Tunachokijua kuhusu mpango mpya wa Israel wa kuudhibiti mji wa Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Kelly Ng na Hugo Bachaga
- Nafasi, Maripota BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika kile kinachoonekana kama ukurasa mpya wa vita vinavyoendelea Ukanda wa Gaza, serikali ya Israel imeidhinisha mpango wa kijeshi wa kuutwaa mji wa Gaza jiji kubwa lenye historia, watu na maisha ya kawaida kabla ya mzozo huu kuchukua mkondo wa sasa.
Kwa mamilioni ya Wapalestina, Gaza City si tu jiji, bali ni nyumbani.
Ndiyo maana mpango huu mpya umeibua maswali mengi na kupingwa si tu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, bali hata ndani ya Israel kutoka kwa familia za mateka walioko mikononi mwa Hamas, wanajeshi wastaafu, hadi wananchi wa kawaida.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa lengo lake ni kuhakikisha usalama wa Israel kwa muda mrefu kwa kuliondoa kundi la Hamas, kulikomboa jiji hilo kutoka mikononi mwa wapiganaji, na kuliweka chini ya usimamizi wa kile alichokiita "mataifa ya Kiarabu".
Yaliyomo katika mpango huo bado haijajulikana, lakini hiki ndiyo tunachokijua kufikia sasa kuhusu mpango huu mpya;

Chanzo cha picha, Majdi Fathi/NurPhoto via Getty Images
Je, mpango wa kanuni za kukomesha vita ni upi?
Mpango huu umepewa jina la "Kanuni Tano za Kukomesha Vita", ukielezea malengo makuu yafuatayo:
- Kulivunja kabisa kundi la Hamas na kuondoa silaha zote nzito.
- Kuwarejesha mateka wote iwe wako hai au wamepoteza maisha.
- Kuweka Gaza kuwa eneo huru lisilo na silaha nzito.
- Kudhibiti usalama wa eneo hilo kwa usimamizi wa jeshi la Israel.
- Kuunda serikali mbadala ya kiraia isiyohusiana na Hamas wala Mamlaka ya Palestina.
Hata hivyo, linaloibua sintofahamu ni hili la jeshi la Israel kutangaza kuwa linajiandaa kuudhibiti mji wa Gaza huku likipeleka misaada ya kibinadamu kwa "wakazi wa nje ya maeneo ya vita."
Bado haijabainika ikiwa hii inamaanisha msaada mpya na kama msaada huu utatolewa kwa wakazi wa Gaza na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza unaoungwa mkono na Israel na Marekani au utaratibu mwingine.

Chanzo cha picha, Khames Alrefi/Anadolu via Getty Images
Kwanini ni jiji la Gaza pekee linadhibitiwa na Israel?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Japo Netanyahu awali alisema Israel inalenga kuuteka Ukanda wote wa Gaza, mpango huu mpya unaelekeza nguvu kwenye Gaza City tu jiji lililokuwa na wakazi zaidi ya milioni moja kabla ya vita.
Israel imetangaza kuwa inadhibiti asilimia 75 ya Gaza, huku Umoja wa Mataifa ukikadiria kuwa asilimia 86 ya eneo la Gaza imo chini ya amri ya jeshi au maeneo ya mapigano.
Jiji hilo limezingiriwa na ardhi ambayo awali ilikuwa chini ya udhibiti wa Israel.
Mpango huo unalenga vikosi vya Israel kudhibiti mji huo mkubwa zaidi katika eneo hilo kwa mara ya kwanza wakati wa mzozo huo.
Kwa mujibu wa mwanahabari wa BBC wa mashariki mwa milki za kiarabu Hugo Bachaga, huenda kutwaa jiji hili ni hatua ya kwanza kuelekea kulidhibiti eneo lote la Gaza.
Wengine wanasema Israel inafanya hivi kama njia ya kuishinikiza Hamas wakubali masharti kwenye mazungumzo yaliyokwama.
Katika mahojiano na Fox News, Netanyahu alisema kuwa Israel "haitaki kuidhibiti Gaza" lakini inakusudia kuikabidhi kwa "majeshi ya nchi za Kiarabu."
"Tunataka kuwa na eneo la usalama. Hatutaki kuendesha Gaza," aliambia chombo hicho.

Chanzo cha picha, Tsafrir Abayov/Anadolu via Getty Images
Ni lini Israel itadhibiti jiji la Gaza?
Mpango huo haujafafanuliwa kwa muda rasmi utakaoanza, lakini vyombo vya habari vya Israel vinaeleza kuwa jeshi lao halitaingia jiji la Gaza na kuwa wakaazi watahamishwa kabla ya wao kuingia.
Israel imesema kuwa inaamini "mpango mbadala" uliowasilishwa kwa baraza la mawaziri "hautasababisha kushindwa kwa Hamas au kurejeshwa kwa mateka."
Hata hivyo, haijabainika wazi mpango huu mbadala ni upi au ni nani aliyeupendekeza.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa ni pamoja na pendekezo dogo zaidi lililotolewa na mkuu wa majeshi.
Kulingana na mwandishi mwandamizi wa kimataifa wa BBC Liz Doost, Netanyahu anazungumza "kwa makusudi" kuhusu majeshi ya Kiarabu anayorejelea ni nani, kama alivyofanya siku za nyuma kuhusu mipango yake kwa Gaza.
Huenda anawazungumzia Wajordani na Wamisri ambao wamesema wako tayari kushirikiana na Israel, lakini wameweka wazi kuwa hawataingia Gaza mara tu Israel itakapoikalia kwa mabavu.
Hakuna maelezo zaidi ambayo yameshirikiwa kuhusu ratiba ya jinsi Gaza itakavyotawaliwa baada ya mji huo kutekwa, na Hamas bado haijajibu mpango huo.
Majibu kutoka ndani na nje ya Israel
Familia za mateka wana hofu kubwa wakihisi kuwa mpango huu mpya unahatarisha maisha ya wapendwa wao.
Vile vile viongozi wa kimataifa pia wamemkosoa Netanyahu kuhusu mpango wake mpya.
Ndani ya Israel, baadhi ya maafisa wa kijeshi wanatilia shaka mafanikio ya mpango huu, wakisema Hamas tayari imedhoofishwa vya kutosha na kwamba kuendelea na mashambulizi ni kuongeza maumivu kwa raia wasio na hatia.
Duniani, viongozi kadhaa wameonyesha wasiwasi mkubwa:
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema kwamba hatua hiyo "haitaleta suluhu, bali itaongeza umwagaji damu."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong, ameonya kuwa kuuteka mji wa Gaza kutazidisha janga la kibinadamu.
Mustafa Barghouti, Mkuu wa Mpango wa Kitaifa wa Palestina ameelezea uamuzi wa Israel wa kupanua operesheni za kijeshi huko Gaza kuwa ni uhalifu wa wazi wa kivita.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilitangaza kuwa Israel inakusudia "kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kutoka katika ardhi yao," huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Elina Valtonen akielezea matumaini ya kusitishwa kwa mapigano mara moja huko Gaza na kuachiliwa mara moja kwa mateka wa Israel.
Umoja wa Mataifa kupitia Kamishna wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ametaka vita vikomeshwe mara moja, akisema kuendelea kwa mapigano kutazidisha mateso, mauaji na uharibifu usio na maana.
Makao makuu ya Jumuiya ya Familia za mateka wa Israel pia yametangaza kuwa uamuzi huu "unatupeleka kwenye maafa makubwa kwa mateka na askari wetu."
Kuna ripoti kwamba Wamarekani wammruhusu Netanyahu kuuteka mji wa Gaza.
Lakini ni vyema kutambua kwamba NBC News iliripoti "simu ya wasiwasi" kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Bw. Netanyahu mwishoni mwa mwezi Julai, ambayo rais wa Marekani alielezea kama "habari za uongo."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












