Januari imeanza, unaijua asili ya majina ya miezi 12 ya mwaka?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka mpya ni mojawapo ya sherehe kubwa duniani kwa nchi zinazofuata kalenda ya Gregory, ambayo imetumika kwa karne nyingi.
Lakini Januari kuwa ndio mwezi wa kwanza wa mwaka, haikuwa hivyo huko nyuma. Kulikuwa na wakati ambapo Machi ulikuwa ndio mwezi wa kwanza wa mwaka.
Kalenda tunayotumia leo imepitia mageuzi na marekebisho kadhaa kwa maelfu ya miaka, tangu asili yake katika ustaarabu wa kale wa Kirumi.
Kuanzia kuundwa kwake kwa mara ya kwanza na Romulus, mwanzilishi wa Roma pamoja na kaka yake Remus, Warumi waliipa majina miezi 10 ya kalenda yao. Na kisha wakaongeza miezi miwili zaidi, Januari na Februari.
Januari

Chanzo cha picha, Getty Images
katika kalenda ya kale, chini ya amri ya mfalme wa Kirumi Numa Pompilius (753-674 KK) miezi ya Januari na Februari iliongezwa mwishoni mwa kalenda ya miezi 10, kwa lengo la kurekebisha hesabu ya muda wa mwaka wa jua.
Kwa hivyo mwezi huu hapo awali ulikuwa wa pili kutoka mwisho hadi mabadiliko yalipofanyika chini ya kalenda ya Julian, yaliyofanywa na Julius Caesar na kuuweka kuwa mwezi wa kwanza.
Kwa Kilatini uliitwa Ianuarius, na jina lake lilitokana na Janus, mungu wa Kirumi wa mwanzo. Mungu huyu pia alichukuliwa kuwa mungu wa mwisho, kwa hivyo alionyeshwa akiwa na nyuso mbili, akiangalia yaliyopita na yajayo.
Februari
Tofauti na Januari, Februari haikupewa jina la mungu, bali ni sikukuu ya Kirumi ya Februari.
Sikukuu hii ilisherehekewa kama ibada ya utakaso au upatanisho, kwani Februari kwa Kilatini inamaanisha "kutakasa." Ilifanyika mwishoni mwa mwaka wa Kirumi, kwa hivyo mwezi huu pia ulikuwa wa mwisho, kabla ya mageuzi na kuufanya kuwa wa pili.
Machi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika kalenda ya asili ya Kirumi, Machi ilikuwa mwanzo wa mwaka na uliitwa Martius, kwa heshima ya Mars, mungu wa vita.
Kwa Warumi, mwanzo wa mwaka haukuwa katikati ya majira ya baridi, kama ilivyo leo, bali wakati wa majira ya machipuko.
Ilikuwa wakati mwafaka wa kuanza kilimo na shughuli za kijeshi.
Kuanza mwaka wakati wa majira ya kuchipua ni jambo ambalo limetumika kwa muda mrefu katika tamaduni mbalimbali.
Kwa mfano, Uingereza ilisherehekea mwaka mpya katika mwezi huu hadi kupitishwa kwa kalenda ya Gregory mwaka 1752.
Aprili
Kuhusu Aprili, kuna nadharia kadhaa kuhusu asili ya jina lake.
Moja hurejelea kitenzi cha Kilatini, aperire, maana yake kufungua, labda kuashiria kustawi kwa kilimo.
Dhana nyingine ni ile ya Aphrodite, mungu wa kike wa Kigiriki wa upendo.
Mei
Mwezi huu ulikuwa Maius, uliowekwa wakfu kwa Maia, mungu wa uzazi na majira ya kuchipua. Mungu huyu pia alikuwa mama wa mungu Mercury.
Hata hivyo, baadhi wanasema jina hilo huenda lilitokana na maiores, yaani, wazee katika utamaduni wa Kirumi.
Juni

Chanzo cha picha, Getty Images
Asili ya Juni, au Iunius katika kalenda ya Kirumi, ilikuwa ni kwa heshima ya Juno, malkia wa miungu ya Kirumi na mke wa Jupiter.
Mungu huyu wa kike pia alichukuliwa kuwa mlinzi wa malezi na ndoa.
Lakini asili ya jina hilo pia hujadiliwa, wengine husema limetokana na jina iuniores yaani, vijana.
Julai
Mwezi huu haukuitwa Iulius hapo awali, neno la Kilatini la Julai, bali uliitwa Quintilis kwa sababu ulikuwa mwezi wa tano wa mwaka katika kalenda ya Kirumi (Quintus inamaanisha tano).
Mwezi huu ndipo Julius Kaisari alizaliwa, kwa hivyo baada ya kifo chake mwaka 44 KK, Warumi walibadilisha jina hilo kuwa Iulius kwa heshima yake.
Ilikuwa chini ya utawala wake ndipo marekebisho makubwa ya kwanza ya kalenda ya siku 365 yalipoanzishwa, ambayo yaliiweka Januari kama mwanzo wa mwaka (na Februari kama wa pili).
Kwa karne nyingi, kalenda ya Julian ndiyo iliyotawala.
Agosti
Sawa na Julai, mwezi wa Augustus, au Agosti, hapo awali ulikuwa mwezi wa sextus (wa sita) kwa hivyo ulijulikana kama Sextilis.
Ulibadilishwa jina mwaka 8 KK kwa heshima ya Kaisari Augusto, mfalme wa kwanza wa Roma (27 KK-14 BK).
Septemba

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufuatia mpangilio wa nambari wa miezi katika kalenda ya awali, Septemba ulipewa jina kutokana na nafasi yake.
Ulikuwa mwezi wa saba na Warumi waliupa jina hilo kutokana na neno la Kilatini septem, au saba.
Oktoba
Jina Oktoba, jina la Kilatini, lilitokana na neno octo, ambalo linamaanisha nane.
Kama ule uliopita, haukuwa umetengwa kwa mungu au mfalme, bali kwa nafasi ya nane iliyochukua katika mwaka huo.
Novemba
Hadithi ya mwezi wa Novemba si tofauti: pia ulitokana na neno novem, au tisa, kwa sababu ya nafasi yake katika kalenda ya asili ya Kirumi.
Desemba
Mwezi wa mwisho Desemba, mwezi wa kumi wa mwaka kwa Warumi, kutokana na neno la Kilatini decem, ambalo linamaanisha kumi.
Desemba ilikuwa mwezi wa kumi wa mwaka kwa Warumi katika kalenda yao ya awali, ambayo ilianza Machi, jina lake likitokana na neno la Kilatini " decem" (linamaanisha kumi).
Mageuzi ya Papa Gregory XIII ya 1582, miezi hiyo haikubadilishwa majina. Hata baada ya Januari na Februari kuongezwa mwanzoni mwa mwaka, na kufanya Desemba kuwa mwezi wa kumi na mbili, ulibaki na jina lake la nambari.
Na tangu wakati huo kalenda ya Gregory imekuwa ikitumika katika sehemu kubwa ya dunia.















