Je, Morocco walipendelewa kwenye fainali ya Afcon 2025?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ahmed Bahajj
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Senegal ndio mabingwa wa awamu ya 35 ya michuano ya soka barani Afrika afcon yalioandaliwa nchini Morocco.

Hii ni baada ya kuwachabanga wenyeji Morocco bao moja kwa nunge kwenye fainali ya kihistoria iliyokuwa na matukio mengi yenye utata yaliochafua hadhi ya mashindano hayo katika ulimwengu wa soka.

Tukio kuu katika fainali hiyo litakalosalia katika kumbukumbu ya historia ya michuano hiyo ni katika dakika ya 98 pale Senegal walipotoka uwanjani na kususia mechi hiyo kwa muda wa dakika 17.

Chanzo kikiwa ni uamuzi wa refa Jacques Ndala aliyewatuza Morocco penalti baada ya kutumia uamuzi wa VAR. Malick Diouf wa Senegal alidaiwa kumchezea rafu mshambulaiji wa Morocco Brahim Diaz.

Kwa jadhba na ghadhabu, kocha wa Senegal Pape Thiew aliwaamrisha wachezaji wake kutoka kabisa uwanjani akilalamika kuwa wamedhulumiwa.

Mchezaji aliyebaki uwanjani ni Sadio Mane tu, nahodha wa Senegal aliyewashauri wenzake kurejea, na baada ya dakika 17 walirejea na kukubali kuendelea na mchezo.

Kwa bahati nzuri kwa Senegal, Brahim Diaz aliyefunga mabao 5 kwenye michuano hIiyo, aliipiga penalti hiyo iliyonyakwa na kipa Eduad Mendy wa Senegal. Hakufunga

.

Chanzo cha picha, Getty Images

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika muda wa dakika 30 za ziada Senegal waliojikakamua walifunga bao dakika nne kipindi cha kwanza cha muda wa ziada ,mfungaji akiwa Pape Gueye.

Bao hilo la komboa ufe, liliwatosheleza Senegal kunyakuwa kombe mbele ya mashabiki wa Morocco waliotazama kwa huzuni na uchungu usioelezeka.

Morocco hawakupata bao la ukombozi kwa hiyo Senegal waliibuka kidedea na kushinda kombe hilo.

Sasa swali ni, je hatua ya Senegal kutoka uwanjani na kususia kuendelea na mechi hiyo imetia doa kwa kiasi gani ushindi wao kwenye michuano hiyo?

Katika kipengee cha 21 cha shirikisho la kimataifa la soka FIFA: Iwapo timu itakataa kuendelea na mchezo kufuatia kutoridhika na uamuzi wa refa, basi timu pinzani inayosalia uwanjani inastahili kupewa alama tatu na ushindi wa mechi. Kwa hiyo iwapo Senegal hawangerudi mchezoni, basi Morocco wangepewa kombe hilo.

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili kushuhudiwa katika Afcon, mwaka 1996 Nigeria ilitoka uwanjani nao pia Togo walifanya vivyo hivyo mwaka 2010, wote wakihisi kuonewa na mwamuzi.

Mashabiki wa Senegal walikabiliana na maafisa wa usalama baada ya kutolewa kwa penalti hiyo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa Senegal walikabiliana na maafisa wa usalama baada ya kutolewa kwa penati hiyo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi ya wachezaji wa zamani wa soka kama Obi Mikel, Effan Ekoku wa Nigeria wote wamesema tukio hilo limeharibia ushindi wa Senegal na kuiharibia sifa michuano ya Afcon 2025. Walihoji kuwa Senegal hawangetoka uwanjani katikati ya mechi.

Hata hivyo, malalamishi ya Senegal yalianza kabla ya fainali hiyo. Shirikisho la soka la Senegal lililalamikia usimamizi wa michuano hiyo kwa kuwahudumia vibaya.

Walidai walipewa sehemu duni za kupumzika na pia za kufanya mazoezi. Isitoshe walidai pia hawakupewa usalama wa kutosha baada ya tukio la kuzingirwa na mashabiki wa Morocco kwenye basi lao katika kisa ambacho kingezua rabsha.

Mgala muuwe ila haki yake mpe. Sadio Mane licha ya vurugu zote hizo, alipongezwa kama shujaa wa mechi hiyo baada ya kuwarai wenzake kurejea uwanjani, pia amesifiwa kuwa balozi mzuri wa dimba la Afcon.

Kwa Brahim Diaz, mfungaji bora wa Morocco katika michuano hii, fainali hii itasalia daima katika kumbukumbu zake za soka kama jinamizi. Alipoteza penalti dakika ya 98 ambayo iwapo angeifunga, ingewapa Morocco ushindi wa AFCON baada ya kusubiriwa kwa miaka 50.

Penati hiyo ya aina ya Panenka aliyoikosa iliwakatisha tamaa wachezaji na ,mashabiki wa nyumbani.

''Iweje aamue kuweka mbwembwe nyingi wakati alihitaji kufunga tena penati hiyo?'' Walilia kwa uchungu mkali.

Hatua za awali za michuano hii, kulikuwa na madai kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Tanzania walisema kuwa Morocco wakiwa mcheza kwao walikuwa wanapendelewa na marefa katika michuano hii, madai yaliobuliwa na mashabiki wa Sengal waliopigana na maafisa wa usalama kwenye fainali kufuatia uamuzi wa refa kuipa Morocco penati.

Yote tisa kwenye mchezo wa soka, asiyekubali kushindwa si mshindani, Senegal ndio washindi rasmi wa michuano ya Afcon ya mwaka 2025 licha ya ushindi huo kukumbwa na utata huku swali likisalia je, ni kweli Morocco walipendelewa na waamuzi katika michuano ya AFCON 2025.

Bila shaka mchezo hautaki hasira.