Marekani iko tayari kwa mashambulizi mengine Venezuela - Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa nchi yake iko tayari kufanya mashambulizi mengine dhidi ya Venezuela iwapo itahitajika, akisisitiza kuwa Marekani itasimamia nchi hiyo hadi pale mpito salama wa uongozi utakapoweza kufanyika.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Marekani iko tayari kwa mashambulizi mengine Venezuela- Trump

    s

    Chanzo cha picha, Trump

    Maelezo ya picha, Maduro akiwa kwenye ndege baada ya kukamatwa na Marekani

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa nchi yake iko tayari kufanya mashambulizi mengine dhidi ya Venezuela iwapo itahitajika, akisisitiza kuwa Marekani itasimamia nchi hiyo hadi pale mpito salama wa uongozi utakapoweza kufanyika.

    Kauli hiyo imetolewa muda mfupi baada ya operesheni kubwa ya kijeshi iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas.

    Akizungumza na wanahabari, Trump alisema operesheni hiyo ilitekelezwa kwa kutumia nguvu “kubwa na ya kutisha” ya kijeshi kupitia anga, ardhi na baharini.

    Aliielezea kama moja ya mashambulizi yenye ufanisi na nguvu zaidi katika historia ya kijeshi ya Marekani, akiongeza kuwa hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyepoteza maisha wala kifaa chochote cha kijeshi kuharibiwa.

    Trump alisema lengo kuu la operesheni hiyo lilikuwa kumkamata Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, pamoja na mkewe, lengo ambalo amesema limefanikiwa. Alimtaja Maduro kama “dikteta haramu” na kumshutumu kwa kuhusika na uingizaji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya nchini Marekani, pamoja na kuongoza mtandao wa Cartel de los Soles, madai ambayo Maduro amekuwa akiyakanusha.

    Rais huyo wa Marekani alisema awali walikuwa wamejiandaa kufanya wimbi la pili la mashambulizi, wakiamini lingeweza kuhitajika. Hata hivyo, kutokana na mafanikio ya operesheni ya kwanza, alisema huenda hatua hiyo isihitajike kwa sasa, ingawa alisisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua kubwa zaidi endapo hali italazimisha.

    Aliongeza kuwa Nicolás Maduro na mkewe wanasafirishwa kuelekea Marekani, huku uamuzi ukitarajiwa kufanyika kuhusu kushtakiwa kwao kati ya New York na Miami. Trump aliwahakikishia Wavenezuela walioko Marekani kuwa mateso yao yatafikia mwisho.

  2. Trump asema hakuna vifo kwa wanajeshi wa Marekani katika mashambulizi Venezuela

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyefariki dunia wakati wa mashambulizi makubwa dhidi ya Venezuela, ingawa alikiri kuwa kulikuwa na majeruhi wachache upande wa Marekani.

    Akizungumza na kituo cha Fox News, Trump alisema “kulikuwa na majeruhi wachache lakini hakuna vifo upande wetu”, akiongeza kuwa wanajeshi walioumia wako katika hali nzuri.

    Trump amesema alizungumza na Rais wa Venezuela Nicolás Maduro takribani wiki moja kabla ya mashambulizi hayo na kumtaka “asalimu amri”. Alidai kuwa Marekani ililazimika kuchukua hatua “ya kisasa na yenye nguvu zaidi” baada ya mazungumzo hayo kushindikana.

    Kwa mujibu wa Trump, Maduro alikamatwa katika eneo “lililokuwa kama ngome na sio nyumba ya kawaida”, likiwa na ulinzi mzito wa chuma. Rais huyo wa Marekani alisema operesheni hiyo iliahirishwa kwa siku kadhaa kutokana na mazingira kutokuwa rafiki ikiwemo hali ya hewa.

    Trump pia amethibitisha kuwa Maduro na mkewe waanafirishwa kwenda New York, ambako wanakabiliwa na mashtaka ya jinai. Alisema wanasafirishwa kwa kutumia helikopta na meli, na kudai kuwa wanawajibika kwa vifo vya raia wengi, wakiwemo Wamarekani.

    Kuhusu mustakabali wa Venezuela, Trump alisema Marekani itakuwa “imehusika kwa nguvu” katika sekta ya mafuta ya nchi hiyo. Aliongeza kuwa bado anafikiria iwapo ataunga mkono kiongozi wa upinzani María Corina Machado kuchukua uongozi, huku akidai kuwa uchaguzi uliomrejesha Maduro madarakani haukuwa wa haki.

    Trump amesema kukamatwa kwa Maduro ni ujumbe kwa dunia kwamba Marekani “haitachezewa tena”, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga pia kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya, ambayo anadai inaua mamia ya maelfu ya watu kila mwaka nchini Marekani.

  3. Tunachokijua na tusichokijua kuhusu shambulio la Marekani na nani anaiongoza Venezuela?

    s

    Shambulio kubwa la kijeshi limefanywa na Marekani ndani ya Venezuela, likilenga makazi na kambi za kijeshi katika mji mkuu Caracas. Hali hii imezua maswali makubwa kuhusu nani atakayechukua madaraka na madhara halisi ya tukio hili.

    Tunachokijua:

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amethibitisha kuwa Marekani imefanya “shambulio kubwa” dhidi ya Venezuela. Trump pia amesema Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mke wake wamekamatwa na kuondolewa nchini humo kupelekwa nje ya nchi. Operesheni hii ilifanywa na kikosi maalum cha jeshi la Marekani kinachojulikana kama Delta Force, kwa mujibu wa maafisa.

    Venezuela imetangaza hali ya dharura ya kitaifa na kudai shambulio la kijeshi ni uvamizi usiokubalika. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa Marekani haitachukua hatua nyingine dhidi ya Venezuela baada ya tukio hili. Tukio hili ni moja ya operesheni kubwa za kijeshi za Marekani katika bara la Amerika tangu Vita baridi, na linafuata wiki kadhaa za mvutano ulioonekana kukithiri.

    Tusichokijua:

    Hali halisi ya Rais Maduro na mke wake bado haijathibitishwa wazi. Idadi ya waliopoteza maisha au kujeruhiwa kutokana na shambulio hilo haijajulikana, na kiasi cha uharibifu katika sehemu mbalimbali za Venezuela bado hakijafahamika.

    Vilevile, idadi na maeneo ya mashambulio hayajathibitishwa rasmi. Sababu kamili za Trump kuchukua hatua hii bado hazijafahamika, ingawa anaandaa mkutano wa habari kuelezea maelezo zaidi.

    Nani anaiongoza au kuiongoza Venezuela?

    Iwapo itathibitishwa kuwa Maduro amekamatwa na kuhamishwa nje ya nchi, utawala wa Venezuela unaweza kuhamia mikononi mwa viongozi wengine.

    Kwa sasa, ni vigogo watatu wa Chavismo wanaofuatiliwa kwa karibu: Makamu wa Rais Delcy Rodríguez, Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello, na Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino. Wote walionekana kwenye televisheni masaa machache baada ya shambulio na wanaweza kupewa madaraka.

    Waziri wa Ulinzi Padrino na Cabello wana ushawishi mkubwa ndani ya jeshi, ambao linaweza kuwa watiifu kwa yeyote kati yao.

    Rodríguez, kwa upande mwingine, ana mamlaka makubwa ya kiraia na kiuchumi, lakini hana ushawishi wa moja kwa moja kwa wanajeshi kama Cabello na Padrino. Pia kuna swali kubwa kuhusu hatua za upinzani, chini ya Maria Corina Machado, ambao wanadai mabadiliko halisi ya kisiasa na huenda hawataridhika na kuondolewa tu kwa Maduro kutoka Ikulu.

  4. Maduro kushtakiwa kwa makosa ya jinai Marekani

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rubio asema Maduro atakabiliwa na mashitaka Marekani, na hakuna hatua zaidi zinatarajiwa Venezuela – Seneta wa Marekani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema hakutakuwa na hatua zaidi zitazochukuliwa dhidi ya Venezuela kufuatia kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro.

    Seneta Mike Lee alithibitisha kukamatwa kwa Rais Maduro na kueleza kuwa atakabiliwa na mashitaka ya jinai nchini Marekani, kufuatia mawasiliano ya simu na Rubio.

    “[Rubio] hatarajii kuwepo kwa hatua zaidi kuhusiana na Venezuela sasa baada ya Maduro kuwa mikononi mwa Marekani,” amesema Seneta Lee.

    Lee aliongeza kuwa mashambulizi ya Marekani yalifanywa ili “kulinda na kuhakikisha wale wanaotekeleza amri ya kukamatwa wanashirikiana kwa ajili ya usalama.”

    Awali, Lee alisema kupitia chapisho lake kwenye X: “Natarajia kujua kama, na ikiwa kuna sababu za kikatiba zinazoweza kueleza hatua hii bila kuwa na tangazo la vita au idhini ya kutumia nguvu za kijeshi.”

  5. Venezuela yasema haijui aliko Rais Maduro, yataka uthibitisho wa uhai wake

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema serikali yake haijui mahali alipo Rais Nicolás Maduro wala mkewe, Cilia Flores, kufuatia madai ya Marekani kwamba wamekamatwa baada ya mashambulizi makubwa ya kijeshi.

    Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Rodríguez alidai kuwa Marekani inapaswa kutoa “uthibitisho wa uhai” wa Rais Maduro na mke wa rais, akisema serikali ya Venezuela ina wasiwasi mkubwa kuhusu hatima yao.

    “Tunaitaka serikali ya Marekani kutoa uthibitisho wa uhai wa Rais Maduro na Mama wa Taifa. Rais alikuwa tayari ametuonya kuwa hali kama hii inaweza kutokea,” alinukuliwa akisema, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Venezuela.

    Rodríguez aliongeza kuwa raia wameanza kufahamu kwamba rais alikuwa ametoa maelekezo ya wazi kwa vyombo vya ulinzi kuanza kutekeleza mipango yote ya kulinda taifa kwa mshikamano kamili.

    Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino López, alitangaza awali kwamba vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo vitasmabazwa katika maeneo yote ya nchi.

    Katika hotuba ya video kwa taifa, Padrino López alitoa wito wa mshikamano wa kitaifa mbele ya kile alichokiita “uvamizi mbaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya Venezuela”, akisema jeshi linafuata maelekezo ya Rais Maduro ya kuhamasisha vikosi vyote vya ulinzi.

    “Wametushambulia, lakini hawatatutawala,” alisema waziri huyo wa ulinzi, huku akisisitiza kuwa Venezuela itapinga uwepo wowote wa majeshi ya kigeni katika ardhi yake.

    Taarifa hizi zinafuatia mashambulizi ya Marekani yaliyolenga maeneo ya kijeshi mjini Caracas na sehemu nyingine za nchi, huku hali ya sintofahamu ikiendelea kuhusu hatima ya uongozi wa Venezuela.

  6. Venezuela yachunguza vifo na majeruhi kufuatia mashambulizi - Waziri wa ulinzi

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mandhari ya usiku ya makazi ya Chavista cha 23 de Enero mjini Caracas, baada ya kusikika kwa mfululizo wa milipuko tarehe 3 Januari 2026.

    Bado kuna maswali mengi kuhusu mashambulizi ya asubuhi ya leo.

    Haijafahamika ni uharibifu gani uliofanywa kwenye miundombinu ya kijeshi iliyolengwa, wala idadi kamili ya waliouawa au kujeruhiwa.

    Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino, amesema serikali inaendelea kukusanya taarifa kuhusu watu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa, huku akidai kuwa mashambulizi hayo pia yalilenga maeneo ya raia.

    Ameongeza kuwa Venezuela itapinga vikali uwepo wa majeshi ya kigeni nchini humo.

  7. Marekani imemkamata Rais wa Venezuela Maduro baada ya mashambulizi makubwa - Trump

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani imefanya “mashambulizi makubwa” dhidi ya Venezuela na kwamba imemkamata Rais wa nchi hiyo, Nicolás Maduro, pamoja na mke wake.

    Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema: “Marekani imefanikiwa kutekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolás Maduro, ambaye yeye pamoja na mke wake wamekamatwa na kusafirishwa nje ya nchi.”

    Trump aliongeza kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Marekani, akisema maelezo zaidi yatatolewa baadaye. Pia ametangaza kutakuwa na mkutano na waandishi wa habari lbaadaye katika makazi yake ya Mar-a-Lago.

    Hadi sasa, serikali ya Venezuela haijatoa tamko rasmi kuthibitisha au kukanusha madai hayo ya kukamatwa kwa maduro.

    Maafisa wameiambia CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, kwamba Maduro, amekamatwa na kikosi cha Delta Force cha jeshi la Marekani. Delta Force ni kikosi cha juu kabisa cha jeshi la Marekani kinachojihusisha na operesheni za kupambana na ugaidi.

  8. Venezuela yatangaza hali ya dharura taifa zima

    s

    Chanzo cha picha, Google

    Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ametangaza hali ya dharura katika eneo lote la taifa hilo kufuatia mashambulizi ya Jumamosi yanayoelezwa kufanywa na Marekani. Taarifa ya serikali inasema hatua hii ni hatua ya “dhahiri ya kulinda uhuru wa kisiasa na rasilimali za taifa.”

    Rais Maduro ameiagiza jeshi la taifa hilo kutekeleza mipango yote ya ulinzi “kwa wakati unaofaa na katika hali zinazofaa,” huku akihimiza vyombo vyote vya kijamii na kisiasa kushiriki katika kuhamasisha wananchi kushiriki na kudai mashambulizi hayo ni ya kikoloni.

    Taarifa hiyo pia inasema kwamba mashambulizi ya Marekani yamelenga “kubeba rasilimali za kimkakati, hasa mafuta na madini” na kuharibu uhuru wa kisiasa wa Venezuela.

    Hali hii ya dharura inapanua mashinikizo ya kisiasa na kiusalama yanayokabili nchi hiyo na inaweza kuathiri maisha ya raia na uchumi wa ndani.

  9. Marekani yafanya mashambulizi ya kijeshi ndani ya Venezuela

    s

    Viongozi wa Marekani wameripotiwa kuwa Rais Donald Trump ameiagiza jeshi la nchi hiyo kufanya mashambulizi kwenye maeneo ya kijeshi nchini Venezuela, ikiwemo baadhi ya vituo vya kijeshi katika Caracas.

    CBS News inaripoti kuwa Ofisi ya Pentagon ilirejelea maelezo yote kwa Ikulu ya Marekani.

    Hatua hii inafuata wiki kadhaa za shinikizo na malalamiko ya utawala wa Trump dhidi ya Maduro, akidai kuwa rais huyo wa Venezuela anahusika katika biashara ya madawa ya kulevya na uhalifu unaohusiana na kuingiza dawa hizo Marekani.

    Mashambulizi haya yanapanua mvutano uliopo katika eneo na kuongeza hatari ya mzozo mkubwa wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili.

  10. Venezuela yashambuliwa huku mvutano na Marekani ukiendelea

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ripoti kadhaa kutoka vyombo vya ndani na nje zimemeripoti kuhusiana na mlipuko katika sehemu mbalimbali za jiji la Caracas, ikiwemo kambi za kijeshi.

    Mashuhuda wanasema kwamba uwanja wa ndege wa kijeshi La Carlota, ulioko katikati ya jiji, pamoja na kambi kuu ya kijeshi ya Fuerte Tiuna, uliguswa na mlipuko huo unaoelezwa ni mashambulizi makubwa, na video zinazozagaa mtandaoni zinaonyesha milipuko katika maeneo yote mawili.

    Sehemu kadhaa za jirani sasa hazina umeme, na ripoti zisizo rasmi zinasema ndege zimeonekana zikiruka juu ya jiji. Tukio hili linafanyika wakati ambapo mvutano kati ya Marekani na Venezuela uko katika kiwango cha juu, huku Washington ikiendelea na mashambulio dhidi ya boti za haraka katika bahari ya Carribean, ambazo inadai zinabeba dawa za kulevya.

    Marekani inasema Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, hakuingia madarakani kwa njia halali na anahusika moja kwa moja na biashara ya dawa za kulevya nchini humo. Serikali ya Venezuela inasema hatua za hivi karibuni za Marekani ikiwa ni pamoja na kukamata meli za mafuta ni jaribio la kumfanya Rais Maduro aondolewe madarakani na kudhibiti rasilimali za mafuta za nchi hiyo.

    Maafisa wa serikali ya Trump wameripotiwa kuwa wamepokea taarifa za mlipuko na kuhusu ndege zilizorandaranda katika anga ya Caracas asubuhi ya Jumamosi, kulingana na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani. Tukio hili linaongeza shinikizo lililokuwepo kwa Maduro baada ya wiki kadhaa za malalamiko na mashinikizo kutoka kwa utawala wa Marekani.

  11. AFCON 2025: Safari ya timu 16 kusaka robo fainali inaanza leo

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raundi ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inaanza leo, ikiwa hatua muhimu inayobaini ni timu zipi 8 zitakazotinga robo fainali. 16 bora imepangwa kuchezwa siku nne mfululizo, na kila siku inatoa fursa kwa mechi mbili kuchezwa.

    Leo, Januari 3, Senegal inakabiliana na Sudan katika mechi ya kufungua raundi hii, huku Mali ikicheza dhidi ya Tunisia. Timu hizi nne zinahusisha baadhi ya mabingwa wa awali na wachezaji wenye ubora wa kimataifa.

    Kesho, Januari 4, Morocco itacheza na Tanzania, wakati Afrika Kusini inakabiliana na Cameroon. Mechi hizi zinaangazia mchanganyiko wa timu zilizo na rekodi za kihistoria na timu kama Tanzania inayoonja hatua hiyo kwa mara ya kwanza.

    Januari 5 inatoa mechi mbili nyingine zenye mvuto mkubwa, wakati Misri ikikabiliana na Benin, na Nigeria ikicheza na Msumbiji. Mechi hizi zinajumuisha baadhi ya wachezaji wakubwa wa Bara la Afrika, na ni hatua ya kuamua ni nani atakayokuwa tayari kufikia robo fainali.

    Januari 6, Algeria itacheza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Ivory Coast ikikabiliana na Burkina Faso. Mechi hizi za mwisho za raundi ya 16 bora zitamaliza hatua hii ya mtoano.

  12. Dereva wa bondia Anthony Joshua aliyehusika na ajali iliyoua wawili ashitakiwa Nigeria

    s

    Chanzo cha picha, Social media

    Dereva wa bondia Anthony Joshua amefunguliwa mashtaka nchini Nigeria kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu wawili wa timu ya bondia huyo. Katika ajali hiyo bondia huyu alipata majeraha machache, polisi wamesema.

    Adeniyi Mobolaji Kayode, mwenye umri wa miaka 46, alifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu ya Sagamu siku ya Ijumaa, ambapo alishtakiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo kusababisha vifo kwa kuendesha gari bila kuchukua tahadhari.

    Ajali hiyo ilitokea Jumatatu katika barabara kuu ya Lagos–Ibadan, katika jimbo la Ogun, baada ya gari aina ya Lexus SUV walilokuwa wakisafiria kugonga lori lililokuwa limesimama barabarani.

    Katika ajali hiyo, makocha binafsi wa Joshua, Latif Ayodele, na Sina Ghami, walifariki dunia papo hapo. Anthony Joshua, aliyekuwa abiria ndani ya gari hilo, alijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kabla ya kuruhusiwa kutoka siku ya Jumatano.

    Kwa mujibu wa vyanzo vya polisi, waendesha mashtaka waliwasilisha mashtaka manne dhidi ya dereva huyo, yakiwemo kuendesha gari kwa uzembe, kutokuwa makini barabarani na kuendesha bila leseni halali.

    Mahakama ilimpa dhamana ya naira milioni tano, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi tarehe 20 Januari.

    Maafisa wa serikali za majimbo ya Ogun na Lagos walisema Anthony Joshua alikuwa na huzuni kubwa kufuatia vifo vya watu hao wawili waliokuwa marafiki zake wa karibu.

    Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, Joshua alitembelea chumba cha kuhifadhia maiti ambako miili ya marehemu ilikuwa ikiandaliwa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

    Masaa machache kabla ya ajali, bondia huyo alikuwa amechapisha video kwenye mtandao wake wa Instagram akicheza tenisi na Latif Ayodele.

    Promota wa Joshua, Eddie Hearn, alitoa salamu za rambirambi akisema vifo hivyo vimeacha pengo kubwa kwa timu na familia zao.

    Anthony Joshua, mwenye umri wa miaka 36, ana asili ya mji wa Sagamu na alikuwa akielekea huko kuwatembelea ndugu zake kwa ajili ya sherehe za mwaka mpya, kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia.

  13. Chanzo cha moto ulioua 40 baa Uswisi chatajwa

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waendesha mashtaka nchini Uswisi wanasema mishumaa maalum iliyotumika kusheherekea mwaka mpya huenda ndiyo kichoosababisha moto ulioua zaidi ya watu 40 katika baa ya Le Constellation, Uswisi wakati wa sherehe za kuukaribisha Mwaka Mpya.

    Mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la Valais, Beatrice Pilloud, alisema ushahidi wa awali unaonyesha mishumaa hiyo aina ya fountain candles ilikuwa imefungwa kwenye chupa za shampeni na ilikuwa imewekwa karibu sana na dari ya baa hiyo.

    Alisema moto ulianza kwa haraka na kusambaa kwa kasi kubwa, hali iliyozidishwa na mazingira ya ndani ya jengo, na kusababisha waliokuwemo kukosa muda wa kutosha kujiokoa.

    Wachunguzi wanaendelea kukagua mabaki ya baa hiyo, kuchambua video zilizorekodiwa na kusambazwa mitandaoni, pamoja na kuwahoji manusura ili kubaini kwa uhakika chanzo cha moto huo.

    Uchunguzi huo pia unaangazia ukarabati uliowahi kufanyika katika jengo hilo, aina ya vifaa vilivyotumika hususani vifaa vya kuzuia kelele vilivyowekwa kwenye dari, pamoja na mifumo ya kukabiliana na moto na njia za kutokea wakati wa dharura.

    Wamiliki wa baa hiyo wamesema marekebisho yote yalifanywa kwa kuzingatia kanuni za usalama, huku waendesha mashtaka wakisisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea na hakuna hitimisho la mwisho lililotolewa.

  14. ADF waua zaidi ya 15 Mashariki mwa DRC

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Majeshi ya Serikali na yale ya kikanda yamekuwa yakipambana na waasi kulinda amani DRC

    Waasi wanaohusishwa na kundi la Islamic State wameua angalau watu 15 katika vijiji vitatu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, maafisa wa eneo hilo wamesema.

    Mashambulizi hayo yalitokea usiku wa Alhamisi katika wilaya ya Lubero, mkoani Kivu Kaskazini, yakilenga zaidi raia.

    Kundi la Allied Democratic Forces (ADF), lililoanza kama waasi nchini Uganda lakini baadaye kujikita katika misitu ya mashariki mwa Congo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, linatambuliwa na Islamic State kama tawi lake.

    Kwa mujibu wa Macaire Sivikunula, mkuu wa eneo la Bapere ambako vijiji vilivyoshambuliwa vipo, raia tisa waliuawa katika kijiji cha Kilonge, raia wawili katika kijiji cha Katanga, huku raia wawili na wanajeshi wawili wakiuawa katika kijiji cha Maendeleo.

    Alisema waasi hao waliwaua waathiriwa wengi kwa kutumia silaha za jadi kama mapanga, ingawa pia kulikuwa na mapigano ya risasi kati ya waasi na wanajeshi katika kijiji cha Maendeleo.

    Afisa wa jeshi anayesimamia Lubero, Alain Kiwewa, alisema baadaye Ijumaa kuwa idadi ya waliothibitishwa kufariki imefikia 16.

    Msemaji wa jeshi la Congo, Luteni Marc Elongo, alisema wanajeshi wa serikali wanaendelea kuwafuatilia waasi, bila kutoa maelezo zaidi.

    Kwa upande wake, Kakule Kagheni Samuel, kiongozi wa mashirika ya kiraia katika eneo la Bapere, alisema waasi hao pia walichoma nyumba kadhaa katika maeneo hayo.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Congo, MONUSCO, lilisema Novemba kuwa waasi wa ADF waliua raia 89 ndani ya wiki moja katika mashambulizi mfululizo.

    Mwezi Septemba, ADF ilidai kuhusika na shambulizi lililoua zaidi ya watu 60 wakati wa mazishi mashariki mwa Congo.

    Maafisa wa eneo hilo wamesema mazishi ya waathiriwa wa mashambulizi ya karibuni bado hayajaanza kwa sababu wanangoja wanajeshi kulinda usalama wa eneo, wakihofia waasi hao wanaweza kuwavamia raia wakati wa shughuli za mazishi na kuua tena.

    Ghasia za ADF ni tofauti na vita vinavyoendelea kati ya serikali ya Congo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, mapigano ambayo yaliua maelfu ya watu na kusababisha mamia ya maelfu kuyahama makazi yao mwaka jana, hali iliyosababisha juhudi za upatanishi kufanyika zikiongozwa na Marekani na Qatar.

  15. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja