Marekani yawaomba raia wake wote kuondoka Iran mara moja
Mashirika ya ndege yanaendelea kupunguza au kufuta safari za ndege kwenda na kutoka Iran, huku huduma kadhaa zikisimamishwa hadi Ijumaa.
Muhtasari
- Maelfu ya wafuasi wa Museveni wakusanyika Kampala kwa kampeni ya mwisho
- Somaliland yalaani hatua ya Somalia kufuta mikataba ya ushirikiano na Falme za Kiarabu
- Niger yawafutia leseni ya madereva wa malori waliokataa kusafirisha mafuta Mali
- Marekani yawaomba raia wake wote kuondoka Iran mara moja
- Kuwarejesha wakimbizi wa Burundi kutoka Tanzania ni kuweka maisha hatarini - MSF
- Trump awatoza ushuru wanaofanya biashara na Iran
- Marufuku kubeba Bendera ya Taifa kwenye vituo vya kupiga kura - Tume ya uchaguzi Uganda
- Trump kukutana na kiongozi wa upinzani wa Venezuela Ikulu
- Kundi linaloungwa mkono na Israeli lamuua afisa mkuu wa polisi wa Hamas Gaza
- Wairani watumia Starlink ya Musk kuepuka kuminywa kwa intaneti, vyanzo vinasema
- Makombora ya Urusi yashambulia Ukraine, mmoja auawa, maafisa wa wanasema
- Urusi yasema raia wa Greenland wanaweza kupiga kura kujiunga nao
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Uchaguzi Uganda 2026: Mamlaka ya mawasiliano yaamuru mtandao wa intaneti kuzimwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) imeagiza kusitishwa kwa huduma za intaneti katika kipindi cha uchaguzi uliopangwa Alhamisi, Januari 15.
Kulingana na taarifa iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, na ripoti kutoka kwa vyombo vya habari kadhaa vya ndani Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) imesema agizo hilo litaanza kutekelezwa kuanzia saa kumi na mbili jioni Jumanne, Januari 13, 2026, ikinukuu "pendekezo" kutoka kwa Kamati ya Usalama ya Mashirika ya Kimataifa.
Kufikia sasa, watumiaji wa data ya kawaida ya simu za mkononi wanasema hawawezi kufikia mtandao, huku baadhi ya maeneo ya biashara, kama vile hoteli kubwa, yanaendelea kupokea huduma hiyo.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa UCC imewaagiza watoa huduma kuzima kwa muda ufikiaji wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, huduma za data za simu za mkononi na njia nyinginezo za mawasiliano zinazotegemea intaneti kwa muda wote wa zoezi la kupiga kura na baada ya uchaguzi.
Tume pia sema uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia mamlaka yake chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Uganda, ambayo inaipa mamlaka ya kudhibiti huduma za mawasiliano kwa maslahi ya usalama wa taifa na usalama wa umma.
Mashirika kadhaa, hata hivyo, hayakujumuishwa kwenye agizo hilo, wafanyakazi walioidhinishwa wataruhusiwa kufikia intaneti katika kipindi hicho kupitia njia salama, iliyoidhinishwa kam vile VPN
UCC iimewashauri Waganda kufanya mipango mbadala ya mawasiliano katika kipindi kuzimwa kwa intaneti na kuwahakikishia kwamba huduma zitarejeshwa mara tume itakapojiridhisha kuwa mchakato wa uchaguzi umekamilika kwa usalama.
Hii sio mara ya kwanza kwa Uganda kudhibiti mtandao wa mawasiliano wakati wa uchaguzi, jambo ambalo mamlaka inadai kuwa ni muhimu ili kuzuia kuenea kwa taarifa ghushi na machafuko yanayoweza kutokea licha ya kukosoaji na mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za kidijitali.
Uchaguzi wa Januari 15 unatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu shughuli za kisiasa na usalama zikiongezeka kote nchini huku Rais aliye madarakani Yoweri Museveni akipigania kuchaguliwa tena baada ya kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 40.
Soma zaidi:
Maelfu ya wafuasi wa Museveni wakusanyika Kampala kwa kampeni ya mwisho

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Uganda Yoweri Museveni anafanya mkutano wake wa mwisho wa kampeni katika mji mkuu, Kampala, huku kampeni zikikamilika kabla ya uchaguzi wa Alhamisi.
Usalama umeimarishwa kote jijini, huku wanajeshi na magari ya kivita yakiegeshwa kwenye barabara kuu.
Kiongozi wa upinzani Bobi Wine, ambaye anagombea urais kwa mara ya pili, alifanya mkutano wake wa mwisho siku ya Jumatatu.
Maelfu ya wafuasi wa Rais Yoweri Museveni wanakusanyika katika Viwanja vya Sherehe za Kololo mjini Kampala huku kampeni za uchaguzi mkuu zikielekea ukingoni.
Bw Museveni, ambaye amekuwa mamlakani kwa takriban miongo minne, anaomba ridhaa ya mwisho kwa wapiga kura kabla ya uchaguzi wa Alhamisi.
Amesimamia mabadiliko ya katiba akiondoa ukomo wa muhula na umri.
Wachambuzi wanasema kushikilia kwake kwa uthabiti taasisi za serikali na vikosi vya usalama kunaacha nafasi ndogo ya matokeo ya kushangaza.
Mpinzani wake mkuu, kiongozi wa upinzani Bobi Wine, ameonya kuwa atapinga matokeo ikiwa wizi wa kura utashuhudiwa.
Hapo awali Umoja wa Mataifa umesema uchaguzi huo unafanyika katika hali ya wasiwasi ya kisiasa, inayoashiria kuzuiliwa kwa wafuasi wa upinzani.
Soma zaidi:
Somaliland yalaani hatua ya Somalia kufuta mikataba ya ushirikiano na Falme za Kiarabu
Somaliland imepinga uamuzi wa Somalia wa kufuta makubaliano na Falme za Kiarabu, ikisema Mogadishu haina mamlaka dhidi ya mikataba inayohusiana na Berbera.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Somaliland ilisema Somalia haina mamlaka ya kisheria au mamlaka ya kiutawala juu ya Berbera, ambayo ilielezea kama sehemu ya eneo huru la Somaliland.
Taarifa hiyo ilisema Somalia si mshirika wala mdhamini wa mikataba yoyote iliyohitimishwa na Somaliland, hivyo basi haina uhalali wa kisheria wa kusitisha au kufanyia marekebisho mikataba hiyo.
Ilisema mikataba yote kati ya Somaliland na UAE bado ni halali, na inawabana kikamilifu.
Somaliland pia iliisifu UAE kwa kile ilichoeleza kuwa michango ya muda mrefu katika maendeleo, utulivu, na ukuaji wa uchumi Somaliland na Pembe ya Afrika.
huku hayo yakijiri Puntland pia inasema serikali ya Somalia haina mamlaka ya kufuta mikataba iliyotiwa saini na utawala wa Puntland.
Katika taarifa yake, serikali ya Puntland ilisema makubaliano yanayohusiana na bandari ya Bosaso na ushirikiano wa kiusalama na UAE bado yanaendelea kutekelezwa.
Ilitaja vifungu vya katiba ya Puntland na katiba ya shirikisho ya muda, ikisema kuwa tawala za kikanda zina haki ya kushiriki mikataba ya maendeleo na usalama.
Soma zaidi:
Madereva wa malori wa Niger waliokataa kusafirisha mafuta Mali wafutiwa leseni

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Niger imefuta leseni za makumi ya waendeshaji huduma za usafiri na madereva kwa kukataa kupeleka mafuta katika taifa jirani la Mali ambako wanakabiliwa na tishio la kushambuliwa na wanamgambo wenye itikadi kali za kidini.
Washirika hao wa kundi la al-Qaeda waliweka kizuizi cha mafuta nchini Mali mnamo Septemba na kuanza kushambulia mgafari ya mafuta kwenye barabara kuu.
Nchi hiyo isiyo na bandari inategemea uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi na mwezi Julai ilikuwa imetia saini mkataba na Niger wa kusambaza lita milioni 85 za mafuta kwa muda wa miezi sita katika eneo lake kubwa la jangwa la kaskazini, ambako makundi mbalimbali ya wanamgambo yanaendesha shughuli zao.
Niger ni nchi inayozalisha mafuta na mshirika mkuu wa Mali - mataifa yote mawili yako chini tawala za kijeshi ambazo zinakabiliwa na ghasia za wanamgambo wa kijihadi.
Misafara ya malori ya mafuta kutoka Niger katika safari ya takribani kilomita 1,400 (maili 870) imekuwa ikabiliwa na mashambulizi ya wanamgambo licha ya ya kupewa ulinzi na jeshi.
Novemba mwaka jana, Niger ilisafirisha malori 82 za mafuta nchini Mali, ambazo zilisaidia kutuliza adha ya usambazaji wa nishati uliokumbwa na vizuizi vya hivi majuzi - kwani misafara ya mizigo iliyokuwa ikisafiri kutoka Senegal na Ivory Coast pia imeathirika.
Habari za hivi punde, Man Utd yafikia makubaliano ya kumteua Carrick kama meneja wa muda

Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester United imefikia makubaliano kimsingi ya kumteua Michael Carrick kama meneja wa muda.
Kiungo huyo wa zamani wa Man Utd na England anachukua nafasi ya Ruben Amorim aliyetimuliwa wiki iliyopita.
Carrick anatarajiwa kushikilia nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu.
Marekani yawaomba raia wake wote kuondoka Iran mara moja

Chanzo cha picha, Getty Images
Ubalozi wa Marekani nchini Iran siku ya Jumatatu umetoa taarifa mtandaoni ya onyo la usafiri ikiwataka raia wa Marekani kuondoka Iran mara moja huku machafuko yakiendelea kusambaa kote nchini humo.
"Raia wa Marekani wanapaswa kutarajia kuendelea kuminywa kwa intaneti, kupanga njia mbadala za mawasiliano, na, ikiwa ni salama kufanya hivyo, kufikiria kuondoka Iran kwa njia ya ardhini hadi Armenia au Uturuki," ilisema ubalozi huo mtandaoni katika taarifa kwenye tovuti yake.
Pia iliongeza kuwa raia wenye uraia mara mbili wa Marekani na Iran lazima waondoke Iran kwa pasipoti za Iran kwani serikali ya Iran haitambui uraia pacha.
"Raia wa Marekani wako katika hatari kubwa ya kuhojiwa, kukamatwa, na kuwekwa kizuizini nchini Iran," Taarifa hiyo ilisema.
Kulingana na taarifa hiyo, mashirika ya ndege yanaendelea kupunguza au kufuta safari za ndege kwenda na kutoka Iran, huku huduma kadhaa zikisimamishwa hadi Ijumaa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa muda mrefu imeweka kiwango cha 4 cha tahadhari ya "Usisafiri" kwa Iran, ikionya kwamba raia wa Marekani hawapaswi kusafiri eneo hilo kwa sababu yoyote na kwamba wale walio Iran wanapaswa kuondoka mara moja kutokana na hatari kubwa za kiusalama.
Mapema Jumatatu, katibu wa habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alisema diplomasia inasalia kuwa mbinu inayopendelewa zaidi na Marekani katika kushughulikia suala la Iran, ingawa utawala wa Trump haujaondoa uwezekano wa chaguzi za kijeshi kutakapokuwa na lazima ya kufanya hivyo.
Soma zaidi:
Kuwarejesha wakimbizi wa Burundi kutoka Tanzania ni kuweka maisha hatarini - MSF

Chanzo cha picha, AFP
Shirika la misaada la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) limeonya kwamba mipango ya kuwarejesha zaidi ya wakimbizi 50,000 wa Burundi kutoka kambi magharibi mwa Tanzania inaweza kusababisha mgogoro wa kibinadamu.
Mnamo Desemba 2025, serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa itaondoa hadhi ya wakimbizi kwa Warundi na kufunga kambi za wakimbizi nchini humo kabla ya Juni 2026.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, MSF ilisema mchakato wa kuwarejesha makwao lazima utangulize usalama, afya na utu, ikionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kunaweza kuweka maisha hatarini.
"Kanuni hiyo haina kujadiliwa: mchakato wa kurudi nyumbani haupaswi kamwe kuweka maisha hatarini," MSF lilisema.
MSF, ambayo imetoa huduma za afya katika Kambi ya Wakimbizi ya Nduta tangu 2015, ilisema wakimbizi wengi wana hali dhaifu za kiafya na wanakabiliwa na hatari kubwa ikiwa mchakato wa kurejeshwa nyumbani utaharakishwa au kutopewa usaidizi ipasavyo.
Kwa mujibu wa Idara ya Wakimbizi ya Tanzania, kufikia Desemba 2025 nchi hiyo ilikuwa ikipokea wakimbizi wapatao 238,956, wakiwemo Warundi 152,019, WaCongo 86,256 na wakimbizi 681 kutoka nchi nyingine.
Mashirika ya kibinadamu yamekuwa yakisisitiza kwa muda mrefu kwamba kurejea nyumbani kwa wakimbizi kuwe kwa hiari, salama na kuliko tayarishwa vyema, kulingana na viwango vya kimataifa.
Mamlaka za Tanzania na Burundi hazijajibu hadharani maonyo ya MSF.
Trump awatoza ushuru wanaofanya biashara na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatatu amesema ameweka ushuru wa 25% kwa bidhaa kutoka nchi zenye uhusiano wa kibiashara na Iran, hatua ambayo inaweza kuweka shinikizo kwa Tehran huku maandamano ya kupinga serikali yakiingia wiki ya tatu.
Trump alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba ushuru huo "ulianza kutekelezwa mara moja", bila kutoa maelezo ya kile kinachomaanisha "kufanya biashara" na Iran.
China ndiyo washirika wakubwa wa kibiashara wa Iran, ikifuatiwa na Iraq, Falme za Kiarabu, Uturuki na India.
Ushuru huo mpya unakuja baada ya Trump kutishia kuingilia kijeshi ikiwa Iran itawaua waandamanaji.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, alisema Jumatatu kwamba chaguzi za kijeshi ikiwemo mashambulizi ya angani bado "yanatathminiwa".
Pia unaweza kusoma:
Marufuku kubeba Bendera ya Taifa kwenye vituo vya kupiga kura - Tume ya uchaguzi Uganda

Chanzo cha picha, OTHER
Tume Huru ya Uchaguzi Uganda (EC) imepiga marufuku wapiga kura kubeba ama kupeperusha Bendera ya Taifa katika vituo vya kupiga kura ikionya dhidi ya nembo ya taifa kutumiwa kisiasa wakati wa zoezi la kupiga kura.
"Bendera ya Taifa ni ya Waganda wote. Sio nyenzo ya kufanya kampeni na haistahili kuletwa kwenye vituo vya kupiga kura," alisema Simon Byabakama, Jaji wa Mahakama ya rufaa ya Uganda.
Aliongeza kuwa matumizi ya Bendera ya Taifa yanadhibitwa na sheria inayopiga marufuku utumiaji wa Nembo za Taifa kwa madhumuni ya kisiasa na kibiashara bila idhini kutoka kwa Wizara ya Sheria na Masuala ya Katiba.
Aidha, Tume ya Uchaguzi pia ilipiga marufuku kuvaa tisheti zenye nembo ya chama, kubeba picha za wagombea au kuonyesha rangi za chama katika vituo vya kupiga kura.
"Vituo vya kupiga kura ni sehemu inayotakiwa kusalia kutoegemea upande wowote. Wapiga kura wanaombwa kuacha nyenzo yoyote yenye kuhusishwa na chama na picha za wagombea nyumbani," alisema Byabakama.
Hatua hii inawadia huku kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, akiwasihi wafuasi wake kubeba bendera ya taifa wakati wa kampeni kama ishara ya utaifa.
Raia wa Uganda watapiga kura Januari 15, 2026 kuchagua viongozi watakaohudumu madarakani kwa muhula mwingine.
Soma zaidi:
Trump kukutana na kiongozi wa upinzani wa Venezuela Ikulu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, María Corina Machado, atakutana na Rais Donald Trump siku ya Alhamisi, Ikulu ya Marekani imethibitisha.
Ziara hiyo inafanyika wiki chache tu baada ya Rais wa Venezuela Nicolás Maduro kukamatwa huko Caracas na vikosi vya Marekani. Lakini Trump alikataa kumuidhinisha Machado, ambaye harakati zake zilidai ushindi katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa wa 2024, kama kiongozi wake mpya.
Badala yake Marekani ilimuunga mkono Delcy Rodríguez, makamu wa rais wa zamani wa Maduro.
Machado alisema wiki iliyopita alisema anatumai kumshukuru Trump binafsi kwa hatua aliyochukua dhidi ya Maduro na angependa kumtunuku Tuzo ya Nobel.
Trump aliiita hatua hiyo "heshima kubwa", lakini Kamati ya Nobel baadaye ilifafanua kwamba haiwezi kukabidhiwa mtu mwingine.
Soma zaidi:
Kundi linaloungwa mkono na Israeli lamuua afisa mkuu wa polisi wa Hamas Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanamgambo wa Palestina wanaoungwa mkono na Israeli wamesema Jumatatu kwamba wamemuua afisa mkuu wa polisi wa Hamas kusini mwa Ukanda wa Gaza, tukio ambalo Hamas iliwalaumu "washirika wa Israeli."
Taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani inayoongozwa na Hamas ilisema watu wenye silaha walifyatua risasi kutoka kwenye gari lililokuwa likipita, na kumuua Mahmoud Al-Astal, mkuu wa kitengo cha polisi wa jinai huko Khan Younis, kusini mwa eneo hilo na kuelezea washambuliaji hao kama "washirika katika uvamizi huo".
Hussam Al-Astal, kiongozi wa kundi linalopinga Hamas lenye makao yake katika eneo lililo chini ya udhibiti wa Israeli mashariki mwa Khan Younis, alidai kuhusika na mauaji hayo katika video aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook.
"Kwa wale wanaoshirikiana na Hamas, hatima yenu ni kuuawa. Kifo kinawajia," alisema, akiwa amevalia sare nyeusi ya kijeshi na akiwa ameshika bunduki.
Reuters haikuweza kuthibitisha kwa uhuru mazingira ya shambulio hilo. Afisa wa kijeshi wa Israeli alisema jeshi halikujua kuhusu operesheni zozote katika eneo hilo.
Kuibuka kwa vikundi vya ndani vyenye silaha kupambana na Hamas kunaongeza shinikizo kwa Hamas kufikia umoja mjini Gaza, eneo lililosambaratishwa na vita vya miaka miwili.
Pia unaweza kusoma:
Wairani watumia Starlink ya Musk kuepuka kuminywa kwa intaneti, vyanzo vinasema

Chanzo cha picha, Netblocks
Baadhi ya Wairani bado wanatumia huduma ya intaneti ya setilaiti ya Elon Musk ya Starlink licha ya kukatizwa kwa mawasiliano kote nchini humo, watu watatu waliozungumza na Reuters ndani ya nchi walisema.
Mamlaka ya Iran katika siku za hivi karibuni imeanzisha msako mkali dhidi ya waandamanaji ikiwa ni pamoja na kufungwa karibu kabisa kwa huduma ya intaneti, ambayo hutolewa kupitia nyaya za fiber-optic na minara ya simu za mkononi.
Lakini Starlink, ambayo hutoa huduma yake moja kwa moja kutoka kwa maelfu ya satelaiti za obiti ya chini ya ardhi, bado inafanya kazi katika baadhi ya maeneo nchini Iran, licha ya kupigwa marufuku na mamlaka huko, watu watatu wanaotumia Starlink nchini humo waliiambia Reuters.
Mmoja wao, huko Magharibi mwa Iran, alisema anawajua watu kadhaa wanaotumia Starlink na kwamba watumiaji katika miji na miji ya mpakani hawakuathiriwa sana.
Alp Toker, mwanzilishi wa kikundi cha ufuatiliaji wa intaneti cha NetBlocks, alisema amesikia kutoka kwa watu katika eneo hilo kwamba bado kuna ufikiaji wa Starlink nchini Iran, ingawa huduma inaonekana kuwa dhaifu.
"Haiko vizuri, lakini bado inapatikana," alisema.
Pia unaweza kusoma:
Makombora ya Urusi yashambulia Ukraine, mmoja auawa, maafisa wa wanasema

Chanzo cha picha, EPA
Vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi katika miji miwili mikubwa zaidi ya Ukraine mapema Jumanne, maafisa wa Ukraine wamesema, na kumuua mtu mmoja katika mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv.
Mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, Tymur Tkachenko, alisema mji mkuu ulishambuliwa na makombora. Meya Vitali Klitschko alisema ulinzi wa anga ulikuwa ukiendeleza shughuli zake.
Walioshuhudia mlipuko huo walizungumza na shirika la Reuters, lakini hakukuwa na taarifa za haraka kuhusu majeruhi au uharibifu.
Huko Kharkiv, kilomita 30 (maili 18) kutoka mpakani na pia eneo ambalo ni shabaha ya mara kwa mara ya Urusi, Gavana wa Mkoa Oleh Syniehubov alisema mtu mmoja amefariki katika shambulizi lililotekelezwa nje kidogo ya jiji.
Mamlaka za eneo la Syniehubov ilisema watu watatu walijeruhiwa.
Soma zaidi:
Urusi yasema raia wa Greenland wanaweza kupiga kura kujiunga nao

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi Dmitry Medvedev amesema kuwa raia wa Greenland wanaweza kupiga kura kujiunga na Urusi ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump hatachukua hatua haraka ili kulinda kisiwa cha Aktiki, Interfax iliripoti Jumatatu.
"Trump anahitaji kuharakisha. Kulingana na taarifa ambazo hazijathibitishwa, ndani ya siku chache kunaweza kuwa na kura ya maoni ya ghafla, ambapo Greenland nzima yenye watu 55,000 inaweza kupiga kura ya kujiunga na Urusi," Interfax iliripoti, ikimnukuu Medvedev, rais wa zamani wa Urusi.
"Na kisha ndivyo ilivyo. Hakuna nyota mpya ndogo kwenye bendera (ya Marekani)."
Trump amefufua tena azma yake ya kuchukua udhibiti wa Greenland, eneo la Denmark linalojitawala, akisema Marekani inahitaji kumiliki eneo hilo ili kuizuia Urusi.
Rais wa Marekani amesema eneo lake na rasilimali zake zinaifanya Greenland kuwa muhimu kwa usalama wa taifa, na kusababisha pingamizi kali kutoka Denmark na Greenland.
Ingawa Urusi haidai kutaka Greenland, kwa muda mrefu imekuwa ikifuatilia jukumu la kimkakati la kisiwa hicho katika usalama wa Aktiki, kutokana na nafasi yake katika njia za Atlantiki Kaskazini na uwepo wa kituo kikuu cha kijeshi cha Marekani na kituo cha ufuatiliaji wa anga za juu.
Soma zaidi:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara, tarehe ni 13/01/2026.
