Moja kwa moja, Trump asema atatekeleza kwa 'asilimia 100' tishio la ushuru kwa Greenland, EU yaahidi kulinda maslahi yake

Donald Trump ameapa kwa '100%' kutekeleza tishio lake la kutoza ushuru kwa nchi za Ulaya zinazopinga mpango wake kuidhibiti Greenland.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Uwanja wa mpira wa watoto wa Kipalestina wakabiliwa na agizo la kubomolewa na Israel

    Uwanja wa mpira wa watoto wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa unakabiliwa na tishio la kubomolewa hivi karibuni, licha ya kampeni ya kimataifa ya kuununua.

    Wanaounga mkono wanasema uwanja huo unatoa fursa adimu ya michezo kwa wachezaji vijana wa Kipalestina.

    Hata hivyo, Israel inasisitiza kuwa umejengwa bila vibali vinavyohitajika. Katika ardhi hii iliyogawanyika kwa kina, mambo mengi yanapinganiwa; kuanzia utambulisho na imani za watu wanaoishi hapa, hadi kila inchi ya ardhi wanayosimamia.

    Hivi karibuni, mzozo huo umejumuisha pia kipande kidogo cha nyasi bandia kilichowekwa chini ya kivuli cha ukuta mkubwa wa zege unaoitenga Israel na sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Huko Bethlehem, klabu ya mpira, inayodai kuwa ilipata ruhusa ya mdomo mwaka 2020 kwa ajili ya uwanja huo inaamini kuwa tishio la kubomolewa linahusiana zaidi na mambo kuliko sheria za mipango miji.

    “Waisraeli hawataki tuwe na aina yoyote ya matumaini, hawataki tuwe na fursa yoyote,” Mohammad Abu Srour, mmoja wa wajumbe wa bodi ya Kituo cha Vijana cha Aida, aliniambia.

    Wazo, alidokeza, ni kufanya maisha kuwa magumu kwa makusudi.

    “Mara tu tunapopoteza matumaini na fursa, tutaondoka. Hii ndiyo maelezo pekee kwetu.” Tuliwasiliana na chombo cha Israel kinachosimamia masuala ya kiraia katika Ukingo wa Magharibi ili kupata maoni.

    Ingawa agizo la kubomolewa lilitolewa kwa niaba yake, tulielekezwa badala yake kwa jeshi la Israel, ambalo linasimamia kazi zake.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitupa taarifa ifuatayo: “Kando ya uzio wa kiusalama, kuna agizo la kutaifisha na marufuku ya ujenzi; kwa hiyo, ujenzi katika eneo hilo ulifanywa kinyume cha sheria,” ilisema.

    Wanaposubiri kuona kitakachofuata, watoto wa Aida wanatumaini kuwa uangalizi wa kimataifa unaweza kutosha kubadilisha mawazo ya mamlaka.

    Lakini kwa sasa, wakati mgogoro mpana ukiendelea, mustakabali wa uwanja mmoja mdogo wa mpira uko hatarini.

  2. Mtoto wa Museveni 'anajigamba' jinsi alivyowaua watu 22 - Bobi Wine

    Bobi Wine

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa upinzani wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, anadai kuwa watu zaidi ya 100 wameuawa tangu wiki iliyopita na sio 22 kama alivyoandika mtandaoni mtoto wa Rais Yoweri Museveni na Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Muhoozi Kainerugaba.

    ''Jana usiku mtoto wa Museveni alipokuwa akitoa vitisho vya kuniua alionekana ''kufurahishwa'' na hatua ya kuuawa kwa wafuasi wetu 22 (kwa kweli, amewaua zaidi ya 100 tangu wiki iliyopita)'', aliandika kwenye mtandao wa X, alipokuwa akijibu vitisho vilivyotolewa dhidi yake na Jenerali Muhoozi.

    Bobi Wine pia anasema wanajeshi wamezingira boma lake na kuwaamuru watu wote waliokuwa ndani ya nyumba hiyo kutoka nje kama ni wanaume.

    Wine hajaonekana hadharani kwa siku kadhaa na anasema amejificha, akidai alitoroka uvamizi wa polisi nyumbani kwake.

    Jenerali Muhoozi Kainerugaba amempa saa 48 kiongozi huyo wa upinzani kujisalimisha kwa polisi.

    Polisi wa Uganda hata hivyo wanasema kuwa Bobi Wine bado yuko nyumbani na amewazuia waandishi wa habari kukaribia makazi hayo.

    Pia uanweza kusoma:

  3. Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania aaga dunia, Rais Samia amuomboleza

    Rais Samia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu mzee Edwin Mtei akimkumbuka kuwa mmoja wa watumishi na viongozi wenye mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa kwenye eneo la fedha, uchumi na mipango.

    Mzee Mtei alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (1966-1974).

    Aidha Rais Samia amesema Mzee Mtei ataenziwa katika historia ya siasa ya vyama vingi kama miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, pia mmoja wa waasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

    Akizungumza na Mwananchi, Freeman Mbowe ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema, amesema Mzee Mtei ameugua kwa kipindi kirefu na hali yake ilibadilika ghafla na wakati wanamchukua kwa gari la wagonjwa kumpeleka hospitali ya Seliani alifariki dunia akiwa njiani. Mwananchi imeripoti.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche imeeleza kuwa chama hicho kimepoteza moja ya nguzo imara.

  4. Tanzania yapanda katika orodha ya timu bora FIFA

    Timu ya Taifa, Taifa Stars ya Tanzania

    Chanzo cha picha, Taifa stars instagram

    Shirikisho la kimataifa la soka FIFA limetoa orodha mpya ya timu bora za soka mwaka huu wa 2026.

    Morocco wamepanda kwa kiwango kikubwa zaidi katika timu za wanaume wakifika hadi nafasi ya nane,licha ya kupoteza katika fainali ya michuano ya soka barani Afrika AFCON dhidi ya Senegal.

    Senegal walipanda hadi kufika nafasi ya 12 kutoka nafasi ya 17 waliyopata mwaka 2024.

    Mwaka jana Morocco walikuwa katika nafasi ya 11, na nafasi bora waliyowahi kushika katika orodha hiyo ya FIFA ni 10 ikiwa ni mwaka 1998.

    Hata hivyo timu ya Afrika iliyowahi kuchukua nafasi bora zaidi kwenye orodha hiyo ni Nigeria iliyokuwa nafasi ya 5 Aprili mwaka 1994.

    Michuano ya AFCON ya 2025 imekuwa na ushawishi mkubwa katika soka la kimataifa na hivyo kuchangia timu nyingi za Afrika kupanda orodha hiyo.

    Washindi wa shaba katika dimba hilo Nigeria wameorodheshwa katika nafasi ya 26 ,Cameroon nao wako katika nafasi ya 45 nao Misri waliotolewa nusu fainali wameorodheshwa nafasi ya 31 wakiwa wamepanda kwa alama nne pia wakiwa nafasi tatu nyuma ya Algeria.

    Gabon waliporomoka kwa alama nyingi hadi nafasi ya 86 baada ya kutolewa mapema kwenye dimba la Afcon.

    Mabingwa wa Ulaya Hispania wanaongoza orodha hiyo mbele ya bingwa wa dunia Argentina walio nafasi ya pili.

    Ufaransa ni watatu wakifuatwa na England nafasi ya 4 huku Brazil wakishikilia nafasi ya 5.

    Ureno na Uholanzi wako nafasi ya sita na saba mtawalia.

    Je timu za Arika Mashariki ziko wapi?

    Taifa stars ya Tanzania imepanda kwa nafasi mbili na kufikia nafasi ya 110 baada ya kushamiri kwenye dimba la Afcon wakitoka hatua ya raundi ya16 mara ya kwanza kwenye historia.

    Uganda nao wameshuka kwa nafasi tatu baada ya kuboronga kwenye AFCON,wameorodheshwa nafasi ya 88 baada ya kushindwa kushinda hata mechi moja kwenye michuano hiyo.

    Harambee star s wa Kenya wamedorora kwenye orodha hiyo baada ya kukosa kushiriki Afcon kwa mara ya tatu,wako nafasi ya 113.

    Unaweza kusoma;

  5. “Sihitaji kurekebisha uhusiano na familia yangu,” asema Brooklyn Peltz-Beckham

    Sir David na Lady Victoria Beckham hawajawahi kuthibitisha hadharani mgogoro uliokuwa ukiripotiwa sana na mtoto wao mkubwa na mke wake, Nicola.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Sir David na Lady Victoria Beckham hawajawahi kuthibitisha hadharani mgogoro uliokuwa ukiripotiwa sana na mtoto wao mkubwa na mke wake, Nicola.

    Brooklyn Peltz-Beckham amesema kuwa hataki “kurekebisha” uhusiano wake na familia yake, katika maoni yake ya kwanza hadharani akijibu ripoti kuhusu uhusiano wake na wazazi wake.

    Katika mfululizo wa machapisho kwenye Instagram, mtoto wa kwanza wa Sir David Beckham na Lady Beckham aliwalaumu wazazi wake kwa “kumshambulia” yeye na mkewe kwenye vyombo vya habari, akisema walijaribu “bila kuchoka kuharibu” uhusiano wake na Nicola Peltz Beckham.

    Baada ya miezi ya uvumi kuhusu mgogoro katika familia yenye hadhi kubwa, alisema kuwa alijaribu kuweka hali hiyo kuwa ya faragha lakini hakuwa na namna isipokuwa kuzungumza mwenyewe na kusema ukweli.

    BBC imewasiliana na wawakilishi wa Sir David na Lady Beckham kwa maoni. Wawili hao hawajawahi kuthibitisha kuwepo kwa mgongano huo.

    “Nimekuwa kimya kwa miaka na nimefanya kila jitihada kuweka mambo haya kuwa ya faragha,” alisema mwanamitindo mwenye umri wa miaka 26 katika mfululizo wa machapisho kwa wafuasi wake milioni 16.

    “Kwa bahati mbaya, wazazi wangu na timu yao wameendelea kwenda kwa vyombo vya habari, na kuniacha bila chaguo ila kuzungumza mwenyewe na kusema ukweli kuhusu baadhi tu ya uongo uliochapishwa.

    “Sihitaji kurekebisha uhusiano na familia yangu. Siko chini ya udhibiti wowote, ninasimama kwa ajili yangu mwenyewe kwa mara ya kwanza maishani mwangu.”

    Aliongeza: “Hivi karibuni, nimeona kwa macho yangu binafsi jitihada wanazofanya kueneza uongo mwingi katika vyombo vya habari, mara nyingi kwa kuharibu watu wasio na hatia, ili kuhifadhi taswira yao wenyewe. Lakini naamini ukweli daima hujitokeza.”

  6. Mbunifu wa mitindo wa Italia, Valentino, afariki dunia akiwa na umri wa miaka 93

    Gwyneth Paltrow na Valentino Garavani wakiwa katika uzinduzi wa filamu

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mbunifu mashuhuri wa mitindo kutoka Italia, Valentino Garavani, anayejulikana kama Valentino, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.

    Akiwa mmoja wa magwiji wa mitindo ya karne ya 20, mavazi ya Valentino yalivaliwa na watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa, akiwemo Elizabeth Taylor, Nancy Reagan, Sharon Stone, Julia Roberts na Gwyneth Paltrow.

    Alishiriki kuanzisha jumba la mitindo la Valentino mwaka 1960, na alihesabiwa pamoja na Giorgio Armani na Karl Lagerfeld kama miongoni mwa wabunifu wakubwa kabisa katika taaluma hiyo.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye Instagram, Taasisi ya Valentino Garavani na Giancarlo Giammetti ilisema: “Alifariki kwa amani nyumbani kwake mjini Roma, akiwa amezungukwa familia yake.”

    Taasisi hiyo ilisema kuwa mwili wa Valentino utapatiwa heshima ya mwisho katika Piazza Mignanelli mjini Roma kati ya tarehe 21 na 22 Januari.

    Ibada ya mazishi ya Valentino itafanyika siku inayofuata katika Basilika ya Mtakatifu Maria wa Malaika na Mashahidi, kwa mujibu wa taasisi hiyo.

    Valentino alizaliwa katika eneo la Lombardy mwezi Mei mwaka 1932, na alijulikana kwa mitindo iliyodhihirisha anasa, utajiri na fahari kubwa.

  7. Waziri Mkuu wa Hispania aahidi kutafuta chanzo cha ajali mbaya ya treni ya mwendo kasi

    Ajali ya treni

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ameahidi kufuatilia kwa kina sababu za treni mbili za mwendo kasi kugongana kusini mwa Hispania, ajali iliyosababisha vifo vya takribani watu 40, huku waokoaji wakiendelea kuchunguza mabaki ya treni hizo.

    Baada ya kutembelea eneo la ajali, Sánchez pia alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya waathiriwa.

    Zaidi ya watu 120 wengine walijeruhiwa baada ya mabehewa ya treni iliyokuwa ikielekea Madrid kuacha reli na kuvuka hadi njia ya reli ya upande wa pili, kisha kugongana na treni nyingine iliyokuwa ikisafiri kuelekea Adamuz, Jumapili jioni.

    Ajali hiyo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

    Mwendeshaji wa mtandao wa reli, Adif, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 19:45 kwa saa za huko (18:45 GMT) siku ya Jumapili, takribani saa moja baada ya moja ya treni kuondoka Málaga kuelekea kaskazini hadi Madrid, ilipoacha reli katika sehemu ya reli iliyonyooka karibu na mji wa Córdoba.

    Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Óscar Puente, nguvu ya mgongano ilisukuma mabehewa ya treni ya pili hadi kwenye tuta la udongo. Aliongeza kuwa wengi wa waliopoteza maisha na kujeruhiwa walikuwa katika mabehewa ya mbele ya treni ya pili, ambayo ilikuwa ikisafiri kusini kutoka Madrid kuelekea Huelva.

    Timu za uokoaji zilisema mabaki ya treni yaliyopinda na kuharibika vibaya yalifanya iwe vigumu kuwaokoa watu waliokuwa wamenaswa ndani ya mabehewa.

    Sánchez alitembelea eneo la ajali hiyo pamoja na maafisa wakuu wa serikali siku ya Jumatatu alasiri.

  8. Zaidi ya waumini 160 wametekwa nyara katika mashambulizi dhidi ya makanisa Nigeria – viongozi wa dini

    Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makundi yenye silaha yamewateka nyara makumi ya watu waliokuwa wakihudhuria ibada katika makanisa mawili katika jimbo la Kaduna, Nigeria, kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo.

    Kiongozi mmoja mwandamizi wa kanisa alisema waumini zaidi ya 160 walitekwa nyara na watu wenye silaha wakati wa ibada ya Jumapili.

    Hili ni tukio la hivi karibuni katika wimbi la utekaji nyara wa halaiki nchini Nigeria, ambapo Wakristo na Waislamu wote wamekuwa wakilengwa.

    Makundi hayo, yanayojulikana kijijini kama “bandits”, mara kwa mara hufanya mashambulizi kama hayo katika maeneo ya kaskazini na kati mwa nchi ili kupata fedha za fidia.

    Akielezea shambulio la Jumapili, polisi wa eneo hilo walisema watu waliokuwa na “silaha za kisasa” waliingia kwa nguvu katika makanisa hayo mawili yaliyopo Kurmin Wali, jamii ya msituni katika kata ya Afogo, mnamo saa 11:25 kwa saa za huko.

    “Washambuliaji walikuja kwa idadi kubwa, wakaziba njia za kuingia makanisani na kuwalazimisha waumini kutoka na kuingia porini,” alisema Mchungaji Joseph Hayab, mkuu wa Shirika la Kikristo la Nigeria (CAN) kwa kanda ya kaskazini, alipoliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu.

    Akizungumza na Reuters, Hayab aliongeza: “Taarifa nilizopokea kutoka kwa wazee wa makanisa zinaeleza kuwa waumini 172 walitekwa nyara, huku tisa wakifanikiwa kutoroka.”

    Mwezi Novemba, wanafunzi na walimu zaidi ya 300 walitekwa nyara kutoka shule moja ya Kikatoliki. Baadaye waliachiliwa kwa makundi mawili tofauti. Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa msururu wa matukio ya utekaji nyara yaliyopewa uzito mkubwa na vyombo vya habari vya kimataifa.

    Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama, zikiwemo utekaji nyara wa kuomba fidia unaofanywa na magenge ya kihalifu, uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kaskazini-mashariki, ghasia za kujitenga kusini-mashariki, pamoja na mapambano kati ya wafugaji na wakulima katika eneo la kati juu ya upatikanaji wa ardhi na maji.

    Unaweza kusoma;

  9. Trump asema atatekeleza kwa “asilimia 100” tishio la ushuru kwa Greenland, EU yaahidi kulinda maslahi yake

    Kaja Kallas, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), alisema kuwa umoja huo “hauna nia ya kuanzisha mzozo, lakini utasimama kidete kulinda msimamo wake.”

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Kaja Kallas, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), alisema kuwa umoja huo “hauna nia ya kuanzisha mzozo, lakini utasimama kidete kulinda msimamo wake.”

    Donald Trump ameapa "100%" kutekeleza tishio lake la kutoza ushuru kwa nchi za Ulaya zinazopinga ombi lake la kuchukua udhibiti wa Greenland.

    Washirika wa Ulaya wameungana kuunga mkono uhuru wa Greenland.

    Waziri wa mambo ya nje wa Denmark alisisitiza kwamba rais wa Marekani hawezi kutishia kumiliki eneo la Denmark.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper alisisitiza msimamo wa Uingereza kwamba mustakabali wa Greenland ni kwa "Wagreenland na Wadenmark pekee" kuamua.

    Siku ya Jumatatu, Trump alikataa kuondoa mpango wa matumizi ya nguvu na akasisitiza kwamba ataendelea na ushuru unaotishiwa kwa bidhaa zinazofika Marekani kutoka Uingereza na nchi nyingine saba washirika wa NATO.

    Alipoulizwa na NBC News kama angeweza kutumia nguvu kuiteka Greenland, Trump alijibu: “Hakuna maoni.”

    Rais wa Marekani alisema atatoza Uingereza ushuru wa asilimia 10 kwa “bidhaa zote bila ubaguzi” zitakazopelekwa Marekani kuanzia tarehe 1 Februari, na ushuru huo utaongezeka hadi asilimia 25 kuanzia tarehe 1 Juni, hadi pale makubaliano yatakapofikiwa ya Washington kuichukua Greenland kutoka Denmark.

    Trump alisema hatua hiyo hiyo itatumika kwa Denmark, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Finland, nchi zote ambazo ni wanachama wa muungano wa Nato ulioanzishwa mwaka 1949.

    Alipoulizwa kama atatekeleza tishio hilo la ushuru, Bw Trump aliambia NBC News: “Nitafanya hivyo, asilimia 100.”

    Unaweza kusoma;

  10. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo