Sheikh Hasina: Waziri Mkuu wa Bangladesh aliyekimbia nchi ni nani?

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bi Hasina amesimamia maendeleo ya kiuchumi ya Bangladesh lakini wakosoaji wanasema pia amegeuka kuwa kiongozi wa wa kiimla
    • Author, Anbarasan Ethirajan & Tessa Wong
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina Wazed amejiuzulu na kuondoka nchini humo, baada ya wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi na kupelekea machafuko makubwa nchini kote.

Ripoti zinasema, bibi huyo mwenye umri wa miaka 76 alikimbia kwa helikopta Jumatatu hadi India, wakati maelfu ya waandamanaji wakivamia makazi yake katika mji mkuu wa Dhaka.

Hilo limemaliza utawala wa Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi nchini Bangladesh, kwa zaidi ya miaka 20 jumla.

Anasifiwa kwa kusimamia maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo ya Kusini mwa Asia, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni Bi Hasina ameshutumiwa kwa kugeuka kuwa kiongozi wa kiimla.

Pia unaweza kusoma

Aliingiaje madarakani?

Alizaliwa katika familia ya Kiislamu huko Bengal Mashariki mwaka 1947, Bi Hasina anatokea familia ya wanasiasa.

Baba yake Sheikh Mujibur Rahman, 'Baba wa Taifa' la Bangladesh, alikuwa kiongozi mzalendo aliyeongoza uhuru wa nchi hiyo kutoka Pakistan mwaka 1971 na kuwa rais wa kwanza.

Wakati huo, Bi Hasina alikuwa tayari anajuulikana kwa kuwa kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dhaka.

Rahman aliuawa pamoja na watu wengi wa familia yake katika mapinduzi ya kijeshi mwaka 1975. Bi Hasina na dadake mdogo ndio pekee walionusurika kwani walikuwa safarini nje ya nchi wakati huo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kuishi uhamishoni nchini India, Bi Hasina alirejea Bangladesh mwaka 1981 na kuwa kiongozi wa chama cha kisiasa cha babake, Awami League.

Aliungana na vyama vingine vya kisiasa kufanya maandamano mitaani ya kuunga mkono demokrasia, wakati wa utawala wa kijeshi wa Jenerali Hussain Muhammed Ershad. Vuguvugu hilo lilimfanya Bi Hasina akawa mwanasiasa wa kitaifa haraka sana.

Aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1996. Alipata sifa kwa kutia saini mkataba wa kugawana maji na India na mapatano ya amani na waasi kusini-mashariki mwa nchi hiyo.

Lakini wakati huo huo, serikali yake ilikosolewa kwa mikataba mingi ya kibiashara inayodaiwa kuwa ni mbovu na kwa kuwa mtiifu sana kwa India.

Baadaye alishindwa na mshirika wake wa zamani aliyegeuka kuwa mpinzani, Bi Begum Khaleda Zia wa chama cha Bangladesh Nationalist Party (BNP), mwaka 2001.

Wanawake wote wawili wametawala siasa za Bangladesh kwa zaidi ya miongo mitatu na wanajulikana kama "Begums wanaovutana." Begum ina maana ya mwanamke wa Kiislamu wa daraja la juu.

Waangalizi wanasema ushindani wao mkali umesababisha mlipuko wa mabomu katika mabasi, kutoweka na mauaji ya kiholela ya mara kwa mara.

Bi Hasina hatimaye alirejea mamlakani mwaka 2009 katika uchaguzi uliofanyika chini ya serikali ya mpito.

Akiwa mwathirika wa kisiasa, amekamatwa mara kadhaa akiwa upinzani na vile vile majaribio kadhaa ya kumuua, likiwemo moja la mwaka 2004 ambalo liliharibu usikivu wake. Pia amenusurika juhudi za kumlazimisha Kwenda uhamishoni kwa kesi nyingi mahakamani zinazomshutumu kwa ufisadi.

Mafanikio yake ni yapi?

Bangladesh, taifa lenye Waislamu wengi, lilikuwa mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani, limepata mafanikio makubwa ya kiuchumi chini ya uongozi wake tangu 2009.

Sasa ni moja wapo ya taifa lenye uchumi unaokua kwa kasi katika eneo hilo, hata kupita jirani yake mkubwa India.

Pato la taifa kwa mtu mmoja limeongezeka mara tatu katika muongo uliopita na Benki ya Dunia inakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 25 wameondokana na umaskini katika miaka 20 iliyopita.

Sehemu kubwa ya ukuaji huu imechochewa na sekta ya nguo, ambayo inachangia idadi kubwa ya mauzo ya nje ya nchi na sekta hiyo imekuwa katika miongo ya hivi karibuni, ikisambaza nguo katika masoko ya Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia.

Serikali ya Bi Hasina imefanya miradi mikubwa ya miundombinu kwa kutumia fedha za nchi hiyo, mikopo na usaidizi wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na daraja kubwa la Padma lililogharimu dola za kimarekani bilioni 2.9 huko Ganges.

Ni utata gani unaomzunguka?

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Akiunga mkono vuguvugu la kutaka demokrasia katika miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, Bi Hasina alikua mwanasiasa wa kitaifa.

Maandamano ya hivi karibuni yalikuwa changamoto kubwa kwa Bi Hasina tangu aingie madarakani. Yamekuja baada ya uchaguzi wa Januari 2024, uliokuwa na utata mkubwa, ambapo chama chake kilichaguliwa tena kwa muhula wa nne mfululizo.

Alikaidi na kulaani wito wa kumtaka ajiuzulu, na kuwaita maandamanaji kama "magaidi" na akaomba msaada "kuwakomesha magaidi hawa kwa udhibiti mkubwa."

Machafuko ya Dhaka na kwingineko yalianza kwa kutaka kukomeshwa kwa upendeleo katika kazi za utumishi wa umma lakini yakageuka kuwa harakati kubwa ya kupinga serikali.

Kufuatia janga uviko 19, Bangladesh imekuwa ikipambana na kuongezeka kwa gharama ya maisha. Mfumuko wa bei umeongezeka, akiba yake ya fedha za kigeni imeshuka kwa kasi kubwa, na deni lake la nje limeongezeka maradufu tangu 2016.

Wakosoaji wanalaumu usimamizi mbovu wa serikali ya Bi Hasina, na wanasema mafanikio ya awali ya kiuchumi ya Bangladesh yaliwasaidia tu wale walio karibu na chama cha Bi Hasina kutokana na ufisadi uliokithiri.

Pia wanasema maendeleo ya nchi hiyo yamekuja kwa gharama la kuharibu demokrasia na haki za binadamu, na wanadai utawala wa Bi Hasina umechukua hatua kandamizi na za kimabavu dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa, wakosoaji na vyombo vya habari.

Serikali na Bi Hasina wamekanusha madai hayo.

Lakini katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wengi kutoka chama cha BNP wamekamatwa, pamoja na maelfu ya wafuasi wao kufuatia maandamano dhidi ya serikali - hatua ya ajabu kwa kiongozi ambaye aliwahi kupigania demokrasia ya vyama vingi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yameelezea wasiwasi wao kuhusu mamia ya kesi za watu kutoweka na mauaji ya kiholela ya vikosi vya usalama tangu 2009.

Serikali ya Bi. Hasina inakanusha kutekeleza mambo hayo, lakini huzuia waandishi wa habari wa nje kuingia na kuchunguza madai hayo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa naYusuf Jumah