Je, Marekani ina haki ya kuingia Nigeria kupambana na ugaidi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump, ametishia kuchukua hatua za kijeshi nchini Nigeria, akiishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kuruhusu mauaji ya Wakristo- - "Ikiwa serikali ya Nigeria itaruhusu mauaji ya Wakristo kuendelea."
Trump hakutaja ni mauaji gani anayoashiria, lakini madai ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wakristo wa Nigeria yamekuwa yakienea kwa miezi ya hivi karibuni.
Makundi yanayofuatilia ghasia vinasema hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Wakristo wanauawa zaidi ya Waislamu nchini Nigeria.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Bw. Trump alisema Washington inaweza kuingia Nigeria kwa nguvu za kijeshi ili kukabiliana na wale aliowaita magaidi wa Kiislamu wanaofanya ukatili.
Pia alitishia kusitisha misaada yote ya Marekani kwa Nigeria.
Rais huyo ambaye aliteuliwa kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel, pia alitoa matamshi makali kuhusu Nigeria, akisema "Marekani haitasita kuchukua hatua."

Chanzo cha picha, Tinubu X
Rais wa Nigeria Bola Tinubu amesisitiza kuwa kwamba kuna mshikamano wa kidini nchini humo na kuongeza kwamba changamoto za usalama zinaathiri watu "wa dini zote".
Pia alisema wanamgambo hao hawakuwalenga waumini wa dini fulani na kwamba bali wanalenga waumini wa dini zote.
Awali mshauri wake Daniel Bwala aliambia BBC kwamba hatua zozote za kijeshi dhidi ya makundi ya kijihadi zinapaswa kutekelezwa kwa pamoja.
Bwala alisema Nigeria itakaribisha msaada wa Marekani katika kukabiliana na wanamgambo wa kijihadi lakini akabainisha kuwa Nigeria ni nchi "huru".












