Marekani haiko vitani na Venezuela, Rubio asema, huku Maduro akiwa kizuizini New York

Rais Maduro na mke wake wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kufanya ugaidi wa dawa za kulevya na kuingiza nchini humo kokeni, kumiliki bunduki za rashasha na vifaa vya uharibifu dhidi ya Marekani.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufiki a hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. 'Hatuko vitani na Venezuela,' Rubio asema

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anazungumza na vyombo kadhaa vya habari vya Marekani.

    Amekuwa kwenye NBC, ambapo aliulizwa kama Marekani iko vitani na Venezuela.

    "Hatuko vitani na Venezuela," amesema.

    "Namaanisha tuko vitani dhidi ya mashirika ya biashara ya dawa za kulevya. Hiyo si vita dhidi ya Venezuela."

    Anasema kukamatwa kwa boti "zinazoleta dawa za kulevya kuelekea Marekani" kutaendelea.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Marekani 'ina chaguzi zote' ikiwa Venezuela haitashughulikia masuala ya uhamiaji na dawa za kulevya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amezungumza na wanahabari na alipoulizwa nini kitatokea ikiwa wasiwasi wa Marekani kuhusu uhamiaji na biashara haramu ya dawa za kulevya havitapata ufumbuzi kutoka kwa Venezuela.

    Marco amesema Marekani "ina chaguzi zote tulizokuwa nazo kabla ya kukamatwa [kwa Maduro]".

    Hii ina maana kwamba meli za mafuta zilizowekewa vikwazo zinazoelekea Venezuela zitakamatwa "zinapoingia au zinapotoka" kama inavyoruhusiwa na amri za mahakama ya Marekani.

    "Siwezi kutathmini jinsi hali hii itavyoathiri mustakabali wao," amesema Rubio, ambaye anasisitiza kwamba njia mbadala ni "sekta ya mafuta ambayo inawanufaisha watu" na si wachache tu.

    Rubio alipoulizwa jinsi Marekani inavyokusudia kufikia maeneo ya mafuta.

    Amesema hili halihusu kufikia maeneo ya mafuta, kwa sababu hakuna mafuta yanayoweza kuingia au kutoka hadi mabadiliko yatakapofanywa katika utawala wa sekta hiyo.

    Soma zaidi:

  4. Picha zinaonyesha athari za shambulizi la Marekani huko Venezuela

    .

    Chanzo cha picha, CBS News

    Picha zilizoshirikishwa na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, zinaonyesha matokeo ya mashambulizi ya anga ya Marekani siku ya Jumamosi katika kituo muhimu cha kijeshi cha Fuerte Tiuna huko Caracas.

    .

    Chanzo cha picha, CBS News

    .

    Chanzo cha picha, CBS News

    Soma zaidi:

  5. Vikosi vya Israeli vyaua Wapalestina watatu Gaza, mamlaka za mitaa zasema

    Vikosi vya Israeli vimewapiga risasi na kuwaua Wapalestina watatu katika matukio tofauti katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili, mamlaka za afya za eneo hilo zilisema.

    Madaktari waliripoti kwamba waliokufa ni pamoja na mvulana wa miaka 15, mvuvi aliyeuawa nje ya maeneo ambayo bado yanamilikiwa na Israeli katika eneo hilo, na mtu wa tatu ambaye alipigwa risasi na kuuawa mashariki mwa jiji katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Israeli.

    Jeshi la Israeli halikutoa maoni yoyote kuhusu matukio hayo yaliyoripotiwa.

    Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani mara kwa mara tangu kuanzishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Oktoba, ikisema yanalenga kuzuia mashambulizi au kuharibu miundombinu ya wanamgambo.

    Israel na Hamas zimekuwa zikilaumiana kwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

    Israeli ilidumisha udhibiti wa zaidi ya asilimia 50 ya Gaza chini ya awamu ya kwanza ya mpango wa Trump, ambao ulihusisha kuachiliwa kwa mateka walioshikiliwa na wanamgambo huko Gaza na Wapalestina walioshikiliwa na Israeli.

  6. Mahakama kuu Venezuela yamteua Makamu wa Rais kuwa rais wa muda

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mahakama Kuu ya Venezuela imetoa uamuzi kwamba Delcy Rodríguez, ambaye amekuwa akihudumu kama makamu wa rais wa Maduro, achukue nafasi ya rais wa muda katika kipindi hiki chenye kutarajia mabadiliko.

    Mahakama kuu inasema kumweka Rodríguez katika nafasi hiyo ni muhimu "ili kuhakikisha mwendelezo wa utawala na ulinzi kamili wa Taifa", kulingana na Reuters.

    Mahakama itajadili suala hilo ili "kuamua mfumo wa kisheria unaotumika ili kuhakikisha mwendelezo wa serikali, utawala wa serikali, na ulinzi wa eneo lililo huru katika kipindi ambapo Rais wa Jamhuri amelazimika kutokuwepo", kulingana na Reuters.

    Soma zaidi:

  7. Katibu Mkuu wa UN 'asikitishwa sana' na vitendo vya Marekani nchini Venezuela

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "ana wasiwasi mkubwa" na operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela, akiongeza kuwa ina "athari za kutia wasiwasi kwa eneo hilo", kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa UN.

    "Bila kujali hali ilivyo nchini Venezuela, matukio haya ni mfano hatari," inasema taarifa hiyo.

    "Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza umuhimu wa heshima - kwa wote - kwa sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Ana wasiwasi mkubwa kwamba kanuni za sheria za kimataifa hazijaheshimiwa."

    Pia alitoa wito kwa Venezuela kushiriki katika "mazungumzo yenye kujumuisha kila mmoja" kwa kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

    Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umeitishwa Jumatatu na Colombia kwa usaidizi wa Urusi na China.

    Soma zaidi:

  8. Trump asema Marekani 'itaongoza' Venezuela baada ya kukamata Rais Maduro

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani "itaiongoza" Venezuela hadi "mabadiliko salama, sahihi na ya busara" ya kisiasa yatakapohakikishwa, baada ya mashambulizi ya Marekani kusababisha kukamatwa kwa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro.

    Makampuni ya mafuta ya Marekani pia yatarekebisha "miundombinu iliyoharibika" ya mafuta Venezuela na "kuanza kupata pesa kwa ajili ya nchi," Trump alisema.

    Marekani ilianzisha mashambulizi dhidi ya Venezuela siku ya Jumamosi ambapo Maduro na mkewe, Mke wa Rais Cilia Flores, walikamatwa na vikosi vya Marekani na kuondolewa nchini humo.

    Venezuela ilitangaza hali ya hatari ya kitaifa na kulaani "uchokozi wa kijeshi" wa Marekani, huku makamu wa rais wa nchi hiyo akisema Maduro ndiye kiongozi wake pekee.

    Maduro na Flores walisafirishwa kutoka mji mkuu wa Caracas kwa helikopta ya Marekani mapema asubuhi ya Jumamosi na kutangazwa baadaye kuwa wamefikishwa New York.

    Baadaye walisafirishwa hadi Kituo cha Jeshi la Wanamaji cha Marekani cha Guantanamo Bay huko Cuba kabla ya kuhamishiwa kwenye ndege nyingine kuelekea Jimbo la New York, na kisha kupelekwa kwa helikopta hadi Kituo cha Magereza cha Jiji la New York huko Brooklyn.

    Mwanasheria Mkuu wa Marekani Pam Bondi alisema Maduro na Flores wameshtakiwa katika Wilaya ya Kusini mwa New York.

    Rais Maduro na mke wake wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kufanya ugaidi wa dawa za kulevya na kuingiza nchini humo kokeni, kumiliki bunduki za rashasha na vifaa vya uharibifu dhidi ya Marekani.

    "Hivi karibuni watakabiliwa na mkono wa sheria katika mahakama za Marekani," Bondi aliandika kwenye X.

    Hapo awali, Maduro alikanusha vikali kuwa kiongozi wa kundi la wahalifu na ameishutumu Marekani kwa kutumia "vita vyake dhidi ya dawa za kulevya" kama kisingizio cha kujaribu kumng'oa madarakani na kutwaa akiba kubwa ya mafuta ya Venezuela.

    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kuwasili kwa Maduro jijini New York, Trump alisema: "Biashara ya mafuta nchini Venezuela imekuwa ikiharibika, imeharibika kabisa kwa muda mrefu."

    "Tutakuwa na makampuni yetu makubwa sana ya mafuta ya Marekani, makubwa zaidi duniani, yataingia, yatumie mabilioni ya dola, kurekebisha miundombinu iliyoharibika vibaya, miundombinu ya mafuta, na kuanza kupata pesa kwa ajili ya nchi."

    Nchi hiyo ya Amerika Kusini ina takriban mapipa bilioni 303 ya mafuta ghafi, yakichangia takriban 20% ya rasilimali za mafuta duniani, kulingana na Utawala wa Taarifa za Nishati wa Marekani.

    Soma zaidi:

  9. Hofu na matumaini ya Wavenezuela baada ya kukamatwa kwa Maduro

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Huku hali ikiendelea kutulia huko Caracas, Wavenezuela wanazungumzia taarifa za kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro na Marekani kwa matumaini, hofu, na kutokuwa na uhakika.

    Watu walianza kujitokeza mitaani Jumamosi baada ya usiku uliokumbwa na milipuko katika eneo la Bonde la Caracas, huku hisia zikiwa tofauti kuanzia wanaosherehekea hadi wenye kushutumu.

    Dina, mkazi wa eneo hilo, aliambia BBC kwamba kwa sasa, anaishukuru Marekani kwa "kumuondoa Maduro madarakani" kwa sababu sasa, "angalau anaweza kuona tena matumaini".

    Hata hivyo, hali ya kisiasa bado ni ya kusuasua, sehemu ya sababu hakusema jina lake halisi kwa BBC.

    Jorge, Mvenezuela mwingine anayeishi karibu na Caracas, aliambia BBC kwamba ingawa anashukuru "kuungwa mkono na Trump na Marekani nzima", anahofia siku zijazo hazitakuwa rahisi.

    "Sasa kwa kuwa wanamchukua Maduro, nini kitatokea?" Jorge aliambia BBC. "Hatuna uhakikisho wa chochote. Hivyo kuna hali ya kutokuwa na uhakika. Hatujui siku zijazo mambo yatakuwa namna gani."

    Wafuasi wa serikali ya Maduro pia wamekuwa wakikusanyika katika mitaa ya Caracas, wakitaka Marekani imwachilie kiongozi wao. Meya wa Caracas Carmen Meléndez, mfuasi imara wa serikali, alijiunga na mkutano huo kupinga kile alichokiita Maduro "utekakwa nyara".

    Mapema Jumamosi, vikosi vya Marekani chini ya Rais Donald Trump vilitekeleza mfululizo wa mashambulizi yaliyolenga mji mkuu wa Venezuela, na hatimaye kumkamata kiongozi huyo wa nchi hiyo.

    Soma zaidi:

  10. Ulimwengu wazungumzia kutekwa kwa Maduro

    .

    Nchi mbalimbali zimezungumzia hatua ya wanajeshi wa Marekani kumkamata Maduro.

    • Uingereza: Waziri Mkuu Keir Starmer amesema serikali yake "haitatoa machozi" kwa sababu ya utawala wa Maduro kufikia ukomo wake, lakini alikataa kuhusishwa na utoaji maoni juu ya ikiwa hatua hiyo ya kijeshi iliyochukuliwa na Marekani ilivunja sheria za kimataifa au la.
    • Urusi: Wizara ya mambo ya nje iliitaka Marekani "kufikiria upya msimamo wao na kumwachilia huru rais aliyechaguliwa kihalali wa nchi inayojitawala na mwenzi wake", na ikasema kuna haja ya kuwa na "mazungumzo" kati ya Venezuela na Marekani.
    • China: Wizara ya mambo ya nje ilisema "imeshtushwa sana na kulaani vikali matumizi ya wazi ya nguvu ya Marekani" na kuitaka Marekani "kufuata sheria za kimataifa"
    • Umoja wa Mataifa: Katibu Mkuu António Guterres amesema "alikuwa na wasiwasi mkubwa" na kuonya kuhusu "mwanzo hatari", akihimiza kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa
    • Cuba: Rais Miguel Diaz-Canel ameshutumu vikali Marekani kwenye mitandao ya kijamii, kwa kufanya "shambulizi la jinai" dhidi ya Venezuela na kutoa wito wa hatua za haraka za kimataifa.
    • Mexico: Katika taarifa kwenye mtandao wa X, Rais Claudia Sheinbaum alisema, "Mexico inalaani uingiliaji kati wa kijeshi nchini Venezuela."Pia alijumuisha katika chapisho lake makala katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambayo inasema: "Wanachama wa Shirika, katika uhusiano wao wa kimataifa, wataepuka tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa Nchi yoyote, au kwa njia nyingine yoyote isiyoendana na Madhumuni ya Umoja wa Mataifa."
    • Brazili: Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amelaani mashambulizi ya mabomu ya Marekani kwa kumkamata Maduro na kusema huko ni kuvuka "mpaka kusikokubalika".

    Soma zaidi:

  11. Rais wa Venezuela afikishwa New York baada ya kukamatwa na wanajeshi wa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ndege inayoaminika kuwa imembeba Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mkewe, Cilia Flores, imetua karibu na Kituo cha Walinzi wa Kitaifa wa Anga cha Stewart huko New York.

    Maduro atachukuliwa kwa helikopta hadi jijini na kusafirishwa hadi gereza la Kituo cha Magereza cha Jiji, maafisa waliambia NBC News ambapo atakabiliana na mashtaka ya dawa za kulevya, saa chache baada ya jeshi la Marekani kumkamata yeye na mkewe katika shambulizi kubwa lililofanywa na Marekani huko Caracas, ikiwa ni kilele cha kampeni ya Rais Trump na wasaidizi wake ya kumwondoa madarakani.

    Inasemekana kuwa rais wa Venezuela atafikishwa mahakamani Jumatatu jioni.

    Wakati huo huo, akaunti ya mtandao wa X ya White House imechapisha tena video iliyochukuliwa awali yenye kumuonyesha Nicolas Maduro akiwa amefungwa pingu huku akisindikizwa na maafisa wa usalama katika makao makuu ya DEA huko Manhattan.

    Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ametangaza hali ya dharura katika eneo lote la taifa hilo kufuatia mashambulizi ya

    Siku ya Jumamosi Marekani ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Venezuela na kumlazimu Rais Nicolás Maduro kutangaza hali ya dharura katika eneo lote la taifa hilo.

    Hatua hii ilifuata wiki kadhaa za shinikizo na malalamiko ya utawala wa Trump dhidi ya Maduro, akidai kuwa rais huyo wa Venezuela anahusika katika biashara ya madawa ya kulevya na uhalifu unaohusiana na kuingiza dawa hizo Marekani.

    Marekani pia imekuwa ikidai kuwa Maduro, hakuingia madarakani kwa njia halali.

    Soma zaidi:

  12. Karibu msomaji wetu kwa taarifa zetu mubashara. Tarehe ni 04/01/2026.