Madaktari Iran wadai kuzidiwa na majeruhi huku maandamano yakiendelea

BBC imepokea ujumbe kutoka kwa daktari katika hospitali moja akisema haikuwa na madaktari bingwa wa kutosha kukabiliana na ongezeko la wagonjwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Jeshi Iran laapa kulinda mali ya umma huku ikijaribu kutuliza ghasia zinazoongezeka

    .

    Chanzo cha picha, Middle East Images / AFP via Getty Images

    Jeshi la Iran limesema siku ya Jumamosi kwamba litalinda miundombinu ya kimkakati na mali ya umma na kuwasihi Wairani kuzuia "njama za adui", huku taasisi ya makasisi ikiongeza juhudi za kuzima maandamano makubwa zaidi nchini humo kuwahi kutokea.

    Taarifa hiyo ya kijeshi ya Iran ilikuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa onyo jipya kwa viongozi wa Iran siku ya Ijumaa, na baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio siku ya Jumamosi kutangaza kuwa: "Marekani inawaunga mkono watu jasiri wa Iran."

    Ghasia kutokana na maandamano zimeendelea usiku kucha. Vyombo vya habari vya serikali vilisema jengo la manispaa lilichomwa moto huko Karaj, magharibi mwa Tehran, na kuwalaumu "waasi".

    Soma zaidi:

  2. Netanyahu atumai 'kupunguza' utegemezi wa misaada ya kijeshi wa Israel kwa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema katika mahojiano yaliyochapishwa Ijumaa kwamba anatumai "kupunguza" utegemezi wa Israeli kwa msaada wa kijeshi wa Marekani katika muongo mmoja ujao.

    Netanyahu amesema Israel haipaswi kutegemea misaada ya kijeshi ya kigeni lakini imeacha kutangaza wakati ambapo Israel itaacha kabisa kutegemea Marekani.

    "Nataka kupunguza utegemezi wa kijeshi ndani ya miaka 10 ijayo," Netanyahu aliambia The Economist. Alipoulizwa kama hiyo ilimaanisha kupunguza utegemezi "kabisa," akajibu, "Ndiyo."

    Netanyahu alisema alimwambia Rais Donald Trump wakati wa ziara yake ya hivi karibuni kwamba Israeli "inathamini sana" "msaada wa kijeshi ambao Marekani imetupatia kwa miaka mingi, lakini pia tulipo tumekomaa na tumejiongeza kiuwezo."

    Pia unaweza kusoma:

  3. UN yasema wakimbizi 53 wa Congo wafariki nchini Burundi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Zaidi ya wakimbizi 50 wanaokimbia mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamefariki katika nchi jirani ya Burundi, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa liliambia Reuters Ijumaa jioni.

    Kati ya jumla ya vifo 53 vilivyorekodiwa, watu 25 walikufa kutokana na mlipuko wa kipindupindu, shirika hilo lilisema, huku wengine sita wakifariki kutokana na upungufu wa damu na matatizo mengine yanayohusiana na utapiamlo, lilisema.

    U.N ilisema inashirikiana na wizara ya afya na washirika wengine kuchunguza chanzo cha vifo vingine.

    Zaidi ya WaCongo 100,000 wametafuta hifadhi nchini Burundi tangu mapigano karibu na mpaka yalipozidi mapema Desemba na waasi kuuteka mji wa Uvira, UNHCR ilisema.

    Jean Jacques Purusi, gavana wa jimbo la Kivu Kusini ambapo Uvira iko, alielezea hali nchini Burundi kama "matatizo" na "mgogoro uliosahaulika kabisa na jumuiya ya kimataifa na vyombo vya habari."

    Wizara ya mambo ya ndani na kijamii ya Congo ilisema inaongoza misheni ya kibinadamu kuwasaidia WaCongo waliokimbia makazi yao nchini Burundi, kwa kutoa chakula, dawa, na vitu visivyo vya chakula.

    Soma zaidi:

  4. Madaktari Iran wadai kuzidiwa na majeruhi huku maandamano yakiendelea

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Huku maandamano nchini Iran yakiendelea na mamlaka ya Iran ikitoa maonyo yaliyoratibiwa kwa waandamanaji, daktari na muuguzi katika hospitali mbili waliiambia BBC kwamba vituo vyao vya matibabu vilikuwa vimejaa watu waliojeruhiwa.

    Daktari mmoja alisema hospitali ya macho ya Tehran ilikuwa iko katika hali ngumu, huku BBC pia ikipokea ujumbe kutoka kwa daktari katika hospitali nyingine ikisema haikuwa na madaktari bingwa wa kutosha kukabiliana na ongezeko la wagonjwa.

    Siku ya Ijumaa, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Iran ilikuwa katika "matatizo makubwa" na akaonya "ni vyema isianze kufyatua risasi kwa sababu sisi pia tutaanza kufyatua risasi".

    Katika barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Iran iliilaumu Marekani kwa kuyageuza maandamano hayo kuwa kile ilichokiita "vitendo vya uasi na uharibifu mkubwa".

    Soma zaidi:

  5. Trump aonya juu ya mashambulizi zaidi Nigeria ikiwa Wakristo 'wataendelea kuuawa'

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kwamba anaweza kuagiza mashambulizi zaidi ya anga dhidi ya Nigeria ikiwa Wakristo wataendelea kuuawa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

    Katika mahojiano mapana na New York Times, Trump aliulizwa kama mashambulizi ya Siku ya Krismasi katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Sokoto, yanayolenga wanamgambo wa Kiislamu yalikuwa sehemu ya kampeni pana ya kijeshi.

    "Ningependa kuifanya iwe shambulizi la mara moja. Lakini wakiendelea kuwaua Wakristo itakuwa mashambulizi ya kila mara," alisema.

    Serikali ya Nigeria imekataa shutuma za awali za Trump kwamba inashindwa kuwalinda Wakristo kutokana na mashambulizi ya jihadi, ikisema kwamba "Waislamu, Wakristo na wale wasio na imani sawa" wanalengwa.

    Soma zaidi:

  6. Morocco yatinga nusu fainali huku ikididimiza ndoto ya Cameroon

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wenyeji Morocco walijihakikishia nafasi katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) la 2025 kwa ushindi mkubwa dhidi ya Cameroon mjini Rabat.

    Bao moja katika kila kipindi, lililofungwa na Brahim Diaz na Ismael Saibari, lilitosha kuwashinda wapinzani wao, ambao walikuwa tishio mara chache sana.

    Baada ya kufikia rekodi yao ya kihistoria ya kufika nusu fainali nchini Qatar, timu ya Regragui imebakisha ushindi mara mbili ili kutwaa taji la kwanza la bara la nchi hiyo tangu 1976.

    Morocco sasa hawajashindwa katika mechi 25 - rekodi inayojirejelea hadi walipotolewa katika hatua ya 16 bora katika fainali za 2023 - na wameingia katika nne bora katika Afcon kwa mara ya kwanza tangu 2004, walipopoteza dhidi ya Tunisia katika fainali.

    Atlas Lions watakuwa katika nafasi nzuri watakaporejea nyumbani tena Jumatano (20:00 GMT) kucheza na washindi wa robo fainali ya Jumamosi kati ya Algeria na Nigeria (16:00 GMT).

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mabosi wa kampuni ya mafuta wasema kwa sasa Venezuela 'haifai kwa uwekezaji'

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais wa Marekani Donald Trump ameomba angalau dola bilioni 100 (pauni bilioni 75) katika matumizi ya sekta ya mafuta huko Venezuela, lakini mkurugenzi mtendaji mmoja ameonya kwamba nchi hiyo ya Amerika Kusini kwa sasa "haifai kwa uwekezaji".

    Wakurugenzi wa makampuni makubwa zaidi ya mafuta ya Marekani waliohudhuria mkutano huo walikiri kwamba Venezuela ina akiba kubwa ya mafuta na kwamba ni fursa inayovutia.

    Lakini walisema mabadiliko makubwa yanahitajika ili kufanya eneo hilo kuwa linalovutia uwekezaji. Hakuna ahadi kubwa za kifedha zilizotolewa mara moja.

    Trump alisema ataachilia mafuta ya taifa hilo la Amerika Kusini baada ya vikosi vya Marekani kumkamata kiongozi wake Nicolas Maduro katika shambulio la Januari 3 lililofanyika eneo la mji mkuu.

    Trump alisema "mojawapo ya faida ambayo Marekani itapata ni bei ya chini zaidi ya mafuta".

    Lakini wakuu wa kampuni za mafuta waliokuwepo walionyesha tahadhari.

    Afisa mkuu mtendaji wa Exxon Darren Woods alisema: "Meli zetu zimekamatwa huko mara mbili na kurudi tena mara ya tatu kutahitaji mabadiliko makubwa kutoka kwa kile ambacho tumekiona kihistoria na kile ambacho kinaendelea kwa sasa."

    "Kwa sasa eneo hilo halifai kwa uwekezaji."

    Venezuela imekuwa na uhusiano mgumu na makampuni ya mafuta ya kimataifa tangu mafuta yagundulike katika eneo lake zaidi ya miaka 100 iliyopita.

    Soma zaidi:

  8. Trump asema Marekani inahitaji 'kumiliki' eneo la Greenland ili kuzuia Urusi na China kulichukua

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Donald Trump amesema Marekani inahitaji "kumiliki" eneo la Greenland ili kuzuia Urusi na China kufanya hivyo.

    "Nchi zinapaswa kuwa na umiliki na kutetea umiliki, hutetei mikataba ya kukodisha. Nasi nilazima tutatetea eneo la Greenland," Trump aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa, akijibu swali kutoka kwa BBC.

    Tutafanya hivyo "kwa njia rahisi" au " ngumu", aliongeza. Ikulu ya White House ilisema hivi karibuni kwamba utawala unafikiria kununua eneo linalojitawala kiasi la mwanachama mwenzake wa Nato, Denmark, lakini haikuondoa uwezekano wa kulinyakua kwa nguvu.

    Denmark na Greenland zinasema eneo hilo haliuzwi. Denmark imesema hatua za kijeshi zitasababisha mwisho wa muungano wa ulinzi wa trans-Atlantic.

    Licha ya kuwa eneo lenye watu wachache zaidi, eneo la Greenland kati ya Amerika Kaskazini na Aktiki linaifanya iwe mahali pazuri pa mifumo ya tahadhari ya mapema iwapo kutatokea mashambulizi ya makombora, na kwa ajili ya ufuatiliaji wa vyombo vya anga katika eneo hilo.

    Rais wa Marekani amerudia kusema kwamba Greenland ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani, akidai bila ushahidi kwamba "ilikuwa imefunikwa na meli za Urusi na China kila mahali".

    Marekani tayari ina wanajeshi zaidi ya 100 waliowekwa katika kambi yake ya Pituffik katika ncha ya kaskazini-magharibi mwa Greenland - kituo ambacho kimekuwa kikiendeshwa na Marekani tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    Chini ya makubaliano yaliyopo na Denmark, Marekani ina uwezo wa kuleta wanajeshi wengi kadri inavyotaka Greenland.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 10/01/2025.