Mapinduzi Niger: Je ni nchi gani zimekuwa na mapinduzi mengi zaidi Afrika?

Wafuasi wa mapinduzi nchini Niger wamekuwa wakionyesha uungaji mkono wao katika mji mkuu Niamey

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa mapinduzi nchini Niger wamekuwa wakionyesha uungaji mkono wao katika mji mkuu Niamey
    • Author, Peter Mwai
    • Nafasi, BBC News

Mapinduzi ya kijeshi yalikuwa yakitokea mara kwa mara barani Afrika katika miongo kadhaa baada ya uhuru na kuna wasiwasi kwamba yanaanza kutokea mara kwa mara.

Mapinduzi yaliyofanyika nchini Niger, yakiongozwa na wanajeshi wa kitengo cha walinzi wa rais, ni tukio la hivi punde zaidi katika msururu wa mapinduzi ambayo yamefanyika katika miaka ya hivi karibuni.

Kulikuwa na mbili nchini Burkina Faso mwaka wa 2022 pamoja na majaribio ya mapinduzi yaliyotibuka huko Guinea Bissau, Gambia na taifa la kisiwa cha Sao Tome na Principe.

Mnamo 2021, kulikuwa na majaribio sita ya mapinduzi barani Afrika, manne kati yao yalifanikiwa.

Mwaka jana, afisa mkuu wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, alionyesha wasiwasi wake kuhusu "kuzuka upya kwa mabadiliko ya serikali kinyume na katiba".

Ni wakati ganimapinduzi yanakuwa mapinduzi?

Ufafanuzi mmoja uliotumika ni ule wa jaribio lisilo halali na la wazi la jeshi- au maafisa wengine wa kiraia- kuwaondoa viongozi walio madarakani.

Utafiti uliofanywa na watafiti wawili wa Marekani, Jonathan Powell na Clayton Thyne, umebainisha zaidi ta majaribio 200 kama hayo barani Afrika tangu miaka ya 1950.

Karibu nusu ya hizi zimefanikiwa - yalifafanuliwa kuwa yalidumu kwa zaidi ya siku saba.

Zimbabwean soldier

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kulikuwa na sherehe baada ya jeshi la Zimbabwe kuingilia kati dhidi ya utawala wa Rais Mugabe mwaka 2017

Wakati mwingine, wale wanaoshiriki katika uingiliaji kati kama huo wanakanusha kuwa ni mapinduzi.

Mnamo mwaka wa 2017 nchini Zimbabwe, mapinduzi ya kijeshi yalimaliza utawala wa miaka 37 wa Robert Mugabe. Mmoja wa viongozi hao, Meja Jenerali Sibusiso Moyo, alionekana kwenye runinga wakati huo, akikataa katakata kwamba yalikuwa mapinduzi ya kijeshi.

Mwezi Aprili mwaka jana baada ya kifo cha kiongozi wa Chad, Idriss Déby, jeshi lilimteua mwanawe kuwa rais wa mpito anayeongoza baraza la mpito la kijeshi. Wapinzani wake waliita "mapinduzi ya kifalme".

"Viongozi wa mapinduzi karibu kila mara wanakanusha hatua yao ilikuwa mapinduzi katika jitihada za kuonekana kuwa halali," anasema Jonathan Powell.

Mapinduzi ya kijeshi yamefanyika mara ngapi Afrika?

Idadi ya jumla ya majaribio ya mapinduzi barani Afrika ilisalia kuwa thabiti kwa wastani wa karibu nne kwa mwaka katika miongo minne kati ya 1960 na 2000.

Jonathan Powell anasema hii haishangazi kutokana na kuyumba kwa nchi za Afrika katika miaka ya baada ya uhuru.

Bar chart of Africa coups

"Nchi za Afrika zimekuwa na hali ya kawaida inayochochea mapinduzi, kama vile umaskini na utendaji duni wa kiuchumi. Wakati nchi inapokabiliwa na mapinduzi mara ya kwanza, hiyo ni ishara ya kufanyika kwa mapinduzi zaidi."

Mapinduzi yalipungua hadi karibu mbili kwa mwaka ndani ya miongo miwili kuelekea hadi mwaka 2019.

Tumesalia na miaka mitatu tu katika muongo wa sasa na wakati mwaka wa 2020 ni mapinduzi moja tu yaliripotiwa nchini Mali, kulikuwa na idadi kubwa zaidi ya wastani wa 2021 na mapinduzi sita au majaribio ya mapinduzi yaliyorekodiwa.

Yalifanikiwa nchini Chad, Mali, Guinea na Sudan na mapinduzi hayo yalitibuka nchini Niger na Sudan.

Mnamo Septemba 2021, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionyesha wasiwasi kwamba "mapinduzi ya kijeshi yamerudi," na alilaumu ukosefu wa umoja kati ya jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na uingiliaji wa kijeshi.

"Mgawanyiko wa kisiasa wa kijiografia unadhoofisha ushirikiano wa kimataifa na ... hali ya kutojali inazidi kushika kasi," alisema.

Judd Devermont kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa chenye makao yake makuu nchini Marekani, anaamini kuwa mbinu "ya upole" ya mashirika ya kikanda na kimataifa "imewezesha viongozi wa mapinduzi kufanya makubaliano machache wakati wa kujiandaa kwa kukaa kwa muda mrefu madarakani"

Mahamat Idriss Déby Itno

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mahamat Idriss Déby Itno alimrithi babake kama kiongozi wa Chad mnamo Aprili 2021.

Ndubuisi Christian Ani kutoka Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal anasema maasi ya wananchi dhidi ya madikteta wa muda mrefu yametoa fursa ya kurejea kwa mapinduzi barani Afrika.

"Wakati maasi ya wananchi ni halali na yanaongozwa na watu, mafanikio yake mara nyingi yanatokana na uamuzi unaochukuliwa na jeshi," anasema.

Ni nchi gani zimekuwa na mapinduzi mengi zaidi?

Sudan ilikumbwa na majaribio mengi zaidi ya mapinduzi yaliyofikia 17 - sita kati ya majaribio hayo hayakufaulu.

Mnamo mwaka 2019, kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir aliondolewa madarakani kufuatia maandamano ya miezi kadhaa.

Bashir menywewe aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka1989.

Nigeria ilikuwa na sifa ya mapinduzi ya kijeshi katika miaka iliyofuata baada ya uhuru - nane kati ya Januari 1966 na unyakuzi wa madaraka uliofanywa na Jenerali Sani Abacha mwaka 1993.

Ramani

Hata hivyo, tangu mwaka 1999 uongozi wa nchi hiyo ya Afrika iliyo na watu wengi zaidi umekuwa ukifanyika kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.

Historia ya Burundi imegubikwa na mapinduzi 11 tofauti, megi yakichochewa na mvutano kati ya jamii za Wahutu na Watutsi.

Sierra Leone Ilikumbwa na mapinduzi matatu ya kijeshi kati ya mwaka 1967 na 1968, na nyingine moja mwaka 1971. Kati ya 1992 na 1997, ilishuhudia majaribio ya mapinduzi mara tano.

Ghana pia imekabiliwa na mapinduzi kadhaa ya kijeshi, mara nane ndani ya miongo miwili. Ya kwanza ilikuwa mwaka 1966, wakati Kwame Nkrumah alipoondolewa madarakani, na mwaka uliofuata kulikuwa na majaribio ya mapinduzi yaliofanywa maafisa wa kijeshi lakini hawakufaulu.

Kwa ujumla, Afika imekumbwa na mapinduzi mengi kulika bara lolote lile.

Kati ya mapinduzi 13 yaliyorekodiwa duniani tangu mwaka 2017, yote isipokuwa moja - Myanmar mnamo Februari 2021 - yamekuwa Afrika.

Presentational grey line
BBC Verify logo