Mji wa Nigeria unaomuenzi bondia Antony Joshua

Anthony Joshua na Francis Ngannou

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pambano kati ya Joshua (kushoto) na Ngannou (kulia) linaibua mzozo wa muda mrefu wa kimichezo kati ya Nigeria na Cameroon.

Ndondi iko katika familia ya Anthony Joshua, kulingana na binamu yake Raymond Ajakaye, anayeishi mjini Sagamu nchini Nigeria ni nyumbani kwa mababu wa familia ya Joshua.

Shughuli katika mji huo zinatarajiwa kusitishwa siku ya Ijumaa wakati mamia ya watu watapokusanyika kutazama maonyesho maalum ya pambano la bondia huyo wa uzani wa juu dhidi ya raia wa Cameroon Francis Ngannou - kumshangilia mtu wanayemwona kuwa wao.

"Iko katika familia, sisi sote ni wambanaji, kutoka kwa babu yangu, wajomba zangu na baba yake," Ajakaye aliambia BBC Michezo Afrika.

"Tulipambana sana. Hapa ndipo nafikiri tulipata kipaji cha ndondi."

Ukiwa karibu na Lagos kusini-magharibi mwa Nigeria, Sagamu una wakazi wapatao nusu milioni.

Kama ilivyo kwa nchi nzima, idadi hiyo ya watu inaelekea kwenye safu ya umri mdogo, ikimaanisha kuwa vijana wengi wamepata msukumo katika urithi wa familia ya Joshua na mafanikio yake katika mchezo wa ndondi.

Hilo limekuwa athari yake, mji huo una Klabu yake ya Mashabiki wa Anthony Joshua, yenye maelfu ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii, huku mtaa pia ukibadilishwa jina kwa heshima ya bingwa huyo wa Olimpiki mwenye umri wa miaka 34 na bingwa mara mbili wa uzito wa juu duniani.

"Barabara hiyo iliitwa Cinema Road kwa miaka mingi lakini ilibadilishwa na serikali kwa kutambua mafanikio ya Joshua," anasema Ajakaye.

"Tuna ofisi iliyoundwa hapa ili kuwa mahali pa kukutana kwa mashabiki wake wote."

Sio tu kwamba barabara hutumika kama mahali pa kukutania, lakini pia kuna mipango iliyowekwa ya kujenga ukumbi wa mazoezi ya kumwinda Antony Joshua ajaye.

Anthony Joshua Way -
Maelezo ya picha, Shule ya msingi iliyopewa jina la bondia wa Uingereza huko Sagamu.

Mapenzi ya Joshua kwa Nigeria

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anthony Oluwafemi Olaseni Joshua alizaliwa nchini Uingereza Oktoba 1989 na mama Mnigeria na baba mwenye asili ya Nigeria na Ireland.

Ingawa mara zote amekuwa akipigana chini ya bendera ya Uingereza, alitumia sehemu ya utoto wake nchini Nigeria, akisoma shule ya bweni, na ushawishi ambao Afrika - na hasa Nigeria - imekuwa nao kwake ni wazi kwa wote kuona na kusikia.

Joshua ana tattoo ya bara kwenye bega lake la kulia, na mpaka wa Nigeria pia ukiangaziwa, huku akiwa ametumia muziki wa wasanii wa Nigeria kama vile Burna Boy na Femi Kuti, mtoto wa nguli wa muziki wa Afrobeat Fela Kuti, kumsindikiza kwenye matembezi ya awali wakati wa pigano.

Mapigano yake yanaonyeshwa kwenye skrini zilizowekwa maalum mbele ya kasri la Akarigbo huko Sagamu, mtawala mkuu wa mji wa Nigeria.

"Familia ya Joshua inajulikana sana katika mji huu. Mama yake anatoka katika ukoo wangu na tunahusiana kama binamu," Osiberu aliambia BBC Sport Africa.

"Antony Joshua yuko sawa na anajituma kwa kile anachofanya, ni mnyenyekevu sana na haruhusu mafanikio yake yafike kichwani mwake. Zaidi ya hayo, anapenda kuunganishwa na mizizi yake.

"Tunamtakia kila la kheri na tutaendelea kumuombea."

Anthony Joshua
Maelezo ya picha, Anthony Joshua alipozuru Sagamu 2021

Joshua alitembelea mji huo miaka mitatu iliyopita wakati ukifunguliwa tena kufuatia janga la Covid-19, akikutana na Osiberu na wanachama wengine wa kilabu cha mashabiki wake.

"Sote tuna uhusiano mkubwa, ingawa hatukutani mara kwa mara na kurudi kwake sio mara kwa mara kutokana na kazi yake," aeleza Ajakaye.

"Ni mtoto mwenye heshima nyingi na amelelewa vizuri, akiwaheshimu wazee wake."

Wakati Yoshua anaingia ulingoni kwa pambano, usiku wa mapigano huko Sagamu umekuwa hadithi.

Kayode Segun-Okeowo, rais wa Klabu ya Mashabiki wa Anthony Joshua, anasema imekuwa desturi kwa mji huo kujitokeza kumshangilia mtoto wake.

"Klabu ilianzishwa mwaka 2016 na tuna mashabiki wengi wa Anthony Joshua hapa," anasema.

"Tumeandaa hafla za kutazama moja kwa moja kwa mapigano yake mengi na kuandaa sherehe za ushindi kwa ajili yake.

"Matarajio yangu kwa pambano lake lijalo ni chanya. Joshua amewashinda mabondia bora. Sioni Ngannou akimshinda Anthony Joshua wetu."

Anthony Joshua

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Anthony Joshua akionyesha kwa madaha tattoo ya ramani ya Afrika kwenye bega lake la kulia

Kila wakati Joshua anapoingia kwenye ulingo, mji wa Sagamu unaingia kwenye mtafaruku. Ijumaa haitakuwa tofauti kwani mashabiki wa ndondi na wasio wa ndondi watakusanyika kumtazama mwana wao kipenzi.

Pambano kati ya Joshua na Ngannou linarejesha uhasama wa muda mrefu wa kimichezo kati ya Nigeria na Cameroon.

Lakini kwa watu katika eneo hili la Nigeria, ujumbe uko wazi - kunaweza kuwa na mshindi mmoja tu.

Imetafsiriwa na Jaison Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi