Je, Uturuki na Urusi zinaushughulikiaje mgogoro wa Syria, na tofauti zao ni zipi?

Pamoja na mashambulizi ya hivi karibuni nchini Syria ambayo yamesababisha hasara kubwa kwa utawala wa Assad, macho yote yamegeukia tena harakati za kidiplomasia kati ya Ankara na Moscow.
Nchi hizo mbili, ambazo zilikuwa na jukumu muhimu katika kila kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria vilivyoanza mwaka 2011, ziko katika nafasi zinazopingana katika mgogoro wa hivi karibuni na kushikilia sera za kila mmoja kuwajibika na kuongezeka kwa mvutano.
Mkutano kati ya rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais Recep Tayyip Erdoğan tarehe 3 Disemba ulikuwa muhimu katika suala la kufunua mitazamo ya pande zote.
Putin alimtaka Erdogan kuachana na makundi ya kigaidi yanayoshambulia utawala wa Assad.
Erdogan, kwa upande mwingine, anamtarajia Putin aihimize Damascus zaidi kupata suluhu la kisiasa.
Hali ya utulivu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria tangu mwaka 2020 ilivurugika kufuatia mashambulizi yaliyoanzishwa na makundi yanayoongozwa na Hayat Tahrir al-Sham (HTS) dhidi ya vikosi vya serikali, hatua ambayo imeanzisha enzi mpya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wakati HTS iliuteka mji wa Aleppo kwa muda mfupi, jeshi la taifa la Syria linaloungwa mkono na Uturuki (SNA) lilichukua hatua dhidi ya uwepo wa vikosi vya ulinzi wa watu (YPG) huko Tel Rifaat na Manbij.
Uhasama huo kati ya Ankara na Moscow, ambazo zina uwepo mkubwa wa kijeshi na ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo, umewahusisha tena katika mzozo huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mawasiliano ya kwanza kati ya nchi hizo mbili yalifanyika kati ya mawaziri wa mambo ya nje Hakan Fidan na Sergey Lavrov mnamo Novemba 30.
Mkutano wa viongozi hao ulifanyika Desemba 3.
Taarifa zilizoandikwa baada ya mkutano wa Erdoğan na Putin zilikuwa muhimu katika kufichua tathmini na matarajio tofauti ya vyama kuhusu mchakato huo.
Ankara: Serikali inapaswa kuzungumza na upinzani
Taarifa iliyotolewa na Uturuki, ilielezwa kwamba Ankara inaunga mkono uadilifu wa eneo la Syria lakini "utawala wa Syria lazima ushiriki katika mchakato wa kupata suluhisho la kisiasa" ili kuwezesha suluhu la kudumu na la haki.
Umoja wa Mataifa ulizindua mchakato wa Geneva, uliowezesha kuwaleta pamoja watawala na upinzani nchini Syria ili kupata suluhisho la kisiasa kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama nambari 2254, lakini hawakuweza kupigia hatua kutokana na kizuizi cha utawala wa Damascus.
Uturuki na nchi nyingine za Magharibi zinawatuhumu washirika wa Urusi na Iran kwa kutoishinikiza serikali ya Assad au hata kutafuta suluhisho la kisiasa.
Ankara pia inaishutumu Moscow na Tehran kwa kutounga mkono juhudi za muda mrefu za Uturuki za kurejesha uhusiano na Syria.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, ilibainika kuwa Erdoğan alifikisha ujumbe kwa Putin kwamba "suala muhimu zaidi katika muktadha wa hali ya hivi karibuni nchini Syria ni kwamba raia hawadhuriwi."
Inadhaniwa kuwa Erdogan alikuwa akizungumzia mashambulizi yaliyofanywa na Urusi na Syria katika mkoa wa Idlib katika wiki za hivi karibuni alipotoa kauli hizi.
Vyanzo vya usalama mjini Ankara vinasema kuwa HTS na makundi mengine ya upinzani yalianzisha operesheni ya sasa kujibu mashambulizi ya hivi karibuni.
Kremlin: Uvamizi wa 'kigaidi' lazima ukome
Kauli ya Kremlin kuhusu mkutano kati ya viongozi hao wawili ilikuwa na lugha tofauti.
Ilibainika kuwa Putin alifikisha ujumbe kwa Erdogan kwamba "uvamizi wa kigaidi" ulioanzishwa dhidi ya serikali ya Syria lazima usimame mara moja na utawala lazima uungwe mkono ili kuanzisha utaratibu wa kikatiba na utulivu nchini kote.
Taarifa hiyo ilisema Putin alielezea matarajio yake kwamba Ankara itatumia ushawishi wake katika eneo hilo kufikia malengo hayo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji wa wizara ya mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova pia alisema katika mkutano na waandishi wa habari mnamo tarehe 4 Disemba kwamba Urusi inaunga mkono kwa nguvu zote vita vya uongozi wa Syria dhidi ya "makundi ya kigaidi."
Zakharova alidai kuwa makundi ya upinzani yalipokea ndege zisizo na rubani na msaada wa mafunzo kutoka kwa mataifa ya kigeni.
Licha ya tathmini tofauti, msisitizo wa kawaida wa Ankara na Moscow ulikuwa kuendelea na uratibu na diplomasia kati ya washirika wa mchakato wa Astana na ushiriki wa Tehran.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu wanatarajiwa kukutana pembezoni mwa mkutano wa Doha nchini Qatar tarehe 7 na 8 Disemba, lakini mkutano huo bado haujathibitishwa.
Ni majanga gani yaliyotokea katika siku za nyuma?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uturuki na Urusi wameendeleza uhusiano wa kiuchumi na nishati tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Hatahivyo, katika miaka 10 iliyopita, wameingia katika mgogoro mara nyingi kutokana na matatizo ya kijiografia, hasa yale yanayotokana na Syria.
Uturuki imeyaunga mkono makundi ya upinzani dhidi ya utawala wa Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Urusi, kwa upande mwingine, imeelekeza uzito wake wa kijeshi kwenye eneo la Syria tangu mwaka 2015 na kuzuia kupinduliwa kwa serikali ya Damascus.
Tarehe 24 Novemba , 2015, Uturuki ilidungua ndege ya kivita ya Urusi kwa misingi kwamba ilikiuka anga ya Uturuki jambo lililosababisha mgogoro usio wa kawaida kati ya Ankara na Moscow.
Mgogoro huo ulisitishwa mnamo mwezi Juni 2016 kutokana na mazungumzo ya siri ya diplomasia kati ya vyama.
Hata hivyo, mauaji ya balozi wa Urusi nchini Uturuki Andrey Karlov mjini Ankara katika siku za mwisho za mwaka huo huo yalirudisha umakini kwa nchi hizo mbili.
Mchakato wa Astana ulianzaje?
Uturuki na Urusi wameshiriki katika ushirikiano mkubwa ili kupunguza ghasia na vifo vya raia nchini Syria baada ya kipindi cha mvutano.
Walichukua hatua ya kwanza katika mchakato huu mwishoni mwa mwaka 2016, wakati wa kuzingirwa kwa serikali ya Aleppo, wakati wa mchakato wa kuanzisha ukanda salama kwa ajili ya kuwahamisha wapinzani na raia kutoka mji huo.
Mchakato huu baadaye ulibadilishwa jina na kuwa mchakato wa Astana mwaka 2017, ukishirikisha Iran.
Ulinzi wa pamoja wa doria kati ya Uturuki na Urusi iliyofanyika Idlib mwaka 2020.
Mbali na mikutano iliyofanyika katika mji mkuu wa Kazakhistan wa Astana, viongozi wa nchi hizo tatu waliandaa mikutano ya kupokezana na walitaka kuratibu maendeleo ya kisiasa na kijeshi kuhusu Syria.
Hatahivyo, jaribio la Urusi la kuivamia Ukraine mnamo mwezi Februari, 2022 lilisababisha Syria kunaswa zaidi katika ajenda ya Moscow.
Makubaliano ya Idlib
Hali nyingine iliyoileta Uturuki na Urusi katika mgogoro mkubwa ile iliyoukumba mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa Syria.
Kutokana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2016, maeneo manne ya kupunguza mapigano yalitangazwa nchini Syria, lakini kutokana na mashambulizi ya Urusi na Syria, mikoa mitatu ilitekwa na makundi ya upinzani katika maeneo hayo yalielekezwa Idlib.
Miongoni mwa makundi hayo ni mashirika kama vile HTS na Al Nusra, ambayo yalitangaza kuwa yamejitenga na al-Qaeda.
Ingawa Uturuki na Urusi walikubaliana kuanzisha eneo salama lisilo na silaha huko Idlib mwaka 2018, mashambulizi ya utawala wa Damascus katika eneo hili hayakutoa matokeo yaliyohitajika.
Kifo cha wanajeshi 34 wa Uturuki kilichotokana na shambulio la anga yaliyofanywa na jeshi la anga la Urusi katika eneo hilo mwezi Februari 2020, ambayo yaliupiga msafara wa kijeshi wa Uturuki, lilisababisha mvutano mpya katika eneo hilo.
Kufuatia mvutano huu, Erdogan na Putin walikutana tena na kutangaza makubaliano mapya halali kuanzia Machi 6, 2020.
Hali ya kutokuwa na mzozo, ambayo ilifikiwa na makubaliano kwamba vikosi vya Uturuki na Urusi vitaanzisha doria za pamoja katika njia salama ambazo wangeanzisha, iliendelea hadi tarehe 27, Novemba 2024.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi kuhaririwa na Seif Abdalla












