Wapiganaji wa Hamas waliojificha kwenye mahandaki wawasilisha kikwazo kipya kuhusu kusitisha mapigano Gaza

Chanzo cha picha, AFP
Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump na mjumbe wake wa mzozo wa Gaza, walirejea Mashariki ya Kati Jumatatu.
Wakati huo huo, wapatanishi wanakabiliwa na kikwazo kipya katika juhudi zao za kusukuma mazungumzo kuhusu makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Israeli na Hamas katika awamu mpya na ngumu zaidi.
Mambo muhimu bado hayajatatuliwa, kama vile kupokonya silaha Hamas, ujenzi mpya na utawala wa baadaye wa Gaza, au kupelekwa kwa kikosi cha usalama cha kimataifa katika eneo hilo.
Bila ratiba ya mazungumzo hayo, ambayo yanaweza kuhitaji makubaliano makubwa kutoka kwa Israeli na Hamas, maswali mazito yanaibuka kuhusu uwezekano wa kupata maendeleo yoyote.
Kuongezea hili ni tatizo jipya: wapiganaji kadhaa wa Hamas wanaaminika kujificha kwenye handaki chini ya mji wa kusini wa Rafah, nyuma ya kile kinachoitwa "Mstari wa Njano" unaoweka mipaka ya eneo lililo chini ya udhibiti wa Israeli.

Chanzo cha picha, Israel GPO via EPA
Wapiganaji wa Hamas chini ya ardhi
Wiki iliyopita, mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff alisema msamaha unaweza kutolewa kwa wapiganaji wanaoweka silaha zao chini, na kwamba unaweza kutumika kama mfano wa kile ambacho Washington ilitarajia kutekeleza katika sehemu nyingine ya Gaza.
Witkoff alisema wapiganaji 200 wamenaswa, ingawa idadi hiyo haijathibitishwa.
Kulingana na ripoti za habari, Kushner na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu walizungumzia suala hilo Jumatatu wakati wa mkutano huko Yerusalemu.
Hamas hapo awali ilisema kwamba wapiganaji hao hawatajisalimisha na imedai wapewe njia salama, ombi ambalo Israel imekataa hadi sasa.
Msemaji wa serikali ya Israel alisema kwamba Netanyahu na Kushner walihutubia awamu ya kwanza, iliyopo sasa, ili kuwaokoa mateka waliobaki, pamoja na mustakabali wa awamu ya pili ya mpango huu unaojumuisha kupokonya silaha Hamas, kuondoa kijeshi Gaza na kuhakikisha kwamba shirika la Kiislamu halina ushawishi tena katika Ukanda wa Gaza.
Vita huko Gaza vilianza kufuatia shambulio lililoongozwa na Hamas mnamo Oktoba 7, 2023 kusini mwa Israeli, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Tangu wakati huo, zaidi ya watu 69,000 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo takwimu zake Umoja wa Mataifa unaziona kuwa za kuaminika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutokuwa na uhakika na kukwama
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano, ambayo ilianza kutumika mwezi uliopita, ililenga kusimamisha vita, kuwaachilia mateka wote, na kuhakikisha ongezeko kubwa la misaada ya kibinadamu huko Gaza.
Hamas imewakabidhi mateka 20 wakiwa hai na mabaki ya 24 wakiwa wamekufa, huku miili minne ikiwa imesalia Gaza.
Kwa upande mwingine, Israeli imewaachilia huru wafungwa 250 wa Kipalestina kutoka magereza yake na 1,718 walioshikiliwa bila mashtaka au kesi katika Ukanda huo, pamoja na mabaki ya Wapalestina 315 kutoka Gaza.
Israel na Hamas zote mbili zimeshutumiwa kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano: Israeli inadai kwamba Hamas imechelewesha kwa makusudi kurudi kwa mabaki ya mateka, huku Hamas ikisisitiza kwamba Israeli imewaua Wapalestina wasiopungua 240 na inazuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu.
Hamas hapo awali ilikataa kuweka silaha chini, ikisema itafanya hivyo mara tu taifa la Palestina litakapoanzishwa. Israeli inakataa kuhusika kokote katika utawala wa Gaza na Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono na Magharibi, ambayo ni chombo kinachotawala sehemu za Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Nchi zinasita kuwaweka wanajeshi katika kikosi cha kimataifa bila malengo yaliyo wazi, zikihofia kwamba wanajeshi wao wanaweza kuishia kukabiliana na wapiganaji kutoka Hamas na vikundi vingine vya Palestina.
Jeshi la Israel kwa sasa linachukua 53% ya eneo la Gaza na linatarajiwa kujiondoa zaidi katika hatua inayofuata ya mpango huo.
Bila dalili yoyote ya maendeleo yanayotarajiwa katika mazungumzo, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mgawanyiko wa Gaza kati ya eneo linalodhibitiwa na Israel na lingine linalotawaliwa na Hamas, vyanzo viliambia shirika la habari la Reuters, huku mazungumzo kuhusu ujenzi upya yakionekana kuwa mdogo kwa eneo linalodhibitiwa na Israel.
Nchi za Kiarabu tayari zimeelezea wasiwasi kwamba utengano wa sasa unaweza kuwa mgawanyiko wa kudumu wa Gaza.
Mpango wa Trump haujumuishi njia ya kuelekea kuwa taifa la Palestina, dhana ambayo Israel inakataa.















