Kuishi kwa hofu ya Lakurawa - kundi la wanamgambo lililoshambuliwa na Trump nchini Nigeria

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma/BBC
- Author, Makuochi Okafor
- Nafasi, BBC Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Hofu kubwa imetanda kwa muda mrefu katika nyanda kame za juu kaskazini-magharibi mwa Nigeria - hata kabla Marekani kuwashambulia wanamgambo wenye itikadi kali za kidini ambao wamefanya eneo hili kuwa ngome yao usiku wa Krismasi.
Wanamgambo hao wenye silaha nzito, ambao huvalia mavazi ya kujificha kufunga vilemba, wameishi katika sehemu ya Tangaza, eneo la kijijini la jimbo la Sokoto karibu na mpaka na Niger, kwa miaka kadhaa.
Kundi hili la wanamgambo linalojulikana kama Lakurawa linatokea maeneo ya kaskazini mwa Nigeria katika Sahel.
Wenyeji wa Tangaza, wengi wai Waislamu wenye msimamo wa wastani, wanaamini wanatoka Niger na Mali - na wanawaogopa.
Hivi majuzi, mamlaka zote za Marekani na Nigeria zimesema wanamgambo hao wana mafungamano na makundi ya Islamic State (IS) katika eneo la Sahel - Japo IS haijajihusisha na shughuli zozote za kundi hilo au kutangaza kuwa na uhusiano na Lakurawa kama ilivyofanya na makundi mengine katika eneo hilo ambayo inayaunga mkono.
Wakati BBC ilipotembelea Nukuru, mojawapo ya vijiji kadhaa vya Tangaza karibu kilomita 10 kutoka mahali ambapo makombora ya Marekani yalipiga, watu wengi walikuwa na wasiwasi mkubwa na hawakutaka kuzungumza juu ya Lakurawa - kwa kuohofia kuchukuliwa hatua.
Hata hivyo baada ya kuhakikishiwa kwamba utambulisho wao haungetajwa ndipo baadhi ya wanaume walikubali kuhojiwa, huku wakizungumza kwa sauti ya chini.
Tulikuwa tumesafiri hadi katika eneo hatari, takriban kilomita 12 kutoka mpaka wa Niger, siku ya Jumamosi tukisindikizwa na polisi na walinzi wa ziadawa.
Katia hali za kawaida polisi hawafiki katika eneo hili kwani wanasema hawana uwezo wa kutosha kukabiliana na wanamgambo iwapo watavamiwa.
Timu yetu haikuweza kufika eneo la mashambulizi kwa sababu ya changamoto za kiusalama - na ilishauriwa kutochukua muda mrefu katika eneo hilo ili kuepusha uwezekano wa wanamgambo kutega mabomu ya ardhini kwenye njia yetu ya kutoka.
Mkulima, ambaye anaishi karibu na Nukuru, alisema muda mfupi baada ya shambulizi la anga la Marekani la Alhamisi usiku, baadhi ya wanamgambo waliokuwa wakikimbia walikusanyika pamoja na wanavijiji.

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Walikuja wakiwa juu ya pikipiki kama 15 hivi," aliiambia BBC, akielezea kwamba kulikuwa na wapiganaji watatu katika kila pikipiki.
Aliwasikia wakiwapigia simu wenzao, kuwasihi kuondoka haraka iwezekanavyo, kabla ya kutoroka kwa kutumia pikipiki.
"Nahisi walikuwa wameshtutuka sana - sisi pia tulikuwa na hofu," alisema. "Hawakuwa na mwili wowwote wa mtu aliyeuawa, walikuwa na mizigo tu."
Haijabainika iki kuna watu wowote waliojeruhiwa katika shambulio hilo lililoamuriwa na Rais Donald Trump dhidi ya kambi mbili.
Lakini wakazi wa Nukuru - kitongoji kidogo chenye takriban nyumba 40 na matope zilizoezekwa kwa nyasi na maghala yao yaliyotumika kuhifadhi mazao yaliyovunwa miezi michache iliyopita - wanaweza kuthibitisha mirindimo ya makombora hayo.
"Milango na paa zilikuwa zikitikisika, paa kuukuu zilipasuka," mzee wa miaka 70 alituambia.
"Tulishindwa kulala kwa sababu kila mahali kulikuwa kunatetemeka. Hatukujua ni nini, na tulisikia vitu vikianguka kutoka angani, na baadaye moto ukazuka."

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma/BBC
Hata hivyo wanakijiji wanahofia wanamgambo hao wanaweza kujipanga upya. Ni wepesi na hutumia pikipiki kufikia kwa haraka eneo hilo lisilo na miundombinu muhimu ya usafiri.
Ni rahisi kuona jinsi kundi hilo limeweza kupata nafasi hapa kwani kuna dalili ndogo sana ya uwepo wa serikali.
Hakuna shule, hospitali au barabara za lami. Sehemu kubwa ya eneo hilo inaweza kufikiwa kwa kutumia magari yenye uwezo wa kusafiri kkwenye njia mbovu za jangwa.
Katika kiji cha Nukuru, chombo kikuu cha usafiri chawakazi kilionekana ni punda.
Wanasema kwamba kadiri siku zinavyosonga wanamgambo wa Lakurawa walijikita katika jamii yao - sasa wamejiimarisha kama mamlaka inayoongoza.
Wakulima na wanakijiji hawana budi ila kukubaliana na masharti na kodi zao kwani wanamgambo wamejihami kwa silaha. Wasipotekeleza wajibu wa huvamiwa na kuibiwa mifugo yao.
Mkulima huyo aliyezungumza na BBC alisema wapiganaji hao walipitia kitongoji chake siku mara kwa mara wakielekea katika vijiji vingine.
"Tulijua wao ni Lakurawa kutokana na mtindo wao wa mavazi," alisema, akiashiria sare zao za kujificha na vilemba vyao kwa kawaida huvaliwa na wanaume katika maeneo ya jangwa ya Mali na Niger.
Baadhi ya wapiganaji hao wanazungumza Kifulfude - ukoo wa kabila la Fulani linalozungumzwa katika nchi nyingi za Afrika Magharibi - lakini wanaelewana lafudhi na wenyeji wa Hausa wa eneo hilo, alisema.
Nyakati za usiku, wapiganaji hao hurudi kwenye kambi zao zilizojitenga, ambazo ziko nyanda za juu kupata nafasi nzuri ya kujilinda dhidi ya mashambulizi. Hakuna wanawake au familia zinazosadikiwa kuishi katika kambi hii ya muda.
Awali Lakurawa walipofika katika majimbo yenye Waislamu wengi ya Sokoto na Kebbi, walijidhihirisha kama kikundi cha kidini ambacho kilitaka kusaidia jamii iliyo hatarini katika eneo lisilo salama.
Nigeria inakabiliwa na masuala kadhaa tata ya usalama. Kwa muda wa miaka 15 iliyopita, eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi limekuwa likikumbwa na uasi mbaya wa kidini mikononi mwa makundi ya kijihadi kama Boko Haram.
Lakini hivi karibuni maeneo ya kaskazini-magharibi ya nchi hiyo yamehangaishwa na magenge ya wahalifu, wanaojulikana kama majambazi, ambao hupata pesa kwa kuwateka nyara na kuwashikilia watu ili kuwakomboa.
Wakati wanamgambo wa Lakurawa walipohamia vijiji vilivyo kando ya mpaka wa Niger-Nigeria, majambazi hao walihamia kwingine.
Mwanzoni hatua yao ilipokelewa vyema na baadhi ya wenyeji - lakini furaha yao ilikuwa kwa muda mfupi. Watu katika eneo la Tangaza wanasema wapiganaji hao wa kidini waliwageukia, na kuanza kutekeleza sheria kali na kueneza hofu.
Mkazi wa Nukuru aliangazia itikadi kali za kidini ambazo ziliwekwa na wanamgambo - ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mambo wanayoona kuwa ni kinyume na sheria za Kiislamu za Sharia.
"Hatuna uhuru wa kuishi tunavyotaka," kijana huyo aliambia BBC. "Huwezi hata kucheza muziki kwenye simu yako - hawataichukua tu, bali pia watakuadhibu."
Muziki unaonekana kuwa wa kukengeusha kutoka kwa majukumu ya kidini au kuhimiza tabia chafu na baadhi ya madhehebu ya Kiislamu yanayofuata sharia kali - na wakosaji wamechapwa viboko.
Baadhi ya wanamgambo wa Lakurawa wanadhaniwa kuoa katika jamii za mpakani - kuziweka familia zao mbali na kambi - na kuajiri vijana.
Baadhi ya waajiri hawa hutumiwa kama watoa habari, huku wengine wakiwasaidia wanamgambo kufanya biashara au kukusanya vifaa kutoka kwa wakaazi.

Chanzo cha picha, Gift Ufuoma/BBC
Shambulizi la Alhamisi lilikuwa la pili kutekelezwa dhidi ya kundi hilo katika operesheni ya Siku ya Krismasi.
Krismasi iliyopita, wanajeshi wa Nigeria walifanya mashambulizi dhidi yao karibu na Gidan Sama na Rumtuwa, kilomita kadhaa kutoka Nukuru. Takriban raia 10 waliuawa.
Mwezi mmoja baadaye, siku kadhaa baada ya kuapishwa kwa Donald Trump, serikali ya Nigeria iliorodhesha kundi hilo kuwa shirika la kigaidi.
Wanamgambo hao walishtakiwa kwa wizi wa mifugo, utekaji nyara na mashambulizi dhidi ya maafisa wakuu serikalini.
Hatua hiyo iliipa serikali mamlaka makubwa ya kuchukua hatua kali dhidi ya kundi hilo.
Wakati Trump alipotangaza mashambulizi Siku ya Krismasi, alisema ni kwa sababu kikundi hicho "kinawaua Wakristo wasio na hatia, katika viwango ambavyo havijawahi kuonekana kwa miaka mingi".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Maitama Tuggar amekuwa na kibarua kigumu cha kueleza shambulizi la hivi karibuni lilikuwa "operesheni ya pamoja" na "haina uhusiano wowote na dini fulani".
Wengi wa wanavijiji na wakulima wanaoishi katika kivuli cha wapiganaji ni Waislamu, si Wakristo.
Lakini iwapo operesheni ya Marekani na Nigeria itaweza kusambaratisha uwezo wa kundi la Lakuwara katika maisha yao, bila shaka watafurahia kuondokana na minyororo ya ugaidi.
Taarifa ya ziada ya Abayomi Adisa na Gift Ufuoma

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












