Wito wa haki na uwajibikaji waongezeka nchini Syria baada ya utawala wa Assad kuanguka

- Author, Sebastian Usher
- Nafasi, mchanganuzi BBC's Middle East
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mamlaka mpya ya Syria imetoa ahadi ya kutoa haki kwa uhalifu uliofanywa chini ya utawala wa Assad.
Hata hivyo, ni kibarua kigumu, kwani wengi wamepata madhara makubwa ya kila aina katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sebastian Usher alikutana na watu huko Damascus ambao wanaamini upatikanaji wa haki ni muhimu katika jinsi wanavyoiangalia mustakabali wa Syria.
Katika kingo za Douma, moja ya vitongoji vya Damascus vilivyoharibiwa zaidi na vita, katika chumba kilichozungukwa na kivuli karibu na jiko, Umm Mazen anasimulia miaka 12 aliyojitahidi kutafuta habari za watoto wake wawili, ambao walikamatwa katika miaka ya mwanzo ya maandamano na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuzama katika mfumo wa usalama wa enzi ya Assad.
Kwa mtoto wake mkubwa, Mazen, alifanikiwa kupokea cheti cha kifo, lakini kwa Abu Hadi, hakuna chochote kinachojulikana kumhusu.
Mtoto wake wa tatu, Ahmed, alitumikia miaka mitatu katika mfumo wa usalama, ikiwa ni pamoja na miezi nane katika jela ya Saydnaya, kwa wafungwa wa kisiasa.
Meno yake ya mbele yalivunjwa na nyundo ya mtesaji, anasimulia tukio moja ambapo aliamini aliisikia sauti ya kaka yake Mazen akiitikia jina lake katika wito wa majina katika gereza hilo, lakini hakuna kilichofuata.
Haki gani anayotafuta Umm Mazen kwa uharibifu wa familia yake?
"Kunapaswa kuwa na haki ya kimungu, kutoka kwa Mungu," anasema.
"Niliwaona baadhi ya wanaume wa mtaa wakileta shabiha (mfuasi mwenye silaha wa utawala) ili auawe."
"Nikamwambia: 'Msimuue. Badala yake, mteseni kama alivyowatesa vijana wetu'."
"Watoto wangu wawili walikufa – au labda wamekufa, lakini kuna maelfu ya vijana wengine ambao waliteswa."
"Namuomba Mungu kwamba Bashar [al-Assad] abaki katika jela ya chini ya ardhi na kwamba Urusi, ambayo ilikuwa ikimlinda, isiweze kumsaidia."
"Namuomba Mungu amuweke chini ya ardhi na aachwe akosekane kabisa – kama alivyowatupa vijana wetu katika jela zake."

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakili Hussein Issa alipigania haki kwa mamia ya raia wa Syria waliotuhumiwa uhalifu wa kisiasa chini ya utawala wa Assad.
Alikumbana na shinikizo la mara kwa mara kutoka kwa mamlaka kuhusu utetezi wake, lakini alisisitiza na kufanikiwa kuokoa baadhi ya wateja wake kutoka kuangamizwa na mfumo wa usalama.
Lakini kwa wale waliowekwa katika mahakama maalum za ugaidi, mara nyingi hakukuwa na chochote kilichoweza kufanywa.
Sheria ya ugaidi ilikua na athari kubwa zaidi huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea.
Sasa, akiwa kwenye ofisi yake akitazama milima ya Damascus, wakili mwenye umri wa miaka 54 anasema anaamini kwamba majaji wengi walioshiriki katika utawala wa Assad wanapaswa kutimuliwa na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo, wengine kutoka enzi hiyo, anasema, bado wanaweza kuwa na jukumu katika mfumo mpya wa mahakama.
Kuhusu changamoto kubwa ya kuleta haki kwa uhalifu wa miaka 50 iliyopita, Bw. Issa anasema kwamba kuanzisha mfumo wa kisheria unaoweza kufanya hivyo ni jukumu muhimu kwa mamlaka mpya za Syria.
"Endapo mfumo huu hautakuwa mzuri, mustakabali wa nchi mpya utakuwa na kiza."
"Hatujui itakuwaje mbaya zaidi. Tayari tunaogopa kwamba baadhi ya pande zinaweza kusababisha mfarakano na migogoro."
"Endapo tutakuwa na mfumo imara na serikali, hatutakuwa na hofu ya mambo haya."
"Endapo hatutakuwa nao, tutakuwa na hofu. Hata hivyo, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye matumaini kwa asili, nadhani utawala mpya utakuwa bora zaidi."

Shughuli katika jengo kubwa la wizara ya haki katika mji mkuu wa Syria zilikuwa zimesitishwa kwa wiki kadhaa baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad.
Sasa, makundi ya mawakili wamekusanyika kwenye kambarao na ushoroba wa jengo hilo wakisubiri kufunguliwa tena kwa mahakama za kiraia na za jinai.
Katika ofisi yake iliyopo ghorofa ya tano, Naibu waziri wa haki, Khitam Haddad, anasema kesi za jinai na za kiraia zitashughulikiwa tena, lakini kazi ya kushughulikia uhalifu uliofanywa chini ya utawala wa zamani haitaanza kwa sasa.
Akisema kuwa ameanza kazi ya kuwa jaji tangu 2013, na aliteuliwa kuwa naibu waziri wa haki mwaka 2023, anasisitiza kwamba kazi hiyo lazima iendelee.
"Nilitambua uwajibikaji binafsi kuhusu suala hili," anasema.
"Ni muhimu kazi iendelee, mawakili warejee kazini na mahakama zirudi, kwa sababu kama raia wa Syria, nataka kazi yangu iendelee na nataka ushindi huu uendelee, ili watu wasiwe na hofu yoyote."
"Nataka kutuma ujumbe wa kweli na wa hali halisi wa kutia moyo, si maneno tu."
Hata hivyo, baadhi ya mawakili tayari wanahofia hatua ya mamlaka ya mpito kuanzisha baraza la kusimamia chama cha mawakili bila kuweka suala hilo kwa kupiga kura.
Katika ombi lao, walisema kuwa njia hii ingeleta aina nyingine ya utawala wa kidikteta.
Kwa sasa, sheria na muundo wa kisheria wa enzi ya Assad bado upo, ikiwa ni pamoja na sheria ya ugaidi.
Inaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kesi yoyote ya wale waliokamatwa kwa uhalifu chini ya utawala uliopita kuletwa mahakamani.

Mamlaka mpya za Syria zimetoa wito kwa Wasyria wasichukue sheria mikononi mwao, huku video zikisambaa zikionyesha kuadhibiwa kwa baadhi ya maafisa wa zamani wakidai ni njia moja ya kupata haki.
Kumekuwa na mashambulizi na kukamatwa – na baadhi ya wale waliokimbia mpaka kuelekea Lebanon au Iraq wamerejeshwa.
Lakini bado kuna swali kubwa kuhusu kama mfumo wa haki – ambao kwa muda mrefu ulikuwa chombo cha ukandamizaji – unaweza kurekebishwa ili kukabiliana na changamoto hii kubwa ya maadili na kiutawala.
Katika milima ya juu zaidi ya Damascus, Wasyria, vijana na wazee, kwa sasa wanapumua hewa safi ya baridi – wakifurahia uhuru katika sehemu walizozuiwa kuingia kwa zaidi ya muongo mmoja.
Katika mikahawa na vibanda vilivyojitokeza katika wiki chache tangu kuangushwa kwa Assad, wanatazama jiji lililo mbele yao – likiwa na kumbukumbu zake za giza na ahadi ya mustakabali tofauti, ambapo haki na uwajibikaji huenda vikaruhusiwa kuwa sehemu ya mabadiliko.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












