Israel yaishambulia Iran kwa makombora, yenyewe yaahidi kulipiza kisasi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Taharuki imetanda mashariki ya kati kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel katika mji mkuu wa Iran, Tehran, Ijumaa asubuhi. Milipuko mikubwa ilisikika kote Tehran, huku Israel ikitangaza kuwa imelenga maeneo ya nyuklia na vituo vya kijeshi.

Mashambulizi haya yanakuja wakati mvutano kati ya nchi hizo mbili umefikia kiwango cha juu kabisa kufuatia maendeleo ya haraka ya mpango wa nyuklia wa Tehran.

Mashambulizi hayo pia yalipiga mji wa Kermanshah magharibi mwa Iran, ambapo wakazi walisema walisikia milipuko na kuona moshi mweusi ukipanda juu ya jiji. Haikubainika mara moja ni nini hasa kililengwa. Milipuko pia ilisikika karibu na mji wa Tabriz nchini Iran, ingawa hali halisi huko bado haijawa wazi.

Iran Yaahidi kulipiza kisasi huku maafisa wakuu wakiripotiwa kuuawa

Kufuatia mashambulizi hayo, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, Ijumaa aliahidi kuwa Israel itakabiliwa na "adhabu kali" kutokana na mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo. Khamenei alitoa taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la serikali la IRNA, ambayo pia ilithibitisha kuwa maafisa wakuu wa kijeshi na wanasayansi wameuawa katika shambulizi hilo.

"Israel imefungua mkono wake mbaya na wenye damu kutenda uhalifu dhidi ya nchi yetu pendwa, ikifunua asili yake mbaya zaidi kuliko hapo awali kwa kushambulia makazi," Khamenei alisema, akisisitiza ukali wa kitendo hicho.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema kuwa Israel ililenga kituo kikuu cha kurutubisha urani huko Natanz na mpango wa kombora la balistiki la nchi hiyo, pamoja na wanasayansi wakuu wa nyuklia na maafisa.

Inahofiwa kuwa Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran (paramilitary Revolutionary Guard), Jenerali Hossein Salami, amefariki. Shirika la televisheni la serikali ya Iran lilitoa maelezo machache kuhusu hatima ya Jenerali Salami. Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, kilichoanzishwa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, ni mojawapo ya vituo vikuu vya mamlaka ndani ya theokrasia ya nchi hiyo.

Mzozo wao unahusisha mpango wa nyuklia

Mvutano kati ya pande hizi uliongezeka kutokana na mpango wa nyuklia wa Iran. Bodi ya Magavana ya Shirika la kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) iliilaani Iran kwa mara ya kwanza katika miaka 20 siku ya Alhamisi baada ya nchi hiyo kukataa kushirikiana na wakaguzi.

Mara baada ya hapo, Iran ilitangaza mara moja kuwa itaanzisha kituo cha tatu cha kurutubisha urani nchini humo na kubadilisha baadhi ya mipango kuwa ya kisasa zaidi.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limethibitisha Ijumaa kuwa shambulizi la Israel limelenga kituo cha kurutubisha urani cha Iran huko Natanz. Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi, alinukuliwa akisema: "IAEA inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Iran. ... Shirika lina mawasiliano na mamlaka za Iran kuhusu viwango vya mionzi. Pia tuko katika mawasiliano na wakaguzi wetu nchini humo."

Mashambulizi haya yanazua hofu kubwa ya kuongezeka kwa ghasia katika eneo ambalo tayari linafahamika kwa mvutano wa kisiasa na kijeshi.