Watanzania wawili ni miongoni mwa mateka wa Hamas, yasema Israel

TH

Chanzo cha picha, EPA

Watanzania wawili na raia mmoja wa Kusini ni miongoni mwa mateka 224 wanaoshikiliwa na Hamas baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 nchini Israel, serikali ya Israel inasema.

Hakuna hata mmoja kati ya hao watatu aliyetajwa.

Balozi wa Tanzania nchini Israel Alex Kallua ameiambia BBC kuwa ofisi yake pia imepata uthibitisho kutoka kwa mamlaka za Israel kuwa raia wawili wa Tanzania ni mateka wa Hamas. Hata hivyo Balozi Kallua hakutoa majina ya wawili hao.

Balozi Kallua pia hakuthibitisha kama mateka hao ndio wale wale wanafunzi wawili ambao hapo awali ofisi yake iliripoti kuwa hawajulikani walipo. BBC imezungumza na familia ya mmoja wao, Joshua Mollel, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kilimo kwenye mojawapo ya eneo la makazi lililolengwa .

Wageni kutoka nchi 25 kwa jumla wanazuiliwa na Hamas, Israel inasema.

Walichukuliwa wakati wanamgambo kutoka Hamas - ambayo Israel, Uingereza, Marekani na kundi la mataifa yenye nguvu yanaitaja kama shirika la kigaidi - walipovuka hadi Israel kutoka Gaza na kuua takriban watu 1,400.

Israel tangu wakati huo imelipiza kisasi kwa mashambulizi ya anga huko Gaza, ambayo wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema yameua takriban watu 6,500.