'Nahitaji msaada': Maelfu ya waliookolewa kwenye Vituo vya utapeli wakwama Myanmar

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafanyikazi wa zamani na waathiriwa utapeli ambao wamekwama katika kambi za muda, hawajui hatma yao.
Muda wa kusoma: Dakika 6

"Hakika naapa, nahitaji msaada," alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya chini upande wa pili wa simu.

Raia wa Ethiopia, anayejitambulisha kama Mike, alisema anashikiliwa pamoja na wengine 450 katika jengo moja nchini Myanmar, kando ya mpaka wa nchi hiyo na Thailand.

Ni miongoni mwa maelfu ya watu waliokuwa wakiachiliwa kwenye kambi maarufu za matapeli ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwenye mpaka kati ya Thailand na Myanmar kwa miaka mingi, katika hatua inayojitokeza inayotajwa kuwa kali zaidi dhidi ya sekta hii katika mpaka wa Thailand-Myanmar.

Lakini wengi wao sasa wameshindwa kuondoka Myanmar kwenye kambi za dharura kwa sababu ya mchakato wa kuwathibitisha na kupanga safari za kurejea makwao ukifanyika polepole sana.

Makundi ya kijeshi yenye silaha yanayowashikilia yana uwezo mdogo wa kusaidia idadi kubwa ya watu – zaidi ya 7,000.

Mmoja wao amesema wameacha kuwatoa watu kwenye kambi hizo kwa sababu hawaondolewi Thailand kwa kasi ya kuridhisha.

BBC inapata taarifa kwamba hali katika kambi hiyo ni mbaya kiafya, chakula ni kidogo, na wengi wa wale walioachiliwa, kama Mike, wanakabiliwa na matatizo ya kiafya.

Yeye mwenyewe anakabiliwa na hali ya wasiwasi, baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika kituo cha matapeli ambako aliteswa mara kwa mara.

Alisema wanapata mlo mara mbili kwa siku, kulikuwa na vyoo viwili tu kwa watu 450, ambao alisema sasa wanajisaidia popote walipo.

Mike alielezea kuwa alialikwa mwaka mmoja uliopita kufanya kazi aliyoahidiwa kuwa nzuri, nchini Thailand, inayohitaji tu ujuzi mzuri wa lugha ya Kiingereza na uandishi.

Badala yake, alijikuta chini ya usimamizi mkali, akilazimika kufanya kazi muda mrefu kila siku ili kutimiza lengo la kutapeli watu mtandaoni alilokabidhiwa na mabosi zake raia wa China.

"Ilikuwa ni uzoefu mbaya zaidi maishani mwangu. Kwa kweli nilipigwa. Lakini niamini, nimeshuhudia mambo mabaya zaidi yakifanywa kwa watu wengine."

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanaozuiliwa katika kambi hizo wamelalamikia hali duni na isiyo safi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mike ni mmoja wa watu wanaokadiriwa kufikia 100,000 wanaoaminika kuletwa kufanya kazi katika shughuli za utapeli kando ya mpaka wa Thailand na Myanmar, nyingi zikiongozwa na wahalifu na wacheza kamari wa Kichina ambao wametumia hali ya kukosa usimamizi wa kisheria katika eneo hili la Myanmar.

Licha ya taarifa za kutisha kuhusu unyanyasaji kutoka kwa wale waliokimbia huko, maelfu bado wanatoka maeneo ambayo ajira nzuri ni adimu, wakihadaiwa kwa ahadi za malipo mazuri.

China, ambapo wengi wa waathiriwa wa ulaghai wanatoka, imechukua hatua ya kufunga shughuli hizo kando ya mpaka wake na Myanmar, lakini hadi mwaka huu China na Thailand zilikuwa hazijachukua hatua zaidi kuhusu mpaka wa Thailand-Myanmar.

Ariyan, kijana kutoka Bangladesh, amerudi Thailand ili kuwasaidia marafiki 17 ambao bado wako huko. Aliahidi kufanya hivi baada ya kutoroka mwenyewe katika moja ya vituo maarufu vya utapeli mwezi Oktoba mwaka jana.

Alituonyesha video fupi, ya kuogofya ya kituo hicho, kilichokuwa bado kinajengwa katika bonde lenye msitu, ambapo alikuwa anashikiliwa, na anakumbuka namna alivyotendewa vibaya akiwa na marafiki zake mikononi mwa bosi wao Mchina.

"Wakikupa sharti la kuingiza kila wiki, $5,000. Ikiwa hufikii lengo wangekupiga kwa shoti ya umeme. Au kukufunga kwenye chumba chenye giza, kisichokuwa na madirisha. Lakini kama ukiwaingizia pesa nyingi, wangekufurahia."

Ariyan alilazimika kuwahadaa wanaume kutoka Mashariki ya Kati na kuwashawishi kutuma fedha kwa ajili ya uwekezaji wa uwongo. Kwa kutumia AI, wahalifu walimfanya aonekane kwenye skrini kama msichana mzuri, huku wakibadilisha sauti yake pia.

Anasema alichukia kufanya hivyo. Anakumbuka mwanaume mmoja ambaye alikuwa tayari kuuza vito vya mke wake ili kufadhili uwekezaji huo wa kitapeli, na alitaka kumwonya. Lakini alisema mabosi wao walikuwa wakifuatilia simu zao zote.

Unaweza pia kusoma
...

Chanzo cha picha, BBC/ Lulu Luo

Maelezo ya picha, Ariyan amerejea kusaidia marafiki 17 ambao bado wako Myanmar

Kuachiliwa kwa wafanyakazi wa utapeli kuliianza zaidi ya wiki mbili zilizopita baada ya Thailand, chini ya shinikizo la China na baadhi ya wanasiasa wake, kukata umeme na mawasiliano ya simu kwa vituo vilivyo kando ya mpaka.

Thailand ilipunguza upatikanaji wa huduma za benki kwa viongozi wa utapeli na kutoa hati za kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa taasisi za kijeshi waliokuwa wakilinda biashara hiyo.

Hii ilidhoofisha biashara hiyo, lakini pia iliwagusa vibaya watu wa kawaida wa kabila la Karen wanaoishi karibu, na kuweka shinikizo kwa makamanda ili kuonyesha utayari wa kumaliza vitendo vya unyanyasaji kwenye vituo hivyo. Walianza kuwasaidia wale waliokuwa wakijaribu kutoroka, na hata kuwahamisha kwa nguvu katika baadhi ya vituo.

Kambi ambayo Mike anahifadhiwa sasa inalindwa na kundi la Democratic Karen, DKBA, kundi la waasi lililotoka katika jamii ya Karen.

Hadi hivi karibuni, lilikuwa likilinda vituo vingi vilivyokuwa vimeibuka katika eneo lake. Unaweza kuviona kirahisi unapopita kando ya Mto Moei unaotenganisha nchi hizo mbili - maeneo makubwa ya majengo mapya upande wa Jimbo la Karen lililoharibiwa na vita, ukilinganisha na mandhari ya vijijini upande wa mpaka wa Thailand.

Thailand inasisitiza kwamba inaharakisha kadri inavyoweza ili kushughulikia wafanyakazi wa vituo vya utapeli na kuwawezesha kurudi nyumbani.

Kundi la wafanyakazi 260 waliokolewa upande wa Mto Moei kwa mashua mapema mwezi huu.

Na takriban raia 621 wa Kichina walirudishwa moja kwa moja China chini ya ulinzi wa polisi kupitia ndege za kukodishwa. Vinginevyo, harakati za wafanyakazi waliokolewa kuhamia Thailand zinaonekana kukwama.

...

Chanzo cha picha, BBC/ Lulu Luo and Jonathan Head

Maelezo ya picha, Vituo kadhaa ya utapeli nchini Myanmar vinaonekana kutoka mpaka wa Thai

Tatizo ni kwamba watu hawa wanatoka katika nchi nyingi tofauti, huku baadhi zikishindwa kufanya juhudi kusaidia watu wao kurejea nyumbani. Takriban 130 kati ya wafanyakazi 260 wa kwanza waliokuja ni kutoka Ethiopia, ambayo haina ubalozi huko Bangkok.

BBC imesema kuwa baadhi ya nchi nyingine za Afrika zitawarudisha watu wao nyumbani ikiwa watalipiwa. Wengi wa wafanyakazi walioachiliwa hawana chochote; hata hati zao za kusafiria zilikuwa zimezuiliwa na wakuu wa vituo.

Thailand inaogopa kurejesha maelfu ya watu ambao itabidi iwatunze bila kikomo. Pia inataka kuwachuja ili kujua ni akina nani ni waathiriwa halali wa biashara ya binadamu na ni akina nani ambao huenda wamefanya vitendo vya uhalifu, lakini haina uwezo wa kufanya hivyo kwa kundi kubwa la watu.

Idara mbalimbali na mashirika, ikiwemo jeshi, yanahusika katika kusimamia tatizo hili, na inabidi wajiunge kuamua nani afanye nini. Hii haijasaidia kwamba baadhi ya maafisa wa juu wa polisi na wahamiaji wamehamishwa kutokana na kushukiwa kwa ushiriki wao katika biashara ya utapeli.

"Kama suala hili halitatuliwi, basi hatutakoma kushughulikia – lazima tufanye kazi kwa umakini," alisema Waziri Mkuu wa Thailand Paetongtarn Shinawatra Jumatano huko Bangkok. Lakini alikuwa akizungumzia tatizo pana la biashara ya utapeli, siyo mzozo wa kibinadamu unaokua miongoni mwa wafanyakazi walioachiliwa.

...

Chanzo cha picha, BBC/Lulu Luo

Maelezo ya picha, Judah Tana anawasaidia waathiriwa ambao wanachukuliwa na kuingizwa kwenye vituo vya ulaghai.

"Bahati mbaya, inaonekana tuko kwenye hali ya kusimama kidogo," anasema Judah Tana, Mzungu kutoka Australia ambaye anasimamia shirika lisilo la kiserikali linalosaidia waathiriwa wa biashara ya binadamu katika vituo vya utapeli kwa miaka mingi.

"Tunasikia habari za kusikitisha kuhusu ukosefu wa vyoo. Wengi kati ya 260 ambao tayari walifika walifanyiwa uchunguzi na kupatikana na virusi vya TB.

Tunapata taarifa kutoka kwa wale ambao bado wako ndani kwamba watu wanatokwa na damu wakikohoa.

Wanashukuru sana kuwa wameachiliwa kutoka kwenye vituo vya utapeli, lakini wasiwasi wetu ni kwamba hatufanyi kazi kwa kasi ya kutosha."

Thailand sasa inaonekana kuwa tayari kurejesha kundi moja la WaIndonesia 94, kwani ubalozi wao umekuwa ukisisitiza kuachiliwa kwao kwa siku kadhaa na umeweka tiketi za ndege kurejea Indonesia.

Lakini bado kuna zaidi ya 7,000 ambao wako ndani ya Myanmar, hawajui kitakachowatokea sasa.

Mike alinieleza kuwa yeye na wengine waliokuwa pamoja naye wanahofia kwamba ikiwa hawataruhusiwa kuvuka mpaka kuingia Thailand hivi karibuni, DKBA inaweza kuwarudisha kwa viongozi wa utapeli, ambapo wanaweza kukutana na adhabu kwa kujaribu kutoroka.

Jioni ya Jumatano, alipatwa wasiwasi na matatizo ya kupumua ilawa mbaya sana, alisema, walimpeleka hospitalini.

"Nataka tu kurudi nyumbani," alisema kwa njia ya simu. "Nataka tu kurudi nchini kwangu. Hicho ndicho ninaomba."