"Vijana wa utawala wa Assad walinibaka, lakini sina hofu ya kuonyesha uso wangu."

- Author, Fergal Keane
- Nafasi, Mwandishi maalum BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Sanduku dogo la kupendeza, lililopambwa kwa umaridadi alizawadiwa na bibi yake. Kumbukumbu maalum, ambayo anashikilia mkononi mwake na kuigusa, ikileta kumbukumbu za zamani.
Rene anafungua sanduku la muziki na muziki unacheza, muziki uleule aliousikia zamani katika sebule ya nyumba yake huko Damascus.
"Hiki ndicho kitu pekee nilichobaki nacho kutoka kwa nyumba ile," anasema.
Mwanamme huyu anaonekana kuwa mtulivu na mwenye huruma.
René Sivan ni mfupi na mwembamba, japokuwa anazungumza kwa sauti ya chini.
Amekuwa akikumbwa na mihemko mseto kwa wiki nzima.
Akifurahia kuanguka kwa utawala wa al- Assad na matukio ya kutamausha aliyoyapitia alipokuwa amezuiliwa jela kwa miezi huko Syria.
''Kuna sura ya mwanamke mmoja ambayo bado inanijia akilini mwangu. Alikuwa amesimama ukutani, akiomba msaada....Bila shaka alikuwa amebakwa.''
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
''Pia kuna kijana mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 16 ambaye pia alinajisiwa, na alikuwa akipiga mayowe akiita mamake amuokoe. Alikuwa akisema, 'Mama..Mama...Mama.''
Alidhulumika kingono kwa muda.
Nilipokutana kwa mara ya kwanza na Rene, alikuwa ametoroka Syria wakati huo.
Ilikuwa takriban miaka 12 iliyopita. Alikuwa amekaa mkabala na mimi akitetemeka na machozi yakimtiririka huku akiwa amejawa na hofu, hakutaka tumpige picha sura yake.
Maafisa wa usalama walikuwa wamemkamata kwa kushiriki maandamano yakudai demokrasia.
Walitambua ni kijana anayejitambulisha na jinsi moja.
Watatu kati ya maafisa waliomshika walimbaka Renee. Aliwasihi wamuachilie lakini walimdhihaki.
''Hakuna aliyetaka kunisikiliza,''anakumbuka tukio hilo la mwaka 2012. ''Nilikuwa peke yangu.''
Afisa mmoja alikuwa akimnajisi kila siku kwa miezi sita aliyokuwa amezuiliwa katika jela hiyo.
Baada ya picha kusambaa za wafungwa mjini Damascus hadi kuenezwa kwa televisheni, Renee alikumbuka mashaka aliyoyapitia gerezani humo.
''Sipo gerezani sasa, niko hapa, lakini bado najiona kwa picha na video za Wasyria. Ninafurahia, lakini najiona kama bado niko hapo..Najiona ni kama ni mimi bado wakati huo. Naona bado maafisa walionidhulumu kingono na kunitesa. Nakumbuka yote yaliyonisibu.''
Anaanza kulia akitutaka tusitishe mahojiano kwa muda. Anasema tumpe nafasi kidogo hisia zimuishe.
Wakati huo naangalia ukutani mwa sebule yake.
Kuna picha ya nyumba yake iliyoharibika huko Syria, picha nyingine ni ya Renee akiwa katika mbio za Utrecht, na pia kuna picha ya padri Franz Von Derlocht, mwenye umri wa miaka 75 ambaye ni mwanaharakati wa dini Syria aliyeuawa mwaka 2014.
Ni Padri Von Derlocht ambaye aliambia Renee, katika jamii ya siri kuwa hali yake ya kuwa wa jinsi moja bado kristo anampenda alivyo na hambagui kutokana na hali yake.
Renee anakunywa maji na kisha ananiarifu tuendelee na mahojiano.
Nafikiria vile amebadilika na yuko tayari sura yake inaswe na kamera zetu.
Ananijibu:''Kwasababu utawala wa kikatili umeanguka sasa sina uoga kwa utawala huo. Assad amejificha katika mji wa Moscow. Kwasababu wahalifu wametoroka Syria na kuiachia nchi hiyo raia wake kama inavyotakikana.''
''Natumaini tutaishi Syria bila kubaguliwa na kuwe na usawa wa hali. Najivunia kuwa raia wa Syia na mimi ni wa jinsi moja.
Lakini, kauli hii haimaanishi fika kuwa anaweza kuishi kama mtu wa jinsi moja huko Syria. Kuwa wa kundi la jinsi moja kulikuwa ni marufuku chini ya utawala wa Assad.
Utawala mpya una mizizi ya dini ya kiislamu na wamekuwa wakiwahukumu watu wa jinsi moja.
''Kuna watu wa jinsi moja Syria wanapigania haki zao,''anasema Rene.
''Ni sehemu ya vuguvugu hilo na wengine wameuawa kutokana na misimamo yao. Serikali ya Syria imewaua kutokana na kuwa wa jinsi moja na waliobaki wanashinikiza haki zao. ''Rene anasema ana imani kutakuwa na mabadiliko Syria.
Pia anaamini kutakuwa na matumaini ya kuishi kwa kabila zote nchini humo hasa Wakurdi na wataishi kwa usalama.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rene ni miongoni mwa Wasyria milioni 6 ambao wametoroka Syria, wengi wao wakiomba hifadhi katika mataifa jirani kama vile Lebanon, Jordan na Uturuki na pia nchi za Ughaibuni.
Hata hivyo mataifa ya magharibi yamesitisha maombi ya hifadhi kutoka kwa Wasyria tangu utawala wa Assad kuanguka, hatua ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu wamepinga vikali na kuikosoa kwa kuharakisha kusitisha mchakato huo.
Kuna takriban Wasyria milioni Ujerumani.
Mmoja wao ni msichana mkurdi ambaye ana ulemavu niliyekutana naye mwezi Agosti mwaka 2015 alipokuwa miongoni mwa wakimbizi waliobahatika kuingia katika kisiwa cha Ugiriki.
Alikuwa akisafiri kuelekea kaskazini kupitia Serbia, Croatia, Slovenia, na Austria.
Ili kufika Ulaya kutoka kaskazini mwa Syria, Nozhin alivuka milima, bahari, na mto, na dada yake Nasrin alimsukuma kwenye kiti cha magurudumu kila hatua ya safari.
"Nataka kuwa mtaalamu wa anga na labda nitakutana na kiumbe kutoka sayari nyingine. Ningependa kumwona Malkia," alisema Nozhin mwaka huo.
Nilikuwa nimeshikilia kando yake kwenye barabara, ambapo maelfu ya wakimbizi waliokuwa wametoka kwa uchovu na kukata tamaa walikuwa wamelala chini kutokana na joto la mchana. Roho yake nzuri na matumaini yake yalileta faraja kwa wengine.
Alikuwa msichana ambaye aliweza kuzungumza Kiingereza vizuri kutokana na kutazama televisheni ya Marekani.
Nozhin alikulia katika mji wa Aleppo na vita vilipoanza, alihama na familia yake kuelekea mji wa Kobani, makazi salama ya Wakurdi, ambayo baadaye yalishambuliwa na vikosi vya ISIS.
Nilimkuta mwaka huu kwenye uwanja wa jiji uliojaa shughuli za biashara za Krismasi mjini Cologne, ambapo mahema ya masoko na wauzaji wa soseji za Kijerumani na divai ya mvinyo wa mchanganyiko walikuwa wakiuza bidhaa zao, na katika sehemu kama hiyo, mateso na safari za Syria inahisi kuwa mbali sana.
Lakini sio kwa Nozhin…
Muda wote wa wiki, hata baada ya familia nzima kwenda kulala, alikaa mbele ya televisheni na kutazama habari.
Hakukuwa anafikiria kuhusu mtihani wa digrii yake ya usimamizi wa biashara. Alijua atafaulu.
Nozhin anajua kwamba wakati kama wa kuanguka kwa Assad hautarudi tena: wakati wa matumaini safi, yasiyoshindika.

"Hakuna kinachodumu," anasema. "Mwisho wa usiku ni giza kupotea."
"Niliijua kuwa singerejea Syria hasa Assad akiwa madarakani, na kwamba kwa mtu kama huyo akiwa madarakani, haiwezekani kwa nchi hii kustawi na kuwa huru. Sote tulijua kuwa ni kwa kuondoka kwake pekee ndipo tungeweza kuanzisha amani.
Sasa kwamba sura hii katika historia ya ardhi hii imemalizika, nadhani changamoto halisi zimeanza."
Kama Rene, anataka Syria iwe na uvumilivu kwa makabila na jamii ndogo na kushughulikia na kutunza haki za watu wenye ulemavu.
"Sihitaji kurudi mahali hapo ili kufika kwenye nyumba yako ya ghorofa ya nne, inabidi upande ngazi tu na hakuna kambarao."
Kama msichana kutoka Kurdistan, anafahamu vyema mateso na maumivu ya watu wa maeneo ya Kikurdi.
Sasa kwamba vikosi vya Wakurdi vimelazimika kurudi kutoka miji ya kaskazini yenye mafuta, Nozhin anaona wazi hatari ya utawala mpya, ambao pia unapokea msaada kutoka Uturuki.
"Tunawajua watu hawa walioko madarakani Syria sasa. Tunawajua nchi na nguvu zinazowaunga mkono, na wao si waungaji mkono wa Wakurdi. Hawatupendi. Huo ndiyo wasiwasi mkubwa sasa hivi."
Pia kuna wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuibuka tena kwa ISIS endapo viongozi wa sasa wa Syria wataishia kushindwa kuhakikisha utulivu nchini.
Yuko katika mawasiliano ya kila mara na familia yake, ambao bado wanaishi katika maeneo ya Wakurdi.
"Wao wanahisi wasiwasi na hofu kuhusu siku zijazo kama tunavyohisi sisi," asema Nozhin.
"Tunawapigia simu kila mara na kila wakati tunahisi wasiwasi iwapo hawajibu simu kwa haraka. Ni hali isiyo na uhakika, iliyojaa mashaka na wasiwasi, na hakuna anayeweza kujua kitakachotokea siku zijazo."
Hali hii ya kutokuwa na uhakika na wasiwasi inazidishwa na mabadiliko ya sera ya hifadhi barani Ulaya.
Msichana huyu, akiwa na uzoefu wa kuishi na ulemavu tangu kuzaliwa na kushuhudia madhila ya vita, akisafiri kutoka Mashariki ya Kati hadi Ulaya hadi kufika mahali salama, bado anaendelea kutunza matumaini katika moyo wake.
Katika takribani muongo mmoja niliomjua, matumaini yake hayajawahi kupotea. Kuanguka kwa Assad kumedhihirisha imani yake zaidi kwa Syria na watu wake.
"Wengi wanangojea tu Syria ianguke katika shimo la kutisha, zito," anasema.
"Sisi si watu wa chuki, uovu, au wivu, na hatuna dhamira ya kuangamiza wengine. Sisi ni watu tuliokulia kwa hofu ya kila mmoja, lakini msingi wetu ni upendo, kukubali, na uvumilivu."
"Tunaweza na tutakuwa nchi bora, ardhi ya upendo, uvumilivu, na amani, siyo mzozo, machafuko, hofu, na uharibifu."
Mioyo mingi nchini Syria na katika nchi nyingine inatumaini kuwa maneno yake yatatimia.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Asha Juma












