"Hijabu ni sehemu ya maisha yangu" - nyota wa voliboli ya ufukweni

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa na umri wa miaka 19, Doaa Elghobashy alijua anakabiria kucheza kwa mara ya kwanza kwenye Olimpiki ya 2016, na angeweka historia mbele ya hadhira ya kimataifa.
Alikuwa sehemu ya timu ya kwanza ya wanawake ya Misri ya mpira wa wavu ya ufukweni kushiriki katika michezo hiyo.
Katika mechi ya ufunguzi kwenye ufuo maarufu wa Copacabana huko Rio de Janeiro, waliruhusu wachezaji kuingia uwanjani na suruali ndefu, shati za mikono mirefu na hijabu, mavazi yanayoakisi imani ya Kiislamu.
Akikabiliana na wapinzani Ujerumani waliovalia bikini, picha ya Elghobashy akigombea mpira ikawa chanzo cha ripoti nyingi na maoni kwenye mitandao ya kijamii.
Mijadala na maoni kuhusu tofauti za kitamaduni na nguvu ya michezo katika kuunganisha watu. Picha ya mechi hii nchini Brazili sasa ni sehemu ya picha za Olimpiki.
Miaka minane baadaye, Elghobashy anatazamiwa kurejea kwenye michezo hiyo kwa mara nyingine.
"Kwangu mimi, kama wewe ni Muislamu, unaweza kucheza voliboli ya ufukweni, unaweza kucheza kila kitu," anasema.
“Ninawaambia wasichana na wachezaji wote wa Waislamu. Ikiwa unataka kucheza, unaweza kucheza na hijabu au bila hijabu. Lakini cheza."
Michezo kwa wote

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hadi Olimpiki ya 2012, wachezaji wanawake wa mpira wa wavu walitakiwa kuvaa bikini, ambayo haipaswi kuzidi sentimita 7 kutoka juu hadi chini kwenye usawa wa mapaja, au mavazi yaliyozoeleka ya kuogelea - sheria ambayo wengine waliiona ni jaribio la uwazi la kuufanya mchezo kuwa wa kuvutia kimapenzi.
Bodi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Wavu (FIVB), ilieleza kuwa lengo inataka kuufungua mchezo huo kwa wachezaji wengi zaidi, huku ikinukuu maoni ya baadhi ya watazamaji ambao walisema wanatamani kungekuwa na wachezeaji aina ya Elghobashy kama ilivyokuwa katika mchezo wake wa kwanza wa Olimpiki.
FIFA, chombo kinachoongoza kandanda duniani, kilifuata kanuni mpya ya FIVB na kuruhusu uvaaji wa hijabu kwa sababu za kidini mnamo 2014.
Beki wa Morocco Nouhaila Benzina akawa mchezaji wa kwanza kuvaa hijab kwenye Kombe la Dunia la FIFA mwaka jana.
Kinyume chake, nchi mwenyeji wa Olimpiki ya 2024 Ufaransa, imepiga marufuku wachezaji wa timu zake kuvaa hijab, huku Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Amélie Oudea-Castera, akisema hatua hiyo imechukuliwa ili kufuata kanuni za kutokuwa na dini.
Mwezi Juni, Amnesty International na makundi mengine kumi yaliiandikia Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, ikiitaka marufuku hiyo kubatilishwa, ikisema inasababisha ubaguzi, kutengwa na kudhalilisha wanariadha wanawake Waislamu.
Bi Elghobashy anaamini uvaaji wa hijabu, ambao utaruhusiwa kwa wanariadha, unatoa "uhuru kwa wote" na anataka mashabiki kuzingatia michezo badala kuzingatia ikiwa wachezaji wamevaa vilemba vya kichwa au la.
"Ninapenda kucheza na hijabu, si bikini," alisema, akiyaita mabadiliko ya sheria ya FIVB kuwa ni ishara ya "heshima."
“Hijabu ni sehemu ya maisha yangu. Lakini sio kwa kila mtu.”
Elghobashy alishinda dhahabu katika Kombe la Afrika la Volleyball ya Ufukweni. Pia alishinda dhahabu katika Michezo ya Afrika ya 2019 na vile vile mataji matatu mfululizo katika Mashindano ya Mataifa ya Kiarabu.
Pia ni mwanachama wa timu za mpira wa wavu za ndani za Misri, lakini anafurahia maisha mchangani zaidi, licha ya medali na vikombe kwenye michezo ya ndani pia.
"Ninapenda voliboli ya ufukweni kuliko voliboli ya ndani," anasema.
"Ninajisikia vizuri uwanjani. Kumbukumbu zangu bora zaidi ni zile za voliboli ya ufukweni. Nina furaha kushiriki michezo ya Olimpiki tena.”
Ataweka Historia tena?

Chanzo cha picha, Getty Images
Juhudi za Misri kufuzu Tokyo 2020 zilizimwa na janga la uviko 19, ikimaanisha kwamba Elghobashy alilazimika kungoja kwa muda mrefu kupata nafasi nyingine katika michezo ya Olimpiki.
Akiwa na mchezaji mwenzake Marwa Abdelhady, lengo lao ni kupenya kwenye kundi la timu za Brazil, Italia na Uhispania.
Kazi hiyo inaweza kuwa ngumu kwa Misri iliyoorodheshwa ya 60 duniani.
Vyovyote vile iwavyo, Elghobashy, mjumbe mpya aliyeteuliwa wa Tume ya Wanariadha wa FIVB, ana furaha kupata fursa nyingine ya kuweka historia.
"Lazima niwe mwanachama hai kwa wachezaji wote wa Kiafrika," alisema.
"Nina furaha sana kuiwakilisha Afrika na wachezaji Waislamu na Waarabu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












