'Hakuna aliyelala nchini Syria jana usiku' - jinsi habari za kupinduliwa kwa Assad zilivyoenea

Mkazi wa Damascus Rania Kataf alisema "hatimaye alivuta pumzi"

Chanzo cha picha, Rania Kataf

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakazi wa Damascus wameelezea namna walivyokuwa wakisubiri kwa wasiwasi habari juu ya kile kinachotokea katika mji mkuu wa Syria usiku kucha.

Baada ya saa kadhaa za ripoti za waasi kukaribia zaidi na zaidi, vikosi vilitangaza kuwa Damascus ni "huru" mbali na mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad mapema Jumapili.

Video ambazo hazijathibitishwa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha watu wakishangilia barabarani na kuwakaribisha wapiganaji hao waasi, pamoja na wafungwa wakiachiliwa huru kutoka katika gereza la Saydnaya.

"Hakuna mtu aliyelala nchini Syria jana usiku... hakuna Msyria aliye ng'ambo aliyelala," Rania Kataf, ambaye anaendesha ukurasa wa Facebook wa Humans of Damascus, alisema.

"Jamii nzima ilikuwa imeshikilia simu zao wakisubiri habari za mwisho.

"Ninahisije? Kuzidiwa .. Sote tunahisi kama tumekuwa chini ya maji, kwa kweli, kwa miaka kumi na tatu, na sote tulipumua tu.

"Na ninajua kwamba kuna watu wengi ambao ni wakubwa zaidi kuliko mimi ambao wamepitia mengi sana."

Alisema alikuwa na "hisia mchanganyiko" tangu mashambulizi ya makundi ya waasi yaanze, lakini hakuwa na hofu tena.

Wasyria wakisherehekea katika Uwanja wa Umayyad mjini Damascus

Chanzo cha picha, Getty Images

Danny Makki, mwandishi wa habari anayeishi Damascus, alielezea matukio ya Jumapili asubuhi huko Umayyad, ambapo ni nyumbani kwa mashirika muhimu ya serikali, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Ulinzi na Vikosi vya Wanajeshi vya Syria.

"Watu walikuwa wakifyatua risasi hewani, watu walikuwa wakicheza, kupiga picha na kulia," alisema.

"Nilizungumza na askari kutoka kwa wanamgambo. Mmoja alisema alikuwa akijiandaa kwa hili kwa muda mrefu.

"Hakuwa akishiriki katika mashambulizi ya Aleppo, lakini alipoona waasi wakiwasili viunga vya Damascus, ndipo alipochukua silaha."

Alisema baadhi ya wapiganaji hao waasi walikuwa wakitumia magari ya jeshi la Syria yaliyotelekezwa.

"Nilipokuwa nikiendesha gari kuzunguka Damascus, niliona jeshi la Syria likitembea wakiwa katika nguo za kiraia barabarani, bila kujua wapi pa kwenda."

Ingawa kuna sherehe, alisema wasiwasi wa watu ulikuwa usalama, na "kuhakikisha kuwa hakuna mapigano ndani ya safu ya upinzani."

Danny Makki

Chanzo cha picha, Danny Makki

Mkazi mwingine wa Damascus, ambaye aliomba kutotajwa jina, aliambia BBC: "Kwa mara ya kwanza kabisa, kuna hisia za kweli za uhuru."

"Tunachohisi kinafanana sana na tulivyohisi wakati wa mapinduzi yalipoanza mwaka wa 2011. Huu ni mwendelezo wa ndoto ambayo ilikuwa imeanza mwaka huo."

Alisema kuwa Wasyria wanahisi hofu na wasiwasi juu ya siku zijazo, lakini "leo, watu wote wa Syria watasherehekea tu."

Yazan Al Amari anasafiri kutoka Deraa kwenda Damascus leo ili kusherehekea

Chanzo cha picha, Yazan Al Amari

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kusini zaidi, Yazan Al Amari ana duka dogo la simu katika mji wa Deraa, ambapo wanamgambo wa kiraia wanaoshirikiana na Hayat Tahrir al-Sham tayari wamedhibiti.

Aliiambia BBC kwamba anasafiri na marafiki zake hadi mji mkuu wa Syria leo kusherehekea.

"Tulipoamka na kuona habari hiyo, mwanzoni hatukuweza kuelewa au kufahamu kabisa. Watu waliogopa sana uvumi.

"Lakini tulipogundua kuwa ni kweli, tulipanda magari yetu, na sasa tuko njiani kuelekea Damascus kusherehekea."

"Watu walihisi kama wako ndotoni," alisema.

"Uliweza kuona watu wakilia. Tuliogopa sana mpaka leo."

Al Amari anasema hii ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi kuweza kuzungumza kwa uhuru.

"Nilikuwa siwezi kuondoka katika mji wangu mdogo au kutembea kwa uhuru hata kidogo. Lakini sasa, ninaweza kwenda popote ninapotaka," alisema.

Lakini watu wengi wanaogopa mambo yasiyojulikana ya wakati ujao.

Mwanamume Msyria huko London aliniambia juu ya hofu kwa familia yake inayoishi katika eneo la pwani la Syria.

"Sisi ni Wakristo wa Othodoksi ya Mashariki, ninaogopa familia yangu itachinjwa," mtu huyo, ambaye aliomba kutotajwa jina, alisema.

"Kila mtu yuko katika hali ya hofu. Wanajaribu kutafuta njia ya kutoka nje ya nchi."

Familia yake inafanya maandalizi ya kuondoka Syria, lakini mipaka ya Lebanon na Jordan imefungwa.

"Mifuko imejaa, tunasubiri tu kuona kama viwanja vya ndege vitafungua safari ya ndege kwenda nchi yoyote jirani. Au kama mipaka ya nchi kavu itaruhusu makundi yoyote maalum kuondoka Syria," alisema.

"Ni ukweli kwamba watu wanasherehekea kwa hofu," alisema.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga