Kwanini Israel imezishambulia nchi hizi 7?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwaka 2025, Israel ilifanya mashambulizi dhidi ya mataifa mengi zaidi ya nchi yoyote duniani, ikiwakilisha moja ya operesheni za kijeshi zenye upanuzi mkubwa zaidi kijiografia katika historia ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Aljazeera kupitia ripoti za Armed Conflict Location and Event Data (ACLED) zinaonyesha kuwa kati ya Januari 1 hadi Desemba 5, Israel imefanya angalau mashambulizi 10,631, katika nchi zisizopungua saba.

ACLED, taasisi huru inayookusanya taarifa za vurugu za kisiasa, maandamano, na matukio mengine muhimu, inasema kuwa mashambulizi haya ni pamoja na yale ya angani na ya kutumia ndege zisizo na rubani, mashambulizi ya risasi, bomu ya mbali, na mashambulizi mengine ya kijeshi.

Hata hivyo, ripoti hizi hazijumuishi vurugu za Israeli dhidi ya Wapalestina au uharibifu wa nyumba unaofanywa kila siku, unaangalia yale yanayohusisha silaha.

Palestina (Gaza na ukanda wa Magharibi)

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Gaza imeendelea kuwa eneo lenye hatari kubwa zaidi. Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 25,000 na kujeruhi angalau 62,000 kwa mwaka huu pekee. Mashambulizi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara, ikiwemo yale ya Oktoba 10, ambapo raia wengi waliuawa au kujeruhiwa. ACLED inaripoti mashambulizi 7,024 Gaza na 1,308 Ukanda wa Magharibi, wakihesabu mashambulizi ya angani, ndege zisizo na rubani, na mabomu.

Hali ya Gaza imekuwa mbaya; nyumba, shule na hospitali zimechakazwa, huku maelfu ya watu wakikimbia makazi yao. Ukanda wa Magharibi pia umeathirika kwa mashambulizi, hasa maeneo kama Jenin, Tulkarem na kambi za wakimbizi za Nur Shams.

Vurugu za wakoloni wa Israeli zimeongezeka, na OCHA inaripoti mashambulizi 1,680 katika jamii zaidi ya 270, wastani wa vitendo ama mashambulizi matano kwa siku, hali inayoongeza hofu na hatari kwa raia wa kawaida.

Mashambulizi haya yanaonyesha wazi kuwa lengo la Israel ni kudhibiti Gaza na Ukanda wa Magharibi kwa kutumia nguvu kubwa ya kijeshi. Watu wengi wanakabiliwa na ukosefu wa usalama, chakula, na maji safi, hali inayochangia mgogoro wa kibinadamu unaoendelea. Kwa mwaka 2025 Gaza ilikuwa mbaya zaidi, ingawa mwishoni mwaka mwaka, hali ikawa ya matumaini.

Lebanon

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lebanon pia imekumbwa na mashambulizi makali ya Israel, licha ya makubaliano ya kusitisha kwa muda mapigano na Hezbollah. Mwaka huu, Israel imefanya mashambulizi 1,653, hasa kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa, pamoja na maeneo ya karibu na Beirut.

Mashambulizi haya yameharibu majengo, nyumba, na miundombinu muhimu, huku wanajeshi wa Israeli wakibaki katika maeneo matano ya juu, wakikiuka ahadi ya kisheria ya kuondoka.

Picha za satellite zinaonyesha maeneo kadhaa yamesambaratika, huku wananchi wakilazimika kukimbia au kuishi katika hofu ya mashambulizi yanayoweza kutokea wakati wowote. Mashambulizi haya yameathiri maisha ya kila siku, biashara na uchumi wa wananchi, na kuongeza mvutano wa kijiografia.

Kwa kiasi kikubwa, vitendo vya Israel katika nchi ya Lebanon vinaashiria kupanuka kwa mashambulizi ya kijeshi bila kujali makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda, na kuendelea kuendeleza mvutano katika eneo hili. Raia wanakabiliwa na hatari ya mara kwa mara, huku jamii za kimataifa zikihimiza Israel kuzingatia sheria za kimataifa na kulinda raia.

Iran

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya mashambulizi ya Israel, Iran nayo ikajibu mapigo

Juni 13, Israel ilifanya shambulio kubwa la anga dhidi ya Iran, ikitumia ndege 200 zikiwemo zisizo na rubani kuangamiza mitambo ya nyuklia, miundombinu ya kijeshi na maeneo ya makazi ya wanasayansi. Shambulio hili liliathiri mikoa 28, huku mashambulizi 379 yakirekodiwa na ACLED. Hii ilisababisha vifo na majeruhi katika jamii mbalimbali, ikiwemo wanasayansi na maafisa wa kijeshi.

Mashambulizi yalichochewa kwa madai ya kuzuia silaha kufika mikononi mwa makundi ya "waasi," huku Marekani ikijiunga na shambulio la ndege kwenye mitambo ya nyuklia ya Natanz, Fordow, na Isfahan. Iran ilijibu kwa kurusha makombora ya balisti dhidi ya miji ya Israeli, hali iliyoongeza hatari ya mgogoro wa kikanda.

Tukio hili linaonyesha kuwa mashambulizi ya Israeli si tu yanahusiana na mipaka ya kawaida, bali pia yanapanua uwepo wa kijeshi katika eneo lenye hofu kubwa ya kisiasa. Raia wa kawaida wanakabiliwa na hatari ya mara kwa mara kutokana na mgongano wa kijeshi unaoendelea.

Syria

Israel imefanya zaidi ya mashambulizi 200 nchini Syria, hasa katika mikoa ya kusini kama Quneitra, Deraa na Damascus. Shambulio la Julai 16 lililenga makao makuu ya Wizara ya Ulinzi na karibu na Ikulu ya Damascus, likiashiria kuongezeka kwa operesheni za kijeshi. Israel inadai kuwa mashambulizi haya yanalenga kuzuia silaha kufika mikononi mwa makundi yanayochukuliwa kuwa "waasi," ikiwemo Hayat Tahrir al-Sham (HTS).

Mashambulizi haya yameathiri raia, majengo ya makazi, na miundombinu muhimu. Picha za satellite zinaonyesha uharibifu mkubwa, huku wananchi wakikabiliana na ukosefu wa usalama na huduma za msingi. Hali ya kisiasa inabaki tete, huku mashambulizi ya Israel yakionyesha ongezeko la hatari na mvutano wa kijeshi katika nchi hiyo ya Syria.

Kwa muda mrefu, Syria imekuwa jukwaa la mashambulizi ya Israel ili kudhibiti uwepo wa kijeshi wa Iran na makundi yanayopingana, hali inayozidisha migongano ya kikanda na kudumisha hali tete ya raia.

Yemen

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Israel imefanya mashambulizi 48 dhidi ya Houthi, licha ya uwepo wa makubaliano ya kupunguza mashambulizi kati ya Marekani na Houthi. Mashambulizi yameathiri mikutano ya serikali, miundombinu muhimu kama bandari ya Hodeidah na uwanja wa ndege wa Sanaa, na kusababisha vifo vya viongozi wa Houthi.

Mashambulizi haya yanahusisha umbali kutoka Israel, hadi kilomita 1,200, na kuonyesha uwezo wa kijeshi wa Israel kufikia maeneo mbali. Watu wa Yemen wanakabiliwa na hali tete ya usalama na upungufu wa huduma za msingi, hali inayochangia mgogoro wa kibinadamu unaoendelea.

Tukio hili linaonyesha jinsi Israel inavyopanua mashambulizi yake kijiografia, kuhusisha nchi mbali ili kudhibiti ushawishi wa Houthi na kulinda maslahi yake katika mgogoro wa Gaza.

Qatar

Septemba 9, Israel ilishambulia Doha, Qatar, wakati viongozi wa Hamas walikuwa wakikutana kujadili mapumziko yaliyopendekezwa na Marekani. Shambulio liliua watu 6, ikiwemo mtoto wa kiongozi wa Hamas, walinzi wake, na afisa mmoja wa usalama wa Qatar. Wakati huo, viongozi wengine wa Hamas walikimbia bila kujeruhiwa.

Shambulio hili lilisababisha malalamiko ya kimataifa, na Marekani ikitoa dhamana ya usalama kwa Qatar dhidi ya mashambulizi ya nje. Tukio hili linaonyesha jinsi mashambulizi ya Israeli yanavyohusisha hata nchi ambazo hazina mgogoro wa moja kwa moja, lakini zinahusiana kisiasa na harakati za Palestina.

Meli za misaada kuelekea Gaza

Mwaka 2025, meli kadhaa za kimataifa za "freedom flotillas" ziliajaribu kufika Gaza kupeleka misaada licha ya kizuizi cha Israeli. Mnamo Mei 2, meli ya Conscience ilishambuliwa mara mbili na na ndege zisizo na rubani (droni) maili 14 kutoka pwani ya Malta, ikisababisha moto na majeraha madogo kwa watu wanne.

Mnamo Septemba 9, Global Sumud Flotilla ilishambuliwa na droni katika bandari ya Sidi Bou Said, Tunisia. Abiria wote walitoka salama, lakini tukio hili lilionyesha uwepo wa hatari kwa wafanyakazi wa misaada. Mnamo Septemba 24, watu waliokuwa kwenye meli karibu na Ugiriki waliripoti kuona milipuko na mashambulizi ya droni mara kadhaa, hali iliyoongeza hofu na kuharibu juhudi za kibinadamu za kuwasaidia Wapalestina.