Kwa nini kuna maandamano Iran na Trump amesema Marekani itafanya nini?

k
    • Author, Raffi Berg, David Gritten, Tom McArthur & Shayan Sardarizadeh
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mamia ya watu inaaminika wameuawa nchini Iran huku maandamano makubwa yakihatarisha mustakabali wa utawala wa sasa. Maelfu yameripotiwa kukamatwa.

Donald Trump pia ametishia mara kwa mara kuchukua hatua za kijeshi ikiwa vikosi vya usalama vitawaua waandamanaji.

Desemba 28, wafanyabiashara wa maduka waliandamana katika mitaa ya Tehran kuelezea hasira zao kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Iran, rial, dhidi ya dola ya Marekani katika soko.

Rial imeshuka hadi kiwango cha chini kabisa katika mwaka uliopita na mfumuko wa bei umepanda hadi 40% jambo ambalo limesababisha kupanda kwa bei kwa bidhaa za kila siku kama vile mafuta ya kupikia na nyama.

Vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran vimeumiza uchumi ambao pia umedhoofishwa na usimamizi mbaya wa serikali na ufisadi.

Wanafunzi wa vyuo vikuu walijiunga na maandamano hayo na yakaanza kuenea katika miji mingine. Kuna wito wa mabadiliko ya kisiasa, huku umati wa watu ukisikia mara kwa mara wakiimba dhidi ya Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.

Maneno ya kumuunga mkono Reza Pahlavi, mwana wa aliyekuwa shah wa Iran anayeishi uhamishoni, yameenea zaidi mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati maelfu ya watu walipokusanyika mitaani Tehran na miji mingine mikubwa.

Kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu la Iran lenye makao yake Marekani, maandamano yametokea katika miji na vijiji 186 katika majimbo yote 31 ya Iran tangu kuanza kwa machafuko hayo. Halijatoa makadirio ya idadi ya watu walioshiriki, ingawa limesema zaidi ya waandamanaji 10,000 wamekamatwa.

Serikali imejibu nini?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Serikali inapambana vikali na waandamanaji. Silaha mbalimbali, kuanzia maji ya kuwasha hadi risasi za moto, zimeripotiwa kutumika dhidi ya waandamanaji na kusababisha vifo. Madaktari wanasema hospitali "zimejaa" maiti na majeruhi.

Mkuu wa mahakama wa Iran ameapa kutoa adhabu "ya haraka na kali," akiitaka mahakama kutoonyesha huruma kwa "waandamanaji."

Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake Marekani linaripoti karibu waandamanaji 500 na maafisa 48 wa usalama wameuawa tangu maandamano yaanze. Miongoni mwa wale wanaoripotiwa kuuawa ni Amir Mohammad Koohkan, 26, ambaye alikuwa kocha wa mpira wa miguu na Aminian, 23, mwanafunzi wa Kikurdi.

BBC Verify imepitia kipande cha video kutoka katika mazishi huko Tehran kinachoonyesha waombolezaji wakiimba "Kifo kwa Khamenei" - Kiongozi Mkuu wa Iran.

Nchi imegubikwa na kukatika kwa intaneti, jambo ambalo wataalamu wanasema lilianza Alhamisi. Mtandao wa setilaiti wa Elon Musk wa Starlink unatajwa kama njia moja ya kutoa intaneti, lakini watumiaji wameonywa intaneti hiyo inaweza kufuatiliwa na mamlaka.

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alidai kuwa vikosi vya usalama vimedhibiti kikamilifu maandamano ya kupinga serikali. Kulingana na televisheni ya serikali, wafuasi wa serikali waliandamana mitaani kwa mshikamano kulaani "vitendo vya kigaidi" vya hivi karibuni.

Serikali pia imetangaza siku tatu za maombolezo kwa kile ilichokiita "mashahidi" waliouawa katika "vita vya kitaifa dhidi ya Marekani na Israel" - Tehran inasema nchi hizo zinachochea machafuko.

Nani anaisimamia Iran?

O

Chanzo cha picha, Ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Irani/WANA (Shirika la Habari la Asia Magharibi)

Maelezo ya picha, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei

Iran, taifa kubwa katika Mashariki ya Kati, linatawaliwa na Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei. Ni taifa lenye idadi ya watu wapatao milioni 90.

Iran ina bunge lakini wengi wa wabunge ni wa tiifu kwa Khamenei, ambaye ana usemi wa mwisho kuhusu masuala muhimu zaidi - ikiwa ni pamoja na jinsi ya kushughulikia maandamano.

Iran ilikuwa mshirika muhimu wa Magharibi hadi mwaka 1979, wakati mfalme Shah alipopinduliwa katika mapinduzi ya Kiislamu na utawala wa Kiislamu wa Shia ukachukua madaraka. Tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa misingi ya kidini. Kukosoa utawala huo hakukubaliki, na uhuru binafsi wa watu umepungua sana.

Sheria inayowataka wanawake kuvaa hijabu imekuwa chanzo mvutano - na ilichochea maandamano makubwa 2022. Iran ina moja ya viwango vya juu zaidi vya watu kunyongwa duniani na imeorodheshwa mara kwa mara miongoni mwa nchi wavunjifu wakubwa wa haki za binadamu.

Nchi za Magharibi zimekuwa na uhusiano mbaya na Iran tangu mapinduzi ya kiislamu, huku Marekani na Iran zikiwa wapinzani wakubwa.

Washington inaishutumu Iran kwa kuvuruga utulivu wa Mashariki ya Kati, hasa kupitia uungaji mkono wake kwa makundi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na Hamas huko Gaza, Hezbollah huko Lebanon na Houthi huko Yemen.

Kwa upande wake Iran inaishutumu Marekani kwa kuingilia siasa za eneo hilo.

Marekani imekuwa mpinzani mkubwa wa mpango wa nyuklia wa Iran, ikidai Iran inalenga kutengeneza bomu la nyuklia - jambo ambalo Iran inakanusha.

Marekani ililipua maeneo ya nyuklia ya Iran mwaka jana , huku vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran kutokana na shughuli zake za nyuklia vikiathiri pakubwa uchumi wa Iran.

Donald Trump amesema nini?

K

Chanzo cha picha, Getty Images

Donald Trump na utawala wake wametishia kuingilia kati kijeshi Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili usiku, rais wa Marekani alisema Tehran imempigia simu ili "kujadiliana" lakini alionya kwamba huenda akachukua hatua kabla ya mkutano kuanzishwa.

Afisa mmoja wa Marekani ameiambia CBS kwamba Trump amepewa taarifa kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

Trump bado hajafafanua mipango ya Marekani, lakini siku ya Jumapili alisema viongozi wa Iran "wanataka kujadiliana," kwa sababu "wamechoka kushambuliwa na Marekani."

Jarida la Wall Street liliripoti kwamba hatua zingine za Trump zinaweza kujumuisha kuunga mkono sauti za kupinga serikali ya Iran kupitia mitandao, kuweka vikwazo zaidi, au kutumia hujuma za mtandao dhidi ya jeshi la Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alionya kwamba nchi hiyo iko tayari kwa vita iwapo itashambuliwa.

Ugumu wa kupata taarifa

Iran inazuia mashirika ya habari ya kimataifa kama vile BBC kufanya kazi ndani ya nchi hiyo. Shirika la utangazaji la serikali na mashirika mengine hufuata miongozo mikali ya serikali.

Waandishi wa habari huru wa Iran mara kwa mara hukabiliwa na mateso na unyanyasaji kwa kuripoti taarifa za kukosoa serikali.

Intaneti pia imezuiliwa, huku majukwaa mengi makubwa ya mitandao ya kijamii na mashirika ya habari ya Magharibi yakipigwa marufuku. Hata hivyo, Wairani ni hodari katika kutumia mbinu mbalimbali kama vile VPN ili kuepuka vikwazo hivi.

Lakini kukatika kwa umeme kunakoendelea kunawatenga Wairani na ulimwengu wa nje. Mawasiliano ya simu hayafanyi kazi.

Hadi kukatika kwa umeme kulipoanza Alhamisi jioni, mamia ya video kutoka katika maandamano hayo - ziliwekwa kwenye mitandao ya kijamii. Wairani walizungumza na waandishi wa habari kutoka nchi za kigeni ili kutoa maelezo ya maandamano hayo.

Tangu wakati huo, mtiririko wa video umepungua sana, na imekuwa vigumu sana kuzungumza na watu ndani ya Iran.

Wairani wachache wanatumia intaneti ya Starlink ya SpaceX, na wamekuwa wakichapisha video chache juu ya kile kinachoendelea.

Baadhi pia wameweza kutumia mitandao ya kijamii ili kutoa maoni yao kwa waandishi wa habari, marafiki na wanafamilia wanaoishi nje ya nchi.