'Kama waliteswa waje washtaki' Polisi Tanzania wawaambia wanaharakati
Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro ameiambia BBC kuwa wanaharakati kutoka Kenya na Uganda Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire kama waliteswa basi waende kushtaki katika mamlaka husika.
Muhtasari
- Wawili wafariki katika mlipuko Uganda
- Uingereza yatishia kumshitaki Abramovich - Kunani?
- Polisi Tanzania wazingira kanisa la Askofu Gwajima
- Bill Gates kutoa sehemu kubwa ya utajiri wake wa $200bn kwa Afrika
- Kundi la kijihadi lafanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Mali
- Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi kuhusu mauaji karibu na eneo la usambazaji wa misaada Gaza
Moja kwa moja
Rashid Abdallah & Ambia Hirsi
'Kama waliteswa waje washtaki' Polisi Tanzania wawaambia wanaharakati

Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro ameiambia BBC kuwa wanaharakati kutoka Kenya na Uganda Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire kama waliteswa basi waende kushtaki katika mamlaka husika.
Muliro ameongeza pia madai yao ni ya kiuanaharakati na ni maoni yao.
Wanaharakati hao walieza jinsi walivyoteswa na mamlka za polisi nchini Tanzania kabla ya kurudishwa katika nchi zao.
"Kama wangekuwa hapa, ningewashirikisha, ningewauliza wanasema nini, wanamaanisha nini... Katika sheria, mambo hayo yanaitwa ushahidi wa tetesi au tetesi," Jumanne Muliro aliiambia BBC. Alisema wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka kwa ajili ya uchunguzi.
Mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita, mkuu wa haki za binadamu wa UN aonya

Chanzo cha picha, EPA
Mashambulizi dhidi ya raia yanajumuisha uhalifu wa kivita, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema, huku akitoa wito wa uchunguzi huru kuhusu mauaji karibu na vituo vya kusambaza misaada huko Gaza katika siku za hivi karibuni.
Volker Türk anasema kwa siku tatu mfululizo watu wameuawa karibu na kituo cha usambazaji chakula kinachoungwa mkono na Marekani na Israel, akisema waliohusika lazima wawajibishwe.
Mashambulizi dhidi ya "raia wanaojaribu kupata kiasi kidogo cha chakula cha msaada huko Gaza" "hayana fahamu", anasema katika taarifa yake, na kuongeza: "Mashambulizi yanayoelekezwa dhidi ya raia yanajumuisha uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa, na uhalifu wa kivita." "Wapalestina wamekabiliwa na chaguo baya zaidi: kufa kutokana na njaa au hatari ya kuuawa wakati wakijaribu kupata chakula kidogo ambacho kinapatikana kupitia utaratibu kwa usaidizi wa kibinadamu wa kijeshi wa Israel," anasema.
"Kizuizi cha makusudi" cha kupata misaada "kinaweza kuwa uhalifu wa kivita," Türk anasema.
"Tishio la njaa, pamoja na miezi 20 ya mauaji ya raia na uharibifu kwa kiwango kikubwa, uhamisho wa mara kwa mara wa kulazimishwa, usiovumilika, maneno ya kudhalilisha utu na vitisho vya uongozi wa Israel kuondoa kanda wa wakazi wake, pia ni vipengele vya uhalifu mkubwa zaidi chini ya sheria za kimataifa," anasema.
Wawili wafariki katika mlipuko Uganda

Chanzo cha picha, Uganda Martyrs Shrine/Facebook
Maelezo ya picha, Kila mwaka maelfu kwa maelfu ya mahujaji na watalii hufika katika eneo la Namugongo kwa ajili ya maadhinisho ya mashahidi wa Uganda Watu wawili wamefariki baada ya mlipuko kutokea katika mji mkuu wa Uganda Kampala wakati nchi hiyo inaadhimisha Siku ya Mashahidi wa Kikristo.
Tukio hilo lilitokea karibu na moja ya makaburi ambapo maelfu ya waumini wa Kikristo walikuwa wamekusanyika.
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, waathiriwa ni mwanamume na mwanamke waliokuwa wakiendesha pikipiki.
Hata hivyo, Chris Magezi, msemaji wa muda wa jeshi hilo amedai waliofariki ni magaidi ambao walikamatwa wakiwa na vilipuzi.
Usalama umeimarishwa katika eneo la tukio. Hata hivyo mamilioni ya mahujaji wamemiminika mjini Namugongo kusherehekea Siku kuu ya Mashahidi wa Kikristo.
Tukio hilo ambalo ni mojawapo ya mahujaji wengi zaidi wa Kikristo barani Afrika, huwavutia mamilioni ya waumini kila mwaka kuwaenzi mashahidi 45 wa Uganda, Wakatoliki 22 na Waanglikana 23 waliouawa kati ya mwaka 1885 na 1887 kwa amri ya Kabaka Mwanga II wa Buganda kwa kukataa kuacha imani yao.
Nchini Uganda, Juni 3 ni sikukuu ya umma, na maelfu ya watu wanaanza safari ya hija kwa miguu.
Uingereza yatishia kumshitaki Abramovich - Kunani?

Chanzo cha picha, UEFA via Getty Images
Serikali ya Uingereza imetishia kumshtaki mmiliki wa zamani wa Klabu ya Soka ya Chelsea Roman Abramovich ili kushinikiza fedha zitakazotokana na mauzo ya klabu hiyo zinawafaidi raia wa Ukraine.
Mapato ya takriban pauni bilioni 2.5 yamezuiliwa katika akaunti ya benki ya Uingereza tangu kuuzwa kwa klabu hiyo, baada ya Bw Abramovich kuwekewa vikwazo kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.
Serikali ya Uingereza inataka pesa hizo zitolewa kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Ukraine, lakini Bw Abramovich anataka ziende kwa "waathiriwa wote wa vita nchini Ukraine".
Katika taarifa ya pamoja, Kansela Rachel Reeves na Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy walisema: "Mlango wa mazungumzo utaendelea kuwa wazi, tuko tayari kufuatilia hili kupitia mfumo wa mahakama tukuhitajika kufanya hivyo."
Soma pia:
Polisi Tanzania wazingira kanisa la Askofu Gwajima

Chanzo cha picha, GWAJIMA FACEBOOK
Polisi jijini Dar es Salaam Tanzania wameripotiwa kulizingira eneo lilipo jengo la kanisa la Ufufuo na Uzima linalomilikiwa na kiongozi wa dini ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.
Hatua hiyo ilikuja saa chache baada ya kusambaa mtandaoni barua kutoka moja ya idara za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Tanzania ikimuarifu Gwajima kuhusu uamuzi wa serikali kulifunga kanisa hilo.
Taarifa za askari polisi kulizingira jengo la kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo eneo la Ubungo, kilomita 12 kutoka katikati mwa Dar es Salaam zilisambazwa mtandaoni na Gwajima mwenyewe kupitia kipande cha picha ya video akiwa amezungukwa na watu aliowaita maaskofu wa kanisa hilo waliovalia makoti na mashati ya rangi ya zambarau.
Baadaye zilisambaa picha zilizowaonesha watu wakirusha mawe na sauti za kuwahimiza waumini kwenda kanisani huku kukiwa na milio ambayo haikufahamika iwapo ilikuwa ni ya gesi ya kutoa machozi au risasi za moto.
Barua ya msajili wa jumuiya za kiraia iliyosambaa ambayo Gwajima anasema hajaipookea, ilielezea kufuta usajili wa kanisa la Glory of Christ Church maarufu Ufufuo na Uzima hivyo kutakiwa kusitisha shughuli zote mara moja kwa makosa ya kutoa mahubiri yanye mwelekeo wa kisiasa na kuichonganisha serikali na wananchi.
Mapema Mei 25 Gwajima alielezea kukerwa na matendo ya utekaji wa watu na mauaji.
Maelezo zaidi:
Bill Gates kutoa sehemu kubwa ya utajiri wake wa $200bn kwa Afrika

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Bill Gates, ambaye alianzisha kampuni kubwa ya teknolojia ya Microsoft, ndiye mtu wa tano tajiri zaidi duniani Mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates anasema kuwa sehemu kubwa ya mali yake itatumika kuboresha huduma za afya na elimu barani Afrika katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Tajiri huyo mwenye umri wa miaka 69 alisema kuwa "kwa kuibua uwezo wa binadamu kupitia afya na elimu, kila nchi barani Afrika inapaswa kuwa kufikia ustawi wa kijamii".
Akizungumza katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, pia aliwataka wavumbuzi wachanga Afrika kufikiria jinsi ya kuimarisha teknolojia ya Akili Mnemba (AI) ili kuboresha huduma za afya katika bara hilo.
Mwezi uliopita Gates alitangaza kwamba atatoa 99% ya utajiri wake mkubwa - ambao anatarajia utafikia $200bn (£150bn) - ifikapo 2045, wakati ambapo taasisi yake itakamilisha shughuli zake.
"Hivi majuzi nilitoa ahadi kwamba utajiri wangu utatolewa katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Sehemu kubwa ya ufadhili huo itatumika kukusaidia kutatua changamoto hapa Afrika," alisema katika hotuba yake katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU).
Serikali ya Marekani imepunguza misaada yake kwa mataifa ya Afrika, ikiwa ni pamoja na programu za tiba kwa watu walioambukizwa Virusi Vya UKIMWI na wale walio na UKIMWI, kama sehemu ya sera ya Rais wa Marekani Donald Trump ya "Marekani Kwanza", na kuibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa huduma za afya katika bara hilo.
Soma pia:
Jeshi la Mali latangaza kuzima shambulio la wanamgambo mjini Tumbuktu

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Jeshi la Mali linasema kuwa limetibua "jaribio la wapiganaji wa kigaidi kuvamia" kambi ya kijeshi ya Timbuktu kaskazini mwa nchi hiyo.
Wakazi wa jiji hilo la kihistoria walielezea kusikia milio ya risasi na makombora, wakisema kuwa wanamgambo walilenga maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege na kambi ya jeshi.
Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X, jeshi la Mali lilisema siku ya Jumatatu kuwa hali imedhibitiwa na kwamba wanajihadi 13 wamezuiliwa na silaha, magari na vitu mbalimbali kupatikana.
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa msako unaendelea kufanywa kote Timbuktu. Lakini haikutaja kundi lililohusika na shambulio hilo.
NIM, kundi la Al-Qaeda linalounga mkono wanamgambo hao wa kijihadi, hapo awali lilidai kufanya mashambulizi hayo, ikiwa ni pamoja na shambulio la Jumapili, lililolenga kambi ya kijeshi ya Boulkessi katikati mwa Mali, wakidai udhibiti wa kambi hiyo.
Zaidi ya wanajeshi 30 waliuawa katika shambulio la Jumapili, kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters, hata hivyo idadi hiyo haijathibitishwa na mamlaka.
Lakini, jeshi la Mali bado halijafichua idadi yoyote rasmi ya maafisa wake walioathiriwa.
Soma pia
Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi kuhusu mauaji karibu na eneo la usambazaji wa misaada Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Miili ilipelekwa katika hospitali ya Nasser baada ya tukio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu mauaji ya Wapalestina karibu na kituo cha kusambaza misaada huko Gaza siku ya Jumapili, huku kukiwa na ripoti kwamba vikosi vya Israel vilifyatua risasi.
Mashahidi waliripoti kupigwa risasi wakati wakisubiri chakula katika kituo cha Rafah kinachoendeshwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza (GHF) unaoungwa mkono na Marekani na Israel.
Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema hospitali yake ilipokea majeruhi 179, 21 kati yao wakiwa wamekufa. Shirika la Ulinzi la Raia linaloendeshwa na Hamas linasema idadi ya waliofariki ni 31.
Siku ya Jumapili, jeshi la Israeli lilikanusha kuwafyatulia risasi raia karibu au ndani ya eneo hilo na kusema ripoti kuhusu tukio hilo ni za uwongo.
GHF pia ilisema ripoti hizo ni "uzushi mtupu" na haijaona ushahidi wa shambulio katika kituo chake au karibu na kituo chake.
Israel hairuhusu mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, kuingia Gaza, na kufanya uhakiki wa kile kinachotokea katika eneo hilo kuwa mgumu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres alisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu: "Nimechukizwa na ripoti za Wapalestina kuuawa na kujeruhiwa wakati wakitafuta msaada huko Gaza jana. Natoa wito wa uchunguzi wa haraka na huru kuhusu matukio haya na wahusika wawajibishwe."
Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilijibu kwa kuyataja maoni yake kama "fedheha" katika chapisho kwenye X, na kumkosoa kwa kutoitaja Hamas.
Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la Hamas la kuvuka mpaka tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Takriban watu 54,470 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wakiwemo 4,201 tangu Israel ianze tena mashambulizi yake mwezi Machi mwaka huu, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu
Nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumanne ya tarehe 3 Juni 2025
