Jinsi vikwazo vya mafuta vya Marekani vinavyoiumiza Urusi na Iran

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Jeremy Howell
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Marekani imeweka vikwazo kwa Urusi na Iran, ikilenga mauzo yao ya mafuta na "meli zao za magendo" ambazo ni ngumu kuzifuatilia. Nchi hizo zimetumia meli hizo kusafirisha mafuta kwa njia haramu.
Vikwazo hivyo vinalenga kuzuia usambazaji wa mafuta kwenda China - mteja mkuu wa mafuta ya Urusi na Iran. Ni vikwazo ambavyo vimesababisha uhaba wa mafuta duniani kote katika wiki za hivi karibuni na kusababisha bei ya mafuta kupanda.
Ikiwa utawala wa Trump utaweka vikwazo vipya na vikali zaidi kwa mafuta ya Urusi na Iran, vikwazo hivyo vinaweza kuchangia bei ya mafuta kupanda zaidi.
Vikwazo dhidi ya Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi inaficha taarifa zake za mauzo ya mafuta, lakini Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) - linakadiria kwa sasa inauza mapipa milioni 7.33 kwa siku nje ya nchi.
Kulingana na Kituo cha Utafiti wa Nishati na Hewa Safi, Urusi ndiyo inayoongoza kwa kupeleka mafuta nchini China. Pia zaidi ya theluthi moja ya mafuta ya India inayoagiza kutoka nje, yanatoka Urusi.
Uingereza na Marekani zilipiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi Machi 2022.
Urusi inapata takribani dola za kimarekani bilioni 190 kwa mwaka kutokana na mauzo yake ya mafuta - mapato ambayo husaidia kufadhili vita vyake.
Vikwazo vilivyowekwa kwa mauzo ya mafuta ya Urusi mwezi Januari yalibabisha bei ya mafuta ghafi ya Brent (bei ya kimataifa) kupanda hadi dola 80 kwa pipa.
Iran na vikwazo
Iran pia inaaminika inauza nje takribani mapipa milioni 1.7, huku mapipa milioni 1.2 au milioni 1.3 yakienda China (Iran pia inaficha taarifa zake za mauzo). Kulingana na baadhi ya ripoti, inauza mapipa 400,000 kwa India.
Tangu 2012, serikali ya Marekani imepiga marufuku uagizaji wa mafuta ya Iran, na pia imepiga marufuku makampuni ya kigeni ambayo yanahusika na mauzo ya mafuta ya Iran kufanya biashara na Marekani.
Inataka kuinyima Iran fedha za kutengeneza silaha za nyuklia na makombora ya balistiki, au kusaidia vikundi vya wapiganaji kama vile Hamas, Hezbollah na waasi wa Houthi.
Donald Trump aliimarisha vikwazo hivi mwaka 2019 na 2020, wakati wa muhula wake wa kwanza kama rais wa Marekani.
Hata hivyo, Iran bado ina uwezo wa kusafirisha mafuta mengi kwenda China, kwa sababu mengi yao yananunuliwa na wasafishaji wadogo.
Mbinu za kukiuka vikwazo

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Urusi na Iran wamejaribu kukwepa vikwazo kwa kusafirisha shehena ya mafuta ghafi katika meli za mafuta ambazo ni za magendo.
Meli hizi za mafuta zimesajiliwa katika nchi ambazo huruhusu maelezo ya umiliki wa meli kubaki kuwa siri. Hii inafanya kuwa vigumu kwa Marekani kuwaadhibu wamiliki wa meli hizo kwa ukiukaji wa vikwazo.
Meli hizo za mafuta huzima mawimbi ya redio ili kufanya safari zao kuwa siri.
Januari 2025, katika siku za mwisho za utawala wa Biden, Marekani iliweka vikwazo kwa meli 183 zinazosafirisha mafuta ya Urusi na Iran, pamoja na kampuni mbili za mafuta za Urusi - Gazprom Neft na Surgutneftegas.
Marekani pia imeweka vikwazo kwa meli za mafuta za Iran mwezi Oktoba 2024, kujibu mashambulizi yake ya makombora dhidi ya Israel, na kuziwekea vikwazo meli za mafuta za Russia na Iran mwezi Disemba mwaka huo.
Homayoun Falakshahi wa Kpler, kampuni ya data, anasema Marekani imewekea vikwazo 23% ya meli zinazobeba mafuta ya Iran, na karibu 9% ya meli zinazobeba mafuta ya Urusi.
"Tunaona kushuka kwa 20% hadi 25% ya kiwango cha mafuta ya Urusi na Iran yanayoingizwa nchini China. Na kuna meli za mafuta zilizo na takribani mapipa milioni 20 ya mafuta yanayosubiri katika bahari ya China, na haziwezi kupakua.
"Hii ni kwa sababu Bandari ya Shandong, bandari kuu ya kupokea mafuta ya Iran, haikubali meli yoyote ambayo yako katika orodha ya vikwazo."
Wasafishaji wa India pia wamesema wataacha kuchukua mafuta yaliyoidhinishwa katika vikwazo na Marekani kutoka Urusi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












