Mbunge Askofu Gwajima: "Tunalinda taifa au tunaharibu taswira ya Tanzania?"

.

Chanzo cha picha, GWAJIMA FACEBOOK

Maelezo ya picha, Mbunge Askofu Gwajima
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mbunge wa Jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima, amelaani vikali vitendo vya utekaji vinavyoripotiwa kuendelea nchini Tanzania, akisema vinaathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya taifa kimataifa na kuvuruga mahusiano ya kidiplomasia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Gwajima alisema kuwa amefanya utafiti wa kibinafsi na kubaini kuwa takribani watu 83 wametekwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Pia unaweza kusoma

'Utekaji sio Utamaduni wa Watanzania'

"Utekaji si utamaduni wetu kama Watanzania, na unapaswa kukemewa vikali.

Ninatoka Kawe, ambapo tukio la aina hii lilimkumba Ally Kibao. Alishushwa kutoka kwenye gari hadharani, na baadaye mwili wake ulikutwa akiwa amefariki. Kama ni baba yako au mtoto wako aliyepitia hali kama hiyo, utajisikiaje?"

Gwajima alitaja tukio la hivi karibuni la kada wa CHADEMA aitwaye Mdude, ambaye anadaiwa kuchukuliwa nyumbani kwake na watu waliovunja mlango mbele ya familia yake, na hadi sasa hajulikani alipo. "Inawezekana unanyamaza sasa, kumbe wewe ndiye unaefuata," alionya.

Polisi wamekanusha kuhusika na matukio yote mawili ya kuuawa kwa Kibao na kutekwa kwa Mdude. Hata hivyo uchunguzi wa matukio yote mawili haijakamilika.

'Je, hii ndiyo picha tunayotaka kuhusu Tanzania?'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi

Alitolea pia mfano wa mwanaharakati kutoka Uganda, Agather, aliyekuja nchini kuhudhuria kesi mahakamani, lakini akadaiwa kuchukuliwa na watu waliodaiwa kuwa wa vyombo vya usalama.

Inadaiwa alivuliwa nguo na kudhalilishwa kabla ya kutupwa mpakani. Vilevile, alitaja tukio la mwanaharakati wa Kenya, Boniface Mwangi, aliyedaiwa kuchukuliwa akiwa Serena Hotel na baadaye kuokotwa mpakani.

Hatuwezi kuharibu taswira ya nchi yetu kwa matendo kama haya."

Mamlaka za Tanzania hazikuzungumzia kushikiliwana madai ya mateso na udhalilishwaji kwa wanaharakati wawili wa kigeni.

Askofu Gwajima alisema haamini kuwa vyombo halali vya dola vinaweza kushiriki katika vitendo vya kihalifu.

"Kama ni chombo cha dola kinamchukua mtu, kinapaswa kujitambulisha na kufuata sheria. Hakiwezi kumchukua mtu hotelini na kumtupa porini."

Alieleza kusikitishwa kwake na madai kuwa baadhi ya watu wanaotekwa huamrishwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan. "Kama mtu amepigwa halafu anaambiwa aseme 'Asante Samia', hiyo ni aibu kwa taifa letu. Inaharibu taswira ya Rais, ya serikali, na hata ya biashara kati ya nchi na nchi."

Askofu Gwajima alisisitiza kuwa vitendo hivyo vinapaswa kulaaniwa na kila Mtanzania, kwani hata watoto wa viongozi wakuu wa nchi wakifanyiwa matendo hayo, hakuna mzazi ambaye angeweza kuvumilia.

'Tutaathirika kama nchi'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanaharakati wa Kenya na Uganda walizuiliwa kuhudhuria kesi ya kiongozi wa Chadema Tundu Lissu

Aliongeza kuwa hali hii inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii, uwekezaji na mahusiano ya kimataifa. "Sasa mtu anaweza kutekwa akiwa hotelini hii siyo Tanzania tunayojivunia."

Gwajima alifafanua kuwa anazungumza kama Mtanzania mzalendo, si kama Mbunge, Askofu, au mwanachama wa CCM. "Fikiria mzazi au mtoto wako anachukuliwa mbele yako, kisha haponekani tena.

Utaumia kiasi gani? Mimi sipo hapa kutoa hukumu, lakini najiuliza: hata kama mtu amekosea, adhabu yake ni kutekwa au kupotezwa?"

Alisisitiza kuwa vyombo vya usalama vya Tanzania vina uwezo mkubwa wa kufuatilia na kupata taarifa.

"Ni vigumu kuamini kwamba hawajui kinachoendelea. Mzigo huu uko mikononi mwa vyombo vya dola, serikali na viongozi wa nchi. Ni lazima tufanye tathmini ya kina kwa sababu hali si shwari."

Marekani yataka uchunguzi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati huohuo Marekani imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na kamili juu ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Tanzania baada ya kushikiliwa kwa wanaharakati wa Kenya na Uganda - Boniface Mwangi na Agather Atuhaire, ambao sasa wameachiliwa.

Mwanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire wa Uganda walizuiliwa nchini Tanzania mapema wiki hii nchini Tanzania, baada ya kwenda nchini humo kuhudhuria kesi ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.

Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani , idara inayohusika na masuala ya Afrika ilisema: '' Marekani ina wasiwasi mkubwa na ripoti za unyanyasaji nchini Tanzania kwa wanaharakati wawili wa Afrika Mashariki - mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire na mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi.

Atuhaire alitambuliwa na @StateDept [Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani] mnamo 2024 kama Mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Wanawake wenye Ujasiri''

Ujumbe huo umeendelea kusema kuwa :''Tunatoa wito wa uchunguzi wa haraka na kamili juu ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu. Tunahimiza nchi zote katika eneo hili kuwawajibisha wale waliohusika na kukiuka haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mateso.''

Mwangi aliachiliwa huru siku ya Alhamisi baada ya Kenya kutoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua ya "haraka na bila kuchelewa" ili kuwezesha ufikiwaji wa kibalozi au kuachiliwa kwa Mwangi, kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa kidiplomasia.

Mwangi ambaye aliachiliwa na kuachwa kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya wa lungalunga alidai kuwa aliteswa alipokuwa Tanzania.