Urusi yaituhumu Ukraine kuua 24 wakishehereka mwaka mpya
Inadaiwa ndege tatu zisizo na rubani za Ukraine zilishambulia eneo la sherehe za mwaka mpya katika kijiji cha pwani cha Khorly, na kuteketeza kwa moto raia kadhaa. Taarifa za urusi zinasema lilikuwa shambulio la makusudi likilenga raia.
Urusi yaituhumu Ukraine kuua watu 24 katika shambulio la droni mwaka mpya
Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imeituhumu Ukraine kwa kuua angalau watu 24, akiwemo mtoto mmoja, katika shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) lililolenga hoteli na mgahawa ambako raia walikuwa wakisherehekea mwaka mpya katika eneo la Kherson kusini mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi.
Ukraine, ambayo mara kwa mara imeishutumu Urusi kwa kuua raia katika mashambulizi yake kwenye miji ya Ukraine, haikutoa majibu ya haraka kwa ombi la Reuters la kutoa maoni kuhusu taarifa hii.
Tuhuma hizo zilitolewa kwanza na Vladimir Saldo, gavana wa eneo hilo aliyeteuliwa na Urusi. Baadaye, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi na wanasiasa wakubwa waliitaja shambulio hilo kama “kitendo cha kigaidi”.
Reuters ilisema haikuweza kuthibitisha mara moja picha zilizosambazwa na ofisi ya Saldo kuhusu athari za shambulio hilo wala madai yaliyotolewa. Katika picha hizo, mwili mmoja ulionekana ukiwa umefunikwa kwa shuka jeupe, huku jengo likionyesha dalili za kuungua vibaya na kinachoonekana kuwa alama za damu ardhini.
Saldo alisema droni tatu za Ukraine zilishambulia eneo la sherehe za mwaka mpya katika kijiji cha pwani cha Khorly, akidai lilikuwa shambulio la makusudi dhidi ya raia. Aliongeza kuwa watu wengi waliteketea kwa moto.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema taarifa za awali zinaonyesha watu 24, akiwemo mtoto mmoja, waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa, wakiwemo watoto sita waliolazwa hospitalini. Wizara hiyo ililitaja tukio hilo kama “uhalifu wa kivita”.
Serikali Gabon yavunja timu ya taifa, yamfukuza kocha na nahodha Aubameyang
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Gabon imetangaza kuivunja timu ya taifa ya soka, kulivunja benchi la ufundi na kumwondoa nahodha Pierre-Emerick Aubameyang katika kikosi cha taifa kufuatia matokeo mabaya kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Michezo wa Gabon kupitia runinga baada ya timu hiyo kumaliza mkiani katika kundi lake na kutolewa mapema kwenye mashindano yanayoendelea nchini Morocco.
Akizungumza baada ya kipigo cha mabao 3–2 dhidi ya Ivory Coast mjini Marrakech, kaimu Waziri wa Michezo, Simplice-Desire Mamboula, alisema uamuzi huo umetokana na kile alichokiita kiwango cha aibu kilichoonyeshwa na timu hiyo.
“Kwa kuzingatia matokeo mabaya ya Panthers katika Kombe la Mataifa ya Afrika, serikali imeamua kulivunja benchi la ufundi, kusitisha timu ya taifa, na kuwaondoa wachezaji Bruno Ecuele Manga na Pierre-Emerick Aubameyang,” alisema waziri huyo.
Gabon, iliyokuwa ikifundishwa na kocha wa zamani Thierry Mouyouma, ilikuwa tayari imetolewa baada ya kupoteza michezo miwili ya awali ya Kundi F dhidi ya Cameroon na Msumbiji. Katika mchezo wao wa mwisho, waliongoza mabao 2–0 dhidi ya mabingwa watetezi kabla ya kupoteza 3–2.
Aubameyang, mwenye umri wa miaka 36, hakushiriki mchezo wa mwisho baada ya kuondoka na kurejea katika klabu yake ya Olympique de Marseille kwa ajili ya matibabu ya jeraha la paja. Kupitia mitandao ya kijamii, alisema matatizo ya timu yalikuwa makubwa zaidi ya mtu mmoja.
Hatua ya serikali kuivunja timu ya taifa ilikuwa kawaida barani Afrika katika miaka ya nyuma, lakini kwa sasa imekuwa nadra kutokana na msimamo mkali wa FIFA dhidi ya kuingilia masuala ya uendeshaji wa soka na serikali.
Wakenya milioni 5 waathiriwa na dawa za kulevya – Rais Ruto
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Kenya, William Ruto, amesema takriban Wakenya milioni tano wameathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya, hali aliyosema ni tishio kubwa kwa afya ya taifa, usalama na mustakabali wa uchumi wa nchi.
Akizungumza katika hotuba ya mkesha wa mwaka mpya iliyorushwa na Citizen TV, Rais Ruto alisema kati ya walioathiriwa, vijana takriban milioni 1.5 wameingia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Kutokana na hali hiyo, Rais Ruto alisema serikali imeamua kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuanzisha kitengo maalumu chenye nguvu ndani ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), kitakachokuwa na uwezo wa kiutendaji unaolingana na kikosi cha kupambana na ugaidi.
Alisema maafisa 700 wataajiriwa na kupelekwa katika kitengo hicho, huku uwezo wa ufuatiliaji, uchunguzi wa kisayansi na ukusanyaji wa taarifa za kijasusi ukiimarishwa ili kuwabaini wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya, wafadhili wao na mitandao ya uhalifu wa kupangwa.
Rais aliongeza kuwa maafisa hao watashirikiana kwa karibu na mamlaka ya kitaifa ya kupambana na matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya (NACADA), Idara ya Ujasusi ya Taifa (NIS), usimamizi wa mipaka pamoja na taasisi nyingine za usalama.
Taiwan yatoa tishio jipya kwa China
Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, ameahidi kulinda uhuru wa nchi yake baada ya China kufanya mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa hicho, ambacho Beijing inadai ni chake.
Akizungumza kwenye hotuba ya Televisheni siku ya Mwaka Mpya, Bwana Lai alisema jamii ya kimataifa inatazama kuona ikiwa wananchi wa Taiwan wana nguvu na dhamira ya kujilinda.
Mazoezi ya China yaliyoanza siku moja kabla ya hotuba hiyo yalionyesha kuzuia bandari muhimu, huku ndege za kivita na meli za jeshi la majini zikihusiana.
Mlipuko waua zaidi ya 10 mwaka mpya wakiwa baa
Chanzo cha picha, UGC
Maelezo ya picha, Picha kutoka katika mitandao ya kijamii, imechukuliwa kutoka barabarani nje ya baa ya Constellation
Watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa baada ya mlipuko na moto katika baa moja katika kisiwa cha michezo ya ski cha kifahari cha Crans-Montana kusini-magharibi mwa Uswisi, polisi wa Uswisi walisema Alhamisi.
Kwa mujibu wa polisi, Reuters imeripoti kwamba angalau watu 10 wamefariki katika tukio hilo, huku baadhi ya vyombo vya habari vya eneo hilo vikidai idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi.
Msemaji wa polisi alikataa kuthibitisha idadi kamili, lakini alisema watu wengi waliokuwa wakipokea matibabu kutokana na majeraha ya moto. Moto ulianza saa saba na nusu usiku katika baa inayoitwa "Le Constellation".
Eneo hilo limefungwa kwa sasa, polisi walisema katika taarifa, na kuongeza kwamba sababu ya mlipuko bado haijafahamika.
Zaidi ya watu 100 walikuwa ndani ya baa wakati wa mlipuko, msemaji wa polisi aliongeza.
Zelensky asema makubaliano ya amani yako tayari kwa asilimia 90
Chanzo cha picha, Reuters/Ukrainian Presidential Press Service
Rais wa
Ukraine Volodymyr Zelensky amesema makubaliano ya amani ya kumaliza vita na
Urusi yako "tayari 90%," katika hotuba ya Mwaka Mpya ambayo kwa kiasi
kikubwa ililenga kuzungumzia uvamizi wa Moscow.
Zelensky amesema
asilimia 10 iliyobaki ya makubaliano ya kumaliza vita vya karibu miaka minne "itaamua
hatima ya amani, hatima ya Ukraine na Ulaya."
Katika
hotuba yake ya dakika 20 kwa taifa, Zelensky amesema Ukraine haitaki amani
"kwa gharama yoyote," badala yake "tunataka mwisho wa vita - sio
mwisho wa Ukraine."
Amesema
ikiwa Ukraine itajiondoa kutoka eneo la mashariki mwa Donbas itamaanisha "kila
kitu kitakuwa kimekwisha," akimaanisha matakwa ya Urusi kwamba
Moscow ipate udhibiti kamili wa eneo hilo la viwanda katika
makubaliano yoyote ya amani.
Moscow kwa
sasa inadhibiti takriban 75% ya eneo la Donetsk, na takriban 99% ya eneo jirani
la Luhansk. Mikoa hiyo miwili inajulikana kwa pamoja kama Donbas.
Hatima ya mikoa hiyo imekuwa kikwazo kikubwa katika mazungumzo, huku Urusi ikiwa haitaki kuachana
na takwa lake la kuwa na udhibiti kamili wa Donbas.
Katika
hotuba hiyo, Zelensky aliwashukuru viongozi ambao wameiunga mkono Ukraine,
lakini akasema "nia lazima iwe ni dhamana ya usalama.”
Kufuatia
mazungumzo kati ya Zelensky na mwenzake wa Marekani Donald Trump huko Florida
mapema wiki hii, kiongozi huyo wa Ukraine amesema Washington imetoa dhamana
ya usalama ya miaka 15 - lakini muda wa utekelezaji wake bado haujawekwa
wazi.
Zelensky amesema
katika hotuba yake. "Ima dunia ivizuie vita vya Urusi, au Urusi iitumbukize
dunia katika vita vyake."
Kwa upande
mwingine, hotuba ya Putin kuhusu Mwaka Mpya ilikuwa fupi zaidi. Akizungumzia
vita nchini Ukraine, ambavyo Moscow inavielezea kama "operesheni maalum ya
kijeshi," Putin amesema:
"Tunajitahidi
kuleta furaha kwa wale wanaohitaji msaada na, bila shaka, kusimama upande wa
mashujaa wetu - washiriki katika operesheni maalum ya kijeshi - kwa maneno na
matendo."
Katika
hotuba hiyo Putin aliwaambia wanajeshi wake "tunawaamini nyinyi na ushindi
wetu".
Kando na
hilo, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un alituma ujumbe wake wa Mwaka
Mpya kusifu "muungano usioshindikana" kati ya Pyongyang na Moscow,
huku akiwasifu wanajeshi wanaopigana katika "nchi za kigeni."
Maafisa wa
Korea Kusini wamesema Korea Kaskazini imetuma maelfu ya wanajeshi kuisaidia
Urusi katika uvamizi wake, pamoja na makombora na silaha za masafa marefu.
Angalau
wanajeshi 600 kati ya hao wamefariki, kulingana na makadirio ya Korea Kusini.
Trump asema atawaondoa wanajeshi katika baadhi ya miji Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa
Marekani Donald Trump amesema atwaondoa wanajeshi katika baadhi ya miji Marekani,
ikiwa ni pamoja na Chicago na Los Angeles, baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu wiki
iliyopita kupunguza mamlaka yake ya kuwatumia wanajeshi kwa ajili ya kazi za
polisi.
"Watarudi
mitaani, labda katika hali tofauti na yenye nguvu zaidi, wakati uhalifu
utakapoanza kuongezeka tena," Trump aliandika kwenye Truth Social.
Wiki iliyopita,
Mahakama Kuu iliamua kwamba Trump hawezi kuwatuma wanajeshi huko Chicago kusimamia
sheria za ndani.
Taarifa ya
Trump pia ilitaja miji ya Portland, Oregon, lakini sio Washington DC, ambapo
wanajeshi wanaendelea kufanya doria.
Uamuzi wa
Trump wa kuagiza kupelekwa kwa wanajeshi katika miji inayoendeshwa na Democratics
umesababisha msururu wa kesi zinazopinga mamlaka yake ya kufanya hivyo.
Wanajeshi hao kwa kawaida huwa chini ya mamlaka ya magavana wa majimbo.
Mamia ya
wanajeshi walitumwa Chicago na Portland, lakini bado hawajapewa jukumu la
kufanya doria katika mitaa ya jiji, huku changamoto za kisheria zikiendelea
mahakamani.
Trump
amesema wanajeshi wanahitajika ili kusimamia sheria na msako dhidi ya uhalifu
na uhamiaji haramu.
Wakosoaji wanamtuhumu kwa kuendesha msako wa
"kimabavu," ambao unatishia demokrasia.
Waandamanaji Iran wajaribu kuingia katika jengo la serikali
Chanzo cha picha, Telegram
Maelezo ya picha, Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii znaonyesha waandamanaji wakivunja lango la ofisi ya gavana huko Fasa
Waandamanaji
nchini Iran wamejaribu kuingia katika jengo la serikali ya mtaa katika jimbo la
kusini la Fars, katika siku ya nne ya maandamano yaliyosababishwa na kushuka
thamani kwa sarafu.
Maafisa
walisema maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa na watu wanne walikamatwa katika
jiji la Fasa.
Ghasia pia zimeripotiwa
katika majimbo ya magharibi ya Hamedan na Lorestan.
Serikali
katika mji mkuu, Tehran, imetangaza siku ya Jumatano kuwa likizo ya benki -
katika juhudi za kutuliza machafuko hayo.
Katika video
iliyoonekana kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na BBC, umati wa watu
unarekodiwa ukivunja lango la ofisi ya gavana huko Fasa.
Kisha,
katika chapisho lingine, wanajeshi wanaonekana wakipiga risasi kujibu. Mawingu
ya gesi ya machozi yanapanda mbele ya maduka yaliyofungwa.
Kote nchini,
shule, vyuo vikuu na taasisi za umma zimefungwa kutokana na sikukuu ya umma iliyotangazwa
na serikali ya Iran.
Maandamano
yalianza mjini Tehran siku ya Jumapili – kutoka kwa wafanyabiashara
waliokasirishwa na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Iran dhidi ya dola ya
Marekani katika soko huria.
Kufikia
Jumanne, wanafunzi wa vyuo vikuu waliingia barabarani na maandamano yameenea katika
miji kadhaa, huku watu wakiimba dhidi ya watawala wa nchi hiyo.
Ili kuzuia
ongezeko lolote la maandamano, usalama mkali sasa unaripotiwa katika maeneo ya
Tehran ambapo maandamano yalianza.
Rais Masoud
Pezeshkian amesema serikali yake itasikiliza "madai halali" ya
waandamanaji.
Lakini
mwendesha mashtaka mkuu, Mohammad Movahedi-Azad, pia ameonya kwamba jaribio
lolote la kuleta vurugu litakabiliwa na "jibu madhubuti."
Kiongozi wa makanisa ya Ufufuo na Uzima Askofu Josephat Gwajima ameibuka kanisani kwake katika mkesha wa mwaka mpya na kuwaeleza wafuasi wake kuwa angali anapinga vitendo vya utekaji nchini Tanzania.
Gwajima alitoa mahubiri kwa mara ya mwisho atika kanisa hilo lililopo Ubungo jijini Dar Es Salaam mwezi Juni 2025 kabla ya kanisa hilo kufungiwa na kuzingirwa na polisi. Kanisa hilo lilifunguliwa mwishoni mwa Novemba mwaka jana kwa maelekezo ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.
“…Unajua magumu yaliyokupata wewe, yalikupata kwa sababu mimi nilikataa utekaji. Mpaka leo nakataa vilele…Mungu hataki, sheria yan chi haitaki, dini nayo haitaki… nan chi nayo haitaki. Hayo yako vilevile,” alisema Gwajima akishangiliwa na wafuasi wake.
Askofu huyo pia amesema kuwa anaamini Tanzania itavuka mapito yake kwa kishindo.
Gwajima ambaye alikuwa mbunge wa chama tawala nchini Tanzania alijitokeza katikati ya mwaka 2025 kuwa mpaza sauti dhidi ya matukio ya utekaji ya watu hususan walioonekana kuwa wakosoaji wa serikali. Serikali imekuwa ikijitenga na matukio hayo ya utekaji lakini ingali inanyooshewa kidole cha lawama.
2026 Tusikubali tofauti za kiitikadi zitugawe- Samia
Chanzo cha picha, IKULU
Serikali ya Tanzania imesema katika kuuanza mwaka 2026 imejipanga kujenga umoja wa kitaifa nchini.
Akitoa hotuba yake ya kuuaga mwaka 2025 na kukaribisha 2026 rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hayo akirejelea matukio yaliyotokea siku ya uchaguzi wa oktoba 2025 ambapo Tanzania ilipita nyakati ngumu.
“Mwaka 2025 pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata,tulipitia pia changamoto na mitihani iliyotugusa sote,mtakumbuka kuwa mwezi Oktoba mwaka huu tulipitia nyakati ngumu zilizohitaji Subira mshikamano na uzalendo.”
Aidha amesisitiza watanzania wanapoendelea kujenga taifa lao wasikubali kugawanyika kiitikadi au kimtazamo.
“Tunapouanza 2026 serikali imejipanga kujenga umoja wa kitaifa nchini, hatua za kuunda tume ya maridhiano zimeanza kuchukuliwa,serikali itashirikiana na wadau wote katika kukubaliana kuhusu muundo wa tume,aina ya wajumbe,majukumu yao na muda wa kazi wa tume hiyo”
“Nitoe rai kwenu ndugu zangu watanzania tusikubali tofauti za kiitikadi au mtazamo zitugawe na kutupotezea malengo yetu y amaendeleo na ustawi wa taifa letu.’’
Oktoba 29, 2025, inatajwa kuwa siku yenye madhara makubwa ya kisiasa nchini Tanzania.
Tukio hilo lilileta uharibifu wa mali, vifo vya watu na majeraha ambayo bado yamesalia kuwa kumbukumbu ngumu vichwani mwa wengi.
Anthony Joshua atolewa hospitali baada ya ajali ya gari Nigeria
Chanzo cha picha, SOCILA MEDIA
Maelezo ya picha, Latif Ayodele (kushoto) na Sina Ghami (kulia) walikuwa marafiki wa karibu na wanachama wa timu ya Anthony Joshua
Bondia wa
Uingereza Anthony Joshua ameruhusiwa kutoka hospitalini nchini Nigeria siku
chache baada ya ajali mbaya ya gari iliyowaua marafiki zake wawili.
Mwanaume
huyo mwenye umri wa miaka 36 alikuwa kiti cha nyuma katika gari aina ya Lexus
SUV lililogongana na lori lililokuwa limesimama kwenye barabara kuu katika
Jimbo la Ogun, karibu na Lagos, siku ya Jumatatu.
Gari yao iliyokuwa
katika mwendo kasi, iliua wanaume wawili marafiki wa karibu wa Joshua, ambao
ni Sina Ghami na Latif "Latz" Ayodele.
Baada ya
kutoka hospitalini Jumatano, Mwingereza huyo alitembelea nyumba ambapo miili ya
marafiki zake imehifadhiwa na "ikitayarishwa kwa ajili ya kurejeshwa
makwao," inasema taarifa ya pamoja ya serikali ya jimbo la Ogun na Lagos.
Akizungumza
na BBC Jumatano, msemaji wa polisi wa Jimbo la Ogun Oluseyi Babaseyi alisema
"uchunguzi bado unaendelea."
Shirika la Kusimamia
Sheria za Barabarani (TRACE) katika jimbo la Ogun, ambapo ajali hiyo ilitokea,
limesema uchunguzi wa awali unaonyesha gari hilo lilipasuka tairi kabla ya
kugonga lori.
Joshua,
ambaye alizaliwa Watford na wazazi wake kutoka Nigeria, alikuwa likizoni nchini
Nigeria baada ya ushindi wake dhidi ya Jake Paul huko Miami Desemba 19.
Mwanadiplomasia wa EU ayakataa madai kuwa Ukraine ilishambulia maeneo ya serikali ya Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kaja Kallas anaishutumu Kremlin kwa kujaribu kuvuruga mchakato wa amani
Mwanadiplomasia
wa ngazi ya juu wa Umoja Wa Ulaya (EU) ameyaita madai ya Moscow kwamba Ukraine ilishambulia
majengo ya serikali ya Urusi kuwa ni "jaribio la
makusudi" la kuvuruga mchakato wa amani.
Kauli ya
Kaja Kallas kwenye mitandao ya kijamii ni kujibu madai ya Kremlin kwamba
Ukraine ilijaribu kushambulia moja ya makazi ya Vladimir Putin kwa kutumia
ndege zisizo na rubani.
"Hakuna
mtu anayepaswa kukubali madai yasiyo na msingi kutoka kwa mchokozi ambaye ameshambulia
ovyo miundombinu na raia wa Ukraine," Kallas aliandika kwenye mitandao ya
kijamii.
Mapema wiki
hii Moscow iliishutumu Ukraine kwa kuilenga nyumba binafsi ya Putin kwenye
Ziwa Valdai kaskazini-magharibi mwa Urusi.
Urusi imesema
itapitia upya msimamo wake katika mazungumzo ya amani yanayoendelea kutokana na
hilo.
Tangu Waziri
wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov alipotoa madai hayo kwa mara ya kwanza, vyombo
vya habari vya serikali ya Urusi na wanasiasa wamelijadili shambulio hilo kwa sauti
za uchochezi.
Andrei
Kartapolov, mkuu wa kamati ya ulinzi ya bunge la Urusi, amesema, “bada ya kile
ambacho [Ukraine] imekifanya, "hakutokuwepo kwa msamaha."
Ingawa
Kremlin awali ilisema haioni umuhimu wa kutoa ushahidi wa shambulio hilo,
lakini siku ya Jumatano jeshi la Urusi lilitoa kile ilichosema ni ushahidi wa
jaribio la shambulio hilo.
Ushahidi
unajumuisha ramani inayodaiwa kuonyesha ndege zisizo na rubani zikirushwa
kutoka maeneo ya Sumy na Chernihiv nchini Ukraine na video ya ndege isiyo na
rubani iliyoanguka kwenye msitu wenye theluji.
Mwanajeshi
aliyesimama karibu na mabaki ya ndege hiyo anadai ni ndege isiyo na rubani
ya Chaklun ya Ukraine.
BBC
haijaweza kuthibitisha video hiyo, wala kubaini mahali ilipodondoka.
Wasifu wa
ndege hiyo isiyo na rubani iliyoharibika unafanana na ndege aina ya
Chakluns zinazotengenezwa Ukraine - lakini vipande vya ndege iliyoonyeshwa
kwenye picha ni vya bei nafuu na vinapatikana kwa wingi mtandaoni, na inawiya
vigumu kuthibitisha kuwa ni kutoka jeshi la Ukraine.
Chanzo cha picha, Wizara ya Ulinzi ya Urusi
Maelezo ya picha, Wizara ya ulinzi ya Urusi imetoa ramani ambayo inadai inaonyesha njia ya ndege zisizo na rubani zilizorushwa na Ukraine
Wizara ya ulinzi ya Urusi pia ilitoa video ya kile ilichosema ni mkazi alielezea kusikia kelele kama roketi wakati wa shambulio hilo.
Hata hivyo, chombo kimoja cha habari cha uchunguzi cha Urusi kilisema kimezungumza na zaidi ya wakazi kumi na wawili wa eneo linalozunguka makazi ya Putin na hakuna aliyesikia chochote kinachoweza kuonyesha kuwa ndege zisizo na rubani 91 zimeingia hapo au zimepigwa na ulinzi wa anga.
"Kama kitu hicho kingetokea, jiji lote lingekuwa likizungumzia," mtu mmoja aliambia kituo hicho.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine alisema kile ambacho Urusi iliwasilisha kama ushahidi kilikuwa "cha kuchekesha." "Hawako makini hata kuhusu kutunga hadithi hiyo," Heorhii Tykhyi aliambia Reuters.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amekanusha vikali madai hayo, akiyahusisha na mchakato unaoendelea unaoongozwa na Marekani wa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Putin hajataja hadharani shambulio hilo linalodaiwa kuwa la ndege zisizo na rubani, lakini akihutubia wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine wakati wa hotuba yake ya mkesha wa mwaka mpya, alisema "tunawaamini nyinyi na ushindi wetu".
Mataifa mbalimbali duniani yanaendelea kuukaribisha mwaka mpya huku saa ya usiku wa manane zikitofautiana katika kanda. hivyo kutofautisha pia wakati wa kuupokea mwaka mpya.
Mataifa ya Pasifiki yalikuwa ya kwanza duniani kuingia mwaka 2026. Mtalii mmoja aliyekuwa huko alituambia aliuadhimisha mwaka mpya “ufukweni pasipo satelaiti, bila dalili za uwepo wa binadamu, katika giza totoro na katikati ya kaa wengi wasiohesabika.”
Baada ya hapo, New Zealand ilifuata kwa kuukaribisha mwaka mpya kwa sherehe za fataki (fireworks) katika jiji la Auckland. Hizi ni picha za mbaadhi ya maeneo na namna walivyopokea mwaka mpya 2026.
Chanzo cha picha, Getty Images
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Auckland', New Zeeland
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Sydney, Australia
Chanzo cha picha, Getty Images
Dunia yasheherekea mwaka mpya kwa nyakati tofauti
Chanzo cha picha, Getty Images
Dunia inasheherekea mwaka mpya wa 2026, sherehe zikianza kwa kutofautiana muda. Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zilianza katika baadhi ya maeneo ya dunia, huku mataifa ya Pasifiki yakiongoza kuingia mwaka 2026 kabla ya sehemu nyingine za dunia. Miji na visiwa kadhaa tayari vimebadilisha kalenda, vimeshaingia mwaka 2026, huku mamilioni ya watu wakishuhudia fataki, sherehe za kitamaduni na mikusanyiko ya kifamilia kuashiria mwanzo wa mwaka mpya.
Jiji la Sydney nchini Australia lilikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza yenye watu wengi kuukaribisha mwaka mpya kwa onyesho kubwa la fataki lililopamba anga la Bandari ya Sydney.
Mamia ya maelfu ya watu walikusanyika kushuhudia tukio hilo, ingawa furaha ilichanganyika na huzuni, baada ya tukio la shambulio lililotokea Bondi Beach mapema mwezi huu, lililoacha majonzi kwa wakazi wa jiji hilo.
Sherehe pia zikafuatwa katika mataifa jirani ya Pasifiki ikiwemo Fiji, Tonga na Samoa, ambapo wakaazi walikusanyika kwa sala, ngoma za kitamaduni na fataki ndogo ndogo. Wakati huohuo, Kisiwa cha Chatham cha New Zealand, kilicho mbali na bara hilo, kiliingia mwaka 2026 dakika 15 tu baada ya Kiritimati, kikifuata ratiba yake maalum ya muda.
Kwa upande wa kipekee, mfamasia mmoja kutoka Uingereza tayari ameukaribisha mwaka mpya akiwa Samoa, kabla ya kusafiri kwenda American Samoa, eneo ambalo lina saa tofauti, ili kuukaribisha tena mwaka mpya mara ya pilli, kitendo anachokielezea kama “kusafiri kwenye muda”.
Mataifa mbalimbali yakafuata kama China, Singapore, Ufilipino, Japan na Korea Kusini, ambako kulifanyika hafla za kupigwa kwa kengele katika miji ya Tokyo na Seoul.
Baada ya hapo, New Zealand ilifuata kwa kuukaribisha mwaka mpya kwa sherehe za fataki (fireworks) katika jiji la Auckland.
Kadri saa zinavyoendelea kusogea, mataifa mengine duniani yameendelea kuupokea mwaka mpya ikiwemo ya Afrika, Ulaya na hatimaye Amerika yanayopokea mwaka mpya kwa kuchelewa kidogo
Hujambo na karibu
Heri ya Mwaka Mpya 2026
Wezi wavunja benki ya Ujerumani na kutoroka na mamilioni
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Shimo lililojitokeza baada ya wezi kutoboa ukuta
Wezi walitumia kipindi cha Krismasi tulivu kuvunja benki ya Ujerumani
na kutoroka na pesa zenye thamani ya euro milioni 10 na vitu vya thamani kutoka
kwenye masanduku ya amana ya wateja, polisi walisema Jumanne.
Polisi walisema katika taarifa kwamba wahalifu walitoboa
ukuta mzito wa zege katika tawi la benki ya Sparkasse katika mji wa magharibi
wa Gelsenkirchen na kisha kuvunja masanduku elfu kadhaa ya amana na kuiba kiasi
kinachokadiriwa kuwa mamilioni ya euro.
Maduka na benki nyingi hufunga nchini Ujerumani wakati wa
Krismasi kuanzia jioni ya Desemba 24, na polisi waligundua shimo hilo baada ya
kengele ya moto kulia mapema Jumatatu, Desemba 29.
Wateja wengi wenye hasira walikusanyika mbele ya benki siku
ya Jumanne huku wakipaza sauti "Turuhusu tuingie!".
Putin aamuru upanuzi wa eneo la salama la Ukraine mwaka 2026 - Jenerali mkuu wa Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Jenerali mkuu wa Urusi amesema vikosi vyake vilikuwa
vikisonga mbele kaskazini mashariki mwa Ukraine na Rais Vladimir Putin ameamuru
upanuzi wa eneo ambalo Moscow inaita ‘eneo salama’ mwaka 2026, mashirika ya
habari ya Urusi yalisema Jumatano.
Mkuu wa Wafanyakazi Valery Gerasimov alisema Putin aliamuru
upanuzi wa eneo salama mnamo mwaka 2026 katika maeneo ya Sumy na Kharkiv ya
Ukraine karibu na mpaka wa Urusi, RIA ilisema, akiongeza kuwa alikagua kikundi
cha wanajeshi wa "Kaskazini".
Matamshi ya Gerasimov yanafuatia ahadi ya Urusi ya kulipiza
kisasi kwa kile ilichodai, bila ushahidi, ilikuwa jaribio la kushambulia makazi
ya Putin, madai ambayo Kyiv ilikanusha, ikisema yalilenga kuvuruga mazungumzo
ya amani huku vita vikikaribia mwaka wake wa nne.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Ukraine kuhusu ripoti ya
Gerasimov.
Kiongozi wa mapinduzi ya Guinea ashinda uchaguzi wa rais, matokeo yanaonyesha
Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi wa mapinduzi ya Guinea Mamady Doumbouya amechaguliwa kuwa rais, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa Jumanne, na kukamilisha kurejea kwa utawala wa kiraia katika taifa hilo la Afrika Magharibi lenye utajiri wa boksiti na madini ya chuma.
Kamanda huyo wa zamani wa vikosi maalum, anayedhaniwa kuwa katika umri wake wa mapema wa miaka 40, alichukua madaraka mwaka wa 2021, na kumwangusha Rais Alpha Conde, ambaye alikuwa madarakani tangu 2010. Ilikuwa moja kati ya mfululizo wa mapinduzi tisa ambayo yamebadilisha siasa katika Afrika Magharibi na Kati tangu 2020.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa Jumanne yalionyesha Doumbouya akishinda kwa asilimia 86.72 ya kura za Desemba 28, wingi wa kura unaomruhusu kuepuka duru ya pili ya uchaguzi.
Mahakama ya Juu Zaidi ina siku nane za kuthibitisha matokeo iwapo kutatokea pingamizi lolote.
Ushindi wa Doumbouya, unaompa muhula wa miaka saba, ulitarajiwa sana. Conde na Cellou Dalein Diallo, kiongozi wa upinzani wa muda mrefu nchini Guinea, wako uhamishoni, jambo lililomfanya Doumbouya kukabiliana na wapinzani wanane.
Mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu na mkosoaji wa serikali akamatwa Uganda
Chanzo cha picha, Dr. Bireete Sarah/X
Polisi nchini Uganda imesema imemkamata mwanaharakati
maarufu wa haki za binadamu Sarah Bireete, mkuu wa shirika la haki za binadamu
na mtoa maoni wa mara kwa mara dhidi ya serikali kwenye televisheni na redio za
eneo hilo.
Polisi ilithibitisha hilo katika chapisho kwenye jukwaa la
mitandao ya kijamii X siku ya Jumanne.
"Yuko chini ya ulinzi wa polisi. Atafikishwa mahakamani
kwa wakati unaofaa," chapisho hilo lilisema, bila kutaja ni lini au
mashtaka gani anakabiliwa nayo.
Bireete, mwanasheria na mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha
Utawala wa Katiba (CCG), amekuwa akikosoa hatua mbalimbali za serikali ikiwemo
kile ambacho upinzani unasema ni kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria na
kuwatesa wafuasi wake.
CCG haikuweza kupatikana mara moja kutoa maoni.
Uchaguzi wa Januari unajumuisha Rais aliye madarakani Yoweri
Museveni, 81, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, dhidi yamwanamuziki aliyegeuka
kuwa mwanasiasa Bobi Wine.
Wine, mwenye umri wa miaka 43, na chama chake cha National
Unity Platform anasema mamia ya wanachama wao wamekamatwa mwaka huu ikiwa ni
pamoja na wakati wa kampeni katika hatua iliyokusudiwa kuwatisha wafuasi wake
na kudhoofisha ari ya chama.
Ukraine yasema watu wajeruhiwa katika shambulizi la Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Urusi imefanya shambulizi usiku kucha la ndege zisizo na
rubani katika eneo la Odesa nchini Ukraine, na kuharibu majengo ya makazi na
miundombinu na kuwajeruhi watu wanne, wakiwemo watoto watatu, mamlaka za
kikanda zilisema Jumatano.
Odesa, yenye bandari kubwa katika Bahari Nyeusi, imekuwa
ikilengwa mara kwa mara na makombora na ndege zisizo na rubani za Urusi wakati
wa karibu miaka minne ya vita, huku mashambulizi yakiathiri mara kwa mara
miundombinu ya nishati, usafiri na bandari pamoja na maeneo ya makazi.
"Droni zisizo na rubani zilishambulia miundombinu ya
makazi, vifaa na nishati katika eneo letu," Oleh Kiper, gavana wa eneo la
Odesa, alisema kwenye programu ya ujumbe ya Telegram.
Katika jiji la Odesa, ambalo ni kitovu cha utawala cha eneo
pana la Odesa, watu wanne walijeruhiwa, ikiwa ni pamoja na mtoto mchanga wa
miezi saba, watoto wengine wawili, na mwanamume wa miaka 42, Serhiy Lisak, mkuu
wa utawala wa kijeshi wa Odesa, alisema kwenye Telegram.
Alisema kwamba vifusi vya ndege zisizo na rubani viliharibu madirisha
ya majengo kadhaa marefu ya ghorofa.
Lisak alichapisha picha zinazoonyesha moshi ukitoka kwenye
jengo la ghorofa usiku, huku miali ya moto ikionekana kwenye madirisha kadhaa
na kile kinachoonekana kama ndege ya maji ya zimamoto iliyolenga sehemu ya
mbele ya jengo.