Maduro ni nani na kwanini Marekani imemkamata?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, André Rhoden-Paul
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe, Cilia Flores, wamekamatwa na Marekani baada ya shambulio kubwa la kijeshi nchini humo, kulingana na taarifa za Rais wa Marekani, Donald Trump.
Trump amesema kuwa operesheni hii ilifanywa kwa ushirikiano na vyombo vya sheria vya Marekani na kwamba Maduro na mke wake wamehamishwa nje ya nchi.
Mlipuko uliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Caracas asubuhi ya Jumamosi, ikiwemo kambi za kijeshi kama La Carlota na Fuerte Tiuna.
Sehemu kadhaa jirani hazina umeme, huku taarifa zisizo rasmi zikisema ndege zilikuwa zikiruka juu ya jiji. Hadi sasa, idadi ya waliopoteza maisha au kujeruhiwa haijajulikana.
Kauli ya Venezuela

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Jibu la Venezuela
Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema serikali haijui Maduro na mke wake wako wapi na imedai "uthibitisho wa maisha" kwao. Waziri wa Ulinzi, Vladimir Padrino López, amesema shambulio hilo limekumba maeneo ya raia na serikali inaendelea kukusanya taarifa kuhusu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa. Serikali pia imetangaza hali ya dharura ya kitaifa na kudai shambulio hilo ni jaribio la Marekani kudhoofisha uhuru wa kisiasa wa taifa hilo na kudhibiti rasilimali zake, hasa mafuta na madini.
Kauli ya Trump

Chanzo cha picha, Reuters
Trump alithibitisha operesheni kupitia mtandao wake wa Truth Social, akiisema: "Marekani imetekeleza shambulio kubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolás Maduro, ambaye pamoja na mke wake, amekamatwa na kuhamishwa nje ya nchi. Operesheni hii ilifanywa kwa kushirikiana na vyombo vya sheria vya Marekani. Taarifa zaidi zitatolewa."
Maduro ni nani na kwanini amekamatwa?
Nicolás Maduro alipata umaarufu wake chini ya utawala wa Rais Hugo Chávez na alichukua urais mwaka 2013 baada ya kifo cha Chávez.
Katika uchaguzi wa 2024, Maduro alitangazwa mshindi licha ya upinzani kudai kuwa mgombea wake Edmundo González alikuwa ameshinda kwa wingi wa kura.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump na utawala wake wamemkosoa Maduro kwa kuhusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya nchini humo, haswa fentanyl na kokeni na kumtuhumu kuwa kiongozi na mshirika mkubwa wa watuhumiwa wakubwa wa dawa za kulevya nchini, Cartel de los Soles.
Aidha Rais Trump amemshutumu Maduro kwa kuhusika na kuingiza maelfu ya wakimbizi wa Venezuela nchini Marekani. Inatajwa wanafikia zaidi ya watu milioni nane kutokana na mzozo wa uchumi na ukandamizaji wa kisiasa tangu 2013.
Trump pia amemshutumu kwa kuhusika katika biashara ya dawa za kulevya, akidai kuwa Maduro anaongoza kundi la Cartel de los Soles. Maduro amepinga vikali tuhuma hizi, akisema Marekani inatumia "vita dhidi ya dawa za kulevya" kama kisingizio cha kumng'oa madarakani na kudhibiti rasilimali kubwa za mafuta za Venezuela.
Hata hivyo, wataalamu wa kudhibiti dawa za kulevya wanasema Venezuela ni nchi ya kupita tu, si mzalishaji mkuu wa dawa za kulevya, huku jirani yake Colombia ikihesabiwa kama mzalishaji mkubwa wa kokaini. Taarifa zinaonyesha asilimia kubwa ya kokaini inayofika Marekani inasafirishwa kupitia Bahari ya Pasifiki, na si Venezuela. Fentanyl, dawa ya sumu kali zaidi kuliko heroin, hutengenezwa Mexico na kuingia Marekani kwa njia ya ardhi.
Mataifa mengine yamesemaje kuhusu shambulio dhidi ya Venezuela?
Mashambulio haya yamesababisha kauli kali kutoka kwa washirika wa muda mrefu wa Venezuela. Urusi imeilaumu Marekani kwa "shambulio la kijeshi" na kusema ni jambo la kushtua.
Iran imeyaelezea mashambulizi ya Marekani kama ukiukaji mkubwa wa uhuru wa taifa hilo, wakati Colombia na Cuba pia zimesema shambulio hilo ni uvamizi wa udhibiti wa kisiasa.
Nchi za Ulaya kama Hispania, Ujerumani na Italia zimesema zinafuatilia kwa karibu hali hiyo na kuhimiza kupunguza mvutano kwa mujibu wa sheria za kimataifa.













