Watoto wangu waliingizwa katika biashara haramu ya binadamu. Nilijiunga na polisi kuwasaka

Foday Musa, who has a white goatee, looks solemn. He wears a yellow and black top and white and black knitted skull cap and behind him is a window with blue painted frames.
Maelezo ya picha, Foday Musa hajawaona watoto wake kwa karibu miaka miwili
    • Author, Saidu Bah
    • Nafasi, BBC Africa Eye
    • Akiripoti kutoka, Makeni
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Foday Musa aliumia sana aliposikiliza ujumbe wa mwisho wa sauti alioupokea kutoka kwa mwanawe. Ujumbe huo una urefu wa sekunde 76 na kijana huyo anasikika akilia, akiomba msaada wa baba yake.

"Ni vigumu sana kuusikiliza. Kusikia sauti yake kunaniuma," Musa aliiambia BBC Africa Eye.

Polisi ilimsaidia kuwatafuta watoto wake wawili ambao walikuwa wahanga wa matapeli.

Ilikuwa Februari 2024 ambapo mwana wa Musa mwenye umri wa miaka 22 na binti yake mwenye umri wa miaka 18, pamoja na vijana wengine watano, waliajiriwa kutoka kijijini kwao katikati ya Guinea katika mji wa Faranah na mawakala wakiwaahidi kufanya kazi nje ya nchi.

Kazi hizo hazikufanikiwa na wale walioitwa waajiri waligeuka kuwa wafanyabiashara haramu wa binadamu. Kundi hilo lilivushwa mpaka na kuingia Sierra Leone na kuwekwa kama mateka.

Kesi hiyo ilichukuliwa na shirika la polisi duniani la Interpol nchini Guinea, ambalo liliomba kikosi chao nchini Sierra Leone kutoa msaada. Mwezi Agosti mwaka jana Musa alisafiri hadi Makeni, katikati mwa Sierra Leone, kwa lengo la kuwatafuta.

Maelfu ya watu kote Afrika Magharibi huingizwa katika biashara haramu ya binadamu, inayojulikana kama QNET.

QNET yenyewe ni kampuni halali ya ustawi na mtindo wa maisha iliyoanzishwa Hong Kong - inaruhusu watu kujisajili kununua bidhaa zao na kuziuza mtandaoni.

Hata hivyo huko Afrika Magharibi, magenge ya wahalifu yanatumia jina la kampuni hiyo kama njia ya kujificha katika shughuli zao haramu.

Wafanyabiashara haramu wa binadamu huwalenga watu kwa ahadi ya fursa za kazi katika maeneo kama vile Marekani, Canada, Dubai na Ulaya, wakiwataka walipe kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya gharama za safari kabla ya kuanza kazi.

Mara tu wanapomaliza kulipa, mara nyingi husafirishwa hadi nchi jirani na kuambiwa watasafiri nje ya nchi mara tu watakapo waajiri watu wengine katika mpango huo.

Lakini hata wanapowaleta watu kutoka katika familia na marafiki, kazi wanazoahidiwa hawapewi.

QNET ina kampeni kote katika eneo hilo, ikihusisha mabango na matangazo katika vyombo vya habari, chini ya kauli mbiu "QNET Dhidi ya Ulaghai" na kampuni hiyo imekataa madai kwamba inahusika na biashara haramu ya binadamu.

Msako waanza

Traders with goods balancing on their heads pass in front of a big billboard in Freetown, Sierra Leone, which says 'QNET AGAINST SCAMS'.
Maelezo ya picha, Mabango kama haya yanajaribu kuwaonya watu wa Afrika Magharibi kuhusu matapeli wanaojifanya waajiri wa QNET.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Musa na familia yake walitoa $25,000 (£19,000) kwa wafanyabiashara haramu - hii ilijumuisha ada ya kujiunga na pesa za ziada zilizolipwa ili kuwarudisha watoto wake nyumbani. Kusafiri hadi Sierra Leone mwenyewe lilikuwa tumaini lake la mwisho.

Mahmoud Conteh, mkuu wa upelelezi katika kitengo cha kupambana na biashara haramu ya binadamu cha Interpol ndani ya polisi wa Sierra Leone, anasema kesi hiyo ilikuwa kipaumbele kikubwa kwa kitengo chake.

Conteh alipopokea taarifa kwamba kuna idadi kubwa ya vijana wamezuiliwa katika eneo moja huko Makeni, Musa alijiunga na polisi walipovamia eneo hilo, akitarajia kuwapata watoto wake.

Kulikuwa na mifuko na nguo zimetapakaa sakafuni. Inadhaniwa watu 10 hadi 15 walikuwa wakilala katika kila chumba.

Timu ya Interpol iliwakusanya watu hao ndani ya jengo hilo na kuwakuta baadhi ya watoto wa miaka 14 walikuwa wakiishi hapo.

"Wengi ni Waguinea. Kuna Msierra Leone mmoja tu na Wengine wote ni Waguinea," anasema Conteh.

Watoto wa Musa hawakuwa miongoni mwao, ingawa kijana mmoja alisema walikuwa hapo wiki iliyopita.

Kundi hilo lilipelekwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi kabla ya 19 kati yao kupelekwa nyumbani Guinea.

Polisi wanasema wamefanya zaidi ya uvamizi 20 kama huu mwaka uliopita, wakiwaokoa mamia ya waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu.

Mara nyingi waathiriwa husafirishwa na wafanyabiashara haramu kutoka nchi jirani, lakini wengine, kama Aminata mwenye umri wa miaka 23, ni raia wa Sierra Leone ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, yeye amesafirishwa ndani ya nchi yake.

Mkasa wa Aminata

Young men and women sitting on a floor, their faces have been blurred. They were found in the house that was raided by police in Makeni.
Maelezo ya picha, Wengi wa waliopatikana katika nyumba hiyo huko Makeni walitoka Guinea

Akiwa ameketi kwenye kiti cha plastiki huku miteremko ya Milima ya Wusum ya Makeni ikiwa nyuma yake, Aminata aliiambia BBC jinsi rafiki yake alivyomtambulisha kwa watu wanaodai kuiwakilisha QNET katikati ya mwaka 2024.

Alifanikiwa katika mahojiano na akaambiwa atakwenda kwenye kozi kabla ya kwenda Marekani kwa masomo zaidi na kufanya kazi.

Kikwazo pekee kilikuwa ilibidi alipe $1,000 ili kujiunga na mpango huo.

Wakiwa wameshawishika kwamba ni kweli, familia yake ilimpa pesa walizokuwa wameweka akiba kwa ajili ya karo yake ya chuo.

"Wanapokuajiri kwa mara ya kwanza, wanakulisha, wanakutunza. Lakini kadri muda unavyopita, wanaacha kufanya hayo," aliiambia BBC, akiendelea kusema kwamba hapa ndipo alipolazimika kujitunza mwenyewe.

"Lazima uuze mwili wako na kwenda kulala na wanaume ili uweze kupata pesa - ili uweze kujitunza."

Aminata anasema, waliambiwa ikiwa anataka kusafiri, inabidi awaajiri watu wengine katika mpango huo.

Ili kufanya hivi, wafanyabiashara hao walimpa nambari ya kimataifa ili aonekane kama tayari yuko nje ya nchi alipowasiliana nao.

"Wanakupeleka uwanja wa ndege na unavaa vizuri kama unakaribia kusafiri. Wanakupa pasipoti, wanakupa karatasi bandia za kusafiria," alielezea.

"Kisha wanakupiga picha ili uweze kuwatumia marafiki na familia yako."

Aminata alifanikiwa kuwashawishi marafiki na jamaa sita kujiunga na mpango huo, bado akitumaini kazi hiyo nchini Marekani ingetimia. Haikufanikiwa kamwe.

"Nilihisi vibaya sana kwa sababu walipoteza pesa zao na waliteseka kwa sababu yangu."

Alishikiliwa mahali fulani nje kidogo ya Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone, kwa takriban mwaka mmoja kabla ya kugundua kwamba kazi hiyo haipo.

Aminata aliposhindwa kuajiri mtu mwingine yeyote, hakuonekana kuwa ana manufaa tena kwa wafanyabiashara hao - na alipoamua kuondoka, hakuzuiwa.

Kurudi nyumbani baada ya kila kitu kilichotokea, hasa wakati kila mtu alifikiri anaishi nje ya nchi, ilikuwa vigumu.

"Niliogopa kurudi nyumbani," alisema.

"Nilikuwa nimewaambia marafiki zangu kwamba nimesafiri nje ya nchi. Nilikuwa nimeiambia familia yangu vivyo hivyo. Nilikuwa nikifikiria kuhusu pesa zote walizonipa ili kufika huko."

Watoto wa Musa wamepatikana?

Hakuna takwimu kuhusu idadi ya waathiriwa wa aina hii ya ulaghai lakini kuna ripoti za mara kwa mara katika vyombo vya habari kote Afrika Magharibi kuhusu magenge yanayowadanganya watu kwamba mipango hii ya ajira za kigeni ni halisi.

BBC ilijiunga na polisi katika takriban misako kumi na miwili kwa siku tatu huko Makeni na kukutana na mamia ya vijana waliokuwa wamesafirishwa kutoka nchi kama vile Burkina Faso, Guinea, Ivory Coast na Mali.

Polisi wanasema wamewakamata washukiwa 12 wa biashara haramu ya binadamu.

Kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya nje ya Marekani, kati ya Julai 2022 - wakati sheria ya Sierra Leone ya kupinga biashara haramu ya binadamu ilipopitishwa - na Aprili 2025, kulikuwa na watu wanne tu waliopatikana na hatia ya biashara haramu ya binadamu.

Musa hakuwapata watoto wake na hakuwa na chaguo ila kurudi Guinea mwishoni mwa Septemba.

Conteh, kutoka Interpol, ameiambia BBC wafanyabiashara hao waliwaachilia watoto wa Foday muda mfupi baadaye.

BBC imethibitisha kwamba binti yake Musa alirudi Guinea, lakini hajarudi kijijini kwao - na hakutaka kuhojiwa.

Hajawasiliana na baba yake, jambo linaloashiria aibu aliyoipata na waathiriwa wengi walionaswa katika ulaghai huo.

Mahali alipo mwana wa Musa hapajulikani. Bado hali ni mbaya kwa baba yao.

"Baada ya yote yaliyotokea, nataka yote yaishe na kuwaona watoto wangu," anasema Musa.

"Tungependa warudi kijijini - ningependa wawe hapa pamoja nami."

Imeripotiwa na Paul Myles, Chris Walter, Olivia Acland and Tamasin Ford