Vita vya Siku 12; Iran yatoa video za mashambulizi ya Israel kwenye kituo cha mfumo wa ulinzi

Katika hali isiyo ya kawaida, Shirika la Utangazaji la Iran (IBRC) lilitoa video za mashambulizi ya Israel dhidi ya kituo cha udhibiti wa ulinzi wa anga na kituo cha ulinzi cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Video hizo zilitangazwa wakati wa mahojiano na Brigedia Jenerali Reza Khajeh, naibu mkuu wa operesheni za ulinzi wa anga za jeshi la Iran.
Katika mahojiano na naibu mkuu wa operesheni za ulinzi wa anga wa Iran, video ya mashambulizi mawili ya Israel katika maeneo ya kijeshi nchini Iran ilionyeshwa. Katika mojawapo ya video hizo mbili, mfumo wa ulinzi unalengwa, lakini eneo lake halijatajwa.
Tarehe iliyorekodiwa na IRIB kwenye video hii ni Juni 13, siku ya kwanza ya uvamizi wa Israeli. Hata hivyo, tarehe iliyorekodiwa kwenye video ya CCTV yenyewe inaonyesha Juni 12, 3:32 AM.
Kulingana na Brigedia Jenerali Khawaja, "maafisa wawili" wa mfumo huo walikuwa wakiondoka kwenye mfumo kabla ya shambulio la Israeli, na kulingana na yeye, "walijeruhiwa vibaya sana."
Hata hivyo, kuhusu picha nyingine iliyotolewa wakati wa mahojiano, naibu kamanda wa Operesheni za Ulinzi wa Anga za Jeshi la Iran alisema kuwa video hii ilikuwa wakati ambapo "Kituo cha Amri ya Kudhibiti Ulinzi wa Tabriz" kililengwa.
Katika picha zilizotolewa kutoka kituo hicho, watu kadhaa wanaonekana wakifanya kazi kabla ya kombora hilo kugonga, na kisha kwenye picha, wengi wao wanaonekana wakitoka kwenye chumba wakati kituo kinashambuliwa.
Brigedia Jenerali Khajeh alisema kuwa watu hao walikuwa wanafahamu kwamba walikuwa karibu kulengwa, na kuongeza kuwa kamanda wa ulinzi wa kituo hicho alikua "mkongwe" kutokana na shambulio la Israel. Katika fasihi ya kisiasa ya Iran, "mkongwe" humaanisha mtu ambaye anapata ulemavu wa kiakili au kimwili wakati wa kutekeleza majukumu yake.
Naibu kamanda wa Operesheni za Ulinzi wa Anga za Jeshi la Iran alisema katika mahojiano haya kwamba maafisa "35" wa vikosi vya ulinzi waliuawa wakati wa vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran.
Alisema katika kipindi hiki, "zaidi ya ndege 196 za Israeli za aina zote zilidunguliwa na ulinzi wa anga wa jeshi na vikosi vya ulinzi wa anga vya IRGC."
Mpango huu ulitolewa wakati uvumi kuhusu vita kati ya Israel na Iran kwa mara nyingine tena ukiongezeka.
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran: Israel haikuingia na ndege za kivita

Chanzo cha picha, IRIB
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Brigedia Jenerali Khajeh amesema kwamba ndege nyingi za Israel zisizo na rubani zilizoanguka ni Hermes 900 na Hermes 450 drone na Heron drone, na zilinaswa zaidi magharibi mwa Iran, katikati mwa nchi, na Tehran.
Naibu waziri wa ulinzi wa jeshi la Iran amesema kuwa shambulio la Israel dhidi ya Iran katika siku za kwanza lilikuwa la "makombora ya baharini na ya balestiki" na kwamba Israel "haikuingia kwanza na ndege za kivita."
Mahojiano haya na video za mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya ulinzi vya Iran yalichapishwa katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni, ni habari zisizo rasmi na ambazo hazijathibitishwa. Baadhi ya vyombo vya habari vya kieneo viliripoti uwepo wa ndege za Israel angani juu ya Iraq na karibu na mipaka ya Iran.
Brigedia Jenerali Khajeh, akijibu swali kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa ndege za kivita za Israel, alisema kuwa hakuna tishio kwa anga ya Iran baada ya vita vya siku 12.
Katika mahojiano haya, alilinganisha kwa uwazi uwezo wa kiulinzi unaopatikana kwa Iran na uwezo wa hali ya juu wa Israel, kwa sababu zikiwemo masuala yanayohusiana na vikwazo, na kuahidi kwamba "lengo la mwisho" la ulinzi wa Iran ni kupata uwezo wa kuzuia "ndege za kivita za hali ya juu" katika anga ya nchi.
Baada ya vita kuanza, ukosoaji uliibuka kuhusu uwezo wa kiulinzi wa Iran, ambao unaendelea hadi leo.
Wakati wa vita hivi, Israel ililenga idadi kubwa ya makamanda waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiwemo kamanda mkuu, kamanda wa Kikosi cha Wanaanga, Mkuu wa Shirika la Ujasusi la IRGC, kamanda wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, kisha kamanda aliyemrithi, pamoja na idadi ya wale waliohusika katika mpango wa nyuklia wa Iran.
Wakati wa vita hivi, Marekani pia ilishambulia vituo vikuu vya nyuklia vya Iran huko Natanz, Isfahan, na Fordow.
Tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza, maafisa wa Iran wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba hawana hamu ya vita lakini wako tayari kwa uwezekano wa kushambulia tena.
Maafisa wa jeshi la Iran wanasema nchi hiyo haikutumia uwezo wake wote kuishambulia Israel wakati wa vita vya siku 12.
















