USAID ni nini na kwa nini Trump anaripotiwa kuwa tayari kuifunga?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Sean Seddon
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mustakabali wa serikali ya Marekani kutoa misaada kwa mataifa ya nje sasa upo mashakani, wafanyikazi wa mashirika ya kutoa misaada wakitakiwa wasiingie kazini huku utawala wa Trump ukipanga kuiunganisha na idara ya kiserikali.
Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) litaendelea kufanya kazi kama tawi la idara ya serikali, lakini mpango huu unahusisha kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha fedha na wafanyakazi wake, ripoti ya CBS News inasema.
Jumatatu wiki hii, Waziri wa mambo ya nje, Marco Rubio, alikosoa uongozi wa USAID kwa "kutokuwa na nidhamu" na kusema kwamba yeye ndiye "kiongozi wa muda".
Rais wa Marekani, Donald Trump, na mmoja wa washauri wake wakuu, bilionea Elon Musk, wamekuwa wakikosoa vikali shirika hilo.
Hata hivyo, hatua ya kufunga shirika hili inaweza kuwa na athari kubwa kwa programu za kibinadamu duniani kote.
Ni nini USAID na majukumu yake ni yapi?
Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) lilianzishwa miaka ya 1960 ili kusimamia programu za misaada ya kibinadamu kwa niaba ya serikali ya Marekani duniani kote.
Linaajiri takriban watu 10,000, wawili kati ya watatu wakifanya kazi nje ya nchi.
Lina makao makuu zaidi ya nchi 60 na linafanya kazi katika nchi nyinginezo.
Hata hivyo, kazi nyingi za kiutendaji hufanywa na mashirika mengine ambayo yamepewa mikataba na kupatiwa fedha na USAID.
Shughuli zake ni nyingi.
Kwa mfano, sio tu kwamba USAID hutoa chakula katika nchi ambapo watu wanateseka na njaa, pia linaendesha mfumo wa upimaji wa kiwango cha njaa duniani, unaotumia uchambuzi wa data kujaribu kutabiri maeneo ambayo upungufu wa chakula unaibuka.
Bajeti kubwa ya USAID hutumika kwa programu za afya, kama vile kutoa chanjo za polio katika nchi ambazo hukumbwa na ugonjwa huo hatari na kusaidia kukabiliana na virusi hivyo ambavyo huenda vikaleta majanga ulimwenguni.
Isitoshe mfuko wa msaada wa kimataifa wa BBC Media Action, ambao hufadhiliwa na mashirika mbalimbali, hupokea ufadhili kutoka USAID.
Kulingana na ripoti ya 2024, USAID imefadhili dola milioni 3.23, na kuifanya shirika la pili ambalo linafadhili mfuko huu kwa fedha nyingi .
Je, USAID inaigharimu serikali ya Marekani kiasi gani?
Kulingana na data za serikali, Marekani iligharamika dola bilioni 68 katika misaada ya kimataifa mwaka 2023.
Jumla ya fedha hizo zimegawanyishwa kwa mashirika na idara mbalimbali, lakini bajeti ya USAID inajumlisha zaidi ya nusu ya fedha hizo ikipokea takriban dola bilioni 40.
Fedha nyingi hutumika katika bara Asia, mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara na Ulaya- hasa katika juhudi za kibinadamu nchini Ukraine.
Marekani ni taifa ambalo linaongoza kufadhili misaada ya kimataifa duniani.
Uingereza ikiwa nafasi ya nne kufadhili misaada ya kimataifa hasa katika shughuli za kibinadamu.
Kwanini Donald Trump na mwandani wake Elon Musk wanataka kusuka upya USAID?
Trump ni mkosoaji wa muda mrefu wa Marekani kutumia fedha zake kufadhili mataifa mengine akisema hauwakilishi thamani kwa kodi wanazotoa Wamarekani.
Amekosoa vikali USAID, akielezea viongozi wake wa juu kama "watu wasiojielewa ."
Kufunga shirika hili kutaweza kupigiwa upatu kutoka kwa wamarekani.
Tafiti za maoni kwa muda mrefu zimeonyesha kuwa wapiga kura wa Marekani wanapendelea serikali yao kupunguza matumizi ya misaada ya kigeni.
Kwa mfano, moja ya hatua za kwanza alizochukua Trump alipochaguliwa tena ilikuwa kusaini agizo la kiutendaji linalohusisha kusitisha takriban matumizi yote ya kimataifa kwa muda wa siku 90 ili kupitia upya matumizi hayo.
Notisi ikatolewa ikisitisha shughuli zinazoendelea zisimamishwe mara moja.
Muda mchache baadaye agizo likatolewa kuwa baadhi ya programu za kibinadamu ziendelee, ingawa agizo la awali lilikuwa limevuruga shughuli kadhaa kote ulimwenguni.

Chanzo cha picha, EPA
Programu ambazo hutoa misaada ya dawa katika nchi maskini na pia kufadhili miradi ya maji zilisitishwa kwa haraka.
Mfanyikazi wa huduma za kibinadamu aliiambia BBC kuwa agizo la trump kusitisha miradi hiyo ilikuwa kama mtetemeko wa ardhi.
Mkwaruzano kati ya ikulu ya White House na USAID ulichemka zaidi bada ya wafanyikazi wa USAID kukatazwa kuingia afisini au kufikia data za kifedha katika makao makuu yake.
Mapema wiki hii Elon Musk kupitia mtandao wa X alisema kuwa suala la kusitisha programu za USAID alishauriana na rais kwa kina na kuamua inapaswa kufungwa.
Waziri wa mambo ya nje Marco Rubio amethibitisha kuwa programu nyingi za USAID zitaendelea lakini zitalingana na maslahi ya taifa.
Je, Trump ana uwezo wa kufunga USAID?
Ingawa ni wazi kwamba Ikulu ya White House ina ushawishi mkubwa kwa USAID, nguvu hiyo kisheria ni ndogo.
USAID iliundwa baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Misaada ya Kigeni mwaka 1961.
Sheria hiyo ilimtaka rais wa Marekani kuanzisha shirika ambalo lingesimamia matumizi ya fedha nje ya nchi.
Rais John F. Kennedy alianzisha USAID kwa amri ya kiutendaji.
Trump hawezi kusitisha shughuli za USAID kwa kutia saini agizo la kiutendaji na akichukua mkondo huo zaidi atakabiliwa na mashtaka chungu nzima katika mahakama na bungeni.

Chanzo cha picha, Reuters
Kufunga kabisa USAID kutahitaji hatua ya Bunge, ambapo Chama cha Republican cha Trump kinashikilia wingi wa wabunge katika mabunge yote mawili.
Kutokana na kikwazo kinacho mkodolea macho Trump inadaiwa kuwa serikali yake inapanga kujumuisha USAID kama tawi la idara ya taifa, kinyume na kuwa wakala wa serikali wa kujisimamia.
Athari za kufunga USAID
Kwa kuwa Marekani inatoa kiasi kikubwa cha misaada ya kimataifa, mabadiliko yoyote katika jinsi fedha hizo zinavyotumika yangeonekana kote duniani.
USAID inahusika katika shughuli mbalimbali, kutoka kutoa viungo bandia kwa majeruhi wa kivita nchini Ukraine, hadi kutoa msaada wa kupambana na virusi vya Ebola Afrika.
Baada ya kusitishwa kwa matumizi ya kimataifa kwa siku 90, Marco Rubio alisema kuwa "kila dola" lazima "ithibitishwe" kwa ushahidi kuwa inafanya Marekani kuwa salama, yenye nguvu na yenye ustawi zaidi.
Pia kuna maswali kuhusu ni kiasi gani Marekani itatumia ng'ambo katika miaka ijayo, kama Musk - akiwezeshwa na Trump - anajaribu kupunguza mabilioni kutoka kwa bajeti ya serikali.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi












