Uchambuzi: Hatua ya Trump Venezuela inazisafishia njia tawala za kiimla duniani

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, Mhariri Kimataifa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kwa kukamatwa kwa kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro, Donald Trump ameonyesha kwa nguvu zaidi kuliko wakati mwingine uwezo wake, akiungwa mkono na nguvu ya kijeshi ya Marekani.
Chini ya amri yake, Marekani imemweka Maduro kizuizini na sasa inakusudia "kuendesha" Venezuela.
Rais wa Marekani alitangaza hatua hiyo katika mkutano na wanahabari na wenye athari kubwa kwa sera ya mambo ya nje ya Marekani duniani kote, uliofanyika katika klabu na makazi yake ya Mar-a-Lago huko Florida. Trump alisema Marekani itakuwa na udhibiti wa Venezuela "hadi pale ambapo mpito salama wa uongozi, sahihi na wa busara utawezekana".
Alieleza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alikuwa amezungumza na Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, ambaye alimwambia, "tutafanya chochote mtakachohitaji".
Trump aliongeza kuwa Rodríguez alikuwa mpole, lakini kwa maoni yake, "hana chaguo jingine".
Trump hakutoa maelezo ya kina kuhusu mkakati huo, akisema tu kwamba Marekani "haiogopi kuweka wanajeshi ardhini endapo italazimu".
Swali kubwa ni iwapo anaamini anaweza kuitawala Venezuela kwa udhibiti wa mbali.
Je, onyesho hili la kuunga mkono maneno kwa nguvu ya kijeshi, lililosifiwa waziwazi Mar-a-Lago na Marco Rubio pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth litatosha kuibadilisha Venezuela na kuwashinikiza viongozi wa Amerika ya Kusini kutii?
Ilionekana kana kwamba Trump anaamini hilo linawezekana. Hata hivyo, ushahidi unaonyesha kuwa mchakato huo hautakuwa rahisi wala wenye utulivu.
Taasisi mashuhuri ya utafiti, International Crisis Group, ilionya mwezi Oktoba kwamba kuanguka kwa Maduro kunaweza kusababisha vurugu na kuyumba kwa utulivu nchini Venezuela.
Mwezi huo huo, gazeti la The New York Times liliripoti kuwa maafisa wa ulinzi na diplomasia katika utawala wa kwanza wa Trump waliendesha majaribio ya kimkakati kuhusu hali ambayo ingetokea iwapo Maduro angeondolewa madarakani.
Hitimisho lao lilikuwa uwezekano mkubwa wa machafuko ya vurugu, huku makundi yenye silaha yakishindania mamlaka.
Kuondolewa na kufungwa kwa Nicolás Maduro ni uthibitisho wa wazi wa nguvu ya kijeshi ya Marekani.
Marekani iliandaa msafara mkubwa wa kijeshi na kufanikisha lengo lake bila kupoteza hata maisha moja ya raia wake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, operesheni ya kijeshi ni hatua ya mwanzo tu.
Rekodi ya Marekani ya kubadilisha tawala kwa nguvu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita si ya kutia moyo.
Hatua za kisiasa zinazofuata ndizo huamua mafanikio au kushindwa kwa mchakato mzima.
Iraq ilitumbukia katika janga la umwagaji damu baada ya uvamizi wa mwaka 2003, na Afghanistan, baada ya miongo miwili ya juhudi na gharama kubwa za kujenga taifa, ilisambaratika kwa siku chache baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2021.
Ingawa nchi hizo hazikuwa katika ukanda wa karibu wa Marekani, historia ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani katika Amerika ya Kusini pamoja na vitisho vya uingiliaji wa baadaye haitoi matumaini makubwa zaidi.
Trump alitumia jina jipya, Donroe Doctrine, kurejelea tamko la Rais James Monroe la mwaka 1823 lililoonya mataifa mengine kutoingilia eneo la ushawishi wa Marekani katika nusu ya magharibi ya dunia. Alisema kuwa, chini ya mkakati mpya wa usalama wa taifa, ubabe wa Marekani katika eneo hilo "hautahojiwa tena".
Alimwonya Rais wa Colombia, Gustavo Petro, kwa kauli kali, na baadaye akasema kupitia Fox News kwamba "hatua fulani italazimika kuchukuliwa kuhusu Mexico".
Cuba pia inaonekana kuwa kwenye ajenda ya Marekani, hasa kutokana na ushawishi wa Rubio, ambaye wazazi wake ni Wamarekani wenye asili ya Cuba.
Marekani ina historia ndefu ya uingiliaji wa kijeshi katika Amerika ya Kusini.
Mwaka 1994, Rais Bill Clinton alituma wanajeshi 25,000 na manowari mbili za kubeba ndege kwenda Haiti ili kulazimisha mabadiliko ya utawala.
Ingawa utawala wa wakati huo ulianguka bila mapigano, miaka 30 iliyofuata imekuwa ya mateso makubwa kwa wananchi wa Haiti, ambayo sasa ni taifa lililoshindwa, likitawaliwa na magenge yenye silaha.
Trump alizungumza kuhusu "kuifanya Venezuela kuwa kubwa tena", lakini hakuzungumzia demokrasia.
Alipuuza wazo la kumpa uongozi María Corina Machado, kiongozi wa upinzani na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2025, akisema hana uungwaji mkono wala heshima ya kutosha. Hakumtaja Edmundo González, ambaye Wavenezuela wengi wanaamini ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa 2024.
Badala yake, kwa sasa, Marekani inaonekana kumuunga mkono Makamu wa Rais wa Maduro, Delcy Rodríguez.
Ingawa kuna dalili za ushirikiano wa ndani uliowezesha jeshi la Marekani kumwondoa Maduro, mfumo wa utawala ulioundwa na mtangulizi wake Hugo Chávez bado unaonekana kusalia.
Ni vigumu kuamini kuwa majeshi ya Venezuela, licha ya fedheha waliyoipata, yatakubali mipango ya Marekani. Viongozi wa kijeshi na raia waliounga mkono utawala wamejitajirisha kupitia mitandao ya rushwa ambayo hawako tayari kuipoteza.
Zaidi ya hayo, wanamgambo wa kiraia, mitandao ya uhalifu, pamoja na waasi wa Colombia waliopata hifadhi nchini Venezuela, bado ni tishio kubwa.
Vikosi hivyo vimekuwa vikiunga mkono Rais Maduro.
Uingiliaji wa Marekani nchini Venezuela unaweka wazi misingi ya mtazamo wa dunia wa Trump.
Hafichi tamaa yake ya kudhibiti rasilimali za nchi nyingine.
Hivi karibuni amemezea mate rasilimali za Ukraine akiwataka wamkabidhibili awape misaada ya kijeshi.
Isitoshe, utajiri mkubwa wa madini wa Venezuela pia ameukodolea macho, pamoja na imani yake kwamba kampuni za mafuta za Marekani ziliporwa wakati sekta hiyo ilipotaifishwa.
"Tutachukua utajiri kutoka ardhini, na utafaidi raia wa Venezuela, na pia watu wanaoishi nje ya Venezuela wale waliokuwa Venezuela, na itaelekezwa Marekani kama sehemu ya gawio."
Kauli zake pia zimeongeza hofu nchini Greenland na Denmark, hasa ikizingatiwa kuwa Marekani haijaacha nia yake ya kudhibiti Greenland kutokana na umuhimu wake wa kimkakati na rasilimali zake Tangu barafu ianze kuyeyuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Hatua dhidi ya Maduro pia ni pigo kubwa kwa dhana ya utawala wa dunia unaoongozwa na sheria za kimataifa. Ingawa dhana hiyo ilikuwa tayari imeyumba kabla ya Trump kuingia madarakani, amezidi kuonyesha kuwa yuko tayari kupuuza sheria asizozipenda.
Washirika wa Ulaya, wakiwemo viongozi kama Waziri Mkuu Keir Starmer, wanahangaika kuonyesha uungwaji mkono wao kwa sheria za kimataifa bila kukemea waziwazi ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaotokana na operesheni hiyo.
Marekani inajihalalishia kuwa jeshi lake lilikiwa likisaidia kutekeleza notisi ya kukamatwa kwa mlanguzi wa dawa za kulevya anayejifanya kama Rais wa Venezuela lakini iko katika mstari mwembamba, hasa ikizingatiwa tamko la Trump kuwa Marekani litadhibiti Venezuela na mafuta yake.
Saa chache kabla ya Maduro na mkewe kukamwatwa, alikutana na wanadiplomasia wa Kichina katika kasri lake lililoko Caracas.
China ililaani vikali hatua ya Marekani, ikisema kuwa inakiuka sheria za kimataifa na uhuru wa Venezuela, na kutishia amani ya Amerika ya Kusini na bahari ya Karibiani. Hata hivyo, China inaweza pia kuona kielelezo kilichowekwa, hasa ikizingatiwa mtazamo wake kuhusu Taiwan.
Hofu hiyo imetajwa wazi na Seneta Mark Warner, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya Seneti ya Marekani, aambaye alisema kuwa mara mstari huo unapovukwa, kanuni zinazozuia machafuko ya dunia zinaanza kusambaratika, na tawala za kiimla zitakuwa za kwanza kuzitumia.
Alituma taarifa akisema kuwa viongozi wa China na wengine watakuwa wanafuatilia yanayoendelea Venezuela.
"Iwapo Marekani inatekeleza haki ya kutumia wanajeshi kuvamia na kukamata viongozi wa kigeni wanaowatuhumu kwa uhalifu ni kipi kitakachozuia China kutekeleza hilo nchini Taiwan? Vladmir Putin akitumia hatua hiyo kukamata rais wa Ukraine?"
Donald Trump anaonekana kuamini kwamba yeye ndiye mtunga sheria, na kwamba kile kinachoruhusiwa kwa Marekani chini ya uongozi wake hakiwezi kutarajiwa kwa wengine. Hata hivyo, huo si ukweli wa jinsi mamlaka ya dunia yanavyofanya kazi.
Hatua zake mwanzoni mwa mwaka 2026 zinaashiria kipindi kingine cha miezi 12 cha misukosuko ya kimataifa.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












