'Jehanamu Duniani': Watu mashuhuri waliowahi kuzuiliwa kituo cha Brooklyn aliko Maduro

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais wa Venezuela Nicolás Maduro anazuiliwa katika Kuzuizi cha Metropolitan (MDC) cha Brooklyn.
Inafahamika kwamba atazuiliwa katika kituo hicho kabla ya kukabiliwa na mashtaka ya dawa za kulevya na silaha katika mahakama ya shirikisho ya Manhattan wiki ijayo.
Gereza hilo linajulikana kuwa na mazingira makugumu ya kuishi, vurugu na madai ya usimamizi duni.
Kizuizi cha MDC ndiyo gereza pekee la serikali katika Jiji la New York na kimeshughulikia kesi nyingi za watu maarufu ikiwa ni pamoja na Sean "Diddy" Combs, R. Kelly, El Chapo, mshirika wa Jeffrey Epstein Ghislaine Maxwell.
Katika makala hii tuangalie watatu wa kwanza tu waliojikuta katika Kizuizi cha Jiji cha cha Brooklyn.
Sean "Diddy" Combs

Chanzo cha picha, Reuters
Nguli wa muziki aliyefanikiwa sana, Sean "Diddy" Combs, ambaye alikabiliwa na msururu wa tuhuma za unyanyasaji wa kingono.
Combs aliwahi kuzuiliwa katika Kituo cha Magereza cha Metropolitan (MDC) huko Brooklyn, NY, kabla ya kuhamishwa katika kizuizi kingine cha New Jersey.
Combs alizuiliwa Brooklyn tangu kukamatwa kwake Septemba 2024 hadi uhamisho wake mwishoni mwa Oktoba 2025 wakati akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.
"Ni mahali pagumu sana kuwa mfungwa," wakili wa Combs, Marc Agnifilo aliteta mahakamani, akimwambia hakimu itakuwa vigumu kwa mteja wake kujiandaa kwa kesi ikiwa ataendelea kuwa hapo.
"Anaamka kwenye kitanda cha chuma chenye godoro la inchi moja na nusu, bila mto, katika seli ya futi 8 kwa 10 ambayo naweza kukuhakikishia ni jambo la kuchukiza," Cohen aliambia kituo cha habari cha CNN.
Kesi ya jinai ya Combs inahusu nini?
Combs, 54, alikamatwa katika hoteli ya New York kwa tuhuma za utapeli, utumwa wa kingono na usafirishaji wa watu kwa madhumuni ya ukahaba.
Waendesha mashtaka wa shirikisho wamemshutumu kwa "biashara ya uhalifu" ambapo "aliwanyanyasa, kuwatishia, na kuwalazimisha wanawake na watu wengine walio karibu naye kutimiza tamaa zake za ngono, kulinda sifa yake, na kuficha tabia yake".
Walisema Combs alitumia dawa za kulevya, vurugu na nguvu ya hadhi yake "kuwashawishi waathiriwa wa kike" katika vitendo vya ngono.
Wanaeleza pia waligundua bunduki, risasi na chupa zaidi ya 1,000 za mafuta ya vilainishi wakati wa uvamizi wa nyumba za Combs huko Miami na Los Angeles mwezi Machi.
R. Kelly

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
R. Kelly alipatikana na hatia katika kesi maarufu ya biashara haramu ya ngono na ulaghai huko Brooklyn, New York, ambayo iliangaziwa sana ulimwenguni.
Mwimbaji huyo wa R&B alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa yake.
Mnamo Septemba 2021, baraza la majaji la shirikisho huko Brooklyn lilimtia hatiani R. Kelly (Robert Sylvester Kelly) kwa makosa yote tisa aliyokabiliwa nayo, ambayo yalijumuisha shtaka moja la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu na makosa manane ya kukiuka sheria ya kupinga biashara haramu ya ngono.
Mnamo Juni 2022, Jaji wa Wilaya ya Marekani Ann Donnelly alimhukumu Kelly kifungo cha miaka 30 jela.
Waendesha mashtaka walielezea jinsi Kelly alivyoendesha biashara ya uhalifu iliyotumia umaarufu wake na mtandao wa washirika, mameneja, na walinzi kuwaajiri wanawake na wasichana walio na umri mdogo.
Kisha angewalazimisha na kuwatendea unyanyasaji wa kijinsia, mara nyingi akiamuru kila kipengele cha maisha yao na kuwaadhibu wale ambao hawakutii. Mara nyingi waathiriwa walishawishiwa kwa ahadi za msaada wa kazi ya muziki.
Washtakiwa kumi na mmoja, wakiwemo wanawake tisa na wanaume wawili, walitoa ushahidi wao juu ya walichopitia kwenye unyanyasaji, udhalilishaji wa kingono, na ukatili.
Mashahidi walielezea kupata msongo wa mawazo, kushinikizwa kutoa mimba, na kufanya ngono wakiwa wadogo.
R. Kelly baadaye alihukumiwa katika kesi ya pili ya shirikisho huko Chicago na kuhukumiwa kifungo cha ziada cha miaka 20, ambacho anakitumikia sambamba na sehemu kubwa ya kifungo chake cha Brooklyn.
El Chapo Guzmán

Chanzo cha picha, Getty Images
El Chapo ambaye jina lake halisi ni Joaquin Archivaldo Guzman Loera, alikuwa mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya kutoka Mexico na kiongozi wa genge la Sinaloa aliwahi kuzuiliwa katika kuzuizi cha Brooklyn ambako maduro anazuiliwa.
Akifikishwa mbele ya Mahakama ya Brooklyn wakati huo, majaji walimpata na makosa ya kuwa kiongozi mkuu wa biashara ya jinai inayoendelea, shtaka linalojumuisha ukiukaji 26 unaohusiana na dawa za kulevya na njama moja ya mauaji kupitia uongozi wake wa kundi la uhalifu lililopangwa la Mexico linalojulikana kama genge la Sinaloa.
Guzman Loera alihukumiwa kwa makosa yote 10 ikiwa ni pamoja na mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya, kutumia bunduki katika kuendeleza uhalifu wake wa dawa za kulevya na kushiriki katika njama ya utakatishaji fedha.
Hukumu hiyo ilifuatia kesi ya wiki 12 katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani. Guzman alikabiliwa na kifungo cha lazima cha cha maisha jela.
El Chapo alishtakiwa huko New York mnamo 2009 kwa mashtaka yanayotokana na mfululizo wa mauaji yanayohusiana na dawa za kulevya huko Queens mnamo 1993. Makao makuu ya wilaya ya mahakama ya shirikisho ambayo inajumuisha Queens yako Brooklyn.
Baada ya kutoroka mara kadhaa, El Chapo hatimaye alihamishwa kutoka Mexico mnamo 2017.
El Chapo alizuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali huko Manhattan. Ili kumpeleka katika mahakama ya shirikisho huko Brooklyn, wakati mwingine polisi walifunga daraja la Brooklyn, na kusababisha msongamano wa magari.
Gereza linaloelezewa kama 'Jehanamu Duniani'
Mnamo mwezi Juni, mfungwa mmoja aliyekuwa akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake kwa madai ya kumiliki bunduki, Uriel Whyte, alidungwa kisu hadi kufa na mfungwa mwingine, kulingana na taarifa ya habari ya Ofisi ya Magereza.
Mwezi mmoja baadaye, mfungwa Edwin Cordero alifariki katika mapigano yaliyotokea ndani ya gereza. Wakili wa Cordero aliliambia The New York Times kwamba mteja wake alikuwa "mwathirika mwingine wa kuzuizi cha MDC Brooklyn, gereza la shirikisho lenye watu wengi kupita kiasi, wafanyakazi wachache na lililopuuzwa ambalo ni 'jehanamu duniani'".
Mnamo Januari 2019, kukatika kwa umeme kwa muda mrefu kuliingiza kituo hicho cha magereza katika mgogoro, na kuwaacha wafungwa gizani kwa karibu wiki moja, wakiwa katika hali ya hewa ya baridi kali.
Tukio hilo lilisababisha uchunguzi wa Idara ya Sheria kutathmini kama Ofisi ya Magereza ilikuwa na "mipango ya kutosha ya dharura" kushughulikia hali ya maisha ya wafungwa kwenye kuzuizi hicho.
Kulingana na kesi iliyowasilishwa kwa niaba ya wafungwa, wafungwa walizuiliwa kwenye seli zao kwa siku nyingi na kulazimishwa kuvumilia vyoo vilivyo katika hali mbaya ndani ya seli na mazingira mengine magumu.
Ofisi ya Magereza ilisuluhisha kesi hiyo kwa kuwalipa wafungwa 1,600 jumla ya takriban dola milioni 10 kwa kuvumilia hali ya baridi kali na mazingira mabaya ambayo mwanadamu anaweza kuishi kutokana na kukatika kwa umeme.











