Marekani iko tayari kwa mashambulizi mengine Venezuela- Trump

Chanzo cha picha, Trump
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa nchi yake iko tayari kufanya mashambulizi mengine dhidi ya Venezuela iwapo itahitajika, akisisitiza kuwa Marekani itasimamia nchi hiyo hadi pale mpito salama wa uongozi utakapoweza kufanyika.
Kauli hiyo imetolewa muda mfupi baada ya operesheni kubwa ya kijeshi iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas.
Akizungumza na wanahabari, Trump alisema operesheni hiyo ilitekelezwa kwa kutumia nguvu “kubwa na ya kutisha” ya kijeshi kupitia anga, ardhi na baharini.
Aliielezea kama moja ya mashambulizi yenye ufanisi na nguvu zaidi katika historia ya kijeshi ya Marekani, akiongeza kuwa hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyepoteza maisha wala kifaa chochote cha kijeshi kuharibiwa.
Trump alisema lengo kuu la operesheni hiyo lilikuwa kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, pamoja na mkewe, lengo ambalo amesema limefanikiwa. Alimtaja Maduro kama “dikteta haramu” na kumshutumu kwa kuhusika na uingizaji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya nchini Marekani, pamoja na kuongoza mtandao wa Cartel de los Soles, madai ambayo Maduro amekuwa akiyakanusha.
Rais huyo wa Marekani alisema awali walikuwa wamejiandaa kufanya wimbi la pili la mashambulizi, wakiamini lingeweza kuhitajika. Hata hivyo, kutokana na mafanikio ya operesheni ya kwanza, alisema huenda hatua hiyo isihitajike kwa sasa, ingawa alisisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua kubwa zaidi endapo hali italazimisha.
Aliongeza kuwa Nicolás Maduro na mkewe wanasafirishwa kuelekea Marekani, huku uamuzi ukitarajiwa kufanyika kuhusu kushtakiwa kwao kati ya New York na Miami. Trump aliwahakikishia Wavenezuela walioko Marekani kuwa mateso yao yatafikia mwisho.













