerusalem). Inatoa silaha, fedha na mafunzo kwa makundi yenye silaha katika Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Hezbollah, ambayo ina makao yake nchini Lebanon, wanamgambo wa Shia nchini Iraq, na vikosi tiifu kwa serikali ya Syria.
"Kikosi cha Quds kinaimarisha vikosi vya kirafiki katika maeneo ambayo uwiano wa mamlaka unaweza kubadilishwa kwa manufaa ya Iran," anasema Prof Alemzadeh. "Utawala wa Iran unaona Marekani kuwa adui wake mkubwa," anasema Dk Vakil, "na kufadhili makundi ya kuishambulia katika nchi nyingine."

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imekishutumu Kikosi cha Quds na makundi inayoyaunga mkono - kwa kuwaua mamia ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kwingineko katika Mashariki ya Kati.
Itamaanisha nini iwapo IRGC itatangazwa kuwa kundi la kigaidi?
Kuiorodhesha IRGC kuwa kundi la kigaidi kutafanya kuwa ni kosa kuwa mwanachama wa shirika hilo, au kuliunga mkono.
Mali zake zitazuiwa katika nchi ambazo zimeorodheshwa, na hakuna raia au biashara ambayo itaruhusiwa kuipatia pesa.
"Kuzingatia Kikosi cha Walinzi kitaiumiza Iran kwa sababu ina jukumu kubwa katika shughuli za serikali, ndani na nje," kulingana na Dk Vikal. "Ni sehemu kubwa ya taifa la Iran, hivyo ni shabaha nzuri."
Lakini anaonya Iran inaweza kulipiza kisasi kwa kutangaza vikosi vya kijeshi vya Uingereza na nchi za EU kuwa vikundi vya kigaidi, ambayo inaweza kuwafanya walengwa katika Mashariki ya Kati. Hata hivyo, Prof Alemzadeh ana shaka kuwa hatua hiyo itaharibu shughuli za IRGC. "Haitaleta tofauti kubwa ya kiutendaji, kwani tayari kuna vikwazo vingi vilivyowekwa dhidi ya Iran," anasema.












