'Ndugu yangu mkubwa atarudi lini kutoka Israel?'

 Joshua Mollel alitua Israeli wiki tatu kabla ya shambulio hilo baya

Chanzo cha picha, JOSHUA MOLLEL

Maelezo ya picha, Joshua Mollel alitua Israeli wiki tatu kabla ya shambulio hilo baya
    • Author, Alfred Lasteck & Natasha Booty
    • Nafasi, BBC News, Dar es Salaam naLondon

Baba wa Mtanzania mwenye umri wa miaka 21, ambaye ametoweka tangu wanamgambo wa Hamas waliposhambulia mji wa kibbutz alipokuwa akiishi huko Israel, ameiambia BBC kuhusu uchungu wake, akimtaja mwanawe hadharani kwa mara ya kwanza.

"Mara ya mwisho nilizungumza na Joshua ilikuwa Alhamisi tarehe 5 Oktoba," anasema babake Loitu Mollel. "Nilimwambia 'Zingatia tabia njema kwa sababu uko ugenini, na tumia vyema fursa ya mafunzo unayopata'."

Siku mbili baadaye makao mapya ya Joshua Mollel - Kibbutz Nahal Oz - yalishambuliwa na Hamas.

Alikuwa ameondoka nyumbani kwao kaskazini mwa Tanzania mwezi mmoja tu uliopita

Joshua alifurahi sana kupanda ndege kwenda Israel.

Sio tu kwamba hii ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri nje ya nchi - pia ilikuwa hatua kubwa kuelekea kutimiza matarajio yake maishani.

"Mwanangu anataka kujiingiza shughuli za katika kilimo biashara na kuwa mmoja wa wakulima waliofanikiwa zaidi Tanzania," baba yake anasema kwa kujigamba.

Yeye na mke wake wanatumai kwamba masomo ya Joshua huko Israel hatimaye yataongeza mapato yao kutokana na mafunzo ya kukuza mazao.

Ndugu zake Joshua wanamtazama kama mfano wa kuigwa - kwa hivyo inaumiza kwamba hawajazungumza naye kwenye simu kwa wiki kadhaa.

Tarehe 7 Oktoba wakazi kadhaa waliuawa huko Kibbutz Nahal Oz, na wengine kutekwa na kupelekwa mpaka wa Gaza ambao uko umbali wa mita 800 tu.

Hakuna anayejua kilichompata Joshua, na familia yake ina wasiwasi.

"Hatuwezi kula au kulala - ninapoenda sokoni watu huniuliza kwa nini ninapungua uzani," anasema babake.

tt

Chanzo cha picha, LOITU MOLLEL

Maelezo ya picha, Loitu Mollel anasema yeye na familia yake wanashindwa kulala usiku
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Taarifa kwamba Israel imevamiwa na Hamas ilipotangazwa, nilijaribu kufuatilia kujua iwapo Israel ina ubalozi Tanzania lakini nikaambiwa wanafanya kazi kutoka Kenya.

“Baada ya hapo niliwasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Tanzania na hata nikawasiliana na balozi wa Tanzania aliyeko Tel Aviv.

"Lakini bado sijapata taarifa kuhusu mtoto wangu yuko wapi na yuko katika hali gani."

Tanzania na Israel hazijathibitisha utambulisho wa wanafunzi wawili wa Kitanzania ambao wanasadikiwa kutoweka.

Lakini BBC imefuatilia kubaini wao ni nani, kuzungumza na familia zao ili kupata maelezo kuhusu maisha yao.

Tunajua kwamba Joshua Mollel ni mmoja wa wanafunzi wawili waliopotea, na tunajua utambulisho wa mwingine - lakini wazazi wao wameamua kutowataja hadharani.

"Tunafanya kazi kwa ushirikiano mamlaka ya Israel ili kubaini walipo wanafunzi hao wawili waliotoweka," anasema balozi wa Tanzania mjini Tel Aviv, Alex Kallua. "Hatuwezi kujua kama wameshikiliwa mateka au vinginevyo kwa sababu tunatafuta taarifa sahihi."

tt

Chanzo cha picha, JOSHUA MOLLEL

BBC pia imewasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Israel kupata maoni yake kuhusiana na suala hili.

Takriban Watanzania 350 wanaishi Israel, asilimia 70 kati yao wakiwa wanafunzi wengi wakisomea mambo yanayohusiana na kilimo, kulingana na maafisa wa Tanzania.

Balozi Kallua anasema Watanzania tisa wamerejea salama nyumbani wiki moja iliyopita, na kwamba wafanyakazi wa ubalozi wake "wako makini na wanawasiliana na Watanzania wengine [ambao bado] wako Israel na kuhakikisha wote wako salama. ".

Familia ya Joshua inasema mafunzo yake katika shamba la ngo'ombe wa maziwa la Nahal Oz nchini Israel yaliandaliwa na chuo chake kilichopo katikati mwa Tanzania, Taasisi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo - Katrin. Chuo hicho hakijajibu ombi la BBC la kutoa maoni.

"Hatutaki kulaumu mamlaka kwa kuendesha polepole mpango wa kumtafuta mjukuu wangu, kwa sababu tunaelewa baadhi ya maeneo ya Israel yalishambuliwa na Hamas," babu yake Joshua, Ephata Nanyaro, anasema kidiplomasia.

Lakini hii haipunguzi uchungu wa familia.

"Alionekana mara ya mwisho mtandaoni kwenye [programu ya kutuma ujumbe] WhatsApp mnamo tarehe 7 Oktoba mwendo wa saa 10:00 [13:00GMT] asubuhi," anakumbuka babake Joshua.

"Nimefadhaika sana... Ni ngumu sana. Wasichana wangu wadogo huniuliza kila asubuhi na usiku - 'Baba, tunataka kuzungumza na kaka yetu'.

"Lakini sina la kuwaambia."