Kwa nini Marekani haiyaiti mapinduzi ya Niger kuwa ni mapinduzi?

Chanzo cha picha, AFP
Wanaume waliovalia sare za kijeshi walithibitisha kutwaa madaraka, kisha hofu na shangwe mitaani vikatanga. Hayo ndio yalikuwa mapinduzi ya Niger. Ukafuata mwitikio wa kimataifa - kawaida kulaaniwa na kauli ya kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia.
Hivyo ndivyo hali ilivyo tangu jeshi lilipomwondoa madarakani na kumweka kizuizini Rais Mohamed Bazoum Julai 26. ECOWAS, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, na Ufaransa zote zimejibu kwa kulaani na kuchukua hatua mbalimbali za adhabu.
Marekani pia imejiunga na kulaani lakini imeshindwa kutumia neno "mapinduzi."
Badala yake, inasema ni "jaribio la kutwaa madaraka" na "juhudi ya kunyakua mamlaka kwa nguvu" kutoka kwa Rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Bazoum – ikiongeza kuwa haina uvumilivu wowote kwa mabadiliko yasiyo ya kikatiba.
"Rais Bazoum bado ni rais", anasema Vedant Patel, naibu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. "Hajajiuzulu."
Msimamo wa Marekani unaonekana kuwa na athari ndogo kwa utawala wa kijeshi, unaoongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani, ambaye ametangaza serikali ya mpito.
Uchaguzi wa Maneno una maana gani?
Sheria ya Marekani inakataza usaidizi wa kifedha "kwa serikali ya nchi ambayo mkuu wake wa serikali aliyechaguliwa kihalali ameondolewa madarakani kwa mapinduzi au amri inayoungwa mkono na jeshi.
Utawala wa kijeshi wa Niger umetishia kwa balozi mpya wa Marekani aliyeteuliwa hivi karibuni Kathleen FitzGibbon, kuwa itavunja uhusiano ambao hadi sasa umekuwa ukidorora.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu 2012, Marekani imetumia wastani wa dola milioni 500 nchini Niger kwa ushirikiano unaolenga kuzuia shughuli za wanajihadi katika eneo la Sahel, ambapo makundi yenye uhusiano na al-Qaeda na kile kinachojulikana kama Dola ya Kiislamu wamepata kimbilio la vurugu zao.
Niger ndiyo mpokeaji mkubwa zaidi wa usaidizi wa kijeshi wa Marekani huko Afrika Magharibi, na ya pili kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Uwepo wa Marekani nchini Niger ni pamoja na kambi ya kijeshi ya Air Base 201 katika mji wa kaskazini wa Agadez, na kambi ya Air Base 101 katika mji mkuu Niamey.
Zote mbili zinatumika kwa shughuli za upelelezi na zinahifadhi takribani wanajeshi 1,100 wa Marekani walioko nchini humo. Marekani pia imetoa vifaa vya kijeshi na ndege kwa mshirika wake huyo wa Afrika Magharibi na kutoa mafunzo kwa vikosi vyake.
Washington inaichukulia Niger kama mshirika muhimu kwa kuzingatia hatari ya makundi ya kigaidi katika eneo hilo.
Mwezi Machi, Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza wa Marekani kuitembelea Niger, akiielezea nchi hiyo kama "mfano wa demokrasia katika eneo ambalo lina matatizo kwa sasa."
Hili alilisema si kwa ubora wa demokrasia nchini Niger, bali kuwepo kwa jambo moja tu; uchaguzi wa Rais wakati Bazoum alipomrithi mtangulizi wake Mahamadou Issoufou 2021. Uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kati ya tawala mbili za kiraia.
Kuvuka Sahel, kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Bahari ya Shamu, Guinea, Mali, Burkina Faso, Chad, na Sudan zote zinatawaliwa na tawala za kijeshi.
Mengi ya mataifa haya yanakabiliwa na uasi wa kijihadi, ndiyo maana jeshi la Marekani liko Niger. Likitoa mafunzo maalumu ya kila mwaka ya kukabiliana na ugaidi kwa wanajeshi kutoka karibu vikosi 30 vya Kiafrika.
Marekani inahitaji washirika
Marekani inahitaji washirika wa ndani ili kukomesha uwepo wa makundi yenye itikadi kali ambayo ni tishio sio tu kwa wakazi wa eneo hilo bali pia kwa watu wa Marekani na maslahi yake katika eneo hilo.
Mwezi Machi, wafanyakazi wa usalama wa Marekani walifanya kazi na wenzao wa Niger kuhakikisha Jeffery Woodke, mfanyakazi wa misaada wa Marekani ambaye alikuwa akishikiliwa na Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), tawi la kikanda la al-Qaeda anaachiliwa huru.
Woodke alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake huko Niger mwaka 2016. Alikuwa ni mateka wa tatu wa Marekani kuachiliwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hata hivyo, Marekani inakabiliwa na ukosoaji kwa matokeo yasiyotarajiwa ya hatua zake katika eneo hilo.
Wahusika wa baadhi ya mapinduzi ya kijeshi wa hivi karibu huko Afrika Magharibi ni wahitimu wa programu za mafunzo ya kijeshi za Marekani.
Jenerali Abdourahmane Tchiani, kiongozi wa mapinduzi ya Niger, ambaye alihudhuria mafunzo ya kukabiliana na ugaidi Washington mwaka 2009. Mamady Doumbouya na Assimi Goïta, wakuu wa nchi baada ya mapinduzi ya Guinea na Mali, pia ni wanufaika wa mafunzo ya kijeshi ya Marekani.
Mapinduzi ya Niger - au chochote Washington ingependa kuyaita - yanaakisi changamoto inazokabiliana nazo katika eneo hilo.












