Gwajima: Askofu mwenye utata anayepaza sauti dhidi ya utekaji Tanzania

fc
Maelezo ya picha, Askofu Josephat Gwajima
    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, jijini Dar es Salaam, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), tangu uchaguzi wa 2020, pia ni Askofu wa Glory of Christ Church kwa usajili, maarufu Kanisa la Ufufuo na Uzima, amegonga vichwa vya habari nchini Tanzania katika siku za hivi karibuni.

Ana historia ya matukio na kauli zenye utata (ambazo tutazidurusu huko mbeleni), lakini mara hii Gwajima amejitokeza kama mkosoaji wa matukio ya utekaji na watu kupotea, ambayo yamekuwepo Tanzania kwa kipindi cha muda sasa hata baadhi ya watu waliotekwa kuuawa.

Ukosoaji huo, sasa unaonekana kumuingiza kwenye patashika na viongozi wakuu wa chama chake tawala. Lakini kwanza tuanze na safari yake ya kuingia CCM. Askofu Gwajima hakuwa mwanasiasa mwenye umaarufu katika siasa za chama hicho, kabla ya mwaka 2020.

Uchaguzi wa mwaka huo ndiyo ulimwingiza rasmi katika maisha ya kisiasa, na kuwa mbunge hadi leo. Wakati huo pia aliungwa mkono na kiongozi mkuu wa nchi wakati huo, Rais John Magufuli, wakati wa mbio za kuwania ubunge, baada ya kuwaambia wapiga kura, “nileteeni Gwajima,” tena zaidi ya mara mbili.

Pia unaweza kusoma

Gwajima na utekaji

f

Chanzo cha picha, Mitandao

Maelezo ya picha, Josephat Gwajima, ni Mbunge wa Kawe kupitia CCM

Katika wiki za hivi karibuni, jina Gwajima limevutia vichwa vya habari kwa kuhoji kuhusu matukio ya utekaji na watu kupotea nchini Tanzania, na kueleza kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira ya taifa na vinawaumiza wananchi. “Kama baba yako angetiwa kwenye gari na kesho yake akapatikana amekufa, ungefanyaje?” – alihoji kwa msisitizo.

Kauli yake ya Jumapili Mei 25 ilisambaa haraka mithili ya moto wa nyika majira ya kiangazi, huku akisema atajibu watakaozungumzia kauli yake kulingana na uzito wao. Kauli ya Gwajima kuhusu utekaji haikupokewa vyema na chama chake, kuna wabunge wenzake waliomkosoa. Akiwemo Mbunge wa Kinondoni Abbas Tarimba, CCM. Akisema, "Mungu akulaani huko uliko."

Haikuishia hapo, pia Mwenyekiti wake wa CCM ambaye pia ana kofia ya urais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati akifunga mkutano mkuu maalum wa CCM, Dodoma Mei 30, 2025, alisema, “Niwaombe au sijui niagize vikao vinavyokwenda kuchuja watu. Anayefaa aambiwe anafaa na asiyefaa aambiwe ana kasoro moja, mbili tatu, hatufai kwa huko mbele tunapokwenda.”

Aliendelea kwa kusema, “tukitoa mwanya ndugu zangu, tukipitisha wanaotafuta tu na mie niwemo, ndiyo tunapata wale wanaokwenda huko. Chama kinakuwa Gwajimanised. Kwa hiyo kwa vyovyote vile tusi-Gwajimanise chama chetu, Magwajima tuyaache nje.”

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Juni 2, 2025, vyombo vya habari nchini Tanzania hususani kupitia kurasa za mtandaoni viliripoti kuwa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel R. M. Kihampa, amefuta usajili wa Glory of Christ Tanzania Church, maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima.

Katika barua yake kwa Askofu Gwajima, Bw. Kihampa amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Askofu Gwajima kuonekana akitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa kupitia mimbari ya kanisa hilo, akielezwa kuwa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Lakini saa chache baadaye, Gwajima alitoka hadharani na kukanusha taarifa za Kanisa lake kufungwa. "Kwenye mitandao watu wanapitisha karatasi kwamba Kanisa la Ufufuo na Uzima limefungwa, hakuna wa kufunga kanisa la Mungu duniani, si kweli, ni uongo, ni wahuni."

Usiku wa kuamkia Jumanne, Askofu huyo kupitia video iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii akiwa na viongozi wengine wa dini ya Kikristo, alisema kuwa Polisi wamezingira kanisa lake, na taarifa za vyombo vya habari vya ndani zimethibitisha uwepo wa Polisi katika kanisa lake, baada ya barua juu ya kufungwa kwa kanisa hilo.

Gwajima mwenye Utata

gv

Chanzo cha picha, GWAJIMA

Kabla ya kuingia kwenye shughuli za kisiasa, Gwajima hajaacha kuwa mtu mwenye utata – kupitia kauli zake. Mwanaharakati maarufu nchini Tanzania, Fatma Karume, ameonya wiki hii kupitia X, zamani Twitter kwamba Gwajima haaminiki katika kutetea haki, akikumbushia kauli ya askofu huyo ya kutaka kubadilisha misikiti kuwa Sunday-Schools (shule za watoto wa Kikristo). Kauli ambayo inaelezwa aliitoa mwaka 2015.

Wakati wa janga la UVIKO-19, Gwajima alikuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni hadharani ya kupinga chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Miongoni mwa kauli zake nyingi, alinukuliwa akisema chanjo hizo si salama, ingawa tatizo hakuwa anatoa ushahidi wowote wa madai yake.

Miongoni mwa madai aliyoyatoa wakati wa mahubiri katika kanisa lake, ni kwamba chanjo zina uwezo wa kubadilisha chembe hai za vinasaba (DNA) na kufanya watu kuwa mazombi. Licha ya yeye kutotoa ushahidi, pia hakuna ushahidi uliothibitishwa na watalaamu wa afya duniani kuhusu madai ya aina hiyo.

Vilevile alitoa madai kuwa chanjo hizo zina sumaku, akisema, “ndiyo maana unaona watu, wamechanjwa halafu baadaye inashika sumaku. Wewe unajiuliza si ni maji, maji yanashikaje sumaku? Unashangaa wengine nimechanjwa lakini nawaka taa, kuna vitu vimefanywa vidogo vidogo, halafu mtu anaingizwa ndani ya mwili vikaudhibiti mwili."

Makala ya BBC Swahili, kuhusu Gwajima iliyochapishwa Agosti 2021, inaeleza, “baadhi ya chanjo zina viwango vidogo sana vya chuma aina ya aluminiam, lakini madini hayo hayana nguvu ya sumaku. Viwango hivyo ni salama kwa mwili.”

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2020, katika viwanja vya jimbo la Kawe, akiwahutubia wananchi akisaka kura za ubunge, aliwaahidi wapiga kura wa eneo hilo iwapo wangemchagua, angewapeleka Marekani: “Mkinichagua wananchi wa Kawe wote mtafika Marekani, nina rafiki yangu ni gavana wa Jimbo la Birmingham, Marekani amesema anataka tubadilishane watu nikiwa na jimbo.”

Miaka imepotea na hakuna Mmarekani anayeonekana Kawe, ambaye ametokea Birmingham kupitia mpango wa Gwajima. Pia hakuna mtu wa Kawe aliyesafirishwa kupelekwa Birmingham kupitia mpango huo.

Kadhalika wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2020, Askofu Gwajima aliwaahidi vijana wa jimbo la Kawe kuwa agenunua boti za uvuvi ili kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali wa uvuvi na kufuga samaki kukabilia na tatizo la ajira, jambo ambalo hakuwahi kulitekelezwa hata kwa asilimia chache.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Gazeti la Mwananchi, Luqman Maloto akikumbuka ahadi za Gwajima, ameandika, “Gwajima aliahidi kumrejesha akiwa hai aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Chifupa. Na kuahidi kumfufua Waziri Mkuu aliyefariki kwa ajali akiwa ma mamlakani, Edward Sokoine.” Mwandishi huyo anasema, “inakaribia miongo miwili, hakuna ahadi iliyotimia.”

Februari, 2017, Askofu Gwajia alitoka hadharani kukanusha tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, baada ya jina lake kutajwa kwenye orodha ya mkuu wa mkoa wa Dar wa Salaam wa wakati huo, Paul Makonda. Gwajima alikanusha kuuza au kutumia dawa za kulevya na kusema, ametajwa kwa nia ya kuchafuliwa jina lake.

Miaka sita iliyopita, Gwajima aliingia kwenye mjadala baada ya kusambaa video ya utupu inayoelezwa ni yake. Ingawa mwenyewe aliibuka na kukanusha kuhusu video hiyo, akisema mwanaume anayeonekana akifanya mapenzi na mwanamke katika video, si yeye.

Machi 2015 aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alitangaza kumsamehe Askofu Gwajima baada ya kumtolea maneno makali akimwita msaliti wa viongozi wengine wa kikiristo chini ya Jukwaa la Wakrito Tanzania (CCT), ambao walipinga Katiba iliyopendekezwa baada ya Bunge maalumu la Katiba mwishoni mwaka 2014. Wakati huo hakuishia kwa Kardinali Pengo bali alimshambulia pia Spika wa Bunge wa wakati huo, Anne Makinda.

Utata wote huu uliogubika maisha yake, haujawahi kuwa chanzo cha kupoteza umaarufu au kushuka kisiasa, lakini sasa inaonekana meza ambayo ameamua kuitingisha Gwajima, huenda ikamdondosha kisiasa, hasa ukizingatia kauli ya Rais Samia ambayo iliashiria kumlenga yeye.

Huku uchaguzi wa Okotba 2025 ukikaribia, Gwajima ataamua ikiwa anataka kufumba mdomo kama wenzake wa CCM ili pengine abaki kwenye siasa za chama hicho au ataendelea kuzungumza na kukemea utekaji na watu kutoweka, huku akijua hilo linaweza kuyatamatisha maisha yake ya kisiasa ndani ya CCM.

Imehaririwa na Florian Kaijage