Athari za uvamizi kamili wa Israel huko Gaza kwa wakazi wake na Hamas

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama ilivyotarajiwa na wengi, Mkuu wa jeshi la Israeli Eyal Zamir aliidhinisha mpango wa kuteka mji wa Gaza Jumapili, Agosti 17.
Zamir alisema jeshi litaelekea kutekeleza awamu inayofuata ya Operesheni Gideon katika Ukanda huo.
Wakati wa ziara yake katika Ukanda wa Gaza, Zamir alionyesha kuwa vita vya sasa havina kikomo na ni sehemu ya mpango wa muda mrefu, akisisitiza kwamba jeshi lina "wajibu wa kimaadili" kuwarudisha nyumbani wafungwa walioko Gaza.
Hapo awali Zamir alikuwa amefanya mkutano uliopanuliwa na Kamandi ya Kusini kujadili kupitishwa kwa mipango ya hivi punde ya kukalia Gaza City.
Mnamo Agosti 13, jeshi la Israeli lilitangaza kwamba Zamir ameidhinisha "wazo kuu na la msingi la mpango wa kushambulia Gaza," siku chache baada ya baraza la usalama la Israel kuidhinisha upanuzi wa operesheni za kijeshi ndani ya Ukanda huo.
Lipi lengo la hatua hiyo?
Wataalamu wa Kipalestina wa masuala ya Israel wanakubaliana kuwa uamuzi wa kuikalia Gaza tayari umechukuliwa katika ngazi ya kisiasa ya Israel. Hata hivyo, wanaamini kuwa bado haijajulikana ukubwa wa uvamizi huu utakuwaje, iwapo utazunguka eneo lote la Ukanda wa Gaza, au muda wake utakuwa upi.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, kifungu cha tano cha azimio hilo lililoidhinishwa na Mkuu wa Jeshi la Israel la kuikalia kwa mabavu Gaza kilikuwa wazi katika mjadala wake wa lengo la kile ambacho uongozi wa Israel unakiita udhibiti wa Gaza, ambayo ni kuanzisha serikali ya kiraia katika Ukanda huo.
Kwa maoni ya Netanyahu, kama Wen anavyoonyesha, hii inahusisha kugawa kazi ya kusimamia Ukanda huo kwa familia za Wapalestina na watu binafsi watiifu kwa Israel.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakazi wa Gaza wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu aina ya mipango ya jeshi la Israel ya kukalia kwa mabavu eneo hilo na malengo inayotaka kufikia.
Hii ni katika hali ambayo Israel inazidi kueneza propaganda za vitisho miongoni mwa wakaazi wa Gaza, ikiwataka waondoke kabla ya operesheni hiyo kuanza, huku wakaazi wakibakia kutojua waenda wapi.
Redio ya Jeshi la Israel iliripoti kwamba jeshi litaanza kuwahamisha wakaazi wa Palestina kutoka Gaza City katika wiki zijazo.
Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee alisema Jumamosi, Agosti 16, kwamba Israel itawapa wakazi wa Gaza mahema na vifaa vya makazi kuanzia Jumapili, Agosti 17, kwa ajili ya maandalizi ya uhamisho kutoka maeneo ya mapigano hadi sehemu ya kusini ya Ukanda huo.
Kituo cha habari za Israel i24news kilinukuu vyanzo vya habari Jumapili, Agosti 17, vikisema kwamba jeshi la Israel limechagua eneo "kusini mwa mhimili wa Morag," karibu na Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, kama eneo la kambi ya makazi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao, kabla ya kuanza kwa uvamizi wa Gaza.
Kulingana na idhaa hiyo, Israel itahamisha mamia kwa maelfu ya Wapalestina kwenye kambi hii.
Reuters, ikinukuu vyanzo vya habari, inaripoti kwamba mpango wa kijeshi wa Israel unaweza kuchukua wiki kadhaa, au labda miezi, kukamilika, haswa ikizingatiwa hitaji la kuwahamisha raia kutoka maeneo ya mapigano. Uhamisho huo unatarajiwa kuendelea hadi Oktoba.
Kauli za jeshi la Israel zinaibua wasiwasi kwamba mpango wa kuwakusanya wakazi zaidi wa Gaza katika maeneo ambayo Israel inayaita kuwa maeneo ya kibinadamu ni hatua ya kwanza tu kuelekea kuwaondoa wakazi wa Ukanda huo.
Pia wanazua wasiwasi juu ya msongamano wa watu kusini mwa Gaza, na kuwaweka kwenye hatari zaidi za kukabiliwa na milipuko ya magonjwa.
Upinzani na jinsi Netanyahu anavyojitetea nyumbani

Chanzo cha picha, Reuters
Ndani ya nchi, sauti za familia za mateka wa Israel huko Gaza zinaendelea kupaa, zikitaka kusitishwa kwa vita na kurejeshwa kwa mateka.
Wakati huo huo, Mwendesha Mashtaka wa Kijeshi alitoa onyo la wazi la matokeo ya kisheria ya kuteka maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza, akisema kuwa jukumu la Israel la kutoa huduma za kimsingi kwa idadi ya watu litaongezeka kwa kiasi kikubwa, na hivyo kusababisha shinikizo kubwa la kimataifa.
Mwendesha mashtaka wa kijeshi wa Israel amesisitiza kuwa, kukalia kwa mabavu maeneo ya ziada na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya Wapalestina katika eneo dogo kutaongeza shinikizo ya kisiasa na kisheria dhidi ya Israel na kudhoofisha uhalali uliotolewa na baadhi ya nchi katika kuendeleza vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kwa upande wake, alitetea mpango wa Israel kuchukua udhibiti wa kijeshi katika mji wa Gaza wakati wa mkutano wa awali na waandishi wa habari, akisisitiza kwamba hakuna njaa katika Ukanda huo.
Netanyahu alisema, "kinyume na madai ya uwongo, hii ndiyo njia bora ya kumaliza vita, na njia bora ya kumaliza vita haraka. Hivi ndivyo tunavyomaliza vita.
Nani atatawala Gaza?
Wakati operesheni hiyo bado haijaanza, mjadala unazidi kuongezeka juu ya nani atatawala Gaza katika siku zijazo, na kupendekeza kuwa Israel inatazamia matukio na kudai kuwa itaweza kuutokomeza kabisa utawala wa Hamas huko Gaza, au kwamba hatimaye itauondoa mara moja na kwa wote.
Ripoti iliyochapishwa na jarida la Israel la "Sof Shavoa" ilionyesha kuwa mapambano juu ya mustakabali wa utawala wa Gaza tayari yameanza, hata kabla ya kumalizika kwa vita hivyo ni wazi.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Misri inakuza wazo la serikali ya kiteknolojia, wakati Israel inazingatia makundi yenye silaha yanayopinga Hamas, bila kutoa mbadala halisi, maarufu.
Kwa mujibu wa jarida hilo, licha ya kupita takriban miaka miwili tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, na operesheni kali za kijeshi zilizofuata, Israel bado haina mpango wazi wa awamu inayofuata.
Jarida hilo lilibainisha kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anarudia kauli za jumla bila kutaja vyama mbadala au asili ya awamu inayofuata.
Hili ndilo linaloifanya Gaza kwa sasa kukumbwa na wakati mgumu, pamoja na njaa na uhaba wa maji huku wakazi wake wakiendele kuteseka.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












