Mapinduzi Burkina Faso: Fahamu kwa nini wanajeshi wamempindua Rais Kaboré

Chanzo cha picha, AFP
Mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso hayajapokelewa vyema lakini sio jambo ambalo halikutarajiwa.
Kuondolewa madarakani kwa Rais Roch Kaboré ni mapinduzi ya nne Afrika Magharibi ndani ya miezi 17 iliyopita.
Nchi jirani ya Mali imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi mara mbili katika kipindi hicho, yakichochewa na wasiwasi juu ya kutoweza kukabiliana na kuongezeka kwa ghasia za wanamgambo wa Kiislamu.
Je, tishio la wanamgambo wa kijihadi ni kubwa kiasi gani?
Sawa na ilivyokua Mali, kuondolewa kwa Bw. Kabore kulichochewa na hali ya kutoridhika miongoni mwa vikosi vya usalama kwa madai ya kutoungwa mkono kikamilifu dhidi ya wanamgambo wanaohusishwa na al-Qaeda na kundi la Islamic State.
Siku ya Jumapili, maasi yaliripotiwa katika kambi kadhaa za kijeshi, katika mji mkuu, Ouagadougou, na miji ya kaskazini ya Kaya na Ouahigouya.
Machafuko hayo yalifuatia miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya serikali ya kumtaka rais huyo ajiuzulu.
Mashambulizi ya wanamgambo yaliyoanza mwaka 2015 yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000 na kuwalazimisha watu milioni 1.5 kuyahama makazi yao, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa. Shule zimefungwa katika maeneo kadhaa za nchi kwa sababu ni hatari sana kuzifungua.
Imani ya umma katika usimamizi wa rais wa mzozo wa usalama ilishuka sana baada ya shambulio katika kijiji cha kaskazini cha Solhan mnamo Juni 2021. Zaidi ya watu100 waliuawa katik ashambului hilo linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo waliovika na kuingia nchini humo kutoka Mali.
Mashambulio ya Solhan yalisababisha maandamano ya kupinga utawala nchini,kumlazimu Bw. Kaboré kufanya mabadiliko katika serikali na kujiteua kama waziri wa ulinzi.
Shambulio lingine katika kambi ya kijeshi ya Inata ya kaskazini mnamo Novemba 2021 lilizidisha hasira dhidi ya serikali.
Zaidi ya maafisa 50 wa vikosi vya usalama waliuawa. Ripoti ziliibuka kuwa kambi hiyo ilituma ujumbe wa dharura kuomba mgao wa chakula na vifaa vya ziada wiki mbili kabla ya shambulio hilo.
Rais alivunja serikali yake na kumteua waziri mkuu mpya na waziri waulinzi kabla ya mazungumzoya maridhiano ya kitaifa na upande wa upinzani.
Je, vurugu za wanamgambo zilieneaje hadi Burkina Faso?
Licha ya hali tete ya kiusalama na kisiasa ya Afrika Magharibi, Burkina Faso ilifurahia utulivu uliodorora hadi uasi wa watu mwaka 2014 ambao ulimwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa muda mrefu Blaise Compaoré.
Jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 lilisababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya jeshi. Bw. Kaboré alichaguliwa mara ya kwanza mwaka huo kwa ahadi ya kuunganisha nchi.
Hata hivyo, wanamgambo kutoka nchi jirani ya Mali -ambapo waasi waliotaka kujitenga mwaka wa 2012 walitekwa nyara na wanajihadi - walifanya shambulio katika mji mkuu wa Burkinabè huku Bw Kaboré akijiandaa kuchukua usukani.
Makundi yenye silaha yalichukua fursa ya uwepo dhaifu wa usalama katika maeneo ya mipakani ya Burkina Faso ili kuendeleza mashambulizi zaidi na kuimarisha uwepo wao.
Wanajihadi pia wamezusha mvutano wa kimadhehebu kati ya jumuiya za Kikristo na Kiislamu zilizokuwepo hapo awali nchini Burkina Faso.
Wanamgambo hao wamechukua fursa ya uwepo mdogo wa serikali na ukosefu wa usaidizi wa kibinadamu, ambao umeacha jamii zikiwa hatarini na kuzidhibiti na kuwasajili vijana kuwa wapiganaji.
Ushiriki wa kisiasa pia umedhoofishwa na uwepo wa wapiganaji.
Mnamo 2020, wapiga kura ambao walikuwa wamekimbia makazi yao katika maeneo ya kaskazini na mashariki hawakuweza kushiriki katika kura ya urais ambapo Bw Kaboré alichaguliwa tena kwa 58% ya kura.
Shinikizo za wanamgambo kwa jamii zilizidisha kutoridhika kwa umma katika muhula wa pili wa rais.
Je, kuna uwiano gani na Mali?
Kuna wasiwasi kwamba muundo unajitokeza.
Matukio kuelekea mapinduzi ya Burkina Fas yanawiana na matukio nchini Mali kabla ya mapinduzi yake ya kijeshi mwezi Agosti 2020.

Chanzo cha picha, Anadolu agency
Msururu wa mahsambulio hatari dhidi ya wanajeshi na raia ulifuatwa na maandamano ya yaliyochochewa na kuongezeka kwa ukosefu wa imani na serikali ya Mali chini ya aliyekuwa Rais wa wakati huo Ibrahim Boubacar Keïta.
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burkina Faso, Eddie Komboigo, amejaribu kuchukua fursa ya kutoridhika kwa umma kuhusu ukosefu wa usalama ili kuongeza ushawishi wake.
Lakini wakati umma nchini Mali uliunga mkono kwa mapana mapinduzi ya kijeshi, Burkina Faso huenda ikakosa utulivu zaidi kwa kusimamiwa na jeshi.
Je, hisia za kupinga Ufaransa zilichangia?
Nchi zote mbili zilikuwa makoloni ya Ufaransa na Ufaransa imeendelea kudumisha uhusiano thabiti wa kiuchumi na kiusalama muda mrefu baada ya uhuru.
Sawa na Mali, vikosi vya usalama vya Burkina Faso vinategemea msaada kutoka Ufaransa ambayo ilipeleka wafanyakazi 5,100 katika eneo hilo chini ya kile kilichoitwa Operesheni Barkhane. Hii ilianza wakati Ufaransa ilipotuma wanajeshi kudhibiti wanamgambo wa kijihadi waliokuwa wakiandamana kuelekea mji mkuu wa Mali, Bamako mwaka 2013.
Lakini uungwaji mkono wa umma kwa ushiriki wa Ufaransa umepungua huku hali ya usalama ikizidi kuzorota.
Mnamo Desemba, wakaazi wa Kaya walizuia msafara wa jeshi la Ufaransa kupeleka vifaa kwa jeshi la Burkina Faso kwa madai ya kuwa vikosi vya Barkhane vinafanya kazi na wanamgambo wa Kijihadi.
Ufaransa imefurushwa katika eneo la Sahel, ambalo linajumuisha nchi zote mbili, katika mzozo wa kidiplomasia na Mali ambao ulisababisha kujiondoa kwa karibu nusu ya kikosi cha Barkhane.
Ombwe la usalama linaweza kutumiwa na wanajihadi, huku kukiwa na wasi wasi kwamba kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kunaweza kudhoofisha ushirikiano wa ulinzi chini ya kikosi cha G5 Sahel ambacho kinajumuisha askari kutoka Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.
Wakati Mali inageukia Urusi ili kuziba pengo hili la usalama, washirika wake wa Sahel - ikiwa ni pamoja na Burkina Faso - wamepinga vikali hatua hii yenye utata.
Je nchi za kanda hiyo zinapaswa kuwa hofu?
Mapinduzi nchini Burkina Faso yanaashiria kwamba waasi hawana wasiwasi hatua itakayochukuliwa na Jumuia ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi Ecowas.
Vikwazo vya hivi majuzi dhidi ya Mali na Guinea, ambazo zilishuhudia mapinduzi Septemba mwaka jana, vilishindwa kudhibiti vitendo vya wanajeshi hao.
Rais wa nchi jirani ya Niger, Mohamed Bazoum, alianza kwa kusuasua madarakani mwaka 2021 kwa jaribio la mapinduzi dhidi ya msingi wa mashambulizi mabaya dhidi ya raia na jeshi.
Amekuwa mkosoaji mkubwa wa hali ya kisiasa nchini Mali na athari zake katika ari ya vikosi vya ulinzi vya kikanda.
Rais wa Niger amekuwa akijaribu kuzima hali ya kutoridhika kwa kijeshi kwa kutembelea vikosi vya ulinzi katika maeneo yenye hali tete, ambayo inaonekana kufanya kazi kwa sasa.
Kukosekana kwa utulivu nchini Mali na Burkina Faso pia kunasababisha wasiwasi wa usalama nchini Ivory Coast, jirani yao wa kusini. Kumekuwa na mashambulizi ya wanajihadi huko tangu Juni 2020 yakilenga vikosi vya usalama.













