Israel yaitambua rasmi Somaliland kama taifa huru

Tangazo hilo linafuatia kutiwa saini kwa kile Israel ilichoeleza kuwa tamko la pamoja na Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Tunakomea hapo kwa sasa. Kwaheri.

  2. Israel yaitambua Somaliland kama taifa huru

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema Israel imeitambua rasmi Somaliland kama taifa huru, linalojitawala, katika kile ambacho kitakuwa ni mara ya kwanza kwa eneo hili linalotaka kujitenga na Somalia kutambuliwa na nchi yoyote.

    Tangazo hilo linafuatia kutiwa saini kwa kile Israel ilichoeleza kuwa tamko la pamoja na Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi.

    Bw Netanyahu alisema makubaliano hayo, yaliyotiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar na kiongozi wa Somaliland, yalifanywa "kwa maslahi ya azimio la Abraham", na kwamba Israel itachukua hatua haraka kupanua ushirikiano katika maeneo ikiwa ni pamoja na kilimo, afya, teknolojia na uchumi.

    Pia alisema amemwalika Rais Abdullahi kufanya ziara rasmi nchini Israel, huku akiishukuru wizara ya mambo ya nje ya Israel na idara za kijasusi kwa kuunga mkono hatua hiyo.

    Somaliland ilikaribisha tangazo hilo, na kuiita kuwa ni hatua ya kihistoria ambayo inaweza kufungua kile ilichoeleza kuwa sura mpya ya kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa.

    Somaliland ilijitangaza uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991 na imekuwa ikiendesha mambo yake yenyewe kwa miongo kadhaa.

    Lakini Somaliland haijatambuliwa kimataifa. Somalia inasema eneo hilo linasalia kuwa sehemu ya ardhi yake.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Thailand yashambulia kwa mabomu eneo la mpakani Cambodia

    Mapigano kati ya Thailand na Cambodia yalianza tena mapema mwezi huu

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Mapigano kati ya Thailand na Cambodia yalianza tena mapema mwezi huu

    Thailand imefanya mashambulizi ya anga katika eneo la mpakani linalozozaniwa na Cambodia siku ya Ijumaa, huku maafisa wa pande zote mbili wakiendelea na mazungumzo kusitisha mapigano

    Jeshi la anga la Thailand limesema limeshambulia "kambi yakijeshi" ya Cambodia baada ya raia kuondoka katika eneo hilo.

    Wizara ya ulinzi ya Cambodia inaishutumu Thailand kwa "mashambulizi ya kiholela" dhidi ya makazi ya raia na kujeruhi watu kadhaa.

    Mapigano yalizuka tena mapema mwezi huu baada ya kusitishwa kwa mapigano mwezi Julai kufuatia siku tano za makabiliano makali ya mpakani.

    Takriban watu 41 wameuawa na karibu milioni moja kukimbia makazi yao tangu uhasama huo uanze tena.

    Nchi zote mbili zimelaumiana kwa kuvunjika kwa makubaliano hayo.

  4. Watu wawili wauawa katika shambulio la kuchomwa kisu Israel

    .

    Chanzo cha picha, Magen Dovid Adom

    Watu wawili wameuawa katika kile polisi wanasema ni "shambulio la kigaidi" kaskazini mwa Israel.

    Polisi wanasema mshambuliaji huyo alimvamia mtu aliyekuwa akitembea kando ya barabara katika mji wa mashariki wa Beit Shean, na kumgonga kwa gari kabla ya kumchoma kisu mwanamke karibu na Ein Harod, takriban 12.5km magharib mwa mji huoi.

    Wanasema mshambuliaji huyo alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na raia waliokuwa na hasira nje ya mji wa Afula.

    Waziri wa ulinzi wa Israel amesema mshukiwa huyo alitoka katika kijiji cha Qabatiya, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

    Huduma ya dharura ya Israel ya Magen David Adom ilisema mzee wa miaka 68 aliuawa na mvulana wa miaka 16 alijeruhiwa katika shambulio hilo huko Beit Shean.

    Ilisema mwathiriwa aliyechomwa kisu huko Ein Harod alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 18.

  5. Serikali ya Ethiopia yashtakiwa kwa kuwatelekeza wakimbizi

    ,

    Chanzo cha picha, EPA

    Human Rights First, shirika la kutetea haki za binadamu nchini Ethiopia, limefungua kesi dhidi ya Baraza la Mawaziri la serikali ya Muungano, Wizara ya Amani, na serikali za kikanda za Tigray, Amhara, na Oromia.

    Shirika hilo linawashutumu kwa kushindwa kuwarejesha wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 1.5 walio chini ya utawala wao kwenye makazi yao.

    Katika kesi yake iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Ethiopia, shirika hilo linaonyesha kuwa katika eneo la Tigray pekee, zaidi ya wakimbizi milioni moja wa ndani wamesalia bila makazi kutoka eneo la Tigray magharibi kufuatia kuzuka kwa vita vya Tigray mnamo Novemba 4, 2020.

    Shirika hilo lilibainisha zaidi kwamba katika eneo la Amhara, zaidi ya wakimbizi nusu milioni waliokimbia kutoka eneo la Oromia katika mji wa Debre kwa sasa wanaishi katika mji wa Berhan.

    Huko Oromia kwenyewe, takriban wakimbizi 85,000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi wanaishi katika makazi ya muda.

    Human Rights First pia inazishutumu mamlaka za kitaifa na kikanda kwa kupuuza wajibu wao wa kuwawezesha wakimbizi hao kurudi salama makwao, na kuwaacha wakiteseka kutokana na matatizo mengi ya kijamii.

    Kulingana na shirika hilo, makazi hayo ya muda hayana maji ya kutosha, chakula, vyoo, elimu na vituo vya afya, hali ambayo inahatarisha maisha ya wakimbizi hao.

  6. Putin adokeza Urusi iko tayari kubadilishana maeneo katika makubaliano ya Ukraine – Kommersant

    Rais Vladmir Putin

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais Vladmir Putin

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amedokeza kuwa nchi yake inaweza kuwa tayari kubadilishana baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya Urusi nchini Ukraine, lakini akasisitiza kuwa anataka eneo lote la Donbas, kwa mujibu wa gazeti la Kommersant.

    Mwandishi wa masuala ya Kremlin wa Kommersant, Andrei Kolesnikov, alisema Putin aliwaeleza wafanyabiashara wakuu wa Urusi mpango huo katika kikao cha faragha cha usiku wa manane kilichofanyika Kremlin tarehe 24 Desemba.

    “Vladimir Putin alisisitiza kuwa upande wa Urusi bado uko tayari kufuata makubaliano aliyoyapendekeza Anchorage. Kwa maneno mengine, ‘Donbas ni yetu,’” gazeti hilo liliripoti.

    Kwa mujibu wa maelezo hayo, Putin anataka kudhibiti Donbas yote, lakini nje ya eneo hilo, uwezekano wa kubadilishana sehemu ya maeneo kati ya pande husika haujaondolewa.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema katika taarifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa na ofisi yake Jumatano kuwa ujumbe wa Ukraine na Marekani ulikaribia kukamilisha mpango wa vipengele 20 baada ya mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini Miami.

    Hata hivyo, alisema pande hizo mbili hazijaafikia mwafaka kuhusu madai ya Ukraine kukabidhi maeneo ya Donbas ambayo bado inayadhibiti, wala kuhusu hatima ya kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na majeshi ya Urusi.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameahidi mara kadhaa kumaliza mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

    Mjumbe wake, Steve Witkoff, pamoja na mkwe wake Jared Kushner, wamekuwa wakifanya mazungumzo na Urusi, Ukraine na mataifa ya Ulaya.

    Maelezo kamili ya mapendekezo ya Marekani bado hayajawekwa wazi, ingawa maafisa wa Urusi wamekuwa wakirejelea mara kwa mara kile wanachokiita “makubaliano ya awali” yaliyodaiwa kufikiwa kati ya Putin na Trump katika mkutano wa kilele uliofanyika Anchorage, Alaska, mwezi Agosti.

    Urusi yadai Donbas Kwa mujibu wa makadirio ya Urusi, nchi hiyo inadhibiti Crimea yote iliyoiteka mwaka 2014, takribani asilimia 90 ya Donbas, asilimia 75 ya mikoa ya Zaporizhzhia na Kherson, pamoja na maeneo madogo katika mikoa ya Kharkiv, Sumy, Mykolaiv na Dnipropetrovsk.

    Soma pia:

  7. Chukwueze wa Nigeria ataka AFCON iheshimiwe sawa na Kombe la Dunia

    Mnigeria anayetaka kuwa kama Arjen Robben

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mnigeria anayetaka kuwa kama Arjen Robben

    Mshambuliaji wa Nigeria, Samuel Chukwueze, ametoa wito wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kupewa heshima sawa na Kombe la Dunia.

    Awali, AFCON ya mwaka huu ilipangwa kuchezwa majira ya joto, lakini baadaye ikaahirishwa hadi Desemba 21 hadi Januari 18.

    Ratiba hiyo imezinyima klabu kubwa za Ulaya huduma za wachezaji wao muhimu katika kipindi nyeti cha msimu wa ligi za nyumbani.

    “Kila mchezaji anatamani kushiriki AFCON. Ni moja ya mashindano bora kabisa duniani,” Chukwueze alisema katika mahojiano na Sports TV.

    “AFCON inapaswa kuheshimiwa kwa namna ileile inayoheshimiwa Michuano ya Ulaya au Kombe la Dunia.”

    Winga wa Fulham anatarajiwa kukosa mechi sita za klabu yake iwapo Nigeria itafanikiwa kufuzu hadi hatua ya 16 bora.

    “Tunaelewa kuwa mashindano haya yaliwekwa katika kipindi kisicho sahihi cha mwaka, lakini yanapokuita lazima uende,” alisema. “Huna chaguo. Klabu haiwezi kukuzuia, na hakuna anayepaswa kuyadhalilisha mashindano ya AFCON. Ndiyo, ratiba si nzuri, lakini kusema si mashindano makubwa au bora haikubaliki.”

    Chukweze aliisaidia Nigeria kuanza vyema mashindano hayo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania katika Kundi C, kabla ya kukutana na Tunisia katika mchezo wao wa pili siku ya Jumamosi.

    Soma pia:

  8. Meli iliyobeba mafuta ya magendo imekamatwa Ghuba, Iran inasema

    Iran imekamata meli ya mafuta ya kigeni karibu na kisiwa cha Qeshm cha Iran katika Ghuba, ikisema ilikuwa imebeba lita milioni 4 za mafuta yaliyoingizwa kimagendo, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Ijumaa.

    Mamlaka haikutaja jina la chombo hicho au kufichua uraia wake. Walisema wafanyakazi 16 wa kigeni walikuwa wamekamatwa kwa mashtaka ya jinai. Televisheni ya Taifa ilisema meli hiyo ya mafuta ilikamatwa Jumatano.

    Tovuti za habari za Iran zilichapisha video na picha za kile walichosema ni meli ya mafuta iliyokamatwa.

    Iran ilisema wiki iliyopita kwamba imekamata meli nyingine ya kigeni iliyokuwa imebeba lita milioni 6 za kile ilichokielezea kama dizeli iliyosafirishwa kimagendo katika Ghuba ya Oman bila kutaja meli hiyo au uraia wake.

    Iran, ambayo ina baadhi ya bei za chini zaidi za mafuta duniani kutokana na ruzuku kubwa na kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu yake ya kitaifa, imekuwa ikitafuta kupunguza usafirishaji mkubwa wa mafuta kwa njia ya ardhini kwenda nchi jirani na kwa njia ya baharini kwenda nchi za Ghuba.

    Soma zaidi:

  9. Kim Jong Un wa Korea Kaskazini aashiria kuendelea kwa utengenezaji wa makombora miaka 5 ijayo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliashiria kwamba nchi itaendelea kutengeneza makombora katika miaka mitano ijayo, alipotembelea makampuni makubwa ya silaha katika robo ya mwisho ya 2025, vyombo vya habari vya serikali KCNA vilisema Ijumaa.

    Kim alisema "sekta ya uzalishaji wa makombora nchini ni muhimu sana katika kuimarisha mbinu za kuzuia vita," kulingana na KCNA.

    Kim aliidhinisha rasimu ya hati za uboreshaji wa makampuni makubwa ya silaha ili ziwasilishwe kwa mkutano mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka wa 2026, KCNA ilisema, ambao utaweka mpango wa maendeleo kwa Korea Kaskazini kwa miaka mitano ijayo.

    Ripoti ya KCNA inafuatia ufichuzi wa Alhamisi wa Kim akisimamia ujenzi wa manowari ya nyuklia yenye uzito wa tani 8,700 akiwa na binti yake, mrithi mtarajiwa, na majaribio ya makombora ya masafa marefu.

    Soma zaidi:

  10. Shughuli ya kuhesabu kura kuanza leo - Tume ya Uchaguzi Somalia

    .

    Chanzo cha picha, Tume ya Uchaguzi

    Tume ya Uchaguzi nchini Somalia imetangaza kwamba shughuli ya kuhesabu kura itaanza mapema leo asubuhi baada ya vituo vya kupigia kura katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kufungwa hapo jana jioni.

    Hii ilikuwa ni siku ya kwanza ya kihistoria ya uchaguzi wa baraza la mitaa katika zaidi ya miaka 57.

    Uchaguzi huo ulifanyika chini ya ulinzi mkali huku jiji likiwa limefungiwa.

    Kulikuwa na wagombea elfu moja mia sita (1600) waliokuwa wakigombea viti mia tatu tisini (390) vya udiwani mjini Mogadishu.

    Ingawa vyama vya upinzani vilichagua kutoshiriki, waangalizi wa ndani wanasema kura ilikuwa huru, ya haki na ya amani. Hili linachukuliwa kuwa hatua muhimu kwa siasa za baadaye za nchi hiyo na kuashiria mwisho wa siasa za koo.

    Wachambuzi wanachukulia kura hii kama mtihani muhimu kwa uchaguzi wa rais mwaka ujao.

  11. Jaji azuia Marekani kumkamata mwanaharakati wa Uingereza anayepinga taarifa potofu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jaji wa Marekani siku ya Alhamisi alizuia kwa muda utawala wa Trump kumkamata mwanaharakati wa Uingereza anayepinga taarifa potofu Imran Ahmed, baada ya mkazi huyo wa kudumu wa Marekani kuwashtaki maafisa juu ya marufuku ya kuingia nchini humo kwa jukumu lake katika kile ambacho Marekani inadai ni udhibiti wa mtandaoni.

    Marekani iliweka marufuku ya viza Jumanne kwa Ahmed na wengine wanne kutoka Ulaya, akiwemo kamishna wa zamani wa EU wa Ufaransa Thierry Breton.

    Inawashutumu kwa kufanya kazi ya kudhibiti uhuru wa kujieleza au kulenga makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani kwa njia isiyo ya haki kwa kutumia kanuni kali.

    Ahmed anaishi New York na inaaminika kuwa pekee kati ya watano waliopo nchini humo kwa sasa.

    Soma zaidi:

  12. Mwendesha mashtaka Korea Kusini ataka Rais wa zamani Yoon afungwe miaka 10 jela

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Mwendesha mashtaka maalum wa Korea Kusini ameomba kifungo cha miaka 10 jela kwa Rais wa zamani Yoon Suk Yeol kwa mashtaka ikiwemo kuzuia majaribio ya kumkamata kufuatia jaribio lake lililoshindwa la kuweka sheria za kijeshi, Shirika la Habari la Yonhap liliripoti Ijumaa.

    Waendesha mashtaka wamemtuhumu rais aliyeondolewa madarakani kwa kujaribu kuwazuia wachunguzi wanaotaka kumkamata mnamo mwezi Januari kwa kujifungia ndani ya jengo la rais.

    Uamuzi wa kushtukiza wa Yoon Suk-yeol - alitangaza usiku katika televisheni ya kitaifa-akitaja hali ya sheria ya kijeshi na tishio kutoka korea Kaskazini.

    Lakini ikagunduliwa mapema kuwa nia ya tangazo hilo sio kutokana na tishio kutoka taifa jirani bali ni changamoto zake za kisiasa.

    Hata hivyo, iliwasukuma maelfu ya watu kufurika nje ya Bunge la taifa wakiandamana huku wabunge kutoka mrengo wa upinzni wakifika kwa haraka kuidhinisha kura ya dharura ya kuondoa agizo hilo.

    Amri ya hali ya hatari ya Yoon ilifuatiwa na kura ya kusimamishwa kazi ikafuata.

    Soma zaidi:

  13. Israel yasema imemuua mwanachama wa kikosi cha Iran nchini Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Israeli lilisema Alhamisi kwamba vikosi vyake vilimuua mwanachama wa Kikosi cha Quds cha Iran huko Lebanon ambaye alikuwa amehusika katika kupanga mashambulizi kutoka Syria na Lebanon.

    Jeshi lilimtambua mtu huyo kama Hussein Mahmoud Marshad al-Jawhari, likimtaja kuwa kiungo muhimu katika upangaji mikakati kwenye kwenye kikosi hicho nambari 840.

    Aliuawa katika eneo hilo au Ansariyeh, jeshi liliongeza katika taarifa, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu kifo chake.

    Al-Jawhari "iliendeshwa chini ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na ilihusika katika shughuli za kigaidi, zilizoongozwa na Iran, dhidi ya Taifa la Israeli na vikosi vyake vya usalama," ilisema taarifa hiyo.

    Israeli na Iran zilipigana vita vifupi mwezi Juni na jeshi la Israeli limekuwa likifanya mashambulizi nchini Lebanon karibu kila siku, katika kile linachosema ni juhudi za kuzuia kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran kujijenga upya.

    Mkataba wa kusitisha mapigano ulioungwa mkono na Marekani uliofikiwa mnamo Novemba 2024 ulimaliza mapigano ya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na Hezbollah na kuhitaji kupokonywa silaha kwa kundi hilo lenye nguvu, kuanzia katika maeneo ya kusini mwa mto karibu na Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mgombea anayeonekana kuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh arejea baada ya miaka 17 uhamishoni

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Tarique Rahman, mgombea anayeongoza kuwa waziri mkuu ajaye wa Bangladesh, amerejea nchini humo baada ya miaka 17 uhamishoni kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria.

    Rahman mwenye umri wa miaka 60 ndiye kiongozi mkuu wa familia yenye ushawishi mkubwa ya Zia na mtoto wa waziri mkuu wa zamani Khaleda Zia.

    Chama anachokiongoza, Chama cha Kizalendo cha Bangladesh (BNP), kinatazamia kurejea madarakani wakati Bangladesh itakapopiga kura mwaka mpya.

    Rahman, ambaye ameishi London tangu 2008, anatarajiwa kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo ikiwa chama cha BNP kitaibuka kuwa chama kikubwa zaidi.

    Kurejea kwa Rahman kunakuja baada ya Waziri Mkuu wa zamani Sheikh Hasina kuondolewa madarakani mwaka jana.

    Alikuwa chini ya uchunguzi mbalimbali wa jinai ulioanzishwa wakati chama chake cha Awami League kilipokuwa madarakani lakini aliondolewa mashtaka yote wakati utawala wake ulipoanguka.

    Hasina anaishi uhamishoni nchini India na chama chake hakiruhusiwi kushiriki katika uchaguzi huo, ambao wengi wanaona kuwa miongoni mwa uchaguzi muhimu zaidi katika historia ya Bangladesh.

    Soma zaidi:

  15. Zelensky apongeza 'mawazo mapya' baada ya mazungumzo na wajumbe wa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa tathmini chanya ya mazungumzo aliyofanya na wajumbe wa Marekani kuhusu jinsi ya kukomesha vita vya Urusi na Ukraine.

    Zelensky alisema mazungumzo ya njia ya simu ya Alhamisi na Steve Witkoff na Jared Kushner, yaliyodumu kwa karibu saa moja, yamechochea "mawazo mapya katika suala la miundo, mikutano, na ... jinsi ya kuleta amani ya kweli karibu".

    Amezungumza siku moja baada ya kutoa maelezo ya mpango mpya wa amani wenye vipengee 20, uliokubaliwa na wajumbe wa Marekani na Ukraine huko Florida.

    Zelensky alisema amewaomba Witkoff na Kushner kuwasilisha salamu za Krismasi kwa Rais wa Marekani Donald Trump "na familia nzima ya Trump".

    Urusi ilisema inachambua mapendekezo yaliyoletwa kutoka Marekani na mjumbe wa Urusi.

    Trump na wajumbe wake wamekuwa wakifanya mazungumzo na Ukraine na Urusi katika juhudi za kufikia makubaliano ya kukomesha vita hivyo vilivyoanzishwa na Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

    Inaonekana kumekuwa na maendeleo katika siku za hivi karibuni huku rais wa Ukraine akisifu "mawazo mazuri" yaliyotolewa na Witkoff na mkwewe Trump, Kushner.

    Zelensky alisema imekuwa "siku ya shughuli nyingi" kwa diplomasia ya nchi yake, alipozungumza kwa undani na wajumbe wa Marekani.

    Alikubali kwamba bado kuna "kinachohitajika kufanywa juu ya masuala nyeti" lakini akaongeza kwamba "pamoja na timu ya Marekani, tunaelewa jinsi ya kushughulikia haya yote".

    Soma zaidi:

  16. Msomaji wetu nakukaribisha katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 26/12/2025.