Je, msimamo wa mataifa ya kiarabu ni upi kuhusu Hamas Gaza?

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kundi la wapiganaji wa Hamas waliokuwa na silaha wakati wa kukabidhiwa mateka wa Israel mwezi Februari.
Muda wa kusoma: Dakika 7

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema anajiandaa "kuchukua udhibiti kamili wa Ukanda wa Gaza na kuwaondoa Hamas." Hata hivyo, katika mahojiano na runinga ya Marekani Fox News, alionyesha kuwa Israel haina nia ya "kusalia katika Ukanda huo kama mamlaka inayotawala."

Matamshi ya Netanyahu yanaongeza shinikizo zaidi kwa Hamas, ambayo tayari inakabiliwa na matakwa ya kikanda na kimataifa ya kupokonywa silaha.

Hamas imekataa ombi hilo, ikisema kwamba haitachukua hatua hiyo isipokuwa taifa la Palestina litakapoanzishwa na uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ukomeshwe.

Hamas ilitangaza msimamo wake kuhusu suala hili katika taarifa iliyotolewa siku chache zilizopita, huku kukiwa na shinikizo kubwa la kutaka kulazimishwa kusalimisha silaha zake zote na kuandaa njia ya mchakato wa kidiplomasia utakaopelekea kutekelezwa kwa suluhu ya serikali mbili.

Katika kongamano la kimataifa lililofanyika mwezi uliopita wa Julai kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kwa ufadhili wa Saudi Arabia na Ufaransa, nchi 17 mbali na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilitoa tamko la pamoja kuhusu utatuzi wa amani wa suala la Palestina na utekelezwaji wa suluhisho la nchi mbili.

Azimio la New York, ambalo lina vifungu 42, limeitaka Hamas kuachia udhibiti wa Ukanda wa Gaza na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Miongoni mwa waliotia saini tamko hili ni Misri na Qatar, ambazo kwa kawaida zinapatanisha mazungumzo kuhusu Gaza. Hata hivyo, Israel na Marekani hawakutia saini Azimio la New York na hawakushiriki hata kidogo katika mkutano huo.

Hamas wataendelea na mapigano

Wakati wa mahojiano ya televisheni na Al Jazeera Mubasher, yaliyotangazwa kutoka Doha, kiongozi wa Hamas Ghazi Hamad alisema vuguvugu hilo halitaacha "hata risasi tupu," na kwamba "silaha zinamaanisha kupigania Palestina."

Amesisitiza kuwa, Hamas iko tayari kuendeleza mapambano yake hadi pale taifa la Palestina litakapoanzishwa.

.

Chanzo cha picha, Amr Alfiky / Reuters

Maelezo ya picha, Ghazi Hamad alisema wakati wa mahojiano ya televisheni na Al Jazeera Mubasher kwamba Hamas haitaacha silaha zake.

Hussam Al-Dajani, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Al-Ummah katika Jiji la Gaza, anaamini kwamba vyombo vya habari vinaangazia Kifungu cha 11 cha Azimio la New York, ambacho kinasema kwamba "utawala bora, utekelezaji wa sheria, na usalama katika maeneo yote ya Palestina itakuwa jukumu la mamlaka ya Palestina pekee."

Kifungu hicho pia kinatoa wito kwa "Hamas iachie udhibiti wake wa Ukanda wa Gaza na kusalimisha silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina."

Al-Dajani anabainisha kuwa, kuna vifungu vingine 41 katika tangazo hilo, baadhi vikitoa wito wa kuanzishwa kwa taifa la Palestina na kuishi pamoja kwa amani na Israel.

Anathibitisha kwa BBC: "Ikiwa vifungu vingine vya Azimio la New York vitatekelezwa, Kifungu cha 11 kitakuwa hitimisho lililotarajiwa."

Serikali ya Palestina kwanza

.

Chanzo cha picha, Haitham Imad/EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Mwakilishi wa Msalaba Mwekundu akiwa amesimama karibu na wapiganaji wa Hamas walipokuwa wakikabidhi miili ya mateka wanne wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza mwezi Februari.

Kundi la Hamas limetengazwa kuwa shirika la kigaidi na Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibi. Hatahivyo Hamas imetangaza kwa zaidi ya hafla moja kwamba itakabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mara tu taifa la Palestina litakapoanzishwa.

Afisa wa usalama wa Hamas hapo awali aliambia BBC kwamba harakati hiyo imepoteza sehemu kubwa ya udhibiti wake Gaza.

Hamas bado inashikilia muundo wa kiserikali katika Ukanda huo. Kitengo chake kipya cha usalama, kinachojulikana kama "Arrow," kinafanya kazi kwa lengo la vuguvugu la kudumisha utulivu wa umma na kuzuia wizi wa misaada kuwasili katika Ukanda huo.

Lakini miezi 22 baada ya vuguvugu la silaha kuanzisha mashambulizi yake kwa Israeli mnamo Oktoba 7, 2023, na majibu ya baadaye ya kijeshi ya Israeli, Hamas na mrengo wake wa kijeshi wanaonekana dhaifu zaidi.

.

Chanzo cha picha, Mohammed Saber / EPA-EFE / REX / Shutterstock

Maelezo ya picha, Mashambulizi ya anga ya Israel yamesababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba na maduka huko Gaza.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuhusiana na hili, Profesa Yossi Mekelberg, mshauri mkuu katika Chatham House, taasisi ya wataalam yenye makao yake makuu London, anasema kwamba Hamas "haikufikiria uzito wa" matokeo ya mashambulizi ya Oktoba 7.

Kwa upande mwingine, vyanzo vya ndani vya Gaza vinaripoti kwamba Hamas bado inamiliki silaha, lakini risasi zake zinapungua.

Duru zinaongeza kuwa wapiganaji wa harakati hiyo wanatumia tena mabaki ya silaha zilizoachwa nyuma na mashambulio ya Israel, ambayo mengi ni mabomu ambayo hayajalipuka, ili kupata vilipuzi vinavyowawezesha kutengeneza vilipuzi vya kujitengenezea wenyewe ili kuwashambulia wanajeshi wa Israel.

Israel inawazuia waandishi wa habari wa kimataifa kuingia Gaza, kwa hivyo hatuwezi kuthibitisha hili kwa uhuru.

Wakati huo huo, Wapalestina huko Gaza wanaonyesha hasira dhidi ya Hamas, huku Amnesty International ikilaani kampeni ya harakati hiyo ya "ukandamizaji na vitisho" dhidi ya waandamanaji wanaoipinga Hamas mwezi uliopita wa Mei.

Msimamo wa nchi za Kiarabu

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy (katikati kushoto) akimkumbatia Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Mustafa kwenye Umoja wa Mataifa Julai 29, 2025.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ambayo ina nchi wanachama 22, zikiwemo nchi ambazo kijadi zinachukuliwa kuwa wafuasi wa Hamas, kama vile Qatar, zilitia saini Azimio la New York, ambalo linaitaka harakati hiyo kupokonywa silaha.

Profesa Mekelberg anaamini kuwa Israel na Marekani zinachukua misimamo yao ya kawaida kuhusu Hamas. Hata hivyo, anasema kwamba sauti ya mataifa ya Kiarabu imebadilika. Anabainisha kuwa kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa nchini hizo za Kiarabu na kikanda kunaweza kuwaacha Hamas ''wametengwa kabisa."

Kikanda, Hamas ina idadi ndogo tu ya washirika iliyobaki. Kufuatia vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran mwezi Julai mwaka jana, uwezo wa Tehran kuendelea kuunga mkono Hamas umepungua sana.

Hizbullah, mojawapo ya madola mashuhuri ya kikanda yenye mafungamano na Iran, pia imedhoofishwa kwa kiasi kikubwa na mashambulizi ya Israel na mauaji ya viongozi wake wakati wa mapigano makali kati ya pande hizo mbili kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hezbollah tayari inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa serikali ya Lebanon kusalimu silaha zake.

Mateka

Hamas inaendelea kuwashikilia mateka waliosalia wa Israeli tangu Oktoba 7, 2023, kama suluhu.

Wanamgambo hao waliwateka watu 251 wakati wa shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa na ambalo liligharimu maisha ya takriban watu 1,200, kulingana na mamlaka ya Israel.

Zaidi ya Wapalestina 60,000 wameuawa kutokana na kampeni ya kijeshi ya Israel huko Gaza iliyofuata, tangu Oktoba 2023, kulingana na data kutoka kwa Wizara ya Afya katika Ukanda huo.

Makadirio ya Marekani yanaonyesha kuwa mateka 20 wa Israel bado wako hai huko Gaza, baadhi yao wamefariki na wengine wamerejeshwa Israel.

Mapema Agosti, Hamas ilitoa video ya mateka aitwaye Eviatar David, akionekana dhaifu na mnyonge.

Kuuawa kwa viongozi wa Hamas

Tangu Oktoba 2023, Israel imewaua viongozi kadhaa waandamizi wa Hamas, akiwemo mkuu wa ofisi ya kisiasa ya vuguvugu hilo, Ismail Haniyeh, ambaye aliuawa katika kile vuguvugu hilo lilieleza kuwa ni "uvamizi" wa Israel kwenye makazi yake katika mji mkuu wa Iran, Tehran, Julai 2024.

Israel pia ilimuua Yahya Sinwar, anayeaminika kuwa mpangaji mkuu wa mashambulizi ya Oktoba 7.

Kwa mujibu wa Mekelberg, viongozi wa Hamas ndani ya Gaza wana maslahi tofauti na viongozi wa nje ya Ukanda huo.

Mbali na kipaumbele cha kunusurika, viongozi wa Hamas huko Gaza wanajaribu "kuhifadhi msimamo wao wa kisiasa, ambao bado unaungwa mkono kwa kiasi fulani, ili kufikia makubaliano," alisema.

Lakini ili vuguvugu hilo lidumishe msimamo wake, viongozi wake waliosalia lazima wafanye maamuzi magumu.

Baada ya Netanyahu kutangaza nia yake ya "kuchukua udhibiti kamili wa Gaza," chaguzi za Hamas zinapungua siku hadi siku.

Mustakabali wa Hamas

.

Chanzo cha picha, Amir Cohen / Reuters

Maelezo ya picha, Majengo yaliyoharibiwa kaskazini mwa Gaza, kama inavyoonekana kutoka upande wa mpaka wa Israeli.

Kutabiri mustakabali wa Hamas kunaonekana kuwa kugumu sana. Harakati hiyo inasema itatoa silaha zake iwapo taifa la Palestina litaanzishwa, matarajio ambayo yanaonekana kutowezekana isipokuwa iwapo serikali ya Israel itabadilisha msimamo wake wa sasa kuhusu suala hilo.

Lakini wachambuzi wanaamini kuwa kupokonywa silaha kwa Hamas, hata kama itatokea, haimaanishi kuangamia kwa vuguvugu hilo.

Yossi Mekelberg anatabiri kwamba Hamas inaweza kuwa na nafasi ya "kujijenga upya katika siku zijazo" na kubakia kuwa mhusika mkuu katika uwanja wa kisiasa wa Palestina, ndani na nje ya ardhi za Palestina.

Lakini yote haya yanategemea msimamo wa Israel kuhusu taifa linaloweza kuwa la Palestina, pamoja na umaarufu wa Hamas, kutokana na hali mbaya inayowakabili wananchi wa Gaza hivi sasa kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 na kampeni ya kijeshi ya Israel iliyofuata.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla