Waziri Mkuu wa Bangladesh ajiuzulu na kutoroka nchi huku waandamanaji wakivamia ikulu
Waziri Mkuu Sheikh Hasina wa Bangladesh amejiuzulu, mwandishi wa BBC nchini humo amethibitisha.
Muhtasari
- Olimpiki 2024:Biles asalia na fedha huku Andrade akishinda dhahabu
- Marekani hatimaye yaondoa wanajeshi wake nchini Niger
- Je, mkuu wa jeshi la Bangladesh aliyetangaza kujiuzulu kwa Sheikh Hasina ni nani?
- Katika Picha: Sherehe na uporaji katika mitaa ya Dhaka
- Amesikitika sana, asema mtoto wa Hasina
- Wito kwa wageni kuondoka Lebanon huku hofu ya vita ikiongezeka
- Mbappe kujiunga na Real hakutaathiri nafasi Bellingham - Ancelotti
- Kwanini Hasina amekimbilia India?
- Umati wa 'washangilia' mjini Dhaka
- Serikali ya mpito kuundwa Bangladesh - Mkuu wa jeshi
- Bangladesh: Matukio ya hivi punde kwa ufupi
- Bangladesh: Waandamanaji wapora makazi rasmi ya Waziri Mkuu
- Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina ajiuzulu
- Takribani watu 90 wauawa katika maandamano ya kuipinga serikali Bangladesh
- Waandamanaji wa Bangladesh wamtaka Waziri Mkuu aondoke madarakani
- Wageni watakiwa kuondoka Lebanon haraka wakati hofu ya vita ikiongezeka
- Wazambia waomboleza kifo cha mwimbaji wa nyimbo za injili makanisani na vilabuni
- Washington yawaambia washirika kwamba shambulio la Iran "linaweza kuanza ndani saa 24 hadi 48"
- Wagner: Mali yasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine
Moja kwa moja
Lizzy Masinga & Ambia Hirsi
Soko la hisa la Marekani lakumbwa na msukosuko

Chanzo cha picha, Getty Images
Masoko ya hisa ya Marekani yalishuka thamani siku ya Jumatatu baada ya bei ya hisa kuanguka barani Ulaya na Asia huku hofu ikiongezeka kwamba uchumi wa Marekani unaelekea kudorora.
Bei ya hisa ya kampuni ya teknolojia ya Nasdaq ilishuka kwa 6.3% zaidi baada ya kupungua kwa kasi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hisa za kampuni zingine kubwa nchini Marekani pia zilishuka thamani.
Masoko ya hisa mjini London, Paris na Frankfurt pia yalishuhudia biashara ya chini, huku masoko ya Asia yakiporomoka baada ya ya Nikkei 225 ya Japan kushuka thamani kwa 12.4% au pointi 4,451 katika anguko kubwa zaidi la pointi katika historia.
Katika siku chache zilizopita, masoko ya hisa ya kimataifa yamekuwa yakishuka thamani.
Skrini za biashara kote Marekani, Asia na, kwa kadiri fulani, Ulaya imejaa sana na kupepesa kwa nambari nyekundu zinazoelekea kusini.
Mabadiliko ya ghafla yanakuja huku hofu ikiongezeka kwamba uchumi wa Marekani - uchumi mkubwa zaidi duniani - unayumba.
Wataalamu wanasema sababu kuu ya hofu hii ni kwamba data za kazi za Marekani ya mwezi Julai, iliyotolewa Ijumaa, zilikuwa mbaya zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Olimpiki 2024: Biles asalia na medali ya fedha huku Andrade akishinda dhahabu

Chanzo cha picha, Getty Images
Simone Biles alikosa medali ya nne ya dhahabu ya Olimpiki ya Paris baada ya kutua kwa fujo na kusalia na nishani ya fedha sakafuni, Rebeca Andrade alipong'ara na kuchukuwa taji hilo.
Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 27 - ambaye alishinda timu, pande zote na dhahabu - alitua kwa miguu yote miwili nje ya eneo la sakafu mara mbili, hatua ambayo ilimnyima alama 0.300 kila moja, na alimalizia kwa alama 14.133 na kusalia na alama 0.033 nyuma ya Andrade.
Mmarekani Jordan Chiles alishinda nishani ya shaba baada ya kupata 13.766. Biles, ambaye kiwango chake cha uchezaji kilikuwa cha juu zaidi kuliko cha Mbrazili huyo, alilipa gharama ya makosa yake huku Andrade akitekeleza utaratibu wake wa kusisimua bila dosari.
Biles hapo awali alianguka kutoka kwenye boriti na kumaliza katika nafasi ya tano.
Andrade alivutia mashabiki waliofurika Uwanja wa Bercy Arena kwa jinsi alivyotumia miguu yake na utaratibu wake wa kupendeza, akinyakuwa alama ya mapema kama mchezaji wa pili wa mazoezi ya viungo.
Biles, ambaye alionekana kuchanganyikiwa na wakati wa fainali ya boriti, kuyumba licha ya kuanza vyema na kutua sakafuni kikamilifu.
Soma pia:
Marekani hatimaye yaondoa wanajeshi wake nchini Niger
Jeshi la Merekani limekamilisha mpango wa kuondoa nchini Niger.
Haya yanajiri zaidi ya mwaka mmoja baada ya utawala wa kijeshi mjini Niamey kuwataka waondoke.
Taarifa ya pamoja ya iliyotolewa na Pentagon na Wizara ya Ulinzi ya Niger siku ya Jumatatu ilisema, "shughuli ya kuondoa wa vikosi vya Marekani na mali zake kutoka kituo cha - Air Base 201 huko Agadez imekamilika."
Taarifa hiyo haikutoa maelezo yoyote kuhusu ni mali gani Marekani huenda imebakisha nchini humo.
Wanajeshi 200 walikuwa katika kituo cha ndege zisizo na rubani cha Agadez, kaskazini mwa nchi kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na wanamgabo wa kijihadi ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo hilo.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa wanajeshi wa Marekani wametoa mafunzo kwa vikosi vya Niger na kuunga mkono operesheni ya kupambana na ugaidi inayoongozwa na washirika dhidi ya makundi ya Islamic State na al Qaeda katika eneo hilo, katika muongo mmoja uliopita.
"Ushirikiano mzuri na mawasiliano kati ya vikosi vya jeshi vya Marekani na Niger vilihakikisha kuwa mauzo haya yamekamilika kabla ya muda uliopangwa na bila matatizo," ilisema.
Waangalizi wa usalama wanasema, kuondolewa kwa majeshi ya Marekani nchini humo, hatimaye kumefungua mlango kwa Urusi kuchukuwa fursa ya kusaidia Niger kuimarisha usalama wake.
Baada ya kupinduliwa kwa serikali ya kidemokrasia inayoongozwa na Mohamed Bazoum mwaka mmoja uliopita, viongozi wa serikali ya kijeshi waliiondoa Ufaransa koloni la zamani la nchi hiyo na kuelekea Urusi.
Watawala wa kijeshi nchini Niger walikuwa wametangulia kuondoa uanachama wa nchi hiyo katika jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS na kujiunga na muungano na nchi jirani za Burkina Faso na Mali - zote zikitawaliwa na wanajeshi.
Nchi za eneo la sahel zimeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya makundi ya kijihadi yenye uhusiano na al Qaeda na kundi la Islamic state.
Katika wiki za hivi karibuni, majirani hao watatu wamepoteza wanajeshi na raia kutokana na mashambulizi ya waasi na makundi ya kijihadi.
Nchini Mali, wanajeshi wanaoshukiwa kuwa mamluki wa wagner pia wameripotiwa kuuawa huku wengine kadhaa wakitekwa nyara katika mashambulizi mapya kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Algeria.
Maelezo zaidi:
Je, mkuu wa jeshi la Bangladesh aliyetangaza kujiuzulu kwa Sheikh Hasina ni nani?

Zaidi ya mwezi mmoja tu baada ya kuwa mkuu wa jeshi la Bangladesh, Jenerali Waker-Uz-Zaman amejipata Machoni pa umma , na kutangaza kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Sheikh Hasina ambaye alikimbia nchi siku ya Jumatatu.
Zaman alisema katika hotuba ya televisheni kwamba baada ya majadiliano na "vyama vyote vya kisiasa", iliamuliwa kuwa serikali ya mpito itaundwa.Haijabainika iwapo jeshi litakuwa na jukumu, lakini Zaman alisema: “Sasa tutakwenda kwa rais wa nchi, ambako tutajadili kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito, kuunda serikali ya mpito, na kusimamia taifa, " alisema.
Bangladesh imekumbwa na maandamano na ghasia zilizoanza mwezi uliopita baada ya makundi ya wanafunzi kutaka kufutwa kwa mfumo tata wa kupeana nafasi za kazi serikalini kwa jamaa za watu waliopigania uhuru wa nchi.
Hilo liliongezeka na kuwa kampeni ya kutaka kuondolewa madarakani kwa Hasina, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 15 na hivi majuzi alishinda muhula wa nne mfululizo mnamo Januari.Takriban watu 250 wameuawa katika ghasia hizo.Zaman, 58, alishika wadhifa wa mkuu wa jeshi Juni 23 kwa kipindi cha miaka mitatu - muda wa kawaida wa kuhudumu katika nafasi hiyo.
Alizaliwa Dhaka mnamo 1966, alimuoa Sarahnaz Kamalika Zaman, binti ya Jenerali Muhammad Mustafizur Rahman, ambaye alikuwa mkuu wa jeshi kutoka 1997 hadi 2000.
Zaman ana Shahada ya Uzamili katika Mafunzo ya Ulinzi kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Bangladesh na Shahada ya Uzamili katika Mafunzo ya Ulinzi kutoka Chuo cha King's College, London, kulingana na tovuti ya Jeshi la Bangladesh.
Kabla ya kuwa mkuu wa jeshi, alihudumu kama Mkuu wa Vikosi vya ulinzi kwa zaidi ya miezi sita - jukumu ambalo alisimamia, pamoja na mambo mengine, operesheni za kijeshi na ujasusi, jukumu la Bangladesh katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, na bajeti.
Katika huduma yake jeshini iliyodumu miongo mitatu na nusu, pia amefanya kazi kwa karibu na Hasina, akihudumu kama afisa mkuu wa kitengo cha Jeshi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.Zaman pia imehusishwa na uboreshaji wa jeshi, tovuti ya jeshi ilisema.Maandamano yalipoitikisa nchi kwa mara nyingine tena mwezi huu, Zaman alitoa wito kwa wanajeshi kuhakikisha usalama wa maisha ya watu, mali na vituo muhimu vya serikali.
Katika Picha: Sherehe na uporaji katika mitaa ya Dhaka
Kama tulivyoripoti hapo awali maelfu ya watu wamemiminika katika barabara za mji mkuu wa Dhaka nchini Bangladesh kusherehekea kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Sheikh Hasina.
Lakini licha ya sherehe hizo visa vya uporaji vimeripotiwa katika mji huo.
Waandamanaji waliovamia makazi rasmi ya Hasina wameiba samani na pia kuharibu sanamu ya Sheikh Mujibur Rahman- baba yake Hasina.
Hizi hapa ni baadhi ya picha:

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Watu wamekuwa wakiwasalimia maafisa wa kijeshi. Hapo awali mkuu wa jeshi alisema serikali ya mpito itaundwa. 
Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Sanamu ya Sheikh Mujibur Rahman huko Ganabhaban - makazi rasmi ya Waziri Mkuu - imeharibiwa na waandamanaji. 
Chanzo cha picha, Shahnewaz Rocky / BBC
Habari za hivi punde, Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh awasili India- ripoti
Taarifa zinazotufikia hivi punde zinasema kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh ametua katika uwanja wa ndege wa Hindon mjini Delhi.
Bado haijabainiki ikiwa Sheikh Hasina anapanga kusalia India au ataendelea na safari, lakini baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vinakisia kuwa huenda yuko njiani kuelekea London. Hili halijathibitishwa.
Amesikitika sana, asema mtoto wa Hasina

Chanzo cha picha, EPA
Mtoto wa Sheikh Hasina ameiambia BBC kwamba machafuko ya kisiasa yaliyoshuhudiwa nchini Bangladesh yamemuathiri sana mamake, akisema "amesikitika kwamba juhudi alizoweka kuimarisha nchi zimevurugwa na watu wachache wanaompinga".
Akiongea na kipindi cha BBC Newshour, Sajeeb Wazed Joy - ambaye alikuwa mshauri rasmi wa Waziri Mkuu hadi leo - anasema mama yake alikuwa akifikiria kujiuzulu tangu jana na alikuwa ameondoka nchini kwa usalama wake mwenyewe baada ya familia yake kusisitiza hilo.
Akitetea rekodi ya mama yake madarakani, anasema: "Ameigeuza Bangladesh. Alipochukua mamlaka ilionekana kuwa nchi iliyofeli. Ilikuwa nchi maskini. Hadi leo, ilizingatiwa kuwa moja ya mataifa yanayoinuka barani Asia. Amesikitika sana.”
Joy anakanusha tuhuma kwamba serikali imetumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji: "Umewapiga polisi hadi kufa - 13 juzi tu. Kwa hiyo unatarajia polisi wafanye nini wakati makundi ya watu wanapiga watu hadi kufa?”
Mamia ya watu wamekufa katika maandamano hayo kufikia sasa, huku idadi kubwa ya watu wakishiriki maandamano.
Wito kwa wageni kuondoka Lebanon huku hofu ya vita ikiongezeka

Chanzo cha picha, EPA
Nchi kadhaa zimewataka raia wao kuondoka Lebanon, huku hofu ikiongezeka ya mzozo mkubwa katika Mashariki ya Kati.
Iran imeapa kulipiza kisasi kwa njia "kali" dhidi ya Israeli,kwa kifo cha mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran siku ya Jumatano. Israel haijatoa maoni.
Mauaji yake yalikuja saa chache baada ya Israel kumuua kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukr huko Beirut.
Maafisa wa nchi za Magharibi wanahofia kwamba Hezbollah, wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran na vuguvugu la kisiasa lenye makao yake makuu nchini Lebanon, linaweza kuwa na jukumu muhimu katika ulipizaji kisasi wa aina hiyo, ambao nao unaweza kuibua jibu kali la Israel.
Juhudi za kidiplomasia za Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinaendelea kujaribu kupunguza mvutano katika eneo hilo.
Idadi inayoongezeka ya safari za ndege zimekatishwa au kusimamishwa katika uwanja wa ndege pekee wa kibiashara nchini Beirut.
Marekani, Uingereza, Australia, Ufaransa, Canada, Korea Kusini, Saudi Arabia, Japan, Uturuki na Jordan ni miongoni mwa nchi zilizowataka raia wao kuondoka Lebanon haraka iwezekanavyo.
Hofu ya kuongezeka kwa uhasama ambao unaweza kuikumba Lebanon iko juu zaidi tangu Hezbollah ilipozidisha mashambulizi yake dhidi ya Israel, siku moja baada ya mashambulizi mabaya ya Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza.
Ghasia nyingi zimezuiliwa katika maeneo ya mpakani, huku pande zote mbili zikionyesha kutovutiwa na mzozo mkubwa zaidi.
Hezbollah, hata hivyo, imeapa kujibu mauaji ya Shukr, yaliyotokea huko Dahiyeh, ngome ya kundi hilo katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.
Mbappe kujiunga na Real hakutaathiri nafasi ya Bellingham - Ancelotti

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Bellingham na Mbappe walikosa ziara ya Real ya kabla ya msimu mpya nchini Marekani - walikuwa wakiwakilisha mataifa yao kwenye Euro 2024. Jukumu Jude Bellingham katika klabu ya Real Madrid halitabadilika kufuatia kuwasili kwa Kylian Mbappe, anasema kocha Carlo Ancelotti.
Bellingham, 21, ambaye ni kiungo wa timu ya Uingereza alicheza katika nafasi ya juu katika klabu hiyo ya Uhispania katika msimu wake wa kwanza, akifunga mabao 23 katika mechi 42 waliposhinda La Liga na Ligi ya Mabingwa.
Mshambuliaji wa Ufaransa Kilian Mbappe, 25, alijiunga na Real msimu huu kwa uhamisho wa bure kutoka Paris St-Germain.
Ancelotti alikanusha madai kuwa Bellingham atacheza katika safu nyinine ili kutoa nafasi kwa Mbappe, akisema: "Hakuna mpango kama huo. Hakuna kinachobadilika.'
"Msimu wa kwanza, alitushangaza sana, kwa sababu alionyesha ubora wa ajabu, kijana aliyekomaa kweli. Msimu ujao hautakuwa tofauti.
"Atakuwa mmoja wa wachezaji bora tulio nao, akisaidia sana timu kwa ubora wake."
Muitaliano huyo pia alimuunga mkono Bellingham baada ya kukosolewa kwa uchezaji wake kwenye Euro 2024, ambapo England ilifika fainali.
"Haya ni maoni lakini Bellingham alicheza vizuri sana kwenye Euro," aliongeza.
Ghasia Uingereza: Waziri Mkuu anatarajiwa kufanya mkutano wa dharura

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anatazamiwa kufanya mkutano wa dharura baadaye - kufuatia wikendi ya machafuko yaliyoshuhudiwa katika maeneo tofauti nchini humo.
Polisi walikabiliana na matukio ya vurugu katika miji ya Rotherham, Middlesbrough na Bolton siku ya Jumapili - huku zaidi ya watu 150 wakisadikiwa kukamatwa.
Katika hotuba kwa taifa kupitia televisheni hapo jana, Keir Starmer alisema "watu katika nchi hii wana haki ya kuwa salama, na bado tunaona jumuiya za Kiislamu zikilengwa, katika mashambulizi dhidi ya misikiti".
Yote hayo yanafuatia shambulio la kisu huko Southport wiki iliyopita, ambalo lilisababisha watoto watatu (wenye umri wa miaka sita, saba na tisa) kuuawa.
Wengine watano walijeruhiwa, pamoja na watu wazima wawili.
Madai ya uwongo yalifuata kwamba mshukiwa - mwenye umri wa miaka 17 aliyezaliwa Cardiff kwa washirika wa Rwanda - alikuwa mkimbizi ambaye aliwasili Uingereza kwa boti mwaka 2023 na uvumi usio na msingi kuwa alikuwa Muislamu.
Mvulana huyo, Axel Muganwa Rudakubana, ameshtakiwa kwa makosa matatu ya mauaji, 10 ya kujaribu kuua na moja la kupatikana na kisu na anazuiliwa rumande ya vijana.
Kwanini Hasina amekimbilia India?

Chanzo cha picha, EPA
Kulingana na ripoti, "mahali salama" Sheikh Hasina anakoelekea ni jirani yake mkubwa - India.
Kwa miaka mingi, India imekuwa mshirika wake mkubwa na hii imefanya kazi vizuri kwa nchi zote mbili.
Bangladesh inashiriki mipaka na majimbo kadhaa ya kaskazini-mashariki mwa India - ambayo baadhi yamekuwa yakipambana na wanamgambo kwa miongo kadhaa, na serikali ya kirafiki huko Dhaka imekuwa ikisaidia kwa hilo.
Wakati wa utawala wake, Hasina alikabiliana na makundi ya wapiganaji wanaopinga India huko Bangladesh, hatua ambayo ilimleta karibu na utawala mjini Delhi.
Pia ametoa haki za usafiri kwenda India kuhakikisha bidhaa kutoka bara zinafika katika majimbo hayo.
Hasina, ambaye alianzisha uhusiano wa karibu na India tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996, amekuwa akihalalisha uhusiano wa karibu wa Dhaka na Delhi.
Wakati wa ziara yake nchini India mnamo 2022, aliwakumbusha watu wa Bangladesh jinsi India, serikali yake, watu na vikosi vya jeshi viliisaidia nchi wakati wa vita vya uhuru mnamo 1971.
Lakini ukaribu wake na Delhi - na uungwaji mkono wake na India - umekosolewa na vyama vya upinzani na wanaharakati ambao wanasema India inapaswa kuwaunga mkono watu wa Bangladesh na sio chama fulani.
Umati wa watu 'washangilia' mjini Dhaka

Chanzo cha picha, Reuters
Umati wa watu wenye furaha wamejitokeza barabarani nchini Bangladesh, kushangilia kuondoka kwa Waziri Mkuu wa muda mrefu Sheikh Hasina.
Watu wanaonekana wakipeperusha bendera huku baadhi ya waandamanaji wakicheza juu ya gari la jeshi lililokuwa limeegeshwa katika mji mkuu wa Dhaka, shirika la habari la AFP liliripoti.
Wakati huo huo, runinga ya Channel 24 ya Bangladesh imekuwa ikiwaonyesha waandamanaji waliojawa na furaha wakiingia kwenye makazi rasmi ya Hasina huko Dhaka, huku wengine wakipungia kamera walipokuwa wakimiminika kwenye boma hilo.
Habari za hivi punde, Serikali ya mpito itaundwa - Mkuu wa jeshi Bangladesh
Mkuu wa jeshi la Bangladesh amehutubia taifa kupitia televisheni muda mfupi uliopita.
Waker-uz-Zaman alisema serikali ya mpito itaundwa.
Aliongeza kuwa anaenda kukutana na Rais Mohammed Shahabuddin, na kwamba ana matumaini kuwa "suluhisho" lingepatikana mwisho wa siku.
Mkuu huyo wa jeshi alisema tayari amezungumza na vyama vya upinzani vya kisiasa nchini humo.
Haijabainika nani ataongoza serikali.
Naye Waker-uz-Zaman pia aliapa "haki" kwa watu wote wa Bangladesh - jambo ambalo waandamanaji wamekuwa wakidai kufuatia vifo vya mamia ya watu katika wiki chache zilizopita.
Bangladesh: Matukio ya hivi punde kwa ufupi
Ikiwa unajiunga nasi sasa hivi, haya ndio yanayojiri nchi Bangladesh kwa muhtasari:
- Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amejiuzulu na kukimbia nchi, BBC inafahamu kwamba Hasina, ambaye ameiongoza Bangladesh tangu 2009, yuko kwenye helikopta kuelekea mji wa Agartala nchini India, kulingana na BBC Idhaa ya Kibengali.
- Mkuu wa jeshi Jenerali Waker-Uz-Zaman anatazamiwa kuhutubia taifa, lakini hotuba yake tayari imechelewa. Inasemekana anakutana na "wadau"
- Kujiuzulu kwa Hasina kunakuja wakati maelfu ya waandamanaji wameingia barabarani katika mji mkuu Dhaka - huku maelfu zaidi wakitarajiwa kufuata, siku moja baada ya makabiliano makali kati ya polisi na waandamanaji kusababisha vifo vya takriban watu 90.
- Baadhi ya waandamanaji wameripotiwa kuvamia makazi rasmi ya Hasina huko Dhaka
- Takriban watu 300 wameuawa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita huku mamlaka ikikabiliana na waandamanaji wanaoipinga serikali
- Maandamano ya wanafunzi yalianza mwezi uliopita kwa madai ya amani ya kukomesha upendeleo katika kazi za utumishi wa umma, lakini tangu wakati huo yamebadilika na kuwa harakati ya kupinga serikali na kufuatiwa na machafuko ya nchi nzima, kumshinikiza Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajiuzulu.
Bangladesh: Waandamanaji wapora makazi rasmi ya waziri mkuu

Chanzo cha picha, Kituo cha 24
Picha sasa zimeibuka zikionyesha waandamanaji wakipora makazi rasmi ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina katika mji mkuu Dhaka.
Baadhi ya waandamanaji wanaonekana wakiwa wamebeba viti na kile kinachoonekana kama sofa kutoka kwa makazi ya Ganabhaban.
Habari za hivi punde, Helikopta ya Hasina inaelekea India
Hasina anaelekea katika mji wa Agartala nchini India, BBC Bangla inaripoti.
Waziri mkuu - ambaye amejiuzulu - mapema aliondoka mji mkuu wa Bangladeshi Dhaka kwa helikopta na dada yake, kulingana na ripoti.
Habari za hivi punde, Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina ajiuzulu

Waziri Mkuu Sheikh Hasina wa Bangladesh amejiuzulu, mwandishi wa BBC nchini humo amethibitisha.
Takribani watu 90 wauawa katika maandamano ya kuipinga serikali Bangladesh

Chanzo cha picha, Getty Images
Takribani watu 90 waliuawa nchini Bangladesh siku ya Jumapili, huku kukiwa na makabiliano mabaya kati ya polisi na waandamanaji wanaoipinga serikali.
Machafuko hayo yanakuja huku viongozi wa wanafunzi wakitangaza kampeni ya kutotii raia kumtaka Waziri Mkuu Sheikh Hasina ajiuzulu.
Maafisa 13 wa polisi waliuawa wakati maelfu ya watu waliposhambulia kituo cha polisi katika wilaya ya Sirajganj, polisi walisema.
Maandamano ya wanafunzi yalianza kwa madai ya kukomesha upendeleo katika kazi za utumishi wa umma mwezi uliopita, lakini sasa yamegeuka kuwa harakati kubwa ya kupinga serikali.
Polisi na baadhi ya wafuasi wa chama tawala walionekana wakiwafyatulia risasi waandamanaji wanaoipinga serikali.
Polisi pia walitumia mabomu ya machozi na risasi za mpira. Idadi ya waliofariki tangu vuguvugu la maandamano kuanza Julai sasa inafikia zaidi ya 280.
Amri ya kutotoka nje usiku kucha imetolewa tangu 18:00 (12:00 GMT).
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, alitoa wito wa kukomeshwa kwa "ghasia za kushtua" na akahimiza kujizuia kutoka kwa wanasiasa wa Bangladesh na vikosi vya usalama.
Alionesha wasiwasi wake juu ya maandamano makubwa yaliyopangwa huko Dhaka siku ya Jumatatu, akionya juu ya hatari ya "kupoteza maisha zaidi na uharibifu mkubwa".
Waandamanaji wa Bangladesh wamtaka Waziri Mkuu aondoke madarakani

Chanzo cha picha, Getty Images
Waandamanaji vijana wamekuwa wakiimba wakimtaka waziri mkuu wao aondoke madarakani.
Bi Hasina mwenye umri wa miaka 76 ametawala taifa hilo la Asia Kusini lenye watu milioni 170 kwa mkono wa chuma tangu 2009.
Lakini anakabiliwa na mvutano mbaya. Kuna amri ya kutotoka nje kwa muda usiojulikana kote Bangladesh na hofu ya kutokea kwa ghasia zaidi huku waandamanaji mamia ya maelfu, wakijiandaa kwa maandamano katika mji mkuu Dhaka.
Yeye mwenyewe amekuwa mkaidi, akiwashutumu wachochezi kama "magaidi". Waziri wa sheria Anisul Huq aliiambia BBC kwamba wito wa kumtaka ajiuzulu "haufai" na waandamanaji walikuwa wakijibu "kihisia".
Bi Hasina alikuwa amejitolea kuketi na kuzungumza na viongozi wa waandamanaji, lakini walikataa ombi hilo.
Kukaidi kwake ni dalili tosha kwamba hayuko tayari kuachia ngazi bila kupigana, jambo la kutia wasiwasi kuwa linaweza kusababisha umwagaji damu zaidi.
Binti wa rais mwanzilishi wa Bangladesh, Sheikh Hasina ndiye mwanamke mkuu wa serikali aliyekaa muda mrefu zaidi duniani.
Miaka yake 15 madarakani imejawa na shutuma za kutoweka kwa watu, mauaji ya nje ya mahakama, na kukandamizwa kwa watu wa upinzani na wakosoaji wake na anakanusha mashtaka, na serikali yake mara nyingi inashutumu vyama vikuu vya upinzani kwa kuchochea maandamano.
Bi Hasina amekabiliana nayo tangu aingie madarakani baada ya ushindi wa utata katika uchaguzi wa Januari.
