Kituo cha sheria Tanzania chapendekeza waziri kutopewa mamlaka ya kumtangaza mtu kuwa gaidi
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimependekeza kuondolewa kifungu kinachompa mamlaka Waziri wa Mambo ya ndani wa Tanzania kumtangaza mtu kuwa gaidi wa ndani ya nchi.
Hata hivyo, iwapo sheria hiyo itapitishwa na Bunge la Tanzania, basi Waziri huyo atakuwa na mamlaka kutangaza mtu au kikundi cha watu kuwa wahusika wa ugaidi.
Mwanasheria ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Flugence Massawe ameeleza kuwa wabunge wanapaswa kupitia kwa umakini vifungo vya sheria hiyo inayotarajiwakwani itakapopitishwa bila kuchakatwa vyema inaweza kuwa na madhara makubwa kwa taifa.
Tayari wadau mbalimbali walishapata fursa ya kukutana naKamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kuchambua mapendekezo hayo ya Serikali yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Massawe alisema, “Tumefikia hatua ya kupinga hayo mapendekezo kwasababu tumeona hayana tija kwa taifa letu, kumpa waziri mamlaka hayo ni hatari kwa kuwa anaweza kuyatumia mamlaka hayo vibaya. Nafikiri tungeangalia pia nchini ya Kenya ilivyo, si mtu mmoja tu anatangaza mwingine ni gaidi bali wenzetu wanaketi katika baraza la mawaziri ili kutangaza…
“…unapompa mtu mmoja mamlaka ya kutangaza gaidi, hata kiuchumi tunaweza kuumia kwani mtu kama mtalii au mwekezaji kutoka nje ataogopa kuja Tanzania. Hii ni hatari sana,” alisema.













