Vikwazo vya kushangaza wanavyoekewa wapinzani wa serikali ya Iran

Chanzo cha picha, Taraneh Alidoosti
- Author, Masoud Azar
- Nafasi, BBC News Persian
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Zaidi ya miaka miwili imepita tangu maandamano ya kitaifa nchini Iran kufuatia mauaji ya Mahsa Amini aliyekuwa amezuiwa katika kituo cha polisi cha maadili. Huku serikali ya Iran ikionekana kunyesha kuwa vuguvugu hilo limepita na kutulia , suala la ulazima wa kuvaa hijabu - unaokataliwa na wanawake wengi unaendelea kuibua wasiwasi kwa mamlaka husika.
Kufikia sasa, serikali imekataa kutekeleza au kulazimisha sheria kali ya uvaaji hijabu ulioidhinishwa na bunge.
Wanawake wengi wanaendelea kutembea bila kuvaa hijabu ambalo ni vazi lililoamrishwa, baadhi yao wakijipata matatani kwa kukaidi amri hiyo.
Majaji wana mamlaka makubwa na wanaweza kutoa adhabu zisizo za kawaida, mara nyingi kwa kuchanganya adhabu za jadi na hatua zinazohusiana na itikadi au ishara za kisiasa.
Taraneh Alidoosti - mmoja wa waigizaji maarufu wa Irani, anayejulikana kwa jukumu lake katika filamu iliyoshinda tuzo ya Oscar 2016 The Salesman - hivi majuzi alijikuta akikabiliwa na vikwazo hivyo.
Mfuasi mkubwa wa vuguvugu la Mwanamke, Maisha, Uhuru, ambalo lilizuka baada ya kifo cha Amini, Alidoosti alikaidi waziwazi sheria ya hijab kwa kukataa kuvaa hijabu.
Ingawa upinzani ulitarajiwa, wachache wangeweza kutabiri kiwango cha vizuizi vilivyowekwa kwake na kwa watu wengine wa umma.
Kesi ya Alidoosti ilianza kuzingatiwa alipozuiwa kupanda ndege kuelekea Kisiwa cha Qeshm kusini mwa nchi.
Wakili wake alisema alikuwa amezuiwa kusafiri au kufanya miamala ya kifedha.
Hii ilikuwa ni pamoja na vikwazo vya awali ambavyo vilimzuia kuondoka Iran.
Hata hivyo, Msemaji wa mahakama ya Iran amekanusha kuwepo kwa marufuku hii.
Hatua za serikali dhidi ya Alidoosti zinaonyesha mkakati mpana zaidi: kudhibiti sauti zenye ushawishi zinazoweza kuhamasisha upinzani zaidi.
Bado hali ya kipekee ya baadhi ya hukumu inaonyesha mahakama inayojitahidi kudumisha udhibiti huku hali ya upinzani ikiongezeka miongoni mwa umma dhidi ya sheria za kuvaa hijabu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wanazuoni wengi na watu maarufu wengine walisusia kuvaa hijab kama ishara ya mshikamano na harakati inayojulikana kama Woman, Life, Freedom.
Azadeh Samadi, mwigizaji mwingine maarufu, alipigwa marufuku ya miezi sita kwenye mitandao ya kijamii.
Katika hukumu isiyo ya kawaida, mahakama pia ilimwamuru aende matibabu ya kisaikolojia kwa ajili ya "kiwango cha utu cha kijamii".
Alilazimika kuonyesha cheti cha afya kuthibitisha kuwa amekamilisha matibabu.
Mwigizaji mstaafu Afsaneh Bayegan alikumbwa na adhabu sawa.
Mbali na marufuku ya mitandao ya kijamii, aliamriwa kufanyiwa matibabu.
Hukumu hizi zilizua hasira miongoni mwa Wairani na wataalamu wa sheria, ambao walijiuliza kuhusu uhalali na misingi ya kimaadili ya hukumu hizi.
Mkurugenzi wa filamu Saeed Roustaee, ambaye filamu zake zinakosoa matatizo ya kijamii na kiuchumi ya Wairani wa kawaida, alikumbwa na adhabu ya kushangaza kama sehemu ya hukumu yake: alizuiwa kuhusiana na watu wanaoshiriki katika utengenezaji wa filamu.
Hukumu hii ililenga kumtenga kitaaluma na kuzuia wengine katika sekta ya filamu kujihusisha na masuala nyeti.
Alilazimika pia kuhudhuria kozi ya utengenezaji wa filamu za kimaadili kwa mujibu wa serikali.
Aidha, alihukumiwa kifungo cha miezi sita kwa "propaganda dhidi ya utawala," na filamu yake Leila's Brothers iliyokuwa ikionyeshwa kwenye Tamasha la Filamu la Cannes ilitumiwa kama ushahidi dhidi yake.
Naye mwandishi wa picha Yalda Moayeri alihukumiwa kifungo cha miaka sita na adhabu nyingine tano, ikiwa ni pamoja na kuandika insha ya kurasa 100 kuhusu kazi za ayatollah ambaye anapinga hijabu, marufuku ya matumizi ya simu na mitandao ya kijamii kwa miaka miwili, na miezi miwili ya huduma za jamii kama kudumisha usafi katika bustani ya wanawake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hukumu moja ya zaidi iliyoibua hisia kali ilikuwa ya Shervin Hajipour, msanii maarufu aliyejulikana kwa wimbo wake Baraye (Kwa Ajili ya), ambao ulijizolea umaarufu kama wimbo wa harakati ya Mahsa Amini.
Hajipour alikabiliwa na mashtaka kwa kutumbuiza wimbo huo na alihukumiwa kifungo na marufuku ya kusafiri.
Mahakama ilimwambia asome na kuandika mukhtasari wa vitabu viwili vya kidini: Haki za Wanawake katika Uislamu na Mwanamke katika Kioo cha Hadhi na Uzuri vilivyoandikwa na mwandishi tajika Ayatollahs.
Upinzani mkubwa dhidi ya hukumu ya Hajipour ulisababisha adhabu hiyo kubatilishwa.
Mkuu wa Mahakama ya Iran, Gholamhossein Mohseni Ejei, alikosoa hukumu hizo akisema zinapaswa kuwa "kizuizi" na zisilete "athari hasi."
Aliagiza hukumu zichukue mambo kama "uwezekano" na "kuepuka aibu" ili kuepuka matokeo yasiyotarajiwa na kuhakikisha hukumu hazileti mjadala usiohitajika.
Usikilizaji wa kesi katika maeneo faragha
Matumizi ya "ubunifu" katika hukumu za mahakama ya Iran siyo jambo jipya.
Kwa miaka mingi, wanaharakati, waandishi wa habari, na wasanii wamekuwa wakitumikia adhabu zisizo za kawaida, mara nyingi zilizolenga kuwaibisha au kuwaondoa katika jamii.
Ingawa kupigwa na kufungwa bado ni sehemu ya mfumo wa sheria, hukumu za hivi karibuni zinaonekana kulenga kudhoofisha uaminifu na ushawishi wa wahusika.
Licha ya mabadiliko ya hivi karibuni katika mfumo wa sheria, ikijumuisha upatikanaji mkubwa wa kusikiliza kesi hadharani na hukumu wazi kwa makosa ya kawaida, kesi zinazohusiana na wanaharakati wa kiraia na kisiasa bado zinafanyika kwa siri.
Wanaharakati mara nyingi wanakutana na vikwazo vya kijamii na kitaaluma bila kufikishwa mahakamani au kupatiwa fursa ya kujitetea.
Katika baadhi ya matukio, hawawezi hata kujua kuhusu hukumu zao mpaka wanapojaribu kupanda ndege na kugundua kuwa wamepigwa marufuku ya kusafiri.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












