Kwa nini uchaguzi wa Uturuki unafuatiliwa kwa karibu barani Afrika

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Marina Daras
    • Nafasi, BBC World Service

Ushawishi wa Uturuki barani Afrika umekuwa ukiongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na yeyote atakayeshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais Jumapili itabidi afikirie wapi pa kuupeleka uhusiano huo.

Tangu Recep Tayyip Erdogan achukue mamlaka nchini Uturuki miongo miwili iliyopita, kwanza kama waziri mkuu kisha rais, amekuwa na hamu kubwa barani Afrika.

Aliona fursa za kiuchumi, kijeshi na kidiplomasia.

Uhusiano kati ya Ankara na bara la Afrika huenda ukaimarika iwapo tu rais atachaguliwa tena.

Mpinzani wake, kiongozi wa Chama cha Republican Kemal Kilicdaroglu, macho yake yameelekezwa Ulaya na Magharibi na kuna uwezekano mdogo wa kuifanya Afrika kuwa kipaumbele.

"Bw Kilicdaroglu alisisitiza haja ya kurekebisha uhusiano na nchi za Magharibi na akasema atajaribu kufufua mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya," anasema Serkan Demirtas, mkuu wa ofisi ya Ankara ya Hurriyet Daily News na mtaalamu wa sera za kigeni wa Uturuki.

"Katika mahojiano, hata alisema kwamba hatua ya digrii 180 itatarajiwa linapokuja suala la sera ya kigeni. Lakini alikosa kueleza kwa kina jinsi mabadiliko haya yataathiri uhusiano na nchi muhimu duniani."

Hata hivyo, Ece Goksedef kutoka Idhaa ya Uturuki ya BBC anadokeza kwamba sera ya kigeni ya Uturuki kuelekea bara hilo itachukua muda kurekebisha, kwa hivyo hakuna uwezekano itabadilika sana kutokana na msingi imara wa uhusiano huu mpya.

Uhusiano wa Uturuki na Afrika ulianza lini?

Mbegu za ushirikiano ulioimarishwa kati ya Afrika na Uturuki zilipandwa wakati wa Erdogan kama waziri mkuu, ambao ulianza 2003.

Bw Erdogan aliona manufaa ya kiuchumi.

"Mapema miaka ya 2000, uchumi wa Uturuki ulishuhudia kuendelea kukua na ulikuwa ukitafuta masoko mapya," anasema mtaalamu wa sera za kigeni Bw Demirtas.

"Soko tofauti lenye zaidi ya nchi 50 na zaidi ya watu bilioni 1.2 linatoa fursa nzuri kwa wauzaji bidhaa nje wa Uturuki na wafanyabiashara."

Biashara ya kila mwaka ya Uturuki na bara hilo iliongezeka kutoka $5.4bn (£4.4bn) hadi $34.5bn kati ya 2003 na 2021, kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, inayoongozwa na kemikali, chuma na nafaka.

Waturuki walikuwa na shauku ya kusisitiza kwamba huo haukuwa uhusiano wa kinyonyaji na mwaka 2013, Waziri Mkuu Erdogan alipofanya ziara nchini Gabon alisema kwamba "Afrika ni ya Waafrika, hatuko hapa kwa ajili ya dhahabu yao".

Vipi kuhusu maslahi ya kijeshi?

Mikataba ya silaha - pia inajulikana kama "diplomasia ya ndege zisizo na rubani" - ni njia ya wazi ya kutengeneza pesa kwa Ankara.

Baada ya kuthibitisha thamani yake nchini Libya, Armenia na Ukraine, ndege isiyo na rubani ya Bayraktar TB-2 sasa inawasilishwa kama silaha kamili ya kulenga vikundi vya kijihadi vinavyojificha katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.

Machi hii, dazeni ya ndege zisizo na rubani ziliwasili kwenye lami ya uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

Mbele ya kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goïta na wanadiplomasia wachache wa Uturuki, waziri wa ulinzi wa Mali alikaribisha kundi hilo jipya la silaha akisema kwamba "zinaweza kusaidia kufanya ufyatuaji wa risasi na mashambulizi ya anga kuwa sahihi zaidi".

Mbali na Mali, Uturuki imeuza ndege zisizo na rubani kwa Burkina Faso, Togo na Niger - mataifa manne ya Saheli yana hamu ya kupambana na ongezeko la wanamgambo wa Kiislamu katika eneo hilo.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uturuki pia imefanya mazungumzo na Benin, ambayo hadi hivi majuzi ilikuwa haijaguswa na waasi wa Kiislamu lakini sasa inashuhudia ongezeko la mashambulizi na uvamizi katika ardhi yake.

Morocco, Tunisia, Ethiopia, Nigeria na Somalia pia zote ni wateja wanaojulikana wa ndege zisizo na rubani zinazotengenezwa na Uturuki.

Ingawa China bado inatawala soko hili katika bara, Uturuki inatoa chaguo nafuu zaidi na muda mfupi wa kusubiri .

Uturuki pia inatoa vifaa vingine vya kijeshi.

Magari ya kivita na na vifaa vya kutegua mabomu ya ardhini , mifumo ya uchunguzi na upelelezi na bunduki pia vimekuwa sehemu ya mikataba mingi ya silaha ambayo Uturuki imetia saini hivi karibuni na nchi za Afrika.

Kwa jumla, mataifa 30 katika bara hilo yana aina fulani ya makubaliano yanayohusiana na usalama na Uturuki - 21 kati yao yaliidhinishwa mnamo 2017 - kulingana na ripoti ya Taasisi ya Kimataifa na Masuala ya Usalama ya Ujerumani.

Pamoja na kuwekeza kikamilifu katika mipango ya kukabiliana na ugaidi, Ankara pia imeongeza misaada yake ya kibinadamu kwa nchi kama Nigeria, Mauritania na Niger.

Diplomasia imebadilika vipi?

Nje ya mikataba ya kijeshi na kibiashara, Bw Erdogan amekuwa akifanya kazi sana katika kuimarisha uhusiano wa Uturuki na Afrika.

Mnamo 2005, Uturuki ilikuwa mwanachama waangalizi wa Umoja wa Afrika kabla ya kuinuliwa hadi nafasi ya mshirika wa kimkakati miaka mitatu baadaye.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Uturuki inasema kumekuwa na ziara rasmi 50 kwa takriban mataifa 30 ya Afrika tangu mwaka 2014.

Rais Erdogan ameitembelea Senegal mara nne - mara nyingi zaidi kama vile amekuwa China au Ujerumani.

Na huko anakokwenda, wajumbe wa wafanyabiashara huenda pamoja naye, na kusababisha miradi muhimu ya miundombinu kutolewa kwa makampuni ya Uturuki, kama bwawa la kuogelea la Dakar Olympic au Uwanja wa Kigali nchini Rwanda, uwanja mkubwa zaidi wa Afrika Mashariki.

Hivi majuzi, Uganda imesitisha mkataba wake na kampuni ya Uchina inayosimamia ujenzi wa reli hadi mpaka wa Kenya na inafikiria kufanya makubaliano na kampuni ya Uturuki badala yake.

Mikutano ya kilele kati ya Uturuki na Afrika daima imekuwa ikihudhuriwa vyema na wakuu wa nchi za bara.

Labda ukweli unaoelezea zaidi ni idadi ya balozi za Uturuki kwenye bara. Ina 44 kote barani Afrika - sawa na Amerika ikiwa na 49 na Ufaransa, 46, ingawa kwa kiasi fulani nyuma ya 53 ya Uchina.

Kitu gani kingine ambacho Uturuki inatoa kwa Afrika?

Uturuki pia imejaribu kuongeza nguvu zake laini katika bara hilo.

Upanuzi wa hivi karibuni wa nyayo zake bila shaka ni uzinduzi wa TRT Afrika.

Shirika la utangazaji la umma la Uturuki la TRT liliazimia kujiondoa kwa washindani kadhaa katika kanda ili kuzindua jukwaa hili la habari za kidijitali katika Kifaransa, Kiingereza, Kiswahili na Kihausa.

Lakini pengine athari kubwa zaidi za kitamaduni zinatokana na michezo ya kuigiza ya Kituruki, ambayo imekuwa maarufu katika nchi kadhaa za Afrika - kutoka Ethiopia hadi Senegal.

Kipengele kisichojulikana sana cha uhusiano na Afrika ni nishati.

Baada ya ziara za rais, kampuni ya Uturuki, Karpowership, imetia saini mikataba ya mitambo yake ya kuzalisha umeme iliyo kwenye meli kusambaza umeme kwa nchi kadhaa za Afrika Magharibi, na wiki iliyopita Afrika Kusini. Hizi huwekwa nje ya pwani na kuchomekwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa, usambazaji kati ya MW 30 na 470 MW kwa kila chombo.

Ikiwa Erdogan atashinda, anatarajiwa kujenga uhusiano huu. Ushindi wa Kilicdaroglu huenda ukaishusha Afrika katika orodha ya vipaumbele lakini hakuna uwezekano wa kufanya lolote kuhatarisha uhusiano wa kina na wenye faida kubwa.