Kwanini Uturuki inataka kujiunga na muungano wa kiuchumi unaoongozwa na Urusi na China?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Selin Girit and Mahmut Hamsici
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 6
"Rais wetu amesema wazi, Uturuki inataka kushiriki katika majukwaa yote muhimu, ikiwa ni pamoja na BRICS," alisema Omer Celik, msemaji wa chama tawala cha Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Lakini hakuthibitisha ripoti za ikiwa Ankara imetuma maombi rasmi ya uanachama, badala yake akasema kuna "mchakato unaoendelea."
BRICS inatarajiwa kujadili kuchukua wanachama wapya katika mkutano ujao katika mji wa magharibi mwa Urusi wa Kazan tarehe 22-24 Oktoba.
Ikiwa Uturuki itakubali kujiunga, itakuwa nchi ya kwanza mwanachama wa NATO kuwa mwanachama wa muungano wa kiuchumi wa nchi zisizo za Magharibi, unaoongozwa na Urusi na China.
Kerim Has, mtaalam wa uhusiano wa Uturuki na Urusi, anasema Uturuki inahitaji uwekezaji wa kigeni na imelazimika kubadilisha uhusiano wake kutokana na tatizo kubwa la kiuchumi ambalo nchi hiyo imekuwa ikilikabili.
"Ikiwa uchumi wa Uturuki utaanguka, itakuwa hasara kwa benki za Ulaya, kwa sababu uchumi wa Uturuki unategemea sana benki hizo," anasema. "Karibu nusu ya biashara ya Uturuki inafanya na nchi za EU."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Baraza la Umoja wa Ulaya, EU ni mshirika mkuu wa biashara wa Uturuki, ikifanya naye 31.8% ya biashara zake. Mwaka 2022, thamani jumla ya biashara kati ya EU na Uturuki ilifikia pauni bilioni 200.
Hii ndio sababu, anasema, nchi za Ulaya zinafumbia macho Uturuki kutoshiriki katika vikwazo dhidi ya Urusi kufuatia vita vyake vya Ukraine.
"Nchi za Magharibi zinaivumilia Uturuki kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na Urusi, na nchi nyingine za BRICS," anasema Has.
"Ikiwa Uturuki kama mshirika wa NATO itakuwa mwanachama wa BRICS, moja ya majukumu yake yatakuwa ni kupunguza sauti na kauli za upinzani dhidi ya Magharibi katika kambi hiyo.
"Jukumu la Uturuki katika BRICS kwa mtazamo usiosemwa wa Marekani na Uingereza, litakuwa ni kuizuia BRICS kuwa mpinzani wa Magharibi."
BRICS ni nini?
Hapo awali iliitwa BRIC, ni kambi ya nchi zinazoendelea kiuchumi, ilianzishwa 2006 na Brazil, Urusi, India na China. Afrika Kusini ilijiunga mwaka 2010, na kambi hiyo ilibadilisha jina na kuwa BRICS.
BRICS iliundwa ili kuzileta pamoja nchi muhimu zaidi zinazoendelea duniani, ili kutoa changamoto kwa nguvu za kisiasa na kiuchumi za mataifa tajiri zaidi ya Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi.
Muungano huo umekuwa ukijipanua katika miaka ya hivi karibuni na sasa unajumuisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Saudi Arabia imesema inafikiria kujiunga, na Azerbaijan imetuma maombi rasmi.
Ripoti zilizoibuka kwenye shirika la habari la Bloomberg Jumatatu iliyopita, zinasema Uturuki pia iliomba rasmi kujiunga na BRICS miezi kadhaa iliyopita.
Rais Erdogan alionyesha nia ya kutaka kuwa mwanachama wa BRICS mapema mwaka 2018, katika mkutano wa 10 wa kilele wa BRICS huko Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwanini Uturuki inataka kujiunga?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rais Erdogan amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili, na anakerwa na ukosefu wa kusonga mbele kwa maombi ya nchi hiyo ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, amekuwa akisema Uturuki inahitaji kuboresha uhusiano wake na Mashariki na Magharibi "kwa wakati mmoja."
"Sio lazima kuchagua kati ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO)," Erdogan alisema akizungumzia shirika la ushirikiano wa kikanda linaloongozwa na China na Urusi. "Kinyume chake tunapaswa kukuza uhusiano wetu na mashirika haya na mashirika mengine."
Mwaka 2022, biashara ya Uturuki na Urusi ilifikia 11% ya biashara yake yote, na biashara na China ilikuwa ni 7.2%.
Kerim Has anaamini kuwa uanachama wa Uturuki katika BRICS utaungwa mkono na Urusi.
"Kipaumbele namba moja cha Urusi ni kuuweka uchumi wake imara ili kuendeleza vita nchini Ukraine, ili kuhakikisha uchumi wa Urusi hauporomoki chini ya vikwazo vya Magharibi," anasema.
"Kwa hivyo, Moscow inapenda kuiweka Uturuki karibu. Wana mahusiano mengi sana, kuanzia nishati hadi biashara na utalii. Pia, kwa Moscow, ni vizuri kuonyesha kwamba ina uwezo wa kukuza uhusiano wa karibu na wenye manufaa na nchi ya NATO.
Kuongezeka kwa hamu ya Uturuki kujiunga na BRICS, SCO, na jumuiya nyingine haipaswi kuonekana kama mabadiliko ya Uturuki kuipa mgongo Ulaya, anasema Yusuf Can kutoka Kituo cha Wilson, taasisi ya fikra tunduizi nchini Marekani.
"NATO inaweza kufaidika kwa kuwa na mshirika anayehusika katika jumuiya hii," anasema.
Mgogoro wa Kichumi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mgogoro wa kiuchumi wa Uturuki unaozidi kuongezeka na utegemezi wake kwa uwekezaji wa kigeni na madeni, zinaonekana kuwa ni sababu za nia ya Ankara kutaka kujiunga BRICS.
Uturuki ni nchi ya 17 kwa uchumi mkubwa duniani kwa mujibu wa takwimu za IMF za 2023.
Kura zote za maoni za hivi karibuni nchini humo zinaonyesha kupanda kwa gharama ya maisha ndio mzigo mkuu kwa Waturuki.
Rais Recep Tayyip Erdogan aliweka shinikizo kwa benki kuu ya Uturuki kuweka gharama za kukopa kuwa chini. Kwa maoni yake, viwango vya riba vilikuwa ndio sababu ya mfumuko wa bei.
Lakini amebadilisha sera ya uchumi mwaka uliopita. Kwa mfano, bodi mpya ya benki kuu ya Uturuki ilipandisha viwango vya riba kutoka 8.5% hadi 50% katika miezi tisa.
Ingawa Waziri wa Hazina na Fedha wa sasa Mehmet Simsek anadai “mpango huo mpya unafanya kazi vizuri, na mfumuko mbaya wa bei umepungua,” ila watu wengi bado wana shaka juu ya siku zijazo.
"Tangu Simsek ateuliwe, mfumuko wa bei umeongezeka maradufu, na pesa ya lira ya Uturuki imeshuka kwa kiasi kikubwa, licha ya viwango vya riba kuongezeka kutoka 8% hadi 50%.," anasema Dk. Umit Akcay kutoka Berlin School of Economics and Law.
Haijulikani ni nini kitatokea kwa uchumi wa Uturuki katika siku zijazo, wataalamu wanasema.
“Hata hivyo, kushuka kwa mfumuko wa bei haimaanishi kuwa mzozo wa gharama ya maisha umekwisha. Bila nyongeza ya kweli ya mishahara au msaada mkubwa kwa tabaka la chini, shida hii itaendelea.
Ikiwa ombi la Uturuki la kujiunga na BRICS litafaulu, linaweza kuwa na athari chanya ya kuleta utulivu katika uchumi wake.
Lakini pia kuna uwezekano kwamba lengo kuu la Uturuki kutaka kujiunga BRICS liko zaidi katika uwanja wa kisiasa kuliko kiuchumi.
Imetafsriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












