Wakenya na Mtanzania miongoni mwa walioachiliwa huru na magenge ya utapeli Myanmar

Chanzo cha picha, Thai News
Zaidi ya watu 250 kutoka mataifa 20, ikiwemo Tanzania na Kenya ambao walikuwa wakifanya kazi katika vituo vya utapeli na wizi wa mtandaoni katika Jimbo la Karen, nchini humo wameachiliwa na moja ya makundi ya kijeshi huko Myanmar, na kupelekwa Thailand.
Wafanyakazi hawa, ambao zaidi ya nusu yao ni wakutoka nchi za Afrika na Asia, walipokelewa na jeshi la Thailand, na sasa wanafanyiwa uchunguzi ili kubaini kama walikuwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Thailand, Paetongtarn Shinawatra, alikutana na kiongozi wa China, Xi Jinping, na kutoa ahadi ya kufunga vituo vya utapeli ambavyo vimeenea katika maeneo ya mpaka wa Thailand na Myanmar.
Serikali yake imefunga upatikanaji wa umeme na mafuta kutoka upande wa Thailand kwenye maeneo ya mpaka huo, pamoja na kuimarisha sheria za benki na hati za kusafiria, ili kuzuia watu wasio waaminifu kutumia Thailand kama nchi ya kupitishia wafanyakazi wa kazi za kimagendo na fedha.
Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Thailand wamekuwa wakiishinikiza serikali kuchukua hatua hizi kwa miaka miwili iliyopita.
Wafanyakazi wa kigeni mara nyingi huvutiwa kufanya kazi katika vituo hivi vya utapeli kwa ahadi za mishahara mizuri, au kwa baadhi yao kudanganywa wakiamini kuwa watafanya kazi nyingine nchini Thailand, na sio Myanmar.
Kichina na Kiingereza 'mtego' kwa wafanyakazi
Wafanyabiashara na wamiliki wa vituo ama ofisi hizo hutafuta wafanyakazi wanaojua lugha za wale wanaolengwa kufanyiwa utapeli, udanganyifu au wizi wa mtandaoni, mara nyingi ni lugha ya Kiingereza na Kichina.
Wamekuwa wakiingizwa katika shughuli za uhalifu mtandaoni, kuanzia ulaghai wa mapenzi unaojulikana kama "pig butchering" na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, hadi utakatishaji wa fedha na kamari haramu.
Baadhi yao waliridhia kufanya kazi hii, lakini wengine walilazimishwa kufanya kazi hiyo, na kuachiliwa kwao kunategemea familia zao kulipa fidia kubwa.
Baadhi ya wale waliofanikiwa kutoroka wamesema walikuwa wakiteswa.

Wafanyakazi hao wa kigeni waliachiliwa na kundi la kijeshi la Ukumbusho la Karen la DKBA, moja ya makundi ya silaha yanayodhibiti maeneo ndani ya Jimbo la Karen.
Makundi haya ya silaha yamekuwa yakituhumiwa kuruhusu vituo hivyo kufanya kazi chini ya ulinzi wao, na pia kuruhusu vitendo vya unyanyasaji wa kutisha dhidi ya wahanga wa biashara haramu ya binadamu wanaolazimishwa kufanya kazi katika vituo hivyo.
Serikali ya Myanmar imekuwa ikishindwa kuongeza udhibiti wake katika maeneo mengi ya Jimbo la Karen tangu uhuru mwaka 1948.

Chanzo cha picha, Thai News Pix
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jumanne, Idara ya Uchunguzi Maalum ya Thailand, inayofanana na FBI ya Marekani, iliomba hati za kukamatwa za makamanda watatu wa kundi lingine la kijeshi linalojulikana kama Jeshi la Kitaifa la Karen (KNA).
Hati hizo zilijumuisha Saw Chit Thu, kiongozi wa kijeshi wa Karen ambaye aliingia makubaliano na kampuni ya China mwaka 2017 kujenga Shwe Kokko, mji mpya unaoaminika kufadhiliwa kwa kiasi kikubwa na fedha za utapeli.
BBC ilitembelea Shwe Kokko kwa mwaliko wa kampuni ya Yatai, ambayo ilijenga mji huo.
Yatai inasema hakuna tena udanganyifu katika mji wa Shwe Kokko.
Imeweka mabango makubwa katika mji mzima yakitangaza kwa lugha za Kichina, Kiburma na Kiingereza kwamba kazi ya kulazimishwa haikubaliki, na kwamba "biashara za wizi na utapeli wa mtandaoni" zinapaswa kukoma.
Hata hivyo, BBC ilielezwa na watu wa eneo hilo kwamba biashara ya udanganyifu bado inaendelea, na ilihoji mfanyakazi mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika mojawapo ya vituo hivyo.

Kama ilivyo kwa DKBA, Saw Chit Thu alijiunga na kundi la waasi la Karen (KNU) mwaka 1994, na baadaye akaungana na jeshi la Myanmar. kutokana na shinikizo kutoka Thailand na China, Saw Chit Thu na DKBA wamesema wanawaondoa wafanyabiashara wadanganyifu kutoka maeneo yao.
Kamanda wa DKBA aliwasiliana na mbunge mmoja wa Thailand Jumatano ili kupanga utaratibu wa kuwakabidhi wafanyakazi 260.
Wafanyakazi hao ambao wanaume ni 221 na wanawake 39, wanatoka nchi za Ethiopia, Kenya, Ufilipino, Malaysia, Pakistan, China, Indonesia, Taiwan, Nepal, Uganda, Laos, Burundi, Brazil, Bangladesh, Nigeria, Tanzania, Sri Lanka, India, Ghana, na Cambodia.
Imehaririwa na Yusuph Mazimu












